Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 2/10 kur. 18-20
  • Nilikuwa Ofisa wa SS Sasa Ninamtumikia Mungu wa Kweli

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nilikuwa Ofisa wa SS Sasa Ninamtumikia Mungu wa Kweli
  • Amkeni!—2010
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vita vya Pili vya Ulimwengu na SS
  • Nakutana na Mashahidi wa Yehova
  • Ni Pendeleo Kuwa Ndugu Yao
  • Chuki Yangu Iligeuka Kuwa Upendo
    Amkeni!—1995
  • Kushika Ukamilifu-Maadili Katika Ujerumani ya Nazi
    Amkeni!—1993
  • Hatukuunga Mkono Vita ya Hitler
    Amkeni!—1994
  • Maovu ya Unazi Yafunuliwa
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2010
g 2/10 kur. 18-20

Nilikuwa Ofisa wa SS Sasa Ninamtumikia Mungu wa Kweli

Limesimuliwa na Gottlieb Bernhardt

Nilikuwa ofisa katika kikosi kikuu cha ulinzi cha Hitler nchini Ujerumani kinachoitwa SS na nilitumika kwenye ngome ya Wewelsburg. Mnamo Aprili (Mwezi wa 4) 1945, niliamrishwa kuwaua wafungwa katika kambi ya mateso iliyokuwa karibu. Wafungwa hao walikuwa Mashahidi wa Yehova. Kikosi cha SS kilidai kila ofisa atii mamlaka bila maswali. Nililazimika kuamua ikiwa ama nitatii amri ama nitafanya jambo ninalojua kuwa sawa. Acha nieleze ni kwa nini.

NILIZALIWA mnamo 1922 katika kijiji fulani karibu na Mto Rhine nchini Ujerumani. Ingawa watu katika eneo letu walikuwa Wakatoliki sugu, familia yetu ilishirikiana na harakati fulani ya kidini (Pietist) iliyoanzishwa katika karne ya 17. Mnamo 1933, nilipokuwa na umri wa miaka 11, Hitler alianza kutawala Ujerumani. Miaka michache baadaye, nilichaguliwa kwenda kwenye shule fulani karibu na Marienburg, ambayo sasa ni Malbork, nchini Poland, kwa sababu nilikuwa nimepita mitihani na nilifanya vizuri katika michezo. Nikiwa huko, mamia ya kilomita kutoka nyumbani, nilifundishwa kuhusu sera za utawala wa Nazi. Wanafunzi walifundishwa mambo kama vile, kuwa na staha, bidii, ushikamanifu, utii, kuwajibika, na kuheshimu sana urithi wetu wa Ujerumani.

Vita vya Pili vya Ulimwengu na SS

Vita vya Pili vya Ulimwengu vilipofyatuka mnamo 1939, nilijiandikisha katika kikosi kikuu cha jeshi kilichoitwa Leibstandarte SS Adolf Hitler kilichoongozwa na Hitler mwenyewe. Kikosi hicho kilitumiwa kuwalinda maofisa wa serikali, na pia kwa ajili ya shughuli za kipekee za kijeshi. Nilijionea vita nchini Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Rumania, Bulgaria, na Ugiriki. Nilipokuwa Bulgaria, nilihudhuria mkutano wa kidini ulioongozwa na kasisi wa jeshi. Nilijiuliza hivi, ‘Je, adui zetu wanafanya mkutano kama huu?’ Pia nilijiuliza: ‘Je, Mungu anabariki vita? Je, yeye huchagua upande atakaotetea?’

Baadaye, nilichaguliwa kwenda kwenye Junkerschule, shule kwa ajili ya vijana ambao watapewa vyeo vya juu katika jeshi. Baada ya hapo, nilipelekwa kwenye kikosi kilicholinda makao makuu ya Nazi huko Berlin ambako wakati mmoja nilimwona Hitler akimzomea mwanasiasa mwenye cheo cha juu mbele ya watu. Nilijiambia, ‘Hiyo ni tabia mbaya sana.’ Lakini sikuthubutu kusema maneno hayo!

Huko Berlin, nilikutana na Inge, ambaye pia alifanya kazi kwenye makao makuu. Tulipokuwa karibu kuoana, ghafula kikosi chetu kilipelekwa kwa ndege kwenye uwanja wa vita huko Urusi, bila nguo za kujikinga na baridi kali! Hali hiyo ilitushangaza sana tukiwa wanajeshi, kwa kuwa katika majira ya baridi kali ya mwaka wa 1941/1942, hali ya joto ilishuka sana na kufikia nyuzi 30 za Selsiasi chini ya sufuri. Nikiwa huko nilipewa nishani ya juu zaidi ya jeshi la Ujerumani inayoitwa Iron Cross kwa mara ya pili. Baadaye, nilipojeruhiwa vibaya sana, nilirudishwa kwa ndege nchini Ujerumani. Mimi na Inge tulioana mnamo 1943.

Mgawo wangu uliofuata ulikuwa kwenye makao makuu ya Hitler yaliyoitwa Obersalzberg, kwenye milima ya Bavaria. Mkuu wa kikosi cha SS, Heinrich Himmler, alikuwa huko pia naye alipanga nitibiwe na daktari wake wa kibinafsi, Felix Kersten. Baadaye, nilikuja kujua kwamba Kersten alikuwa na shamba lililoitwa Hartzwalde, karibu na Berlin. Vita vilipokuwa karibu kwisha, alimwomba Himmler awaruhusu Mashahidi wa Yehova waliokuwa katika kambi ya mateso iliyokuwa karibu wafanye kazi katika shamba lake. Alikubali, naye Kersten aliwatendea Mashahidi kwa heshima. Shahidi mmoja aliyemfanyia kazi nchini Sweden alitia nakala ya Mnara wa Mlinzi ndani ya mkoba wa Kersten kila wakati ili awapelekee Mashahidi nchini Ujerumani.a

Nakutana na Mashahidi wa Yehova

Mwishoni mwa 1944, Himmler aliniweka kuwa msaidizi wa jenerali wa SS aliyekuwa kamanda wa Wewelsburg Castle, ngome iliyojengwa miaka 400 iliyopita karibu na jiji la Paderborn. Himmler alikusudia kufanya Wewelsburg kuwa kituo kikuu cha kuendeleza sera za SS. Karibu na ngome hiyo kulikuwa na kambi ndogo ya mateso iliyoitwa Niederhagen, iliyokuwa na wafungwa wa pekee sana, yaani, Mashahidi wa Yehova, ambao pia waliitwa Wanafunzi wa Biblia.

Mfungwa mmoja aliyeitwa Ernst Specht alikuja mara kadhaa kutibu majeraha yangu. Alikuwa akiniambia, “Habari za asubuhi, ofisa.”

Nilimwuliza, “Kwa nini husemi ‘Heil Hitler (Mwokozi Ni Hitler)!’?”

Akaniuliza hivi kwa busara, “Wewe ulilelewa na wazazi Wakristo?”

Nikamjibu, “Ndiyo. Wazazi wangu walishirikiana na kikundi cha harakati cha Kiprotestanti.”

Akaendelea kusema, “Basi unajua kwamba Biblia inaahidi kuleta wokovu (heil) kupitia mtu mmoja tu, Yesu Kristo. Ndiyo sababu siwezi kusema ‘Heil Hitler!’”

Nikiwa nimeshangazwa na kuvutiwa, nikamwuliza, “Kwa nini wewe ni mfungwa?”

Akajibu, “Kwa sababu mimi ni Mwanafunzi wa Biblia.”

Mazungumzo niliyokuwa nayo pamoja na Ernst na Shahidi mwingine, Erich Nikolaizig, ambaye alininyoa nywele, yaligusa moyo wangu. Hata hivyo, mazungumzo hayo yalikuwa yamepigwa marufuku na hivyo ofisa msimamizi akaniamuru niache kuyaendeleza. Hata hivyo, nilihisi kwamba ikiwa kila mtu nchini Ujerumani—ambayo ni nchi inayodai kuwa ya Kikristo yenye mamilioni ya washiriki wa kanisa—angetenda kama Mashahidi walivyofanya, hakungekuwa na vita. Nilijiambia, ‘Wanapaswa kuheshimiwa, si kuteswa.’

Wakati huo, mjane fulani mwenye huzuni alipiga simu akiomba asaidiwe kumsafirisha mwana wake, ambaye alihitaji kufanyiwa upasuaji haraka aondolewe kidole cha tumbo. Niliagiza gari liletwe upesi, lakini agizo langu lilipingwa na ofisa msimamizi. Kwa nini? Mume wake alikuwa ameuawa akiwa mmoja wa kikundi kilichohusika katika jaribio la kumwua Hitler mnamo Julai 1944. Mvulana huyo alikufa, nami singeweza kufanya lolote. Jambo hilo husumbua dhamiri yangu hadi leo hii.

Ingawa sikuwa nimefikisha umri wa miaka 25, nilianza kuona maisha kihalisi—si kama yalivyoonyeshwa na propaganda ya Wanazi. Wakati huohuo, nilizidi kuwaheshimu Mashahidi wa Yehova na kuyapenda mafundisho yao. Hilo lilinichochea nifanye uamuzi mkubwa zaidi maishani.

Mnamo Aprili 1945, majeshi ya Muungano yalipokuwa yakikaribia, ofisa wangu msimamizi alikimbia kutoka Wewelsburg. Kikosi kiliwasili kikiwa na amri kutoka kwa Himmler ya kubomoa ngome hiyo na kuwaua wafungwa. Kamanda katika kambi ya mateso iliyokuwa karibu alinipa orodha ya majina ya wafungwa waliopaswa kuuawa—wote walikuwa Mashahidi. Kwa nini? Ilisemekana kwamba walijua mahali ambapo sanaa zenye thamani zilizoibwa na Serikali ya Nazi zilikuwa zimefichwa katika baadhi ya majengo hayo. Siri hiyo haikupaswa kufichuliwa! Kwa hiyo, ningefanya nini kuhusu amri ya kuwaua?

Nilimwendea kamanda wa kambi hiyo na kumwambia: “Majeshi ya Marekani yanakuja. Huoni kwamba ni jambo la hekima wewe na wenzako mwondoke?” Hakuhitaji kuambiwa tena! Kisha nikafanya jambo ambalo ofisa wa SS hawezi hata kufikiria kufanya—nilikosa kutii amri, na Mashahidi wakapona.

Ni Pendeleo Kuwa Ndugu Yao

Baada ya vita, mimi na Inge tuliwasiliana na Mashahidi wa Yehova na tukaanza kujifunza Biblia kwa bidii. Mwanamke anayeitwa Auguste pamoja na wengine walitusaidia sana. Majeraha niliyopata wakati wa vita na hali ngumu baada ya hapo zilifanya maisha yawe magumu. Hata hivyo, mimi na mke wangu tulijiweka wakfu kwa Yehova na kubatizwa—mimi nilibatizwa mnamo 1948, Inge alibatizwa mnamo 1949.

Katika miaka ya 1950, Mashahidi kadhaa waliokuwa wamefungwa huko Wewelsburg wakati wa vita walirudi huko kukutana tena. Kati yao kulikuwa na Ernst Specht, Erich Nikolaizig, na mfungwa mwingine mwaminifu, Max Hollweg. Niliona ni pendeleo kuwa ndugu yao, kwa kuwa wanaume hao wa Mungu wenye ujasiri walihatarisha maisha yao ili kunihubiria. Pia, Martha Niemann ambaye alikuwa karani huko Wewelsburg, alihudhuria mkutano huo. Yeye pia alikuwa amevutiwa sana na mwenendo wa Mashahidi na akajiweka wakfu kwa Yehova.

Ninapofikiria kuhusu miaka ambayo imepita, ninaona uthibitisho mwingi kwamba “ulimwengu mzima unakaa katika nguvu za [Shetani Ibilisi]”—jambo ambalo sikuelewa nilipokuwa kijana asiye na uzoefu na nikifuata tu mambo niliyoambiwa. (1 Yohana 5:19) Pia, ninaona wazi tofauti kubwa iliyopo kati ya kutumikia chini ya utawala wa kimabavu, kama wa Hitler, na kumtumikia Yehova. Watawala wa kimabavu wanatazamia watu wawatii bila akili, lakini Yehova anataka tumtumikie kwa sababu ya upendo unaotegemea ujuzi sahihi wa utu na makusudi yake kama yanavyofunuliwa katika Biblia. (Luka 10:27; Yohana 17:3) Naam, Yehova ndiye nitakayemtumikia muda wote wa maisha yangu.

[Maelezo ya Chini]

a Ona Mnara wa Mlinzi la Julai 1, 1972 (1/7/1972), ukurasa wa 399, la Kiingereza.

[Picha katika ukurasa wa 19]

Picha ya arusi yetu, Februari (Mwezi wa 2) 1943

[Picha katika ukurasa wa 19]

Ngome ya Wewelsburg iliyokuwa kituo cha kuendeleza sera za SS

[Picha katika ukurasa wa 20]

Nikiwa na mke wangu, Inge, leo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki