Mashahidi wa Yehova—Wajasiri Licha ya Hatari ya Wanazi
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UJERUMANI
MASHAHIDI WA YEHOVA wanajulikana sana kwa kushikilia imara Neno la Mungu, Biblia. Mara nyingi ujasiri huhitajiwa, na hili huathiri maisha zao na uhusiano wao pamoja na wengine.
Kwa kielelezo, Mashahidi huwastahi sana watu wa makabila yote na wa tamaduni zote. Wanampenda Mungu na jirani yao. (Mathayo 22:35-40) Kwa kweli, wanakubaliana kikamili na mtume Petro, aliyetangaza hivi: “Kwa hakika nahisi kwamba Mungu si mwenye ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye humhofu na kutenda uadilifu akubalika kwake.”—Matendo 10:34, 35.
Mashahidi wa Yehova pia wanajulikana ulimwenguni pote kwa sababu ya kustahi kwao sheria, utengamano, na mamlaka ya kiserikali. Hawajapata kamwe kuwa chanzo cha maasi na hawatapata kuwa hivyo kamwe. Ndivyo inavyokuwa hata wanaponyanyaswa katika nchi fulani kwa sababu ya kuchukua msimamo kama wa mitume: “Lazima sisi tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.” (Matendo 5:29; Mathayo 24:9) Wakati huohuo, Mashahidi hukubali haki za wengine za kuabudu kulingana na miongozo ya dhamiri zao.
Msimamo jasiri wa Kikristo wa Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani na nchi nyinginezo zilizotawalwa na Adolf Hitler ni jambo lililoshuhudiwa. Tukio la kutokeza katika Berlin, Ujerumani, katika mwaka wa 1933 huonyesha mfano wa ujasiri wao, upendo wao kwa Mungu na jirani, na kustahi kwao sheria, utengamano, na uhuru wa kidini.
Hawakuridhiana na Hitler
Zaidi ya miaka 50 iliyopita, utawala wa Hitler wa miaka 12 wenye kuogofya na wa ubaguzi wa jamii na uuaji ulifikia kikomo. Na bado, utawala huo wa Nazi ulisababisha madhara ambayo huhuzunisha wanadamu mpaka leo hii.
Historia hushuhudia kwamba ni vikundi vichache tu vilivyoteta kijasiri dhidi ya tisho la Nazi. Miongoni mwao mlikuwa Mashahidi wa Yehova, waliofafanuliwa kuwa “kikundi kidogo sana chenye nguvu za [adili] za daima katika taifa lililotishwa.” Msimamo wao jasiri umethibitishwa vizuri na wanahistoria wenye kustahikiwa.
Hata hivyo, wachambuzi wachache kutia ndani wengine ambao wakati mmoja walishirikiana na Mashahidi wa Yehova, wanadai kwamba Mashahidi walijaribu kuridhiana na utawala wa Hitler katika siku zake za mapema. Wanadai kwamba wawakilishi wa Watch Tower Society walijaribu bila ya mafanikio kujipendekeza kwa serikali mpya na kwamba angalau kwa muda fulani, walikubali itikadi ya Wanazi, ambayo mwishowe ilisababisha kuuawa kwa Wayahudi milioni sita.
Madai haya mazito ni uwongo mtupu. Ufuatao ni uchunguzi wa wazi wa matukio yanayozungumziwa, ambao unategemea hati zipatikanazo na mazingira ya kihistoria.
Mambo ya Nyuma
Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakitenda katika Ujerumani kwa zaidi ya miaka 100. Kufikia mwaka wa 1933, kulikuwa na Mashahidi wapatao 25,000 waliokuwa wakimwabudu Yehova Mungu na kugawanya fasihi za Biblia kotekote Ujerumani.
Ujapokuwa uhuru uliotolewa na katiba ya Ujerumani ya wakati huo, mara nyingi Mashahidi wa Yehova walikashifiwa hasa na wapinzani wao wa kidini. Mapema katika mwaka wa 1921, Mashahidi, ambao wakati huo waliitwa Ernste Bibelforscher (Wanafunzi wa Biblia Wenye Bidii), walishtakiwa kuwa walishirikiana na Wayahudi katika siasa za uchochezi. Wanafunzi wa Biblia waliitwa Wakomunisti hatari na “vinyangarika vya Kiyahudi,” ingawa uthibitisho wa madai hayo haukupata kutolewa kamwe. Baadaye mwanatheolojia wa Switzerland Karl Barth aliandika hivi: “Shtaka la kwamba Mashahidi wa Yehova wanashirikiana na Wakomunisti laweza kutokea kwa sababu tu ya kuwaelewa vibaya bila makusudi au kimakusudi.”
Gazeti moja la kanisa katika Ujerumani lilidai kwamba Mashahidi na Wayahudi walikula njama za mapinduzi. Kwa kujibu, toleo la Aprili 15, 1930 la chapa ya Kijerumani ya The Golden Age (mtangulizi wa Amkeni!) lilitaarifu hivi: “Hatuna sababu yoyote ya kuona shtaka hili lisilo la kweli kuwa tukano—kwa kuwa twasadiki kwamba angalau Myahudi ni mtu astahiliye angalau kama ilivyo na Mkristo wa kawaida; lakini twakataa uongo uliotajwa juu katika gazeti la kanisa kwa kuwa unakusudiwa kushushia hadhi kazi yetu, kana kwamba haifanywi kwa ajili ya Gospeli bali kwa ajili ya Wayahudi.”
Hivyo, profesa wa historia John Weiss aliandika hivi: “Mashahidi hawakuwa na uzalendo wa ubora wa jamii ya Kijerumani na kwa karne nyingi hawakuchukua kwa uzito kukataa kwa Wayahudi kugeuzwa. Bado Mashahidi walishikilia ile itikadi ya awali ya Kikristo yenye kuwaongoza ya kushawishi wote wanaoweza kugeuzwa kwa Kristo.”
Ni Nini Lililotukia Hitler Alipochukua Mamlaka?
Mnamo Januari 30, 1933, Adolf Hitler aliwekwa kuwa waziri mkuu mpya wa Ujerumani. Mwanzoni serikali ya Hitler ilijitahidi kusitiri asili yake ya jeuri na siasa kali. Kwa sababu hiyo, Mashahidi, pamoja na mamilioni ya Wajerumani wengine mapema mwaka wa 1933, walikiona chama cha National Socialist Party kuwa mamlaka iliyo halali ya wakati huo. Mashahidi walitumaini kwamba serikali ya chama cha Nazi ingeng’amua kwamba Wakristo hawa wenye amani, na wenye kutii sheria hawakuwa tisho la uchochezi kwa utawala huo. Hili halikumaanisha kwamba Mashahidi wa Yehova wangeridhiana kanuni za Biblia. Kama ambavyo ilikuwa katika nchi nyinginezo, Mashahidi walitaka kuiarifu serikali ya Ujerumani ukweli kuhusu dini yao isiyojihusisha na siasa.
Upesi ikaonekana kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kukandamizwa na Nazi. Mara nyingine tena Mashahidi waliitwa kuwa washiriki wa njama iliyodaiwa kuwa ilifanywa na Wakomunisti na Wayahudi. Kampeni ya mnyanyaso ikaanza.
Kwa nini jumuiya ndogo ya kidini kama hiyo ingesababisha kiruu kwa serikali hiyo mpya? Mwanahistoria Brian Dunn atambulisha sababu tatu za msingi: (1) mweneo wa kimataifa wa Mashahidi, (2) msimamo wao kwa habari ya ubaguzi wa jamii, na (3) msimamo wao wa kutokuwamo kuelekea Serikali. Kwa sababu ya maoni yao ya Kimaandiko, Mashahidi Wajerumani walikataa salamu za kumsifu Hitler, kutegemeza National Socialist Party, au baadaye kushiriki katika shughuli za kijeshi.—Kutoka 20:4, 5; Isaya 2:4; Yohana 17:16.
Matokeo yakawa kwamba Mashahidi walivumilia vitisho, mahoji, misako ya nyumbani, na dhuluma nyinginezo zilizofanywa na polisi na kikosi maalumu cha SA (jeshi la Hitler lililoitwa Sturmabteilung). Mnamo Aprili 24, 1933, maofisa walitwaa na kufunga ofisi ya Watch Tower katika Magdeburg, Ujerumani. Msako mkali ulipokosa kutokeza ushuhuda wowote, na chini ya mkazo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, polisi walirudisha mali hizo. Hata hivyo, kufikia Mei 1933, Mashahidi walikuwa wamepigwa marufuku katika majimbo kadhaa ya Ujerumani.
Mashahidi Wachukua Msimamo Wenye Ujasiri
Katika pindi hiyo ya mapema, kwa uangalifu Hitler alijionyesha kuwa mtetezi wa Ukristo. Alitangaza uwajibikaji wake kwa uhuru wa kidini, akiahidi kutendea madhehebu ya Kikristo “kwa haki.” Ili kuimarisha dhana yake, Hitler alionekana makanisani kwa uangalifu sana. Huu ulikuwa wakati ambapo watu wengi katika nchi ambazo baadaye zingepigana na Ujerumani walikuwa wakivutiwa na mafanikio ya Hitler.
Akihangaishwa na mikazo iliyokuwa ikiongezeka katika Ujerumani, Joseph F. Rutherford, aliyekuwa msimamizi wa Watch Tower Society wakati huo, pamoja na msimamizi wa ofisi ya tawi ya Ujerumani, Paul Balzereit, waliamua kuanzisha kampeni ya kuarifu Waziri Mkuu Hitler, maofisa wa serikali, na umma kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuwa tisho lolote kwa watu na Serikali ya Ujerumani. Kwa wazi Rutherford aliamini kwamba Hitler hakufahamu mashambulizi yaliyoelekezwa kwa Mashahidi wa Yehova au kwamba aliarifiwa vibaya na vibaraka wa kidini kuhusu Mashahidi.
Kwa hiyo, ofisi ya Magdeburg ilipanga mkusanyiko ili kutumia sheria inayoruhusu raia wa Ujerumani kuteta. Kwa kuarifiwa kwa muda mfupi tu, Mashahidi wa Yehova kotekote Ujerumani walialikwa Wilmersdorfer Tennishallen katika Berlin mnamo Juni 25, 1933. Karibu wajumbe 5,000 walitarajiwa. Ijapokuwa hali yenye uhasama, zaidi ya 7,000 walihudhuria kijasiri. Wajumbe walikubali azimio lenye kichwa “Tangazo la Mambo ya Hakika.” Tangazo hili liliteta dhidi ya vizuizi vilivyokuwa vimewekewa kazi ya Mashahidi. Lilitoa taarifa iliyo wazi juu ya msimamo wao na kukanusha mashtaka ya kufanya njama za uhaini kwa kushirikiana na vikundi vingine vyovyote vya kisiasa. Lilitaarifu hivi:
“Tumeshtakiwa kimakosa mbele ya wenye mamlaka wa serikali hii . . . Kwa heshima twawaomba watawala wa taifa hili na watu wafikirie kwa haki na bila kupendelea taarifa hii ya mambo ya hakika.”
“Hatubishani na watu wowote au walimu wa kidini, lakini lazima tueleze kwamba kwa kawaida wale ambao hudai kumwakilisha Mungu na Kristo Yesu ndio kwa kweli wanatunyanyasa na ndio hutusema vibaya mbele za serikali.”
Je, Ni Mkusanyiko wa Ujasiri au wa Kuridhiana?
Sasa wengine wanaamini kwamba mkusanyiko wa Berlin wa 1933 na “Tangazo la Mambo Hakika” yalikuwa majaribio ya Mashahidi mashuhuri ya kuunga mkono serikali ya Nazi na chuki yao kuelekea Wayahudi. Lakini madai yao si ya kweli. Yanategemea habari zisizo za kweli na kupotoshwa kwa mambo ya hakika.
Mathalani, wachambuzi hudai kwamba Mashahidi walirembesha Wilmersdorfer Tennishallen kwa bendera za swastika. Picha za mkusanyiko wa 1933 huonyesha waziwazi kwamba hawakuweka bendera zozote za swastika kwenye jumba hilo. Waliojionea wanathibitisha kwamba hakukuwa bendera ndani ya jumba.
Hata hivyo, yawezekana kwamba kulikuwako bendera nje ya jengo. Wanajeshi maalumu wa Nazi walikuwa wametumia jumba hilo mnamo Juni 21, Jumatano iliyotangulia mkusanyiko huo. Kisha siku moja kabla tu ya mkusanyiko, vikundi vya vijana pamoja na vikosi vya SS (Schutzstaffel, ambao hapo awali walikuwa askari walinzi wa Hitler), SA, na wengineo walisherehekea mwanzo wa kiangazi karibu na mahali hapo. Kwa hiyo Mashahidi waliowasili kwenye mkusanyiko wa Jumapili huenda walipata jengo lililopambwa kwa bendera za swastika.
Kama kungalikuwako bendera za swastika zilizopamba sehemu ya nje ya jumba, njia za kuingilia vyumbani, au hata sehemu zake za ndani, Mashahidi wangaliziacha hivyo hivyo. Hata leo, Mashahidi wa Yehova wanapokodi majumba ya umma kwa ajili ya mikutano na mikusanyiko, hawaondoi alama za taifa. Lakini hakuna uthibitisho kwamba Mashahidi wenyewe walipandisha bendera zozote au kwamba walizisalimu.
Wachambuzi wanaongezea kusema kwamba Mashahidi walifungua mkusanyiko kwa kuimba wimbo wa taifa wa Ujerumani. Kwa kweli, mkusanyiko ulianza na wimbo ulioitwa “Tumaini Tukufu la Zayoni,” ambao ulikuwa Wimbo 64 katika kitabu cha nyimbo cha Mashahidi. Maneno ya wimbo huu yalipangwa yafuate muziki uliotungwa na Joseph Haydn wa mwaka wa 1797. Wimbo 64 ulikuwa katika kitabu cha nyimbo cha Wanafunzi wa Biblia katika angalau mwaka wa 1905 hivi. Katika mwaka wa 1922 serikali ya Ujerumani ilitumia muziki wa Haydn na kutumia maneno ya Hoffmann von Fallersleben kutunga wimbo wao wa taifa. Hata hivyo, Wanafunzi wa Biblia katika Ujerumani bado waliimba Wimbo 64 mara kwa mara, kama walivyofanya Wanafunzi wa Biblia wengine katika nchi nyinginezo.
Kuimba wimbo wa Zayoni hakungeweza kamwe kuonwa kuwa jitihada ya kuwatuliza Wanazi. Chini ya mkazo kutoka kwa Wanazi waliowachukia Wayahudi, makanisa mengine yaliondoa maneno ya Kiebrania kama vile “Yuda,” “Yehova,” na “Zayoni” kwenye vitabu vyao vya nyimbo na vya sala zao za ushirika. Mashahidi wa Yehova hawakufanya hivyo. Basi, waliokuwa wakipanga mkusanyiko wakati huo kwa hakika hawakutarajia kujipatia upendeleo wa serikali kwa kuimba wimbo wa kuhimidi Zayoni. Yawezekana kwamba wajumbe fulani walisita kuimba “Tumaini Tukufu la Zayoni,” kwa kuwa melodia ya wimbo huu uliotungwa na Haydn ilifanana na ile ya wimbo wa taifa.
Taarifa ya Msimamo Wao
Serikali ikiwa katika muda wa mabadiliko na nchi ikiwa katika msukosuko, Mashahidi walitaka kutoa taarifa iliyo wazi juu ya msimamo wao kuelekea serikali mpya. Kupitia lile “Tangazo,” Mashahidi walikataa kwa dhati mashtaka ya kujihusisha kifedha au kuwa na uhusiano wa kisiasa na Wayahudi. Hivyo, tangazo hilo lilitaarifu hivi:
“Maadui wetu wanadai kwa uwongo kwamba Wayahudi wametupa msaada wa kifedha kwa ajili ya kazi yetu. Hii si kweli hata kidogo. Kufikia wakati huu hakuna pesa zozote zilizochangwa na Wayahudi kwa ajili ya kazi yetu.”
Baada ya kutaja pesa, “Tangazo” hilo liliendelea kushutumu mazoea yasiyofaa ya biashara kubwa-kubwa. Lilisema: “Ni wafanya biashara Wayahudi wa milki ya Uingereza-Amerika ambao hufanya Biashara Kubwa-Kubwa ikiwa njia ya kutumia vibaya na kuonea watu wa mataifa mengi.”
Kwa wazi taarifa hii haikurejezea Wayahudi kwa ujumla, na twasikitika ikiwa ilieleweka vibaya na kuudhi. Wengine wamedai kwamba Mashahidi wa Yehova waliwachukia Wayahudi kama ambavyo ilikuwa ikifundishwa kwa ukawaida katika makanisa ya Ujerumani wakati huo. Jambo hili si kweli hata kidogo. Kupitia vichapo vyao na mwenendo wao wakati wa enzi ya Nazi, Mashahidi walipinga chuki dhidi ya Wayahudi na kuwashutumu Wanazi kwa kuwatenda vibaya Wayahudi. Bila shaka, fadhili zao kuelekea Wayahudi waliokuwa nao katika kambi za mateso hukanusha kabisa shtaka hili la uwongo.
“Tangazo” hilo lilifafanua waziwazi kazi ya Mashahidi kuwa ya asili ya kidini, likitaarifu hivi: “Tengenezo letu si la kisiasa kwa vyovyote vile. Sisi huendelea tu kuwafundisha watu Neno la Yehova Mungu.”
Pia “Tangazo” hilo liliikumbusha serikali juu ya ahadi zake. Mashahidi walitegemeza kanuni fulani zilizo bora ambazo zilitetewa hadharani pia na serikali ya Ujerumani. Miongoni mwa hizo mlikuwamo maadili ya familia na uhuru wa kidini.
Kwa habari hii, “Tangazo” hilo liliongezea hivi: “Uchunguzi makini wa vitabu vyetu na fasihi zetu utafunua uhakika wa kwamba kanuni hizohizo zilizo bora zinazoshikiliwa na kutangazwa na serikali ya sasa ya taifa zimeandikwa na kuungwa mkono na kukaziwa sana katika vichapo vyetu, na kuonyesha kwamba Yehova Mungu atahakikisha kwamba watu wote wapendao uadilifu watapata kanuni hizi bora kwa wakati unaofaa.”
Hivyo, Mashahidi kamwe hawakukiunga mkono Chama cha Nazi. Isitoshe, kwa kutumia uhuru wa kidini hawakunuia kuacha kuhubiri kwao peupe.—Mathayo 24:14; 28:19, 20.
Kulingana na masimulizi katika 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses, Mashahidi fulani Wajerumani walitamauka kwamba “Tangazo” hilo halikutolewa kwa njia iliyo wazi kabisa. Je, msimamizi wa ofisi ya tawi, Paul Balzereit, alipunguza uzito wa tangazo hilo? Sivyo, kwa kuwa ulinganisho wa maandishi ya Kijerumani na Kiingereza, huonyesha kwamba haikuwa hivyo. Kwa msingi wa uthibitisho uliopo, wazo lililo tofauti lilitegemea maoni ya wengine ambao hawakuhusika moja kwa moja katika utayarishaji wa “Tangazo” hilo. Huenda mikataa yao ilichangiwa pia na uhakika wa kwamba Balzereit alikana imani miaka miwili tu baadaye.
Sasa inajulikana kwamba kupigwa marufuku kwa Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani kulifanywa siku ya Jumamosi, Juni 24, 1933, siku moja tu kabla ya mkusanyiko wa Berlin. Wenye kupanga mkusanyiko pamoja na polisi walipata habari juu ya marufuku hii siku chache baadaye. Kwa sababu ya uvutano uliokuwako na uhasama wa wazi wa maofisa wa Nazi, ni ajabu kwamba mkusanyiko huo uliweza kufanyika. Si kutilia chumvi kusema kwamba Mashahidi 7,000 walihatarisha uhuru wao kwa kuhudhuria mkusanyiko huo.
Baada ya mkusanyiko huo, Mashahidi waligawanya nakala milioni 2.1 za “Tangazo” hilo. Mashahidi fulani walikamatwa mara moja na kupelekwa kwenye kambi za kazi ngumu. Hivyo, serikali ya Nazi ilifunua kikamili asili yake ya uonevu na jeuri na upesi ikaanza kukishambulia vikali kikundi hiki kidogo cha Wakristo.
Profesa Christine King aliandika hivi: “Wanazi walipata kujua kwamba unyama haungeweza kuwakomesha Mashahidi.” Ni kama lilivyotaarifu “Tangazo” hilo: “Nguvu za Yehova Mungu ni kuu kuliko zote na hakuna nguvu zinazoweza kumkinza kwa mafanikio.”a
[Maelezo ya Chini]
a Nafasi haituruhusu kuandaa habari kamili za masimulizi haya ya kihistoria. Hata hivyo, orodha ya marejezo kamili yaweza kupatikana uwaombapo wachapishaji. Waweza kulipata kuwa jambo lenye kuelimisha kutazama kaseti ya vidio ionyeshayo mambo halisi yenye kichwa Jehovah’s Witnesses Stand Firm Against Nazi Assault.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Picha halisi za mkusanyiko uliohudhuriwa na Mashahidi wa Yehova katika mwaka wa 1933 kwenye Tennishallen