Ndoto ya Maana Sana Iliyotimizwa!
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA NIGERIA
ZAIDI ya Mashahidi 500 walikuwa kwenye mlo wa adhuhuri katika Kao la Betheli katika Nigeria siku ya Februari 9, 1994, wakati wangojezi walipoingia wakisukuma vigari vya kubebea kitindamlo cha aisikrimu. “Sherehe gani hii?” baadhi wakajiuliza kwa sauti kubwa. “Si aisikrimu tu, bali ni unamnanamna ulioje—vanila, chokoleti, forsadi, na jozi wee!”
“Aisikrimu ya rangi nne! Ina umaana wa pekee,” akatangaza mwenye kusimamia kwenye mlo. “Hii ni kusherehekea badiliko letu la kuanza uchapaji wa rangi nne!”
Makofi ya ngurumo yaliyofuata hayakuwa ya ile aisikrimu tu katika chumba cha kulia. Yalikuwa pia ya kuthamini matbaa mpya za uchapaji katika kiwanda kilichokuwa tayari kimeanza kutokeza magazeti Mnara wa Mlinzi na Amkeni! kwa rangi kamili. Sasa uchapaji wa rangi kamili ulikuwa halisi ulimwenguni pote. Nigeria lilikuwa ndilo la mwisho kati ya matawi makubwa ya uchapaji kugeuziwa uchapaji wa rangi kamili—hatua iliyokuwa imeanza miaka ya katikati ya 1980. Kuanza na toleo la Machi 15, 1994, la Mnara wa Mlinzi, uchapaji wa rangi mbili ukawa umetokomea Nigeria.
Zile matbaa mpya mbili Koenig na Bauer Rapida 104 zilikuwa zimetoka tawi la Uholanzi. Matbaa hizo ziliandamana na vifaa vingine vya uchapaji: kipiga-picha cha mabamba ya uchapaji, kikunjo, kiunganishi, kilengeta-karatasi na kikata-karatasi. Kwa jumla, vilikuwa vifaa vya tani 130 hesabu ya meta.
Matbaa Zieleazo Hewani!
Ilipoamuliwa kupeleka matbaa hizo tatizo likawa ni jinsi ya kuzisafirisha. Huwezi kuingiza matbaa za tani 35 katika mkoba! Bernd Sauerbier, aliyeratibu usafirishaji huo kutoka Uholanzi, alisema: “Tulilazimika kufikiria jinsi ya kusafirisha mashine hizo kwa njia bora zaidi kuzikinga na dosari.”
Kwa kawaida matbaa hizo husafirishwa katika mabweta makubwa sana ya mbao. Hata hivyo, akina ndugu walihofu kwamba huenda mbao zisiwe za nguvu za kutosha kuhimili ile mitukutiko mikali ya usafiri wa baharini pamoja na upakizi na upakuzi wa shehena bandarini. Njia nyingine rahisi zaidi na salama zaidi ingekuwa kuzipeleka katika vibebeo vya chuma cha pua vyenye urefu wa meta 12. Lakini mashine kubwa sana hivyo ziingizweje na kutolewaje katika vibebeo? Ndugu Sauerbier alisema: “Hii ilitaka jitihada kubwa kwa sababu hatukuwa na uzoefu wa kupakia matbaa ndani ya vibebeo. Hata kampuni iliyotengeneza matbaa hizo haikujua jinsi ya kuzisafirisha kwa njia hii.”
Utatuzi ulihusisha kutumia matakia-hewa (mito-hewa), yaitwayo pia modula za kujazwa hewa. Matakia-hewa haya hayavutii macho, lakini hufanya kazi hodari. Ni visehemu vya kutandazwa chini vilivyofanyizwa kwa alumini na mpira, vikubwa na vizito kidogo kuliko mkoba. Hewa ya kubanwa hupigwa bomba kupitishwa ndani yavyo na kusukumizwa chini. Hii huinua yale matakia-hewa kuyatoa kidogo ardhini pamoja na chochote kilicho juu yayo.
Hivi, hata vile visehemu vya matbaa vyenye uzito wa tani kadhaa vyaweza kutegemezwa juu ya takia-hewa jembamba. Visehemu hivyo huinuka-inuka, vikielea hewani! Kisehemu fulani kikiisha kuinuliwa kutoka ardhini, ni rahisi kukisukuma kwa mkono kokote ukitakako.
Mashahidi walilaza mbao ngumu juu ya sakafu ya vibebeo ili iwe na ulaini wa kutosha kuwezesha kutumia matakia-hewa ndani yavyo. Walilazimika pia kuhakikisha kwamba sakafu ya kila kibebeo ilikuwa tambarare kabisa. Mashine zilipokwisha kuwa ndani ya vibebeo, akina ndugu waliweka fito za chuma cha pua kandokando na juu ya kila kibebeo kufanya shehena iwe salama zaidi. Ilichukua majuma mawili katika Agosti 1993 kupakia visehemu vyote ndani ya vibebeo.
Siku ya Desemba 29, 1993, saa 12:00 jioni, vibebeo vitano vya kwanza viliwasili kwenye mfumo-tata wa Betheli ya Nigeria. Akina ndugu walikuwa wakingoja, wakiwa na hamu na utayari wa kuanza jasho la upakuzi. Walifanya kazi usiku kucha. Kwa kuwa zile mashine zilikuwa zimepakiwa juu ya matakia-hewa, wafanyakazi walipiga bomba hewa ya msongo, kisha vile visehemu vikateremka kwa ulaini kipande kwa kipande kutoka vibebeoni. Halafu kreni zikanyanyua kila kisehemu kukiweka juu ya jukwaa lililojengwa kipekee kwenye mwingilio wa kiwanda. Tena yale matakia-hewa yakafanyishwa kazi, na zile mashine zikasukumwa kwa mkono mahali ambapo zingefanyia kazi, huku umati wa watazamaji wenye idili wakitazama.
Itikio la Kupendezwa Sana na Magazeti ya Rangi Kamili
Saa 1:45 usiku, Februari 3, 1994, zile matbaa zilitokeza Mnara wa Mlinzi la Kiingereza la rangi kamili lililo la kwanza kuchapwa Nigeria. Upesi matbaa hizo zikawa zikichapa magazeti katika Kiyoruba, Kiigbo, Kiefiki, na Kifaransa.
Nakala za kwanza zilipopatikana kwa wale wanaoishi Betheli, ziliitikiwaje? “Nilisisimka wee!” akapaaza sauti mmoja wao. “Uvutio walo wapita kwa mbali kichapo kinginecho chote kilichotokezwa katika nchi hii.”
Mwingine alisema: “Mara tu yalipopatikana, nilijipatia nakala 20, nikapelekea familia yangu na marafiki. Nashindwa kuungoja wakati wa kuyatumia shambani.”
Mwingine bado (wa kike), alipoulizwa alihisije juu ya magazeti mapya hayo ya rangi kamili, alijibu: “Maridadi kabisa! Hii ni ithibati nyingine kwamba Yehova hujali kila mtu ulimwenguni pote!”
Kwa hiyo wafanyakazi kwenye Betheli walipokuwa wakionja aisikrimu yao ya rangi nne, walifikiria magazeti ya rangi kamili. Kama alivyosema mmoja wao, ilikuwa ni “ndoto ya maana sana iliyotimizwa.”
[Picha katika ukurasa wa 21]
Visehemu vya matbaa ya uchapaji vyenye uzito wa tani nyingi vilitegemezwa juu ya takia-hewa jembamba