Miamba ya Matumbawe Inayokufa—Je, Wanadamu Wanahusika?
ULE Mkutano wa Kimataifa juu ya Miamba ya Matumbawe wa 1992 uliripoti kwamba watu wamesababisha kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja vifo vya asilimia 5 hadi 10 vya miamba ya matumbawe ya ulimwengu inayoishi na kwamba asilimia nyingine 60 yaweza kupotea katika miaka 20 hadi 40 ijayo. Kulingana na Clive Wilkinson wa Taasisi ya Australia ya Sayansi ya Bahari, ni miamba ya matumbawe iliyo sehemu za mbali pekee ambayo ina afya nzuri. Gazeti USA Today lilitaja kwamba maeneo yenye “miamba ya matumbawe [iliyoharibika] yatia ndani Japani, Taiwan, Filipino, Indonesia, Singapore, Sri Lanka, na India katika Asia; Kenya, Tanzania, Msumbiji, na Madagaska katika Afrika; Jamhuri ya Dominika, Haiti, Kuba, Jamaika, Trinidad na Tobago, na Florida katika Amerika. Sababu zenye kutokeza madhara zatofautiana, lakini idadi kubwa za watu sehemu za mwambao na ujenzi mwingi katika mwambao ni visababishi vya madhara hayo katika nchi hizo.”
Miamba ya matumbawe husitawi katika maji ya bahari yenye halijoto za kati ya digrii za Selsiasi 25-29, ikitegemea mahali yalipo. Lakini halijoto isiyobadilikana sana ya tumbawe lenye afya ni karibu sana na halijoto yenye kuumiza. Ongezeko la digrii moja au mbili zaidi ya joto la juu la kawaida katika kiangazi laweza kufisha. Ingawa visababishi vingi vinavyofanya matumbawe yapoteze rangi na kufa mahali mahali vyaweza kutambuliwa, wanasayansi wengi wanashuku kwamba kisababishi cha ulimwenguni pote chaweza kuwa ongezeko la joto duniani pote. Gazeti Scientific American liliripoti juu ya mkataa huu: “Ripoti za 1987 za matumbawe kupoteza rangi ilipatana na hangaiko lenye kuongezeka juu ya ongezeko la joto duniani. Basi, haikushangaza kwamba wanasayansi fulani walifikia mkataa wa kwamba miamba ya matumbawe ilikuwa ishara ya onyo la hatari—ishara ya kwanza ya ongezeko la joto la bahari-kuu za ulimwengu. Ingawa inaonekana kwamba halijoto iliyoongezeka ya maji ya bahari ya mahali-mahali ilisababisha matumbawe yapoteze rangi, hakuna hakika kwamba huko kupoteza rangi kunahusiana na ongezeko la joto duniani wakati huu.”
Gazeti U.S.News & World Report lilisema hivi: “Uchunguzi mwingi wa majuzi wa Karibea umeunga mkono wazo la kwamba bahari-kuu zenye joto kupita kawaida zilifanya matumbawe yapoteze rangi kwa wingi hivi majuzi.” Thomas J. Goreau, ambaye ni msimamizi wa Muungano wa Miamba ya Matumbawe wa Dunia, alilinganisha kwa njia ya kuhuzunisha hali ya miamba ya matumbawe na msitu wa mvua wa Amazon wenye kutokomea. “Bado kutakuwa na misitu ya mvua baada ya miaka hamsini,” yeye alisema, “lakini kwa kiwango ambacho miamba ya matumbawe inakufa, haitakuwapo kwa muda huo wa miaka hamsini.”
Uharibifu Ulimwenguni Pote —Kuna Visababishi Vingi
Kandokando ya Pwani ya Pasifiki ya Amerika ya Kati, asilimia zifikazo 95 za matumbawe zilikufa katika 1983. Kupoteza rangi kwa njia iyo hiyo lakini kwa njia isiyodhuru sana kulitokea vilevile katika Pasifiki ya kati na magharibi. Hali mbaya sana ya matumbawe kupoteza rangi ilipata Great Barrier Reef ya Australia na maeneo ya bahari-kuu za Pasifiki na Hindi. Thailand, Indonesia, na Visiwa vya Galápagos pia ziliripoti kupatwa na madhara. Baadaye, matumbawe mengi sana yalipoteza rangi karibu na Bahamas, Kolombia, Jamaika, na Puerto Riko na vilevile kusini mwa Texas na Florida, Marekani.
Uharibifu wa miamba ya matumbawe ulimwenguni pote ulikuwa ukitokea. Gazeti Natural History lilionelea hivi: “Katika muda mfupi kwa kulinganisha ambao mifumo ya ikolojia ya miamba ya matumbawe imechunguzwa, matumbawe hayajapata kuonekana yakipoteza rangi kwa kadiri kubwa hivyo kama majuzi. Peter Glynn, mwanabiolojia kwenye Chuo Kikuu cha Miami, amechunguza matumbawe yenye umri wa miaka 400 katika maeneo yaliyopoteza rangi sana mashariki mwa Pasifiki na hakupata uthibitisho kwamba misiba kama hiyo ilikuwa imetukia wakati uliopita. Hali hiyo ya matumbawe kupoteza rangi sana yaonyesha kwamba kuongezeka kwa joto kwa ujumla katika miaka ya 1980 huenda kulitokeza athari mbaya sana kwa miamba ya matumbawe nayo yaweza kutabiri wakati ujao wa matumbawe ikiwa joto litaongezeka zaidi. Kwa kusikitisha, kuongezeka kwa joto na kudhoofika kwa mazingira kwa hakika kutadumu na kuwa kubaya zaidi, kukiongeza duru za matumbawe kupoteza rangi.”
Gazeti U.S.News & World Report lilitaja kile ambacho kinaweza kuwa kisababishi kingine: “Kupunguka kwa tabaka ya ozoni, ambayo hukinga viumbe vilivyo hai visipate madhara kutokana na mnururisho wa urujuanimno, huenda pia kulichangia uharibifu wa majuzi wa miamba ya matumbawe.”
Katika maeneo ya pwani, ambamo zaidi ya nusu ya watu wa ulimwengu wanaishi, uzembe wa wanadamu umetokeza mkazo mwingi kwa miamba ya matumbawe. Uchunguzi mmoja wa Muungano wa Ulimwengu wa Uhifadhi pamoja na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa ulipata kwamba watu walikuwa wamedhuru au kuharibu kiasi kikubwa cha miamba ya matumbawe katika nchi 93. Maeneo mengi yanayositawi huingiza takataka zayo zisizotiwa dawa moja kwa moja katika bahari-kuu, na kuichafua.
Mikoko, ambayo huishi katika maji ya chumvi na kuchuja uchafu, hukatwa kwa ajili ya magogo na kuni. Matumbawe huharibiwa na kuchimbwa kwa ajili ya ujenzi. Katika Sri Lanka na India, sehemu kubwa sana za miamba ya matumbawe zimesagwa zikawa saruji. Meli zilizo kubwa na ndogo hutia nanga kwenye miamba ya matumbawe au kukwama juu yayo na kuisaga-saga.
Gazeti National Geographic lilifafanua kile kinachotukia katika Hifadhi ya Taifa ya Miamba ya Matumbawe ya John Pennekamp katika Florida: “Boti zao huchafua maji na kila kitu kilichomo ndani yayo kwa takataka za mafuta na uchafu. Waendeshaji wasio stadi hugonga miamba ya matumbawe. Hao huchafua bahari kwa vikombe vya plastiki, mikebe ya alumini, gilasi, mifuko ya plastiki, chupa, na kilometa nyingi za nyavu za kuvua samaki. Takataka hizo haziendi popote—kwa kuwa hizo haziwezi kuharibika.”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Kwa hisani ya Australian International Public Relations
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Kwa hisani ya Bahamas Ministry of Tourism