Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 1/8 kur. 16-18
  • Uanastampu—Hobi Inyweayo Wakati Iliyo Biashara Kubwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uanastampu—Hobi Inyweayo Wakati Iliyo Biashara Kubwa
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Nyeusi-Peni ya Namna ya Pekee
  • Mikusanyo Yaeleza Mengi
  • Stampu Ni Biashara Kubwa
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—2001
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2001
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2003
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 1/8 kur. 16-18

Uanastampu—Hobi Inyweayo Wakati Iliyo Biashara Kubwa

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA UINGEREZA

UANASTAMPU husemwa kuwa ndiyo “hobi kubwa zaidi ulimwenguni.” Stampu za kwanza zilikuwa ‘vipande tu vya karatasi iliyofunikwa upande wa nyuma kwa gundi ya kupaka, ambavyo mtumizi angeweza kushikisha nyuma ya barua kwa kupaka unyevu kidogo,’ kulingana na mrekebishi Mwingereza wa mambo ya posta Bwana Rowland Hill (1795-1879). ‘Vipande vyake vya karatasi’ vilikuja kupendwa na wengi sana hivi kwamba leo stampu za posta zasifiwa kuwa vumbuo lililobadili hali ya mawasiliano kotekote ulimwenguni.

Kwa wakusanyaji na wauzaji, thamani za stampu hutofautiana kuanzia sifuri hadi madonge makubwa ajabu ya dola milioni moja au zaidi. Hili laweza kuwaje ilhali stampu za posta zimezagaa kila mahali? Na ni nini kizipacho uvutio wazo na thamani yazo?

Nyeusi-Peni ya Namna ya Pekee

Stampu za kwanza kupigwa chapa kwa mikono zikionyesha utangulio wa malipo ya posta zilivumbuliwa na mfanya-biashara William Dockwra, aliyeanzisha Posta ya Peni ya London katika 1680. Barua zilizopelekwa kwenye nyumba ya upokezi zilipigwa stampu kwa alama-posta yenye mistari miwili ya pembetatu iliyoandikwa maneno UPOSTI WA PENI UMELIPIWA, tayari kusafirishwa na wajumbe wa Dockwra. Lakini matarishi na wapelekaji wengine walipinga vikali mpango huu kwa sababu walihisi riziki yao ilikuwa imetiwa hatarini. Pia ofisi ya posta ya serikali ilichukua kwamba posta ya Dockwra ilikuwa kuvunja haki yao ya kushughulikia kazi hiyo wakiwa peke yao.

Ilipofika mapema ya karne ya 19 ndipo marekebisho ya posta yalipofaulu kufanya stampu za peni za kusafirisha barua kwa posta zipatikane kotekote nchini. Katika Mei 1840, stampu ya kwanza ya posta yenye kubandikwa ilianza kuuzwa Uingereza na muda si muda ikawa maarufu ikiitwa Nyeusi-Peni. (Ona picha.) Haikutobolewa vitundu, na ilikuwa lazima kila stampu ikatwe kutoka kwenye shiti fulani.

Katika 1843, Brazili ikawa ya pili kwa Uingereza tu katika kutoa stampu za kubandika zilizo halali kutumiwa kotekote katika nchi nzima. Pole kwa pole nchi zile nyingine zilikubali kutumia stampu hizo kwa upelekaji wa barua za nchini. Baadaye, ili kusahilisha upelekaji wa ng’ambo, muungano wa posta ulimwenguni pote ulisitawi. Leo Muungano wa Posta Ulimwenguni Pote, ulio na makao makuu katika Bern, Uswisi, ni wakala maalumu wa Umoja wa Mataifa.

Mikusanyo Yaeleza Mengi

Kadiri mawasiliano ya kimataifa yalivyokuwa yakiongezeka, kila nchi ilibuni na kuchapa stampu za pekee. Baadhi yazo, ziitwazo za maadhimisho, hutoa vielezi vya matukio na watu wenye kutokeza; nyingine, ziitwazo mahususi, zimeonyeshwa wazi kuwa za utumizi wa kawaida katika mfululizo wa viwango vya kutimiza mahitaji tofauti-tofauti ya posta. Muda wa miaka iliyopita simamizi 600 hivi za posta zimetoa stampu mpya zikadiriwazo kuwa 10,000 kila mwaka. Mwanafunzi mzito wa mambo ya stampu (mwanastampu) na mtu afurahiaye tu kukusanya stampu ili kupisha wakati waweza wote wawili kupata angalau machache ya mapendezi yao kati ya zile stampu tofauti-tofauti robo-milioni zilizotolewa kufikia hapo!

Kwa wazi, kukiwa na stampu nyingi na za unamna-namna mkubwa hivyo, hakuna mkusanyaji awezaye kutarajia kuwa na nakala ya kila namna ya stampu iliyopata kutolewa. Badala ya hivyo, wengi huchagua kukusanya stampu kulingana na vichwa vya habari. Anga za juu, Antarktika, Biblia, dini, Esperanto, hali ya hewa, huduma za posta, jiolojia, kuvu, madaraja, makaa-mawe, mapango, maua, michezo, Michezo ya Olimpiki, moto, mruko wa ndege, Msalaba Mwekundu, muziki, nchi, ndege, nishati, nyuki, sinema, tiba, ukulima, Ulaya, UM, upigaji-picha, usafirishaji, uviwanda, na hata wanyama, zote hizo ni habari ziwezazo kukusanywa. Stampu zina kitu chochote kile.

Wakusanyaji wengine hukaza fikira juu ya mitofautiano ya stampu. Hii yahusisha nini? Tazama tena ile Nyeusi-Peni. Je, waziona herufi zilizochapwa katika pembe za chini za stampu? Mwanzoni, stampu hizi zilichapwa katika shiti iliyofanyizwa kwa stampu moja-moja 240 zilizopangwa katika mistari 20 iliyolala sawasawa kila mmoja ukiwa na 12. Stampu ya kwanza katika safu ya kwanza ilikuwa na herufi AA; ya mwisho katika safu hiyo ilikuwa na AL, na kuendelea hivyohivyo kialfabeti kwa kuteremka chini kwenye shiti hiyo hadi TA na TL mwanzoni na mwishoni mwa safu ya 20. Herufi hizo zilitobolewa vitundu kwa mkono katika miraba ya pembeni ya kigezo hicho katika hatua za mwisho za kutayarisha bamba la uchapaji. Mwajiriwa wa ofisi ya posta angeshuku ubuni wa hila ikiwa stampu zilizo katika barua nyingi alizoshughulikia zilionyesha herufi mbili za namna ileile.

Hata ingawa kulitolewa stampu moja-moja za Nyeusi-Peni zikadiriwazo kuwa milioni 68, mkusanyaji mwenye stampu isiyotumiwa leo ana kitu nadra chenye thamani—kuanzia dola 4,200 hadi dola 6,800.

Mbali na mitofautiano isiyoonekana wazi katika kigezo, stampu ambazo huchapwa kutokana na mabamba tofauti ya uchapaji, katika karatasi yenye alama-maji (kigezo hafifu katika karatasi, kionekanacho kishikwapo dhidi ya nuru) zilizo tofauti, na hata zile zenye hesabu tofauti ya vitundu (vishimo kandokando ya kingo), zote huvuta upendezi wa wakusanyaji wataalamu. Ili wafaulu, wataalamu hao huhitaji vibano vya kuinua (Usitumie kamwe vidole vyako!) na kioo cha kukuza ukubwa. Geji hugundua tofauti za vitundu; taa za kiuka-urujuani huonyesha miharibiko, ming’ao iliyofichika, na vijambo vingine.

Wakusanyaji fulani huonyesha upendezi maalumu katika makosa ya kigezo na uchapaji wa stampu. Kwao, jambo kuu ni kuwa na stampu za aina ambayo wakusanyaji wengine wamekosa kuona. Fikiria tofauti katika thamani. Kwa makadirio ya 1990, stampu Nyekundu-Peni ya 1841 iliyokosa herufi A, hilo likiwa ni kosa la stampu ya kwanza kwenye safu ya pili ya shiti, ilikuwa na thamani ya mara 1,300 hivi za ile isiyo na kosa hili!

Stampu Ni Biashara Kubwa

Siku hizi ile hobi ya kukusanya stampu huvutia watega-uchumi wa namna mbalimbali. Mtega-uchumi wa kweli hununua vibebeo vyenye stampu sanifu zilizo nadra ambazo washughulikiaji huamini zaelekea zaidi kupanda thamani katika kipindi fulani hususa. Kitega-uchumi hicho kikiisha kukomaa, muuzaji huchukua hatua ya kuuza mapato ya mteja wake kwa bei za juu zaidi ziwezazo kupatikana. “Alama-posta nyepesi zenye kuonekana ni muhimu kwa stampu zilizotumika kiposta—kwa kulinganisha, stampu zile zipatikanazo kwa wingi zaidi huwa haba kupatikana zikiwa na alama-posta bora au zisizo za kawaida, nazo hustahiki pia malipo bora kwa kadiri hiyohiyo. Hali ya stampu ni ya maana ili stampu iwe ya thamani bora,” aandika mjuzi wa stampu James Watson.

Katika 1979 Daily Mail la London liliripoti kwamba “katika miaka mitano iliyopita, stampu sanifu (zile za tarehe za kutoka 1840 hadi 1870) zimekuwa zikipanda bei zaidi kuliko hisa na namna nyinginezo za vitega-uchumi, na katika visa vingi, hata zaidi kuliko bei za nyumba.” Kibebeo chenye stampu saba nadra zilizokuwa na bei ya dola 84,700 katika 1974 kiliongezeka thamani kikawa dola 306,000.

Katika 1990 tangazo moja la Time International liliripoti hivi: “Stampu, zikiwa kitega-uchumi, zimepita katika mepesi na mazito. Katika miaka ya 1970 bei ziliongezwa haraka sana huku wakisiaji wakitazamia faida kutokana na vibebeo vya kutega uchumi vilivyojazana stampu haba. Lakini London ilipokuwa ikiandaa lile Onyesho la Ulimwengu la Stampu la 1980 layo, mambo yalienda mrama na wakisiaji hao wakakuta kwamba watu pekee waliokuwa tayari kuimarisha soko hilo walikuwa ni wakusanyaji wenyewe, nao walikuwa wametumia akili kujiondoa. ‘Watega-uchumi walipojaribu kupata fedha kwa kubadilishana na stampu zilizokuwa katika vibebeo vyao, walikuta kwamba stampu nyingi hazikuwa haba kama vile walivyokuwa wamedhania,’” basi wakapata hasara. Lo, hili ni onyo lililoje kwa wale watumiao stampu kutega uchumi!

Basi, wewe ukiwa mkusanyaji au hata mwanastampu, lenga kuwa na usawaziko. Furahia stampu zako. Jifunze kutokana nazo—juu ya ulimwengu, jiografia, vikundi vya watu, na tamaduni zao. Usiache ukusanyaji ukunywee mno. Pima kwa uangalifu upendezi wako katika stampu, na ukadirie jambo hilo dhidi ya mambo yaliyo ya maana zaidi maishani.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Nyeusi-Peni

[Picha katika ukurasa wa 18]

Stampu kutoka Austria, Hispania, na Uingereza

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki