Chuki Yangu Iligeuka Kuwa Upendo
Kama ilivyosimuliwa na Ludwig Wurm
Ulikuwa usiku wenye baridi zaidi niliopata kuuona—chini ya digrii 52 Selsiasi. Tarehe: Februari 1942—katikati ya majira ya baridi na wakati wa vita. Mahali: ukanda wa vita katika Urusi karibu na Leningrad. Mimi nilikuwa askari katika Waffen-SS ya Ujerumani (Waffen Schutzstaffel), jeshi teule lenye silaha. Sajini mmoja na mimi tulikuwa tumepewa lile jukumu la kuogofya la kuzika wenzetu zaidi ya 300, walio wengi wakiwa wamekufa katika matundu ya kujificha—wakagandishwa na barafu hadi kifo. Hata hivyo, ardhi iligandamana barafu sana ikawa haiwezekani kuwazika. Badala ya kuwazika, tulirundika zile maiti ngumu nyuma ya nyumba zilizo tupu, sawasawa na magogo ya miti. Ingekuwa lazima zingoje mpaka masika ili zizikwe.
HAITOSHI kusema kwamba mgawo huu mkakamavu ulinisikitisha sana. Kwa uhoi wangu nilibobokwa na maneno nikasema hivi, nikiwa na machozi: “Unterscharführer (sajini), waweza kuniambia mauaji yote haya ya kijinga ni ya nini? Mbona chuki nyingi hivyo ulimwenguni? Mbona tulazimike kufanya vita?” Alinijibu kwa sauti ya chini: “Ludwig, kwa kweli mimi sijui. Nakuambia kweli, hata siwezi kuelewa kwa nini mateso na chuki ni mengi hivyo ulimwenguni.”
Siku mbili baadaye niligongwa shingoni na risasi iliyokuwa ikipasuka ikaniacha nimepooza, bila fahamu, na nusura ya kufa.
Lakini maswali yangu yenye kuendelea yaliniwezesha hatimaye kujionea mwenyewe jinsi chuki na mtamauko ziwezavyo kugeuka kuwa upendo na tumaini. Acha nieleze.
Kukutana Kwangu na Hitler
Nilizaliwa Austria mwaka 1920. Baba yangu alikuwa Mlutheri, na mama yangu alikuwa Mkatoliki. Nilihudhuria shule ya faragha ya Kilutheri, nilikopokea mafunzo ya kidini ya ukawaida kutoka kwa kasisi mmoja. Lakini sikufundishwa juu ya Yesu Kristo kuwa Mwokozi. Mkazo ulielekezwa daima kwa “führer aliyetumwa na Mungu,” Adolf Hitler, na Milki ya Ujerumani-Jumla. Kitabu changu cha mafundisho kilionekana kuwa kile kitabu cha Hitler Mein Kampf (Mng’ang’anio Wangu) badala ya Biblia. Pia nilijifunza kitabu cha Rosenberg Der Mythos des 20ten Jahrhunderts (Hadithi ya Kutungwa ya Karne ya 20), ambamo alijaribu kuthibitisha kwamba Yesu Kristo hakuwa Myahudi bali Mwarya wa hudhurungi safi!
Nilikuja kusadikishwa kwamba Adolf Hitler kweli alitumwa na Mungu, na katika 1933, nikaona fahari ya kujiunga na harakati ya Vijana wa Hitler. Waweza kuwazia jinsi nilivyosisimuka nilipopewa fursa ya kukutana naye kibinafsi. Hadi leo hii, mimi hukumbuka wazi jinsi yeye alivyonitazama kwa macho yake yenye kupenya ndani isivyo kawaida. Niliingiwa sana na jambo hilo hivi kwamba nilipofika nyumbani, nilimwambia mama: “Kuanzia sasa na kuendelea maisha yangu si mali yako. Maisha yangu ni mali ya führer wangu, Adolf Hitler. Nikiona mtu yeyote akijaribu kumwua, nitajibwaga mbele yake niokoe uhai wake.” Miaka mingi baadaye ndipo nilipoelewa kwa nini mama alilia tu na kunishika karibu sana.
Uvutano wa Mapema wa Chama cha Nazi
Katika 1934 Wasoshalisti wa Kitaifa waliasi dhidi ya serikali ya Austria. Wakati wa pambano hili Chansela Engelbert Dollfuss, aliyepinga muungamanisho wa Austria na Ujerumani, aliuawa na Wanazi. Viongozi wakuu wa maasi hayo walikamatwa, wakafanyiwa kesi, na kuhukumiwa kufa. Serikali ya Austria ilianzisha sheria ya kuhukumiwa na jeshi, nami nikawa mtendaji katika ile harakati ya kichinichini ya Chama cha Kisoshalisti cha Kitaifa cha Wafanyakazi Wajerumani—chama cha Nazi.
Ndipo Anschluss, muunganisho, wa Austria kwa Ujerumani ukaja katika 1938, na chama cha Nazi kikawa halali. Muda si muda nikawa miongoni mwa washirika washikamanifu wa chama walioalikwa na Hitler mwaka huohuo kuhudhuria kusanyiko la kila mwaka la chama cha Reich katika Nuremberg juu ya Konde la Zeppelin. Huko nilimwona Hitler akionyesha mamlaka yake yenye kuongezeka. Hotuba zake zenye makeke ya sauti, zilizoduwaza wasikilizaji, zilijawa na chuki dhidi ya wapinzani wote wa Chama cha Nazi, kutia na Uyahudi wa kimataifa na Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa, wajulikanao sasa kuwa Mashahidi wa Yehova. Nakumbuka wazi jisifu lake hili: “Adui huyu wa Ujerumani Kuu, vinyangarika hawa Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa, wataharibiwa kabisa katika Ujerumani.” Nilikuwa sijapata kukutana na yeyote wa Mashahidi wa Yehova, kwa hiyo nilijiuliza walikuwa nani watu hatari hawa aliokuwa akiwasema kwa sumu nyingi hivyo.
Utumishi Wangu Kwenye Kambi ya Mateso ya Buchenwald
Ilipozuka Vita ya Ulimwengu 2 katika 1939, nilijitolea mara hiyo kujiunga na majeshi mateule ya Ujerumani, yale ya Waffen-SS. Nilisadiki kwamba dhabihu zozote nilizohitajiwa kufanya katika vita hii zingekuwa za haki, kwa maana führer wetu alitumwa na Mungu, sivyo? Lakini nilifadhaika katika 1940, vikosi vyetu vilipokuwa vikipita katika Luxembourg na Ubelgiji kuingia Ufaransa, wakati ambapo kwa mara ya kwanza niliona askari mfu akiwa karibu—kijana Mfaransa mwenye sura nzuri. Singeweza kuelewa ni kwa nini wanaume Wafaransa wangetaka kudhabihu uhai wao katika vita ambamo, Mungu akiwa upande wetu, ni wazi Ujerumani ingeshinda.
Nilijeruhiwa katika Ufaransa nikarudishwa kulazwa hospitali katika Ujerumani. Baada ya mimi kupona nilihamishwa nikapelekwa kazini katika eneo la nje-nje la kambi ya mateso ya Buchenwald, karibu na Weimar. Tulipokea maagizo makali kutoka kwa maofisa wetu tusichangamane na walinzi wa Totenkopfverbände (Kichwa cha Kifo) wa SS wala na wafungwa. Tulikatazwa hasa tusiingie katika ile sehemu ya kulala ya wafungwa, iliyozungushiwa ukuta mrefu wenye lango kubwa. Juu ya lango hilo palikuwa na ishara: “Arbeit Macht Frei” (Kazi Huweka Huru). Ni walinzi wa SS peke yao waliokuwa na idhini maalumu za kuingia eneo hili.
Kila siku katika kambi, tuliwaona wafungwa walipokuwa wakipigishwa miguu kwenda kwenye migawo yao ya kazi wakiongozwa na mlinzi wa SS na mfungwa mwingine mwenye daraka aliyeitwa Kapo. Kulikuwako Wayahudi wenye ishara ya nyota ya Daudi juu ya jaketi zao za gerezani, wafungwa wa kisiasa wakiwa na pembetatu yao nyekundu, wahalifu wakiwa na doa lao jeusi, na Mashahidi wa Yehova wakiwa na pembetatu yao ya zambarau.
Singeweza kuepuka kuziona nyuso za Mashahidi zilizong’aa isivyo kawaida. Nilijua walikuwa wakiishi katika hali za upotovu mwingi; na bado walijitokeza kwa fahari iliyokataana na sura yao ya kukonda kimbaombao. Kwa kuwa nilijua machache sana juu yao, niliwauliza maofisa wetu wakuu kwa nini Mashahidi walikuwa wamepelekwa kwenye kambi za mateso. Jibu lilikuwa kwamba wao walikuwa dhehebu la Uyahudi-Umarekani lililohusiana na Wakomunisti. Lakini nilistaajabishwa sana na mwenendo wao usio na dosari, kanuni zao zisizoridhiana, na usafi wao wa kiadili.
Mwisho wa “Mesiya” Wangu
Katika 1945 ulimwengu niliokuwa nimeamini ulianguka. “Mungu” wangu, Adolf Hitler, aliyetukuzwa na makasisi kuwa führer aliyetumwa na Mungu, alithibitika kuwa mesiya bandia. Tausendjährige Reich (Utawala wa Miaka Elfu) wake ulionuiwa ulikuwa magofu kabisa baada ya miaka 12 tu. Yeye alikuwa mwoga pia aliyehepa lawama yake kwa kuchinja mamilioni ya wanaume, wanawake, na watoto kwa kujiua. Habari zilizofuata za mlipuko wa makombora ya kwanza ya atomi juu ya Japani zilisababisha nipatwe na mvunjiko wa neva za akili.
Mabadiliko ya Kutazamisha Katika Maisha Yangu
Muda mfupi baada ya yale matendo ya uhasama ya Vita ya Ulimwengu 2, nilishutumiwa kwa Jeshi la Marekani la CIC (Askari Wakabiliana na Majasusi), sehemu ya majeshi ya Marekani yenye kudhibiti maeneo. Nilikamatwa nikiwa Mnazi na mshirika wa Waffen-SS. Mchumba wangu mwenye upendo, Trudy, hatimaye alipata daktari ambaye, kwa sababu ya athari nilizokuwa nikipatwa nazo kutokana na jeraha la uti wa mgongo, aliwasadikisha CIC kunifungua gerezani kwa sababu ya afya yangu. Ndipo nilipowekwa chini ya ufungio wa nyumbani mpaka nilipoondolewa mashtaka yote ya kuwa mhalifu wa vita.
Nikiwa mdhoofishwa na vita, nilipelekwa hospitali ya kupatia nafuu katika Milima Alp ya Austria kwa uchunguzi wa kitiba. Halafu asubuhi moja ya kupendeza sana wakati wa masika nilipokuwa nikifurahia mandhari ya kuvutia sana na ujoto wa jua na kusikiliza nyimbo tamu za ndege, nilitamka sala fupi kutoka kwenye kina cha moyo wangu: “Mungu, ikiwa kweli wewe upo, ni lazima uweze kujibu maswali yangu mengi yanayosumbua.”
Majuma machache baadaye, nilipokwisha kurudi nyumbani, mmoja wa Mashahidi wa Yehova alifika mlangoni pangu. Nilikubali fasihi ya Biblia kutoka kwake. Ingawa alirudi kunitembelea kwa ukawaida kila asubuhi ya Jumapili, sikufikiria kwa uzito wala kusoma fasihi aliyoacha wakati huo. Hata hivyo, siku moja nilikuja nyumbani kutoka kazini nikiwa nimeshuka moyo kuliko kawaida. Mke wangu alidokeza nisome kitu fulani kujaribu kustarehesha akili yangu—kijitabu kilichoachwa na Mashahidi chenye kichwa Peace—Can It Last? (Amani—Je, Yaweza Kudumu?)
Nilianza kusoma kijitabu hicho nikakuta kwamba singeweza kukiweka chini mpaka nilipomaliza kukisoma chote. Nilimwambia mke wangu: “Kijitabu hiki kilichapwa katika 1942. Kama mtu yeyote angalisema wakati huo kwamba Hitler na Mussolini wangeshindwa vita na kwamba Ushirika wa Mataifa ungetokea tena kwa namna ya Umoja wa Mataifa, watu wangalifikiri mtu huyo alikuwa amevurugika akili. Lakini yale sasa yaliyokuwa yamekwisha kutendeka ndiyo yale hasa kijitabu hicho kiliyasema yangetendeka. Je, tuna Biblia mahali fulani ili niweze kuyachunguza marejezo haya ya Maandiko?”
Mke wangu alienda sehemu ya chini ya kuwekea vitu nyumbani akapata tafsiri ya zamani ya Lutheri ya Biblia. Nilichunguza mistari ya Biblia iliyoorodheshwa katika kijitabu hicho. Muda si muda nikaanza kujifunza mambo niliyokuwa sijapata kuyasikia. Nilijifunza juu ya ahadi ya Biblia ya ulimwengu mpya papahapa duniani chini ya Ufalme wa Kimesiya wa Mungu. Tumaini halisi hili la wakati ujao wenye furaha na usalama laonyeshwa katika maneno ya sala ya kiolezo ya Yesu niliyoirudia mara nyingi nikiwa mvulana: “Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.” Nami nilishangaa sana kujifunza kwamba Mungu Mweza Yote, yule Muumba wa mbingu na dunia, ana jina la kibinafsi, Yehova.—Mathayo 6:9, 10; Zaburi 83:18.
Haukupita muda mrefu kabla sijaanza kuhudhuria mikutano ya Mashahidi wa Yehova. Kwenye mkutano wangu wa kwanza, nilikuta mwanamke mzee-mzee ambaye binti yake na mwana-mkwe wake walikuwa wameuawa katika kambi moja ya mateso ya Ujerumani kwa sababu ya imani yao. Nilihisi kuaibika sana. Nilimweleza baadaye kwamba kwa sababu ya mahusiano yangu ya zamani, mimi mwenyewe niliyajua sana yaliyokuwa yamepata yeye na familia yake, na kwa sababu ya ushirika wangu pamoja na wale waliohusika, yeye alikuwa na haki ya kunitemea mate usoni kwa karaha.
Nilishangaa kwamba, badala ya chuki, machozi ya shangwe yalijazana machoni mwake. Alinikumbatia kwa uchangamfu akasema: “Lo, ni vizuri kama nini kwamba Mungu Mweza Yote, Yehova, huruhusu watu mmoja-mmoja kutoka vikundi vinavyopingana kadiri hiyo waingie katika tengenezo lake takatifu!”
Badala ya ile chuki niliyokuwa nimeiona muda wa miaka mingi kotekote karibu nami, watu hawa walikuwa wakionyesha kikweli upendo wa Mungu usio na ubinafsi—upendo wa kweli wa Kikristo. Nilikumbuka kuwa nilisoma yale aliyosema Yesu: “Kwa hilo wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwenu wenyewe.” (Yohana 13:35, NW) Hili ndilo hasa nililokuwa nimekuwa nikitafuta. Sasa ilikuwa zamu yangu kutoa machozi. Mimi pia nilianza kulia kama mtoto, kwa kuthamini Mungu aliye mzuri hivyo, Yehova.
Bado Nilikuwa na Mengi ya Kujifunza
Baada ya muda niliweka maisha yangu wakfu kwa Yehova Mungu na kubatizwa katika 1948. Lakini muda si muda nikagundua kwamba nilikuwa bado na mengi ya kujifunza. Kwa kielelezo, kwa kuwa nilikuwa nimeongozwa kwa hila sana kufuata mawazo ya Unazi, singeweza kuelewa ni kwa nini tengenezo la Yehova nyakati nyingine lilichapa makala zilizo dhidi ya SS wenye sifa mbaya. Nilitoa hoja kwamba sisi watu mmoja-mmoja hatukuwa tumekuwa wenye kulaumika. Tulikuwa askari tu, na walio wengi kati yetu hatukujua kamwe yaliyokuwa yakitendeka katika kambi za mateso.
Halafu siku moja ndugu mpendwa aliyeelewa tatizo langu na ambaye yeye mwenyewe alikuwa ameteseka miaka mingi katika kambi ya mateso alinizungushia mkono kwenye bega langu na kusema: “Ndugu Ludwig, nisikilize kwa uangalifu. Ikiwa watatizika kuthamini jambo hili na waona kwamba lakusumbua, ebu liweke kando akilini mwako. Halafu mwachie Yehova tatizo lako katika sala. Hakika nakuambia ukifanya hivi, siku itakuja ambapo Yehova atafungua uelewevu wa jambo hili na fadhaiko jingine lolote ulilo nalo.” Nilifuata ushauri wake wenye hekima, na kadiri miaka ilivyopita, nilikuta kwamba ni hivyo hasa ilivyotendeka. Hatimaye nikaja kuelewa kwamba mfumo mzima wa Usoshalisti wa Kitaifa, pamoja na SS wao, ulikuwa sehemu nyingine tu ya kidiabolo ya mfumo mzima wa ulimwengu wa Shetani Ibilisi.—2 Wakorintho 4:4.
Nikarudi Konde la Zeppelin, Nuremberg
Lo, waweza kuwazia jinsi lilivyokuwa jambo kuu la maisha yangu niliporudi Nuremberg katika 1955 na huko nikahudhuria “Triumphierendes Koenigreich” (Ufalme Wenye Shangwe ya Ushindi) Kusanyiko la Mashahidi wa Yehova! Ndiyo, kusanyiko hili lilifanyiwa mahali palepale nilipokuwa nimemsikia Hitler akijisifu kwamba angewaharibu kabisa Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani. Hapa, kwa juma zima, Mashahidi wa Yehova na marafiki zaidi ya 107,000 kutoka kotekote ulimwenguni walikusanyika kwa ibada. Hakukuwa na msukumano; hakukuwa na sauti zilizopaazwa kwa hasira. Familia ya kimataifa yenye muungamano kwelikweli, ikiishi pamoja kwa kufuatia amani.
Ni vigumu kueleza hisia-moyo nilizohisi kwenye kusanyiko hilo nilipokutana na wenzangu wa zamani kutoka Waffen-SS ambao sasa walikuwa watumishi waliojiweka wakfu kwa Yehova Mungu. Lo, tuliungana upya kwa shangwe iliyoje!
Kuutazamia Wakati Ujao kwa Tumaini
Tangu wakfu na ubatizo wangu, nimekuwa na pendeleo la kuongoza mafunzo kadhaa ya Biblia nyumbani katika Austria pamoja na waliokuwa Wanazi. Baadhi yao pia sasa ni Mashahidi wa Yehova walio wakfu. Katika 1956, nilihama Austria, na sasa naishi katika Australia. Hapa nimefurahia pendeleo la kutumikia katika huduma ya wakati wote. Hata hivyo, hivi majuzi uzee na afya mbaya zauwekea utendaji wangu vizuizi.
Mojapo matumaini yangu yenye hamu nyingi ni lile la kuwakaribisha warudi kutoka kwa wafu baadhi ya wanaume na wanawake waaminifu waliokataa kuridhiana na mfumo mwovu wa Nazi wakafishwa katika kambi za mateso kwa ajili ya uaminifu-maadili wao.
Kwa muda uliopo, nimejionea ile sifa haribifu ya chuki ikigeuka kuwa upendo na tumaini, kwa njia halisi kabisa. Tumaini langu lenye nguvu sasa ni lile la kuishi milele katika dunia-paradiso katika ukamilifu wa kibinadamu, bila magonjwa na kifo—tumaini ambalo si kwa ajili yangu tu bali pia kwa ajili ya wale wajitiishao kwa unyenyekevu kwa Mfalme wa Yehova anayetawala sasa, Kristo Yesu. Kwa habari yangu naweza kuyarudia kikweli maneno ya mtume Paulo nikiwa na usadikisho: “Nalo tumaini haliongozi kwenye kukata tamaa; kwa sababu upendo wa Mungu umemwagwa ndani ya mioyo yetu kupitia roho takatifu, tuliyopewa.”—Waroma 5:5, NW.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Nikiwa katika yunifomu yangu ya SS
[Picha katika ukurasa wa 14]
“Ufalme Wenye Shangwe ya Ushindi” Kusanyiko la Mashahidi wa Yehova la 1955 lililofanywa katika Nuremberg mahali ambapo Hitler alikuwa akifanyia mikutano yake ya kila mwaka ya Nazi
[Hisani]
Picha ya U.S. National Archives
[Picha katika ukurasa wa 15]
Nikiwa na mkoba wangu, tayari kuhubiri katika Australia
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 11]
UPI/Bettmann