Maajabu ya Bahari Nyekundu Chini ya Mawimbi
Watu husema kwamba uzuri (urembo) ni wa juujuu tu. Lakini mara nyingi uzuri halisi huwa chini ya sehemu ya juu—na hii haitumiki kwa watu tu. Niligundua hili kuwa kweli kuhusiana na Bahari Nyekundu. Ule mwambao mkame haukunipa kidokezo chochote cha uzuri wa ajabu unaomngojea mwogeleaji mwenye fursa nzuri ya kuchungulia chini ya maji yayo.
BAHARI Nyekundu ina sifa ya kuwa pamoja pa mahali pa kupendeza zaidi ulimwenguni kwa kupeleleza maajabu ya mwamba wa matumbawe. Kwa hiyo nilitaka sana kujionea mwenyewe kama ilikuwa na sifa ya haki.
Mara nilipokwisha kujionea ulimwengu wa chini ya maji, nilitaka kuuelewa vizuri zaidi. Mwanabiolojia wa majini Aaron Miroz, aliye stadi wa uhai wa maji ya Bahari Nyekundu, alijibu maswali yangu.
Kwa nini maji ya Bahari Nyekundu yana utele wa viumbe?
“Bahari Nyekundu huonekana na kutenda kama songamano kubwa, ikikusanya samaki wengi wa Bahari Kuu ya Hindi. Zaidi ya hilo, hapa tuna wingi mkubwa ajabu wa matumbawe. Mwambani waweza mara nyingi kupata kufikia spishi 20 za matumbawe yakikua katika meta moja tu ya mraba. Kifanyacho matumbawe yakue ni ile halijoto safi kabisa ya maji, ambayo hutofautiana kwa digrii chache tu muda wote wa mwaka. Zaidi ya hilo, kiasi kidogo cha mvua katika eneo hilo humaanisha kwamba ni mashapo (takataka za chini) machache yaingiayo baharini. Hili, nalo, hupunguza kiasi cha vichafuzi, ingawa nasikitika kusema kwamba katika miaka 15 iliyopita, hali imekuwa mbaya zaidi.”
Matatizo ni nini katika kulinda usalama wa hazina hii ya majini?
“Wakati wa kushughulika na makao yasiyoharibiwa sana kama mengineyo, uchafuzi ndilo tatizo kubwa zaidi. Katika Bahari Nyekundu, uchafuo hutokana na vyanzo vikuu vitatu: fosfati, mafugo ya samaki, na maji-taka ya kutoka miji ya pwani. Upenzi wa kupiga mbizi waweza pia kusababisha matatizo. Ule mwamba wa matumbawe ulio mwepesi kuharibika waweza kutiwa dosari kwa urahisi na wapiga-mbizi wazembe.”
Mmekuwa mkiuchunguza mwamba wa matumbawe katika Bahari Nyekundu kwa miaka mingi. Ni nini baadhi ya mambo ambayo mmejifunza?
“Tumegundua kwamba samaki wana ratiba zao za malisho. Wengine huanza kujilisha saa moja asubuhi, hujilisha kwa muda wa saa tatu, hupumzika kidogo, kisha hujilisha muda wa saa tatu nyingine alasiri. Wengine hujilisha usiku tu. Ratiba hizi ni za maana. Kama samaki wadogo zaidi wangesongwa daima na wawindaji mchana kutwa, wangesongeka sana washindwe kujilisha. Na samaki, kama wanadamu, waweza kuwa walaji wateuzi. Kwa kielelezo, samaki-vikundi wa samawati hupenda sana vijani maridadi vya basleti, vilivyo kawaida sana katika Bahari Nyekundu. Pia wale samaki tuliowafungia mahali tulipojitengenezea wenyewe wana chakula wakipendacho zaidi—wengine huwapenda tuna, hali wengine hupendelea samaki aina ya dagaa.
“Huenda ukafikiri kwamba kwa samaki, wanadamu wote wana sura moja, lakini sivyo. Samaki na hata wanyama wengine wasio na uti wa mgongo hujifunza kutambua watu. Nakumbuka pweza-mkubwa mmoja aliyepigwa kofi kimchezo na mwanakazi mwenzetu. Hakupenda kupigwa kofi, na hakukubali tena chakula kutoka kwa mtu huyo. Tumekuja kugundua ghafula kwamba watu wapole hufanikiwa zaidi kushughulika na samaki, hali mtu mtaka-mapambano au asiye na subira huwatia wasiwasi.”
Kivutiacho mpiga-mbizi mkosa-ujuzi ni ule uzuri na urangirangi wa namna mbalimbali.
“Hakika, wale samaki wa rangi za kuvutia ni wa kutazamisha. Lakini jambo ambalo watu wengi hawang’amui ni kwamba samaki fulani hutumia rangi zao kama viishara, kidogo kama vile sisi tutumiavyo taa za barabarani. Kwa kielelezo, wakati samaki-kikundi wa rangi nyekundu anapowinda badala ya kuchunga tu eneo lake, rangi yake hugeuka kuwa nyekundu yenye utusitusi mwingi zaidi. Samaki mjinga, ambaye huwindwa na yule samaki-kikundi, aweza kujua kutokana na rangi ya huyo samaki-kikundi ni wakati gani huyo ameenda ‘ofu’ ya kupumzika kuwinda. Katika vipindi hivi vya usalama, samaki mjinga hufukuza mbio samaki-kikundi avamiaye eneo lake.”
Hakuna shaka, uzuri mwingi isivyo kawaida wa uumbaji wa Mungu waweza kugunduliwa mahali pengi pasipotazamiwa. Maisha yangu yaliongezewa maarifa kwa kupeleleza sampuli ndogo tu ya uzuri huu. Ziara fupi hiyo kwenye makao yaliyo chini ya mawimbi iliongezea kina cha uthamini wangu kwa hazina za asili zilizo katika kilindi cha sayari yetu.—Imechangwa.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Samaki-simba alielea-elea kwa starehe hapo kandokando, bila kujali juu ya wawindaji. Wao hukaa mbali naye, kwa kuwa mapezi yake yenye vichomichomi yana sumu kali
[Picha katika ukurasa wa 26]
Ni mara chache ambapo samaki mjinga hukengeuka kutoka makao yake, ambayo huwa miongoni mwa vikono vya anemone mkubwa (kinyama kitengeneza matumbawe). Yeye hawezi kukamatwa na vidole hivyo kwa kuwa yeye husaidia kumsafisha mwenyeji huyo
[Picha katika ukurasa wa 26]
Samaki-vipepeo wana unamnanamna wa rangi. Miili yao iliyobabatana kama chapati ilipepewa- pepewa huku na huku, ikinikumbusha juu ya kipepeo
[Picha katika ukurasa wa 26]
Samaki Picasso, akiwa na milia yake ya madoido na kile kilichoonekana kama rangi njano nyangavu ya kupaka midomo, alinikumbusha juu ya kazi ya msanii asiyeonekana
[Picha katika ukurasa wa 26]
Samaki-malaika aliye maliki ana tabaka ya juu ya urangirangi mwingi ambayo hubadili rangi na muundo anapokua