Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 2/10 kur. 14-15
  • Jua Lilipobadilika na Kuwa Jekundu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jua Lilipobadilika na Kuwa Jekundu
  • Amkeni!—2010
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kulipuka kwa Volkano ya Laki
  • Madhara Yaliyotokea Sehemu za Mbali
  • Mlipuko wa Laki na Ulimwengu wa Sasa
  • Uko Macho Kuelekea Nyakati Zetu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Kuishi Karibu na Jitu Linalolala
    Amkeni!—2007
  • Misiba—Adhabu Kutoka kwa Mungu?
    Amkeni!—1992
  • Onyo Ambalo Hawakutii
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2010
g 2/10 kur. 14-15

Jua Lilipobadilika na Kuwa Jekundu

KATIKA majira ya kiangazi ya mwaka wa 1783, kulikuwa na ukungu mkavu usio wa kawaida katika Kizio cha Kaskazini kwa miezi kadhaa. Jua lilibadilika na kuwa jekundu kama damu, mimea ilikauka, na watu wengi walikufa. Inakadiriwa kwamba makumi ya maelfu ya watu walikufa nchini Ufaransa na Uingereza pekee kutokana na ukungu huo. Watu wengi zaidi walikuwa wagonjwa kiasi cha kwamba ilikuwa vigumu kwa wakulima kupata watu wa kuvuna mazao ambayo hayakuwa yameathiriwa.

Ukungu huo ulisemwa kuwa “mojawapo ya matukio ya ajabu ya hali ya hewa na ya utendaji wa kiasili wa dunia katika miaka elfu moja iliyopita.” Hata hivyo, kufikia wakati huo, ni watu walioishi nchini Iceland peke yao waliojua ni nini kinachosababisha janga hilo—mlipuko wa volkano ambao wataalamu husema kuwa hutokea mara moja baada ya karne kadhaa. Bila shaka, Iceland ndiyo iliyoathiriwa vibaya zaidi na janga hilo, na inakadiriwa kuwa angalau asilimia 20 ya watu nchini humo walikufa.

Kulipuka kwa Volkano ya Laki

Mnamo Juni 8, 1783 (8/6/1783), wakaaji wa wilaya ya Síða kusini mwa Iceland waliona dalili hatari za ule unaoitwa sasa mlipuko wa Laki. Kwa sababu tukio hilo lilirekodiwa na watu katika nchi mbalimbali, wachunguzi walitambua njia hususa ambayo wingu kutoka kwenye volkano hiyo lilipitia kila siku. Jón Steingrímsson, mmoja kati ya watu walioshuhudia tukio hilo nchini Iceland, alisema kwamba aliona “wingu jeusi” likipanda kutoka kaskazini. Moshi mweusi ulisambaa angani, na majivu laini yakasambaa ardhini. Kisha ardhi ikaanza kutetemeka. Alisema kwamba baada ya juma moja “lava yenye moto mkali ilimiminika kutoka kwenye bonde la [Mto] Skaftá,” na kuteketeza kila kitu njiani. Steingrímsson alirekodi tukio hilo kwa miezi minane.

Mlipuko huo uliopitia kwenye ufa wenye urefu wa kilomita 25, ulitokeza lava nyingi zaidi kuliko ya mlipuko wowote wa volkano kuwahi kurekodiwa! Lava hiyo iliruka mamia ya mita hewani, huku nyingine ikimwagika umbali wa kilomita 80 kutoka mahali ilipolipukia, na kufunika sehemu yenye ukubwa wa kilomita 580 za mraba na kujaza Mto Skaftá.

Mwaka uliofuata, jivu na kemikali zenye sumu zilizokuwa juu ya nyasi za Iceland zilisababisha vifo vya zaidi ya asilimia 50 ya mifugo na asilimia 80 hivi ya farasi na kondoo. Njaa ikaenea kotekote. Inakadiriwa kuwa mlipuko huo wa Laki ulirusha tani milioni 122 za gesi ya salfa dioksidi hewani na kuifanya ichangamane na mvuke kutokeza tani milioni 200 hivi za asidi.a

Madhara Yaliyotokea Sehemu za Mbali

Upepo ulibeba ukungu huo hatari hadi sehemu za mbali. Nchini Uingereza na Ufaransa, watu walisema kuwa waliona “wingu jeusi la kipekee au ukungu wenye moshi” ambao hawakuwa wamewahi kuona maishani mwao. Harufu yenye kuchukiza na ya salfa, ilisababisha matatizo ya kupumua, kuhara damu, maumivu ya kichwa, ya macho, na ya koo, na matatizo mengine. Wingu hilo zito la salfa dioksidi na asidi ya salfa liliwadhuru watu wote wazee kwa vijana.

Ripoti moja kutoka Ujerumani ilisema kwamba katika usiku mmoja ukungu huo wenye sumu uliua majani ya miti iliyokuwa kandokando ya Mto Ems. Nchini Uingereza, mboga na majani yalinyauka na kufa kana kwamba yamechomwa na jua. Pia habari kama hizo ziliripotiwa kutoka Hungaria, Italia, Rumania, Slovakia, Skandinavia, Ufaransa, na Uholanzi. Isitoshe, ukungu huo wenye kemikali ulionekana maeneo ya mbali kama vile Ureno, Tunisia, Siria, Urusi, magharibi mwa China, na Newfoundland.

Inaonekana kwamba hali ya hewa iliathiriwa kwa sababu ukungu huo mzito ulizuia miale ya jua isifike duniani. Mnamo 1784, kiwango cha joto barani Ulaya kilipungua kwa digrii 2 Selsiasi kuliko ilivyokuwa nusu ya pili ya karne ya 18. Kiwango cha joto nchini Iceland kilishuka kwa digrii tano Selsiasi. Katika majira ya baridi kali ya mwaka wa 1783/1784, inasemekana kuwa kulikuwa na baridi isiyo ya kawaida katika eneo la Amerika ya Kaskazini hivi kwamba barafu ilionekana “ikielea juu ya Mto Mississippi . . . na kuingia katika Ghuba ya Mexico.”

Wasomi fulani wanaamini kuwa kabila la Kauwerak, ambalo ni la jamii ya Inuit inayopatikana kaskazini-magharibi mwa Alaska, lilikuwa karibu kutoweka kwa sababu ya ukame uliosababishwa na mlipuko wa Laki. Mistari iliyo kwenye mashina ya miti inaonyesha kwamba kiangazi cha mwaka wa 1783 huko Alaska kilikuwa baridi zaidi kuliko majira mengine yoyote ya kiangazi katika muda wa miaka 400. Kwa kweli, habari zinazopitishwa kwa mdomo za jamii ya Kauwerak zinataja kuhusu mwaka ambao majira ya joto yaliisha katika mwezi wa Juni, kisha yakafuatwa na baridi nyingi na njaa.

Mlipuko wa Laki na Ulimwengu wa Sasa

Ni kana kwamba janga hilo la asili la mwaka wa 1783 limesahauliwa, sababu moja ikiwa lilitokea miaka mingi iliyopita, lakini pia wengi kati ya walioathiriwa hawakufahamu kisababishi. Hata hivyo, nchini Iceland mlipuko wa Laki unakumbukwa kuwa msiba mkuu wa asili uliowahi kutokea katika historia ya nchi hiyo.

Wengine walihisi kuwa msiba huo ulikuwa adhabu kutoka kwa Mungu. Hata hivyo, Biblia haiungi mkono jambo hilo. (Yakobo 1:13) Mungu hawaadhibu watu wazuri pamoja na wabaya, kwa kuwa “njia zake zote ni haki.” (Kumbukumbu la Torati 32:4) Haki itaonyeshwa waziwazi wakati ujao Mungu atakapoingilia mambo ya wanadamu. Biblia inasema kuwa kusudi lake litakuwa kuondoa kila kitu kinachosababisha kifo na kuteseka, kutia ndani misiba ya asili.—Isaya 25:8; Ufunuo 21:3, 4.

[Maelezo ya Chini]

a Salfa dioksidi ni mojawapo ya kemikali zinazochafua hewa leo na kutokeza mvua ya asidi. Gesi hiyo hutokana na kuchomeka kwa nishati zenye kaboni kama vile makaa ya mawe, gesi, na petroli.

[Picha katika ukurasa wa 14, 15]

Picha iliyopigwa kutoka angani ikionyesha volkano ya Laki

[Picha katika ukurasa wa 14, 15]

Picha ya lava inayowaka ikirushwa hewani

[Picha katika ukurasa wa 15]

Picha ya setilaiti ya Iceland

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]

Lava fountain: © Tom Pfeiffer; aerial photo: U.S. Geological Survey; satellite photo: Jacques Descloitres, MODIS Rapid Response Team, NASA/GSFC

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki