Mdiria—Ndege Aliye na Rangi Yenye Kupendeza
NDEGE aliye na rangi ya bluu nyangavu anajitumbukiza ndani ya maji na mara moja anatokea tena, akipiga mabawa yake hewani na akiwa amebeba samaki mdomoni mwake. Mara nyingi hivyo ndivyo mdiria hufahamika kwa mara ya kwanza, ndege mwenye rangi yenye kupendeza na aliye na kichwa na mdomo mkubwa. Hata hivyo, si mdiria wote wanaokula samaki. Aina nyingine ya mdiria hula mijusi, nyoka, kaa, au hata wadudu wanaowashika wanapopaa. Isitoshe, ni asilimia 33 tu ya mdiria wote duniani wanaoishi karibu na maeneo yenye maji. Ndege hawa pia hupatikana katika misitu ya kitropiki, visiwa vya matumbawe, na hata jangwani. Aina moja ya mdiria anayeishi jangwani ni yule anayeitwa red-backed, anayepatikana katika eneo kavu la Australia.
Mdiria wanaokula samaki wana ujuzi mwingi wa kuvua. Kwa kawaida ndege huyu huwatazama samaki kwa subira akiwa juu ya tawi la mti ulio karibu. Anapoona samaki, yeye hujitayarisha ili kujitumbukiza majini. Kwa kutumia silika anapima windo lake kwa sababu maji humfanya samaki huyo aonekane yuko mahali tofauti na pale alipo kihalisi. Kisha ndege huyo huruka mara moja kuelekea majini akipigapiga mabawa yake ili kuongeza mwendo. Ikiwa samaki huyo anaogelea juujuu, ndege huyo humnyakua mara moja. Ikiwa sivyo, yeye hukunja mabawa yake nyuma, na kuingia ndani ya maji kama mshale. “Yeye hufanya hivyo kwa ustadi usio wa kawaida, bila kusitasita au kukosea,” kinasema kitabu The Life of Birds. Mdiria wana uwezo wa kushika samaki zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja! Katika maeneo yenye baridi, wengine wameonekana wakiruka kupitia tabaka jembamba la barafu ili kushika windo lao. Nchini Australia, mdiria aina ya azure ameonekana akiwakamata viumbe wadogo wa majini waliotolewa mafichoni na kinyamadege anayetafuta chakula mtoni.
Kuchumbiana na Kujenga Nyumba
Mdiria huchumbiana kwa njia yenye kupendeza sana. Wengine hukimbizana hewani na baada ya hapo yule wa kiume huonyesha ujuzi wake wa kuchimba kiota. Desturi hizo pia zinaweza kutia ndani kulishana, ambapo ndege wa kiume anaonyesha uwezo wake wa kuandaa chakula kwa kumlisha yule wa kike chakula kitamu.
Kiota cha mdiria huwa tofauti na kile cha ndege wa kawaida. Wengine huchimba shimo kando ya mto, ndani ya mtaro, au ndani ya shimo lenye kokoto na kujenga chumba mwishoni mwa shimo hilo. Wengine hujenga ndani ya shimo la sungura au shimo la mti.
Ili mdiria ajenge chumba chini ya ardhi, yeye huchimba shimo lenye urefu wa mita moja hivi. Hatua ya kwanza ya kazi hii inaweza kuwa mgumu sana. Mdiria fulani huanza kufanya kazi hiyo kwa kujirusha kuelekea mchanga ulio kando ya mto, mdomo ukiwa umeelekezwa mbele. Hilo ni jambo hatari sana kwa kuwa ndege anaweza kuumia au hata kufa! Mdiria anayeitwa paradise anayepatikana katika misitu ya mvua ya kitropiki ya New Guinea na kaskazini mwa Australia, huchimba shimo katika kichuguu cha mchwa. Wadudu hao humruhusu aishi pamoja nao, kisha wanarekebisha sehemu alizoharibu baada ya ndege huyo kupata makinda na kuondoka.
Ni kazi ngumu kwa mdiria kulea makinda yake. Mtazamaji mmoja wa ndege kutoka Afrika aliona mdiria waliokuwa na makinda watano. Mbali na kujilisha wenyewe, mdiria hao waliwapelekea makinda wao watano samaki 60 au 70 kila siku. Wakati mmoja, ndege wa kiume alifaulu kulea makinda wake ingawa mke wake alikuwa amekufa siku nne kabla ya kuanguliwa kwa makinda wake. Aina nyingine ya mdiria ambao hawatagi, huwasaidia wazazi kulalia mayai na baadaye kulea makinda hao.
Kutoka Ireland Hadi Visiwa vya Solomon
Mdiria anayejulikana sana hupatikana katika sehemu nyingi kuanzia Ireland iliyo kaskazini-magharibi mpaka Ulaya na vilevile kuanzia Urusi mpaka Visiwa vya Solomon vilivyo kusini-mashariki. Kwa sababu maeneo fulani kati ya hayo huwa na barafu wakati wa majira ya baridi kali, mdiria huyo ni mojawapo ya jamii zinazohamahama, na wengine husafiri umbali wa kilomita 3,000 hivi. Mdiria huyo wa kawaida na yule anayeitwa pied na white-throated, hupatikana huko Israel kandokando ya Bahari ya Galilaya na pia kwenye Mto Yordani. Huenda Yesu aliwatazama ndege hao wenye kupendeza na utendaji wao wa kila siku.—Ona sanduku “Waangalieni kwa Makini Ndege wa Mbinguni.”
Aina nyingine ya mdiria anayejulikana sana ni mkumburu anayepatikana huko Australia. Akiwa na urefu wa sentimita 43 na mdomo wenye nguvu ulio na urefu wa sentimita 8, ndege huyu mkubwa na mwenye rangi ya kahawia anajulikana sana kuwa ndege wa shambani nchini Australia. Mkumburu anayejulikana kutokana na “kicheko” chake chenye kutisha, ni mwindaji ambaye chakula chake hutia ndani nyoka wenye urefu wa mita moja hivi!a
Ingawa mdiria ana maadui wachache, idadi yao hupungua mito inapochafuliwa au mazingira yao yanapoharibiwa. Kwa kweli, angalau aina 25 hivi za mdiria zimeorodheshwa kuwa zinakabili hatari ya kutoweka. Tunatumai kuwa jitihada za kulinda mazingira zitafaulu kulinda ndege huyu maridadi na mwenye kufurahisha.
[Maelezo ya Chini]
a Mkumburu anayeitwa blue-winged na anayepatikana kaskazini mwa Australia, huwa “hacheki.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]
“WAANGALIENI KWA MAKINI NDEGE WA MBINGUNI”
Yesu Kristo alitazama kwa makini sana uumbaji, na mara nyingi, alitumia mambo hayo katika mifano aliyokuwa amefikiria kwa makini ili kufunza maadili na kweli kutoka kwa Mungu. Kwa mfano, Yesu alisema hivi: “Waangalieni kwa makini ndege wa mbinguni, kwa sababu hawapandi mbegu au kuvuna au kukusanya ghalani; na bado Baba yenu wa mbinguni huwalisha wao. Je, ninyi si bora kuliko wao?” (Mathayo 6:26) Kwa kweli, hilo ni somo lenye kugusa moyo sana linaloonyesha vile Mungu anavyowapenda wanadamu!
[Picha katika ukurasa wa 16]