Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 8/22 kur. 6-12
  • Maovu ya Unazi Yafunuliwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maovu ya Unazi Yafunuliwa
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Sihi ili Kueleweka Vizuri
  • Shambulio Laanza
  • Msimamo Shadidi wa Mashahidi
  • Mashahidi Wafunua Ukatili wa Nazi
  • Maafa ya Kambi Yafunuliwa
  • Wanazi Watamaushwa na Mashahidi
  • Ushindi Dhidi ya Ukatili
  • Mashahidi wa Yehova—Wajasiri Licha ya Hatari ya Wanazi
    Amkeni!—1998
  • Washika Uaminifu-Maadili Walio Wajasiri Washinda Mnyanyaso wa Nazi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Chuki Yangu Iligeuka Kuwa Upendo
    Amkeni!—1995
  • Ushuhuda kwa Imani Yao
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 8/22 kur. 6-12

Maovu ya Unazi Yafunuliwa

KATIKA miaka ya 1920, Ujerumani ilipokuwa iking’ang’ana kupata nafuu kutokana na ushinde wayo katika Vita ya Ulimwengu 1, Mashahidi wa Yehova walikuwa na shughuli nyingi za kusambaza kiasi kikubwa sana cha fasihi za Biblia. Hizo hazikutoa tu faraja na tumaini kwa Wajerumani bali ziliwaweka chonjo kuhusu ule ukweaji wa mamlaka ya kijeshi. Kati ya 1919 na 1933, Mashahidi walitawanya wastani wa vitabu, vijitabu, au magazeti manane kwa kila familia zipatazo milioni 15 katika Ujerumani.

Magazeti ya The Golden Age na Consolation mara nyingi yalivuta uangalifu kwa ukuzi wa kijeshi katika Ujerumani. Katika 1929, zaidi ya miaka mitatu kabla ya Hitler kukwea mamlakani, toleo la Kijerumani la The Golden Age kwa ujasiri lilitaarifu hivi: “Usoshalisti wa Kitaifa ni . . . harakati ambayo inatenda . . . moja kwa moja kutumikia adui wa mwanadamu, Ibilisi.”

Kipindi cha kabla ya Hitler kutwaa mamlaka, The Golden Age la Januari 4, 1933, lilisema: “Kunazuka utokeaji wenye kutisha wa harakati ya Usoshalisti wa Kitaifa. Inastaajabisha kwamba chama cha kisiasa chenye mianzo midogo, chenye sera zisizopatana na zile za kawaida, chaweza kwa muda wa miaka michache, kusitawi katika viwango ambavyo vimefunika muundo wa serikali ya kitaifa. Lakini Adolf Hitler na chama chake cha usoshalisti wa kitaifa (Wanazi) wametimiza jambo hili haba mno.”

Sihi ili Kueleweka Vizuri

Hitler alikuja kuwa waziri mkuu wa Ujerumani katika Januari 30, 1933, na miezi kadhaa baadaye, katika Aprili 4, 1933, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova katika Magdeburg ilitwaliwa. Hata hivyo, hiyo amri iliondolewa katika Aprili 28, 1933, na hilo jengo lilirudishwa. Ni nini kingefuata kutukia?

Licha ya uhasama uliokuwa dhahiri wa utawala wa Hitler, Mashahidi wa Yehova walipanga mkusanyiko katika Berlin, Ujerumani, katika Juni 25, 1933. Watu wapatao 7,000 walikusanyika. Mashahidi walijulisha peupe manuio yao wazi: “Tengenezo letu si la kisiasa katika njia yoyote. Sisi husisitiza tu juu ya kufundisha Neno la Yehova Mungu kwa watu, na kufanya hivyo bila kuzuiwa.”

Hivyo Mashahidi wa Yehova walifanya jitihada ya moyo mweupe kutaja mambo yaliyowahusu. Matokeo yalikuwa nini?

Shambulio Laanza

Msimamo thabiti wa kutokuwamo wa Mashahidi, pamoja na uaminifu-mshikamanifu kwa Ufalme wa Mungu, ulikuwa usiokubalika kwa serikali ya Hitler. Wanazi hawakuwa tayari kuvumilia ukataaji wowote wa kuunga mkono mawazo yao.

Mara baada ya mkusanyiko wa Berlin kumalizika, Wanazi walitwaa tena ofisi ya tawi katika Magdeburg Juni 28, 1933. Wao walivunja mikutano ya Mashahidi na kuwafunga. Mara Mashahidi walianza kufukuzwa kutoka kazini mwao. Nyumba zao zilivamiwa, wakapigwa, na kufungwa. Kufikia mapema 1934 Wanazi walikuwa wametwaa kutoka kwa Mashahidi tani 65 za fasihi za Biblia na kuzichoma nje ya Magdeburg.

Msimamo Shadidi wa Mashahidi

Licha ya mashambulio haya ya mwanzoni, Mashahidi wa Yehova walisimama imara na hadharani walitangaza udhalimu na ukosefu wa haki. Toleo la Novemba 1, 1933, la Mnara wa Mlinzi lilitokeza makala “Msiwahofu.” Ilitayarishwa hasa kwa ajili ya Mashahidi Wajerumani, ikiwahimiza wajipe moyo wakabilipo msongo wenye kuongezeka.

Katika Februari 9, 1934, J. F. Rutherford, msimamizi wa Watch Tower Society, alipeleka barua ya kumpinga Hitler iliyotaarifu hivi: “Huenda ukinze kwa kufanikiwa mwanadamu yeyote au wote, lakini huwezi kumkinza Yehova Mungu kwa kufanikiwa. . . . Kwa jina la Yehova Mungu na Mfalme mtiwa-mafuta Wake, Kristo Yesu, nakusisitiza kwamba utoe agizo kwa maofisa wote na watumishi wa serikali kwamba mashahidi wa Yehova katika Ujerumani waruhusiwe kukusanyika kwa amani na bila kizuizi kumwabudu Mungu.”

Rutherford aliweka Machi 24, 1934, kuwa siku yake ya mwisho kufanya hivyo. Alisema kwamba ikiwa kufikia wakati huo kitulizo hakitakuwa kimewajia Mashahidi Wajerumani, mambo ya hakika kuhusu unyanyasaji yangetangazwa kotekote Ujerumani na ulimwenguni pote. Wanazi waliitikia takwa la Rutherford kwa kuzidisha kuwatenda vibaya, na kuwapeleka Mashahidi wa Yehova wengi kwenye kambi za mateso zilizokuwa zimetengenezwa hivi majuzi. Hivyo, wao walikuwa miongoni mwa wafungwa wa kwanza wa kambi hizi.

Mashahidi Wafunua Ukatili wa Nazi

Kama vile Mashahidi wa Yehova waliahidi, walianza kufunua ukatili uliokuwa ukitukia katika Ujerumani. Mashahidi tufeni pote tena na tena walipeleka barua za kupinga serikali ya Hitler.

Katika Oktoba 7, 1934, makutaniko yote ya Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani yalikusanyika kusikia barua ikisomwa ambayo ilikuwa ikipelekewa maofisa wa serikali ya Hitler. Hiyo ilisema: “Kuna mgongano wa moja kwa moja kati ya sheria yako na sheria ya Mungu . . . Hivyo basi hii ni kukuambia kwamba kwa vyovyote viwavyo tutatii amri za Mungu, tutakutana pamoja kwa ajili ya funzo la Neno Lake, nasi tutamwabudu na kumtumikia Yeye kama Alivyoamrisha.”

Siku hiyohiyo, Mashahidi wa Yehova katika nchi nyingine 49 walikutana katika kusanyiko la pekee na kupeleka barua-simu ifuatayo kwa Hitler: “Matendo yako mabaya kwa mashahidi wa Yehova yawashtua watu wote wema duniani na hayaheshimu jina la Mungu. Jiepushe na kunyanyasa mashahidi wa Yehova zaidi; la sivyo Mungu atakuharibu wewe na chama chako cha kitaifa.”

Yaelekea Wanazi waliitikia mara hiyo kwa kuzidisha mnyanyaso wao. Hitler mwenyewe alipaaza sauti hivi: “Vinyangarika hivi vitakomeshwa kabisa katika Ujerumani!” Lakini kadiri upinzani ulivyozidi, ndivyo azimio la Mashahidi lilivyozidi kuimarika.

Katika 1935, The Golden Age lilifunua mbinu za kunyanyasa zifananazo na zile za Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi za utawala wa Nazi na mfumo wao wa ujasusi. Pia lilifunua kwamba ilikuwa nia ya chama cha Vijana wa Hitler kung’oa itikadi ya vijana Wajerumani katika Mungu. Mwaka uliofuata kampeni ya taifa zima ya polisi wa Gestapo ilitokeza kushikwa kwa maelfu ya Mashahidi. Muda mfupi baadaye, Desemba 12, 1936, Mashahidi waliitikia kwa kampeni yao wenyewe, wakitawanywa katika sehemu zote za Ujerumani makumi ya maelfu ya nakala za azimio lipingalo kunyanyaswa kwa Mashahidi wa Yehova.

Katika Juni 20, 1937, Mashahidi ambao walikuwa bado huru walitawanya ujumbe mwingine ambao ulisema kila kitu kuhusu ule mnyanyaso. Ulitaja maofisa na kutaja siku na mahali pa minyanyaso. Polisi wa Gestapo walipigwa na butwaa kwa ufunuaji huu na uwezo wa Mashahidi kuweza kuwafunua kwa mafanikio.

Upendo wa jirani ndio ambao uliwasukuma Mashahidi kuwaonya watu wa Ujerumani wasipumbazwe na matazamio ya ajabu ya utawala wa miaka elfu wenye utukufu wa Utawala wa Nazi. “Ni lazima tuseme ukweli na kutoa onyo,” kikasema kijitabu Face the Facts, kilichotangazwa katika 1938. “Sisi hung’amua serikali za kimabavu . . . kuwa mfanyizo wa Shetani ulioletwa kama kibadala cha ufalme wa Mungu.” Mashahidi wa Yehova walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutendwa vibaya na Nazi, lakini walitangaza kwa sauti kubwa ukatili uliotendwa dhidi ya Wayahudi, Wapolandi, walemavu, na wengine.

Lile azimio “Onyo!,” lililokubaliwa katika 1938 kwenye mkusanyiko wa Mashahidi wa Yehova katika Seattle, Washington, Marekani, lilisema hivi: “Wafashisti na Wanazi, vyama vya kisiasa vyenye mlengo wa kushoto, kwa makosa vimetwaa udhibiti wa nchi nyingi za Ulaya . . . Watu wote watadhibitiwa, uhuru wao wote utatwaliwa, na wote watashurutishwa kukubali utawala wa kikatili wa dikteta na ndipo Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi ya kale yatakuwa yamehuishwa kikamili.”

Rutherford alitangaza kwa ukawaida kwenye redio, akitoa mihadhara yenye nguvu kuhusu jinsi Unazi ulivyo wa kishetani. Hiyo mihadhara ilitangazwa tena tufeni pote na ilichapishwa na kutawanywa kwa mamilioni. Katika Oktoba 2, 1938, alitoa hotuba “Ufashisti au Uhuru,” ambayo alimshutumu Hitler kwa kutumia mitajo hususa.

“Katika Ujerumani watu wa kawaida ni wapenda-amani,” Rutherford akapiga mbiu. “Ibilisi amemweka mwakilishi wake Hitler katika mamlaka, mwanamume ambaye hana akili timamu, mkorofi, mkatili na mkaidi . . . Yeye kwa ukatili huwanyanyasa Wayahudi kwa sababu wakati mmoja walikuwa watu wa agano wa Yehova na walilichukua jina la Yehova, na kwa sababu Kristo Yesu alikuwa Myahudi.”

Kadiri hasira ya Nazi dhidi ya Mashahidi wa Yehova ilipofikia vipeo vipya, shutumu za peupe za Mashahidi zilikuwa zenye kuchoma hata zaidi. Toleo la Mei 15, 1940, la Consolation lilitaarifu hivi: “Hitler ni mtoto kamili sana wa Ibilisi hivi kwamba mihadhara na maamuzi yake yatiririka kumtoka kama mtaro wa maji machafu uliojengwa vizuri.”

Maafa ya Kambi Yafunuliwa

Ingawa umma ulikuwa hauna habari kuhusu kuwapo kwa kambi za mateso hadi kufikia 1945, mafafanuzi ya kina kuzihusu yalitokea mara nyingi katika vichapo vya Watch Tower katika miaka ya 1930. Kwa kielelezo, katika 1937, Consolation lilisimulia majaribio ya kutumia gesi yenye sumu katika Dachau. Kufikia 1940, vichapo vya Mashahidi vilikuwa vimetaja majina ya kambi 20 mbalimbali na viliripoti hali zazo zenye kutisha sana.

Kwa nini Mashahidi wa Yehova walizifahamu kambi za mateso vizuri hivyo? Vita ya Ulimwengu 2 ilipoanza katika 1939, tayari kulikuwa na Mashahidi 6,000 waliozuiliwa katika kambi na jela mbalimbali. Mwanahistoria Mjerumani Detlef Garbe akadiria kwamba Mashahidi kwa wakati huo walifanyiza kati ya asilimia 5 na 10 ya jumla ya idadi ya watu kambini!

Kwenye semina moja kuhusu Mashahidi na lile Teketezo la Umati, Garbe alitaarifu hivi: “Kati ya watu 25,000 waliokubali kuwa Mashahidi wa Yehova mwanzoni mwa Utawala wa Nazi, wapatao 10,000 walifungwa kwa vifungo vya vipindi tofauti-tofauti. Kati ya hawa, zaidi ya 2,000 waliwekwa kwenye kambi za mateso. Hili lamaanisha kwamba mbali na Wayahudi, Mashahidi wa Yehova walikuwa kikundi kilichonyanyaswa zaidi na polisi wa SS kati ya vikundi vyote vya kidini.”

Katika Juni 1940, Consolation lilisema hivi: “Kulikuwa na Wayahudi 3,500,000 katika Poland wakati Ujerumani ilipoanza Uvamizi Wayo wa Haraka . . . , na ikiwa ripoti zifikazo ulimwengu wa Magharibi ni sahihi uharibifu wao waonekana umeendelea sana.” Katika 1943, Consolation lilitaja hivi: “Mataifa mazima kama vile Wagiriki, Wapoland na Waserbia waendelea kuangamizwa kwa mfululizo.” Kufikia 1946, The Golden Age na Consolation yalikuwa yametambulisha jela na kambi za mateso 60 tofauti-tofauti.

Wanazi Watamaushwa na Mashahidi

Ingawa Wanazi walijaribu kukomesha mwenezo wa fasihi za Watch Tower, ofisa mmoja wa Berlin alikiri hivi: “Ni vigumu kupata mahali pa siri katika Ujerumani ambapo fasihi za Wanafunzi wa Biblia zinachapishiwa; hakuna anayebeba majina au anwani na hawasalitiani.”

Licha ya jitihada zao zenye kujisulubu, polisi wa Gestapo hawakupata kamwe kushika zaidi ya nusu ya idadi ya Mashahidi katika Ujerumani kwa wakati wowote ule. Ebu wazia ule mtamauko wa mfumo wa ujasusi wa Nazi wenye matengenezo mengi—haungeweza kukusanya na kunyamazisha jeshi hili dogo au kukomesha uenezi wa fasihi. Fasihi zilipenya hadi mitaani na hata kupenya vizingo vya seng’enge vya kambi za mateso!

Ushindi Dhidi ya Ukatili

Wanazi, waliofikiriwa kuwa wastadi wa kuvunja hiari ya kutenda ya binadamu, walijaribu bila kufaulu kuwafanya Mashahidi wa Yehova wakiuke kutokuwamo kwao kwa Kikristo, lakini ng’o waliambulia patupu. Kile kitabu The Theory and Practice of Hell kilisema hivi: “Ni lazima mmoja akubali kwamba, kusema kisaikolojia, polisi wa SS hawakuweza kamwe kukabili ushindani uliotolewa na Mashahidi wa Yehova.”

Kwa kweli, Mashahidi, wakitegemezwa na roho ya Mungu, walishinda hilo pambano. Mwanahistoria Christine King, mkuu wa Chuo Kikuu cha Staffordshire katika Uingereza, alifafanua wakabiliani kwenye pambano hivi: “Kwa upande mmoja [Wanazi] wakiwa wengi mno, wenye uwezo, waonekanao kutoshindika. Upande ule mwingine [Mashahidi] wachache mno . . . wakiwa na imani yao tu, hakuna silaha nyingine . . . Mashahidi wa Yehova walishinda kabisa kimaadili ule uwezo wa nguvu hizo za polisi wa Gestapo.”

Mashahidi wa Yehova walikuwa wachache, wenye amani wakiwa wamezungukwa katika milki ya Nazi. Hata hivyo, walipambana na kushinda pambano kwa njia yao wenyewe—pambano la haki ya kuabudu Mungu wao, pambano la kupenda jirani zao, na pambano la kusema kweli.

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

Mashahidi Walifunua Kuwako kwa Kambi

INGAWA Auschwitz, Buchenwald, Dachau, na Sachsenhausen yalikuwa majina ambayo hayakujulikana kwa watu walio wengi hadi baada ya Vita ya Ulimwengu 2, yalijulikana vizuri sana na wasomaji wa The Golden Age na Consolation. Ripoti za Mashahidi wa Yehova, zilizopitishwa kisiri kwa kujasiria mno kutoka hizo kambi na kutangazwa katika fasihi za Watch Tower, zilifunua nia ya kuua kimakusudi ya Utawala wa Nazi.

Katika 1933, The Golden Age lilitangaza ya kwanza ya ripoti nyingi za kuwako kwa kambi za mateso katika Ujerumani. Katika 1938, Mashahidi wa Yehova walitangaza kitabu Crusade Against Christianity, katika Kifaransa, Kijerumani, na Kipoland. Kiliandika kwa umakini mashambulizi ya kinyama ya Nazi kwa Mashahidi na kilitia ndani michoro ya kambi za mateso za Sachsenhausen na Esterwegen.

Mshindi wa tuzo la Nobel Dakt. Thomas Mann aliandika hivi: “Nimekisoma kitabu chenu na masimulizi yacho yenye kuogofya kwa hisia-moyo za kina zaidi. Siwezi kufafanua hisia zilizochangamana za karaha na kunyarafisha ambazo zimejaza moyo wangu nilipokuwa nikipitia kurasa za rekodi ya kushuka adili kwa binadamu na ukatili wenye kukirihisha. . . . Kubaki kimya kungekuwa tu kutojali kuhusu kushuka adili kwa ulimwengu . . . Mmefanya kazi yenu katika kutangaza kitabu hiki na kuleta mambo haya ya uhakika kwenye ufahamu wa umma.”—Italiki ni zetu.

[Sanduku katika ukurasa wa 10]

Mashahidi Miongoni mwa Wahamishwa wa Kwanza Kambini

MADAME Geneviève de Gaulle, mpwa wa kike wa aliyekuwa rais wa Ufaransa Charles de Gaulle, alikuwa mshiriki wa French Resistance. Alipotekwa na baadaye kufungwa katika kambi ya mateso ya Ravensbrück katika 1944, alikutana na Mashahidi wa Yehova. Baada ya Vita ya Ulimwengu 2, Madame de Gaulle alitoa mihadhara kotekote katika Uswisi naye alisema mara nyingi kuhusu uaminifu-maadili na ujasiri wa Mashahidi. Katika mahojiano katika Mei 20, 1994, alisema hivi kuwahusu:

“Wao walikuwa miongoni mwa wahamishwa wa kwanza kambini. Wengi tayari walikuwa wamekufa . . . Tuliwatambua kwa beji yao yenye kutofautisha. . . . Walikatazwa kabisa kuzungumza kuhusu itikadi zao ama kuwa na kitabu chochote cha kidini, hasa Biblia, ambayo ilionekana kuwa kitabu kilicho kikuu zaidi cha uasi. . . . Najua kuhusu [mmoja wa Mashahidi wa Yehova], na kulikuwa na wengine nilioelezwa kuwahusu, aliyefishwa kwa kupatikana na kurasa chache za maandiko ya Biblia. . . .

“Kile kilichonipendeza sana kuwahusu ni kwamba wangeliweza kuondoka wakati wowote kwa kutia sahihi ukanaji wa imani yao. Hatimaye, wanawake hawa, walioonekana kuwa dhaifu sana na waliochoka, walikuwa wenye nguvu kuliko SS, ambao walikuwa na uwezo na chochote chenye mafaa mikononi mwao. [Mashahidi wa Yehova] walikuwa na nguvu zao, na lilikuwa azimio lao lenye nguvu kwamba hakuna yeyote angeweza kuwashinda.”

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

Mwenendo wa Mashahidi Katika Kambi za Mateso

KUTOKANA na upendo wa jirani—wenzi wa seli, wenzi katika makao ya kijeshi, wenzi kambini—Mashahidi walishiriki si tu chakula chao cha kiroho bali pia chakula chochote cha kimwili walichokuwa nacho.

Myahudi fulani aliyeokoka kambi ya mateso ya Buchenwald alieleza hivi: “Huko nilikutana na Bibelforscher. Wao daima walitoa ushahidi wa itikadi zao. Kwa kweli, hakuna chochote kingewakomesha kusema kuhusu Mungu wao. Walikuwa wenye msaada sana kwa wafungwa wengine. Pogrom ilipopeleka Wayahudi wengi kwenye kambi katika Novemba 10, 1938, ‘Jehovah’s schwein’ (nguruwe wa Yehova), kama vile walinzi walivyokuwa wakiwaita, walizunguka wakiwagawia posho lao Wayahudi waliozeeka na walioona njaa sana, wao wenyewe wakikaa bila kula kufikia siku nne.”

Vivyo hivyo, mwanamke fulani Myahudi aliyefungwa katika kambi ya Lichtenburg alisema hivi kuhusu Mashahidi: “Walikuwa watu wajasiri, waliostahimili hali zao zilizopita kiasi kwa subira. Ingawa wafungwa wasio Wayahudi walikatazwa kuongea nasi, wanawake hawa hawakushika sheria hii. Walisali kwa ajili yetu kana kwamba tulikuwa familia zao, na kutusihi tusikate tamaa.”

[Sanduku katika ukurasa wa 12]

Jitihada za Kukana Lile Teketezo la Umati Zilitabiriwa

KATIKA toleo lalo la Septemba 26, 1945, Consolation lilitaja kwamba huenda wakati ujao majaribio yakafanywa ili kurudia historia na kukana kile kilichotokea. Ile makala “Je, Unazi Umeharibiwa?” ilisema hivi:

“Waeneza-maoni hufikiri kwamba watu wana kumbukumbu fupi. Ni nia yao kuondoa historia ya wakati uliopita, wakijitokeza katika mwigizo wa kisasa kana kwamba ni wafadhili, rekodi yao yenye kujaa uhalifu ikifichwa.”

Hilo gazeti lilitoa onyo hili la kimbele: “Mpaka Yehova apige vita ya Har-magedoni, Unazi utaendelea kuibuka kama uhalisi wenye kuhuzunisha.”

[Michoro katika ukurasa wa 11]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Michoro hii ya kambi za mateso ilitokea katika vichapo vya Mashahidi katika 1937

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wafanyakazi 150 kwenye ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova katika Magdeburg katika 1931

[Picha katika ukurasa wa 8]

Vichapo vya Mashahidi wa Yehova vilifunua muungamano wa kanisa na Unazi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki