Angahewa Letu Lenye Thamani
MEI 4, 1961, Malcolm Ross na Vic Prather walipazwa juu hadi kimo cha kilometa 34.6. Kwa wakati ule, kuweka rekodi mpya hakukuwa na maana sana kwa Ross. Kilichomvutia yeye kilikuwa ule mwono alipopandisha kwa makini pazia na kwa mara ya kwanza kutazama nje ya sitaha.
“Tulipofikia meta 30,500 ile mandhari,” akumbuka, “ilikuwa yenye uvutio kabisa.” Ross alipigwa na butwaa kwa rangi zilizotia alama tabaka mbalimbali za angahewa. Kwanza, kuna “samawati-nyeupe na nyangavu” ya angavungu, lienealo karibu kilometa 16 juu ya ardhi. Kisha angatando lawa na samawi nzito lizidilo kuwa jeusi zaidi na zaidi mpaka hatimaye anga lawa na weusi. “Katika kicho kinyamavu tulifikiria upendezi mkuu wa angahewa,” Ross akaandika katika National Geographic.
Hakika, angahewa letu lenye upendezi lastahiki kufikiriwa.
Lenye Kutegemeza Uhai
Kama tokeo, angahewa letu ni bahari kuu ya hewa ikumbayo dunia kwa kimo cha karibu kilometa 80. Lina uzani wa zaidi ya tani kwadrilioni 5 na hushinikiza juu ya vichwa vyetu kani ya kilogramu 1.03 kwa sentimeta moja mraba katika usawa wa bahari. Bila ya kanieneo hiyo ya hewa, hatungeweza kujimudu, kwani huzuia vioevu vya miili yetu visivukizwe. Angahewa la juu hukosa kanieneo ya hewa ya kutosha ili kutegemeza uhai wa kibinadamu. Kwa sababu hiyo Ross na Prather walilazimika kuvaa suti za anga zilizotiwa kanieneo. “Bila kanieneo ya bandia,” akaeleza Ross, “damu yetu ingechemka, mishipa yetu ya damu na viungo vingepasuka.”
Bila shaka, twahitaji pia bahari kuu hii ya hewa ili kuendelea kupumua. Hata hivyo, wengi wetu hatuijali kwa sababu hatuwezi kuiona. Mwanamume mwanadini wa nyakati za kale alisema kwa uthamini hivi: “[Mungu] anawapa wote uzima na pumuzi na vitu vyote.”—Matendo 17:24, 25, Zaire Swahili Bible.
Bila ya angahewa letu, hakungekuwa na kipitishio cha kulishikilia juu vumbi ambalo matone ya maji hujifanyiza kulizunguka. Kwa hiyo hakungekuwa na mvua. Lisingalikuwa angahewa letu, tungenyaushwa na miali ya moja kwa moja ya jua, na tungeganda usiku. Kwa kufurahisha, angahewa hutenda kama blanketi, likizuia baadhi ya joto la jua ili kwamba usiku usiwe baridi mno.
Zaidi ya hilo, angahewa huandaa ulinzi kutoka kwa vimondo vitokavyo nje ambavyo vingeweza kudhuru wakaaji wa dunia. “Magimba mazima kutoka angani,” aeleza Herbert Riehl katika kitabu chake Introduction to the Atmosphere, “huwasili katika mipaka ya nje ya angahewa yakiwa na masi ya jumla iliyokadiriwa kuwa tani elfu kadhaa kwa siku.” Hata hivyo, vingi vya vimondo huchanguka katika angahewa kabla ya kufikia uso wa dunia.
Lile angahewa huongezea furaha yetu ya uhai. Latupa sisi anga zenye upendezi za samawati, mawingu meupe yenye kutwesha, mvua yenye kuburudisha, na maawio na machweo bora zaidi. Zaidi, bila ya angahewa hatungaliweza kusikia sauti za wale tuwapendao, wala hatungaliweza kusikiliza muziki tuupendao. Kwa nini? Kwa sababu mawimbi ya sauti huhitaji kitu ambacho yaweza kusafiria. Hewa ni kipitishio kamili cha sauti, ilhali hakuna sauti husikika katika anga la nje.
Mchanganyo wa Ajabu
Katika nyakati za kale watu waliona angahewa kama kitu kimoja. Kisha, mwishoni mwa karne ya 18, wanasayansi walivumbua kwamba imefanyizwa na sehemu kuu mbili za gesi zenye kukamilishana, nitrojeni na oksijeni. Karibu asilimia 78 ya angahewa ni nitrojeni na asilimia 21 oksijeni; asilimia 1 iliyosalia hufanyizwa na gesi kama vile agoni, mvuke wa maji, kaboni dayoksidi, neoni, heli, kriptoni, hidrojeni, zenoni, na ozoni.
Kwa kawaida, oksijeni ni gesi yenye kutegemeza uhai ambayo miili yetu hufyonza kupitia kupumua. Kiwango cha oksijeni katika angahewa ni kamili kwa uhai duniani. Ikiwa kingepungua sana, tungesinziasinzia na hatimaye kukosa fahamu. Ikiwa ukolezi wayo ungeongezeka zaidi, husemwa kwamba hata vitawi vibichi na nyasi za pori vingewaka.
Nitrojeni ni kizimuaji kamili cha oksijeni, hata hivyo huchangia sehemu isiyo duni katika kuendeleza uhai. Viumbe hai wote lazima wawe nayo ili waishi. Mimea hupokea nitrojeni kutoka kwa angahewa kwa msaada wa mmweko wa radi na aina maalumu ya bakteria. Kwa zamu, nasi hupokea nitrojeni kutoka kwa chakula tulacho.
Kwamba angahewa letu hudumisha uwiano sawia wa oksijeni na nitrojeni ni ajabu. Nitrojeni hurudishwa kwenye angahewa, kwa msaada wa kazi yenye thamani ya vijiumbe hai. Na kuhusu oksijeni? Kiasi kingi hutumiwa kabisa katika mioto na kupitia kupumua kwa wanadamu na wanyama. Hata hivyo angahewa hudumisha kiwango chayo cha asilimia 21 ya oksijeni. Jinsi gani? Kupitia usanidimwanga—utaratibu wa kikemikali katika majani mabichi na miani—ambao huachilia zaidi ya tani bilioni moja za oksijeni kwenye angahewa kila siku.
Usanidimwanga hauwezi kutukia bila ya kaboni dayoksidi—gesi-katiti ambayo hufanyiza asilimia 0.03 tu ya angahewa. Kwa msaada wa mwanga, mimea hutegemea kaboni dayoksidi ili kukua na kutokeza matunda, kokwa, nafaka, na mboga. Kaboni dayoksidi pia hurudisha joto kuelekea dunia ili kuiweka sayari yetu ikiwa na joto. Lakini ikiwa kiwango cha kaboni dayoksidi kingeongezeka kupitia uchomaji wa miti mingi, makaa-mawe, gesi, na mafuta, hatimaye hali-joto duniani ingeweza kuwa yenye joto sana hivi kwamba uhai ungekoma. Kwa upande ule mwingine, ikiwa kaboni dayoksidi ingepungua mno, usanidimwanga ungekoma, nasi tungeangamia kwa njaa.
Ozoni ni gesi-katiti nyingine ambayo uhai duniani huitegemea. Ozoni katika sehemu ya juu ya angahewa liitwalo anga la juu hufyonza miali ya kiukaurujuani kutoka kwa jua. Hivyo sisi tulio duniani hukingwa kutokana na miali hii yenye madhara ya kiukaurujuani.
Hakika, kadiri tunavyopata kujua angahewa, ndivyo kunavyokuwa na sababu zaidi ya kustaajabu. Muundo walo wa nitrojeni, oksijeni, na gesi-katiti nyinginezo ni sawia kabisa. Saizi ya dunia pia ni sawia kabisa ili kudumisha usawaziko huo. Dunia ingekuwa ndogo na yenye uzani uliopungua, uvutano wayo ungekuwa hafifu sana, na sehemu kubwa ya angahewa letu lenye thamani ingevuja kuingia angani.
“Kwa upande ule mwingine,” chataarifu kitabu cha sayansi Environment of Life, “kama dunia ingekuwa na uzito zaidi kidogo kuliko ilivyo, kani ya uvutano iliyoongezeka ingefanya kadiri kubwa zaidi za gesi zihifadhiwe. . . . Usawaziko uhitajio uangalifu kati ya gesi za angahewa ungevurugika.”
Hata hivyo, kwa kusikitisha, ule “usawaziko unaohitaji uangalifu” unavurugwa na maisha ya kisasa ya mwanadamu. Hali hiyo ni nzito kadiri gani, na kuna tumaini gani kwamba angahewa letu lenye thamani litaokolewa kutoka kwa uharibifu?
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Machweo Yaonekanapo Bora Zaidi
Angahewa hurudisha miali ya jua katika njia hivi kwamba hupa anga mwonekano unaopendeza wa samawati. Kadiri jua lishukapo kuelekea upeo wa macho, miali yayo hulazimika kupita katika angahewa lililo jingi zaidi. Hili hutokeza unamnanamna ulio wazi wa rangi ambao wakaa-majijini huenda kamwe wasiuone.
Machweo juu ya majiji ya kiviwanda kwa kawaida ni hafifu na hukosa rangi isipokuwa nyekundu hafifu. Ikiwa eneo limechafuliwa zaidi, lasema jarida la New Scientist, “Jua huonekana kama sahani hafifu jekundu ambalo hufifia hata kabla ya kufikia ule upeo wa macho.”
“Katika angahewa lililo safi, lisilochafuliwa,” jarida lililo juu laeleza, “zile rangi za machweo huwa wazi hasa. Jua huwa njano nyangavu na anga jirani huwa uchungwa na njano. Kadiri Jua litokomeavyo chini ya upeo wa macho, rangi hizo hubadilika polepole kutoka kwa uchungwa hadi samawati. Mawingu yaliyotanda kwa chini huendelea kurudisha ule mwanga wa Jua, hata baada ya kuwa limepotea.”
Ebu wazia ule unamnanamna wa machweo marembo yatakayofurahiwa katika ulimwengu ulio huru na uchafuzi!—Ufunuo 21:3-5.