Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 9/22 kur. 14-15
  • Matumbawe—Yamo Hatarini na Yanakufa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Matumbawe—Yamo Hatarini na Yanakufa
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Viunzi Vilivyopoteza Rangi na Uhai
  • “Dhahabu Nyekundu” ya Mediterania
    Amkeni!—2002
  • Ni Nini Kiwezacho Kufanywa ili Kuokoa Miamba ya Matumbawe?
    Amkeni!—1996
  • Miamba ya Matumbawe Inayokufa—Je, Wanadamu Wanahusika?
    Amkeni!—1996
  • Tumbawe Kubwa la Belize—Eneo Linalostahili Kuhifadhiwa
    Amkeni!—2007
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 9/22 kur. 14-15

Matumbawe—Yamo Hatarini na Yanakufa

HAKUNA mahali popote ambapo bahari-kuu ni nyangavu kuliko katika Tropiki. Nyangavu kabisa. Buluu nyangavu. Sakafu nyeupe ya mchanga iliyoko meta 15 chini ya maji huonekana kuwa karibu sana hivi kwamba unaona unaweza kuigusa! Vaa viatu-pezi vya kuogelea na kisetiri cha uso. Rekebisha kipumulio hicho unapoingia ndani ya maji yenye ujoto, viputo vya hewa vikifanya usione kwa muda mfupi. Kisha tazama chini. Hapo! Mwone samaki-kasuku mwenye rangi nyekundu na buluu akiuma-uma matumbawe na kutema vijipande, ambavyo huja kuwa sakafu ya mchanga. Kwa ghafula, rangi nyingi za kung’aa za samaki wa tropiki—nyekundu, manjano, buluu, kimachungwa, na kizambarau—zapita. Kuna hekaheka kila mahali. Hiyo yastaajabisha sana.

Huu ni msitu wa matumbawe. Huo umeinuka kutoka sakafu ya mchanga, ukielekea juu ukiwa na maelfu ya mikono yenye uhai. Mbele tu kuna mfanyizo maridadi sana wa matumbawe aina ya elkhorn, wenye kimo cha meta sita na upana unaokaribia kimo hicho. Kwenye umbali wa meta zipatazo 23 kuna matumbawe aina ya staghorn ambayo ni madogo kuliko yale elkhorn na yana matawi madogo yenye kujaza eneo kama msitu. Matumbawe hayo yamepewa majina yenye kufaa kama nini—karibu yafanane kabisa na pembe za wanyama! Samaki na viumbe vingine vya bahari hupata chakula na himaya chini ya matawi yayo.

Ingawa zamani ilidhaniwa kwamba matumbawe yamefanyizwa kwa mimea, sasa imejulikana kuwa yamefanyizwa kwa mawe ya chokaa yaliyotengenezwa na jumuiya za wanyama waitwao vichaza. Vichaza wengi ni wadogo, wakiwa na kipenyo kipunguacho sentimeta 2.5. Kichaza wa matumbawe mwenye mwili laini hujishikanisha na jirani yake kwa kutumia tishu yenye ute. Mchana matumbawe hufanana na jiwe, kwa kuwa vichaza huingia ndani ya viunzi vyao. Lakini usiku matumbawe hubadilika huku mikono yayo mirefu ikiyumbayumba kwa uanana, jambo lifanyalo mwamba wa tumbawe uonekane ukiwa mwororo na wenye manyoya-manyoya. “Mti” huo wa mawe ambao vichaza huushiriki ni kiunzi cha vichaza wote, wakiwa wameshikanishwa na kalsiamu kabonati iliyotolewa kutoka maji ya chumvi.

Kila aina ya jumuiya ya matumbawe hujenga umbo layo la kipekee la kiunzi. Ulimwenguni pote, kuna zaidi ya aina 350 tofauti-tofauti za matumbawe, zenye maumbo, ukubwa, na rangi za kushangaza. Majina yazo ya kawaida hukukumbusha juu ya vitu vilivyoko katika bara—tumbawe mti, nguzo, meza, au mwavuli—au juu ya mimea—tumbawe carnation, lettuce, zabibubua, au uyoga. Je, waona lile tumbawe-ubongo lililo kubwa? Ni rahisi kuona jinsi lilivyopata jina lalo!

Msitu huu wa chini ya maji umejaa uhai, tokea mimea na wanyama wasioweza kuonekana kwa macho hadi samaki taa, papa, kungamorei, na kasa. Na hapa pana samaki fulani ambao huenda hujapata kuwasikia—juhabahari mwenye rangi ya manjano nyangavu, Beau Gregories wa kizambarau, Vipenziwangwa wenye rangi nyeupe na nyeusi, baragumu wa kimachungwa, kitindasuri mwenye rangi ya buluu nyeusi-nyeusi, hamlets wenye rangi ya nili, simbabahari mwenye rangi ya kahawia hafifu. Na vipi juu ya ushimbu aina ya barbershop, kamba wa bahari, au samaki scarlet hawk? Rangi zote, saizi zote, maumbo yote. Wengine warembo, wengine wa ajabu—lakini wote wakipendeza. Waona, kuna pweza amejificha nyuma ya yale matumbawe-nguzo! Anakula kivaaute ambacho amefungua. Kama ilivyo na misitu ya bara, kuna uhai mwingi sana katika mazingira ya ulimwengu huo wa maji, wote ukitegemea unamna-namna wa msitu wa matumbawe. Duru ya uzaliano ya tumbawe na uwezo walo wa kusafiri na mawimbi ya bahari-kuu ili kujenga jamii mpya za miamba ya matumbawe ilielezwa kwa urefu katika toleo la Amkeni! la Juni 8, 1991, la Kiingereza.

Miamba ya matumbawe hufanyiza maumbo makubwa zaidi ya kibiolojia duniani. Kati ya hayo, Great Barrier Reef, iliyoko katika pwani ya Australia, huenea kwa kilometa 2,010 nayo ina eneo kubwa kama Uingereza na Scotland zikijumlishwa. Tumbawe laweza kuwa na uzito wa tani kadhaa na kuweza kuinuka zaidi ya meta tisa kutoka sakafu ya bahari. Miamba ya matumbawe hukua katika maji yote ya kitropiki yasiyo na kina, kama kina cha meta 60. Hayo yana hali ambazo hutofautiana eneo kwa eneo, hivyo kwa kuchunguza tumbawe, wataalamu waweza kujua bahari-kuu ambayo tumbawe lilikua na hata kujua mahali ambapo lilikua. Mazingira yanayohitajika kwa ajili ya ukuzi wa miamba ya matumbawe ni yale yasiyo na lishe sana majini, na ndiyo sababu bahari mara nyingi ni nyangavu sana katika sehemu ambazo zina matumbawe. Lishe ya tumbawe huandaliwa na miani (iitwayo kwa kisayansi zooxanthellae), ambayo huishi katika mwili wenye kupenyezwa na nuru wa vichaza, na pia na wanyama wasioweza kuonekana kwa macho ambao hushikwa na mikono ya tumbawe. Matokeo ni mwamba wa matumbawe ambao ni makao ya maelfu ya spishi za viumbe vya bahari katika bahari-kuu isiyo na kinga.

Miamba ya matumbawe pia ni mfumo wa ikolojia wa bahari wenye matokeo zaidi kibiolojia kuliko mifumo mingine yote. Gazeti U.S.News & World Report lilifafanua hivi jambo hilo: “Miamba ya matumbawe ni makao katika maji yalinganishwayo na misitu ya mvua ya kitropiki, yenye kujaa aina nyingi sana za uhai: marijanitanzu na sea whips zenye kuyumbayumba, feathery crinoids, neon-hued fish na sifongo, ushimbu, kambabahari na kiti cha pweza, pamoja na papa wenye kuogofya sana na kungamorei wakubwa. Wote hutegemea kuendelea kufanyizwa kwa matumbawe.” Miamba ya matumbawe pia hutegemeza uhai katika bara kwa kuandaa ukingo kati ya mawimbi mazito na kingo za bahari na kwa kuwekea msingi maelfu ya visiwa vya tropiki.

Tumbawe lenye afya ni lenye rangi ya kikahawia, kijani kibichi, nyekundu, au kimanjano, ikitegemea aina ya miani inayoishi katika vichaza wa tumbawe wenye miili yenye kupenyezwa na nuru. Miani isiyoweza kuonekana kwa macho hutumia nuru inayoangaza kupitia wenzi wayo wanyama na kufyonza taka za vichaza, kutia ndani kaboni dioksidi, kwa ajili ya lishe yayo. Kupitia usanidimwanga, nayo miani huandalia tishu za tumbawe oksijeni, chakula, na nishati. Ushirikiano huo pamoja na miani huruhusu tumbawe likue haraka zaidi na kuendelea kuishi katika maji ya tropiki yasiyo na lishe. Miani na tumbawe hufurahia zaidi ubora wa ulimwengu wa mimea na wanyama. Ni ubuni stadi na wenye hekima kama nini!

Viunzi Vilivyopoteza Rangi na Uhai

Si ajabu kwamba kuna utendaji mwingi huko chini! Lakini kile ni kitu gani? Ni viunzi vilivyopoteza rangi na uhai. Matawi yamevunjika na kuchakaa. Mengine tayari yamemomonyoka. Sehemu hii ya msitu wa matumbawe imekufa au inakufa. Hakuna samaki. Hakuna ushimbu. Hakuna kambabahari. Hakuna kitu chochote. Ni jangwa la chini ya maji. Unatazama kwa mshangao. Lashtua kama nini! Mambo mazuri uliyojionea yameharibika. Hata wakati ambapo umerudi kwenye boti, kuna maswali ya kufadhaisha. Ni nini ambacho kilisababisha uharibifu huu? Je, ni aksidenti? Maradhi? Sababu za asili? Unataka kujua majibu.

Ingawa tumbawe la mawe huonekana kuwa lenye nguvu sana, hilo ni dhaifu sana. Mguso wa binadamu waweza kusababisha uharibifu, hivyo wapiga-mbizi wenye hekima huepuka kuligusa, na waendesha boti wenye uangalifu huepuka kutia nanga juu yalo. Hatari nyinginezo kwa matumbawe ni uchafuzi wa kemikali, mimwagiko ya mafuta, maji machafu, ukataji wa miti, dawa na mbolea zinazopelekwa baharini, uchimbaji wa bahari, kuingia kwa matope baharini, na kuingia kwa maji yasiyo na chumvi. Kugongwa kihalisi na mikuku ya boti husababisha uharibifu mkubwa. Na halijoto za kupita kiasi zaweza kuharibu na kuua tumbawe. Mkazo utokeapo, tumbawe huondosha miani mingi, na upesi samaki huila. Hali zenye kuleta mkazo zikidumu kwa majuma au miezi fulani, tumbawe hupoteza rangi na kufa. Tumbawe likifa, mazingira ya mwamba wa tumbawe hufa pia. Mazingira ya kutegemeza uhai hufumuka na kutokomea.

Kupoteza rangi kwa matumbawe kumeenea sana katika bahari-kuu zote za tropiki. Tokeo ni kwamba kuna hangaiko miongoni mwa wanasayansi wa bahari ulimwenguni pote. Matumbawe yapotezapo rangi kwa kiasi kikubwa sana, uharibifu unaotokea hauwezi kurekebishwa. Kadiri ya matumbawe kupoteza rangi na vifo vinavyofuata imefahamishwa kwa ulimwengu kwa njia ya kuhuzunisha na kile ambacho kimetukia kotekote katika bahari za tropiki za ulimwengu katika miaka ya majuzi. Ingawa kumekuwa na visa vya vipindi vya matumbawe kupoteza rangi hapa na pale kwa miaka mingi, visa vya sasa havina kifani navyo vimekumba dunia yote. Kitu fulani kimekuwa kikishambulia matumbawe yaliyo hai ya spishi zilizo nyingi duniani pote, kikisababisha kuharibika kabisa kwa mazingira ya miamba ya matumbawe.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki