Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 11/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kushindwa kwa UM
  • Hakuna Elezo la Kibinadamu
  • Kufa kwa Ndege Kwatoa Maonyo
  • Akina Mama Matineja
  • Msaada wa Kompyuta kwa Viziwi
  • Baki la Usanii la Vita ya Ulimwengu 1 Lapangua Gari-Moshi Relini
  • Kutumia Bunduki-Mkono Kuua Kimakusudi
  • Dubu Wakimbizi
  • Wakimbizi Waonyeshwa Makubwa na Malimwengu Yote Mawili
  • Shamrashamra Hatari
  • Idadi Yenye Kuongezeka ya Wakimbizi
    Amkeni!—1996
  • Kuwasaidia “Wakaaji Wageni” ‘Wamtumikie Yehova kwa Kushangilia’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2017
  • Ulimwengu Ambao Kila Mtu Atafurahia
    Amkeni!—2002
  • Suluhisho Ni Nini?
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 11/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kushindwa kwa UM

“Huko si kushindwa kwa Umoja wa Mataifa tu; ni kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa. Na sisi sote tuna daraka la kushindwa huku,” akaomboleza katibu-mkuu wa UM Boutros Boutros-Ghali akisema juu ya machinjo katika Rwanda. “Ni mauaji ya jamii ambayo yamefanywa. Watu zaidi ya 200,000 wameuawa na jumuiya ya kimataifa ingali inazungumza lipasalo kufanywa.” Kama ilivyoripotiwa Mei 26, katibu-mkuu huyo alisema kwamba alikuwa ameandikia viongozi zaidi ya 30 wa Serikali akawasihi wapeleke vikosi na alikuwa amefanya kazi pamoja na mashirika tofauti kwa jitihada ya kupata utatuzi. “Kwa kusikitisha,” akaongezea, “nilishindwa. Hiyo ni kashfa. Mimi ndimi wa kwanza kusema hilo.” Ni mataifa machache ya Kiafrika yawezayo kulipa gharama za kupeleka vikosi, hasa kwa kuwa UM umekawiza kwa sababu ya magumu yao wenyewe ya kifedha. Mataifa yaliyo mengi ya Magharibi yamekataa kuhusika, na Bill Clinton rais wa Marekani alitaja kwamba kutumia uwezo wa kijeshi wa Kiamerika hakukustahilishwa na mambo yahusikayo. Bw. Boutros-Ghali aliweka lawama juu ya “uchovu wa kuchanga,” kwa kuwa mataifa yagawayo wafanya-kazi na fedha yanaombwa yafanye hivyo kwa ajili ya shughuli 17 tofauti za Umoja wa Mataifa, kulingana na The New York Times.

Hakuna Elezo la Kibinadamu

“Je, kuna lolote liwezalo kueleza kwa nini Rwanda ilipatwa ghafula na uchu wa damu wenye kushtua?” lauliza The Economist la London. “Hata uhasama wa muda mrefu [wa kikabila] hauelezi ni kwa nini ule uuaji wa kikatili ulitokea.” Ingawa Watutsi na Wahutu huenda wakaonekana tofauti kidogo, wao wameishi kwa karne nyingi kando kwa kando na wameshiriki lugha na utamaduni mmoja. Kichapo hicho chalinganisha tofauti yao ya kikabila na ile iliyo kati ya Waskoti na Waingereza. “Na hali sasa wamegeukana, si kwa mizinga wala bunduki za kufyatuliwa mbali bila huruma kwa watu wasiojulikana hususa bali kwa panga, majembe, marungu na mikono mitupu. Majirani wameua majirani, hata marafiki wa zamani za utotoni. Wanaume, wanawake na watoto wamechinjwa hali moja. Kwa nini? Hakuna mtu aelekeaye kuweza kueleza sababu.”

Kufa kwa Ndege Kwatoa Maonyo

Ingawa spishi hodari za ndege—shorewanda, maina, kunguru—husitawi chini ya hali kali, walio wengi wa ndege wa ulimwengu hawafanikiwi hivyo. Kati ya spishi 9,600 za ndege, asilimia 70 wanapungua na spishi 1,000 huenda wakaelekea kutoweka karibuni. “Jambo linaloshtua, zaidi ya zile hasara za moja kwa moja zinazotokea, ni kwamba ndege, tofauti na namna nyingine nyingi za uhai, ni vionyeshi vyema hususa vya afya ya spishi nyinginezo—na vya mifumo-mazingira kamili,” lasema gazeti World Watch. “Tunaloona si onyo tu la mzoroto unaokaribia sana, bali ni sehemu ya mzoroto halisi—kubomoka kwa mfumo wa mazingira utunzao afya ya sayari katika usawaziko ufaao.” Ndege huzuia wanyama na wadudu wasumbuaji wasizidi mno, huchavusha mimea, na kusaidia katika kurudisha misitu kwa kutapanya mbegu za miti katika vinyesi vyao. Lakini maisha zao zatishwa na makao yao yaharibiwa wakati wanadamu wabadilipo mandhari ya nchi—kukata misitu, kutumia ardhi zenye nyasi kulisha mifugo na kulima, kukausha ardhi zenye maji, na kufutilia mbali maeneo makubwa kwa miradi ya mabwawa makubwa—licha ya kuwaua moja kwa moja kwa kuwinda, kutumia mno kemikali, takataka zenye sumu, na mimwago ya mafuta. “Mwendo wa mitoweko ya ndege—pamoja na ile ya wanyama wengine na mimea—waonekana utaelekea kuongezeka kasi,” chasema kichapo hicho.

Akina Mama Matineja

Kila mwaka wanawake zaidi ya milioni 15 walio kati ya umri wa miaka 15 na 20 huzaa ulimwenguni pote, lakadiria Populi, gazeti moja la Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa. Tarakimu hii haitii ndani wasichana walio wachanga kuliko miaka 15, wala haihusishi mitunguo-mimba wala mitunguko-mimba. Katika Afrika pekee karibu asilimia 28 ya wanawake wote huzaa kabla ya umri wa miaka 18. Watafiti wasema kwamba miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa mimba za utineja katika kontinenti hiyo ni kukosa ujuzi juu ya mambo ya ngono, ndoa za mapema, na magumu ya kiuchumi yashawishayo wanawake vijana kuingia katika mahusiano ya baba-sukari pamoja na wanaume wenye umri mkubwa zaidi, walio matajiri. “Si kwamba tu wanawake matineja hukabili, kwa wastani, hatari mara mbili ya kufa wakati wa mimba au kuzaa mtoto kuliko wanawake wenye umri wa miaka 20-34,” lasema Populi, “bali pia vitoto vichanga vya akina mama matineja vyaelekea zaidi kufa.”

Msaada wa Kompyuta kwa Viziwi

Mfumo wa kompyuta uliositawishwa hivi majuzi huenda ukaanza karibuni kuwasaidia viziwi wajifunze kusema kikawaida. Kwa viziwi, kujifunza jinsi ya kusema kwakaribia kuwa kama kujifunza lugha ya kigeni. Uhakika huu ndio uliotokeza cheche za kusitawisha ile programu iliyofanywa na Kitovu cha Utafiti cha Tekinolojia za Lugha kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh, Scotland. Ripoti moja iliyotolewa na huduma ya habari ya Agence France-Presse yasema kwamba kompyuta ya mfumo huo huchanganua usemi wa mwanafunzi na kuonyesha papohapo ni wapi masahihisho na marekebisho yahitajiwa kwa matamshi yafaayo. Kwa kuongezea, programu hiyo itatia ndani mfululizo wa masomo yaliyokusudiwa kuwasaidia viziwi waboreshe pole kwa pole kiimbo na wizani zao za usemi. Mfumo huo utarekebishwa ili uwe wa kuwafundisha lugha za kigeni wanafunzi viziwi.

Baki la Usanii la Vita ya Ulimwengu 1 Lapangua Gari-Moshi Relini

Baki la usanii la Vita ya Ulimwengu 1 lilipangua relini gari-moshi lionewalo fahari na shirika la Reli ya Kitaifa ya Ufaransa, lile TGV (Gari-Moshi la Kasi), katika reli yalo ya Paris-Valenciennes iliyofunguliwa hivi majuzi ya kwenda kaskazini mwa Ufaransa. Gazeti la Paris Le Monde laripoti kwamba aksidenti hiyo ilitukia wakati mazege ya chini ya ardhi yasiyogunduliwa chini ya reli za TGV hilo yalipovunjika kwa ghafula. Eneo la aksidenti hiyo lilikuwa mahali pa mojapo mapigano ya kumwaga damu nyingi zaidi ya lile pambano la 1914-18, lile Pigano la Somme. Ingawa ni kama haiwezekani kuona mapito ya chini ya ardhi kutoka kwenye uso wa ardhi, mapito ya chini ya ardhi, mahandaki yaliyofukiwa, na mashimo ya makombora—masalio ya mapigano ya handakini ya vita ya ulimwengu ya kwanza—yametanda eneo lote kama mashimo ya sega la nyuki. Kikundi cha mafundi kilitumwa kuchana pito lote la reli ili maeneo mengine yawezayo kuleta hatari katika reli hiyo yaonekane na kuimarishwa.

Kutumia Bunduki-Mkono Kuua Kimakusudi

Ni watu wangapi waliouawa kimakusudi kwa bunduki-mkono katika 1992? Katika Australia kulikuwako 13, katika Uingereza 33, katika Kanada 128, katika Japani 60, katika Sweden 36, katika Uswisi 97, na katika Marekani idadi kubwa ajabu ya 13,220, kulingana na takwimu zilizotolewa hivi majuzi. Kama ilivyoripotiwa katika International Herald Tribune, watu 38,317 waliuawa na silaha-risasi katika visa vya kuua binadamu, vya kujiua, na aksidenti katika Marekani wakati wa 1991—vifo zaidi ya 100 kila siku. Bill Clinton rais wa Marekani alisema juu ya hospitali moja ambako idadi ya wenye kulazwa kwa majeraha ya mipigo ya bunduki ilipanda kutoka 449 hadi 1,220 katika muda wa miaka mitano tu. Japo machinjo hayo, watengenezaji hutokeza bunduki-mkono mpya kila sekunde 20.

Dubu Wakimbizi

Wanadamu sio pekee wanaotafuta kimbilio watoke kwenye uharibifu wa vita. “Kwa kuogopeshwa na vita inayoendelea katika ile iliyokuwa Yugoslavia, yule dubu wa kahawia anahama kutoka ile misitu mikubwa yenye ujani wa daima ya Bosnia na kuelekea kaskazini upande wa Italia,” lataarifu New Scientist. “Wanamazingira katika Italia na Slovenia wamejiunga pamoja kujaribu kulinda dubu wakimbizi hao.” Hata hivyo, dubu hao wamekuta hatari nyinginezo kutoka kwa wanadamu. Idadi fulani ya dubu hao wahamaji wameuawa na magari katika barabara za Italia na Slovenia. Wengine wameuawa pia baada ya kushambulia mifugo au wakauawa na wawindaji haramu. Wakulima katika Slovenia huruhusiwa na sheria kuua wanyama waharibuo mazao yao au washambuliao mifugo wao. Fedha zimechangwa kugawia dubu hao chakula na hivyo kuwasaidia wakae katika maeneo yalindwayo.

Wakimbizi Waonyeshwa Makubwa na Malimwengu Yote Mawili

Katika 1993 kulikuwa na ongezeko kubwa la tufeni pote katika idadi ya wakimbizi kufikia zaidi ya milioni 20, asema Sadako Ogata, kamishna wa Tume Kuu ya Umoja wa Mataifa Kwa Ajili Ya Wakimbizi. Kulikuwa na wakimbizi milioni 15 tu katika 1991, wakati mwanamke huyo alipoingia ofisini. Ukosefu wa imara kisiasa na mapambano ya kikabila ndizo sababu kuu za vuvumko la wakimbizi, laripoti gazeti Süddeutsche Zeitung la Kijerumani. Hata hivyo, yaonekana kwamba wakimbizi huonyeshwa makubwa na malimwengu yote mawili. Kwa nini? Kwa sababu katika nchi zao mpya karibishi, akaongezea kamishna huyo, mara nyingi wakimbizi walikuwa zaidi na zaidi shabaha ya kutendwa jeuri. Chuki ya kijamii na dharau kwa wageni ni mambo yanayokuwa yenye kuenea sana, akasema mwanamke huyo.

Shamrashamra Hatari

“Hesabu ya visa vya kuua binadamu yaongezeka asilimia 58 wakati wa sherehe,” laripoti gazeti la Kibrazili O Estado de S. Paulo. Katika São Paulo, “kulikuwa na visa vya kuua binadamu 79 na majaribio 124 ya kuua kimakusudi.” Kwa kuongezea kulikuwa na manyang’anyo 2,227 (277 katika 1993) na mashambulizi 807 (282 katika 1993) katika siku tano hizo, ambapo “wezi walishambulia makao, maduka, viwanda, watu barabarani.” Pia kulikuwa na visa vya kujiua 37 na vya kulalwa kinguvu 25. “Katika Rio de Janeiro, Polisi wa Kiraia waliripoti kwamba jeuri iliongezeka asilimia 14 kwa kulinganishwa na ile sherehe ya 1993. Kulikuwa na visa 63 vya kuua kimakusudi, 10 zaidi ya mwaka uliopita.” Akiandika juu ya “hatari za sherehe” katika gazeti Jornal do Brasil, Dom Eugênio de Araújo Sales, askofu-mkuu kadinali wa Rio de Janeiro, alisema: “Kanisa haliko dhidi ya ile sherehe kwa habari ya utumbuizo na udhihirisho wa shangwe, maana yote mawili hayo yafaa sana ili kuwapa watu usawaziko wa kisaikolojia. Naam, Kanisa lashutumu mivunjo ya sheria ya kiadili, ambayo sisi twapaswa kujitiisha kwayo, tupende tusipende.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki