Uko Macho Kuelekea Nyakati Zetu?
KUWA macho kuelekea hatari kwaweza kufanyiza tofauti kati ya uhai na kifo. Hili laweza kutolewa kielezi na lililotukia katika visiwa viwili vya volkano.
Mlima Pelée, volkano yenye kufisha zaidi ya karne ya 20, ulilipuka Mei 8, 1902, katika kisiwa cha Karibea cha Martinique. Mlipuko huo uliua karibu idadi ya wakazi wote 30,000 wa Saint Pierre, jiji lililo karibu na volkano.
Katika Juni 1991, Mlima Pinatubo ulilipuka labda ukiwa mlipuko mkubwa zaidi katika karne hii. Ulitokea katika eneo la Filipino lenye idadi kubwa ya watu nao ulisababisha vifo vya watu 900 hivi. Hata hivyo, wakati huu mambo mawili yalisaidia kuokoa maelfu ya watu: (1) kuwa macho kuelekea hatari hiyo na (2) utayari wa kutenda kupatana na maonyo.
Tendo Lifaalo Liliokoa Uhai
Mlima Pinatubo ulikuwa umekuwa bwete kwa maelfu ya miaka wakati katika Aprili 1991, ulianza kutoa dalili za mlipuko uliokuwa ukikaribia. Mvuke na salfa dioksidi ilianza kuvuja kwenye kilele. Wakazi wa mahali hapo walihisi mfululizo wa mitetemeko midogo ya dunia, na kuba ya lava iliyoganda ambayo iliashiria msiba, ilianza kuibuka kutoka kwenye mlima. Wanasayansi kutoka Taasisi ya Sayansi ya Volkano na Mitetemeko ya Dunia ya Filipino walikesha sana na hatimaye wakawasadikisha wakuu wa serikali kwamba lingekuwa jambo la hekima kuhamisha wakazi 35,000 kutoka majiji na vijiji vilivyo karibu na hapo.
Yaeleweka kwamba watu husita kuhama nyumba zao bila sababu, lakini kusitasita kulishindwa kwa wonyesho wa vidio ulioonyesha waziwazi hatari za mlipuko wa volkano. Watu wengi waliotoka walifanya hivyo kwa wakati ufaao. Siku mbili baada ya hapo, mlipuko mkubwa zaidi ulivurumisha majivu umbali wa kilometa mchemraba nane angani. Baadaye mitiririko ya matope iliua mamia ya watu. Hata hivyo, labda maelfu waliokoka, kwa sababu watu walikuwa wametahadharishwa kuhusu hatari hiyo nao wakatii maonyo.
Kuponyoka Maafa Makubwa Yaliyotokezwa na Binadamu
Katika karne ya kwanza ya Wakati wetu wa Kawaida, Wakristo waliokuwa wakiishi Yerusalemu pia iliwabidi kuamua kama wangeyaacha makao yao. Kukimbia kutoka katika jiji hilo mwaka wa 66 W.K. kuliwaokoa na uharibifu ambao uliwapata wakazi wale wengine na maelfu ya Wayahudi ambao walikuwa wamekuja Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka wa 70 W.K. Watu zaidi ya milioni moja walikuwa ndani ya jiji hilo lenye kuta wakiadhimisha Sikukuu ya Kupitwa wakati jeshi la Roma lilipofanya isiwezekane kabisa kupata fursa ya kutoroka. Njaa kuu, kung’ang’ania mamlaka, na mashambulizi yenye ukatili ya Waroma yalitokeza vifo vya watu zaidi ya milioni moja.
Maafa makubwa yaliyokomesha maasi ya Wayahudi dhidi ya Waroma hayakuja bila kutangazwa. Miongo kadhaa mapema, Yesu Kristo alikuwa ametabiri kwamba Yerusalemu lingezingirwa. Yeye alisema hivi: “Wakati mwonapo Yerusalemu limezingirwa na majeshi yaliyopiga kambi, ndipo jueni kwamba kufanywa ukiwa kwalo kumekaribia. Ndipo waacheni wale walio katika Yudea waanze kukimbia hadi kwenye milima, na waacheni wale walio katikati yalo waondoke, na waacheni wale walio katika sehemu za mashambani wasiingie ndani yalo.” (Luka 21:20, 21) Maagizo hayo yalikuwa wazi, na wafuasi wa Yesu waliyachukua kwa uzito.
Mwanahistoria wa karne ya nne Eusebia Kaisaria aripoti kwamba Wakristo wa Yudea yote walitenda kulingana na onyo la Yesu. Waroma walipoacha kuzingira Yerusalemu kwa mara ya kwanza katika 66 W.K., Wakristo wengi Wayahudi walienda kuishi katika jiji la Wasio Wayahudi la Pella, katika mkoa wa Roma wa Perea. Kwa kuwa macho kuelekea nyakati zao na kutenda kulingana na onyo la Yesu, waliponyoka kule ambako kumeitwa “mojawapo ya kuzingira kwenye kuogofya zaidi katika historia yote.”
Leo, uangalifu huohuo wahitajiwa. Na ndivyo ilivyo kutenda kihususa. Makala ifuatayo itaeleza sababu ya hilo.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Godo-Foto, West Stock