Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 5/22 kur. 17-21
  • Lahari—Matokeo ya Baadaye ya Mlima Pinatubo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Lahari—Matokeo ya Baadaye ya Mlima Pinatubo
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matokeo ya Baadaye Yenye Kudumu
  • Msiba Tena
  • Upendo Wasukuma Wengine Kusaidia
  • Tuliokolewa Kutoka kwa Lahari!
    Amkeni!—1996
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Uko Macho Kuelekea Nyakati Zetu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Habari za Kitheokrasi
    Huduma Yetu ya Ufalme—1991
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 5/22 kur. 17-21

Lahari—Matokeo ya Baadaye ya Mlima Pinatubo

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA FILIPINO

NYUMBA zimefurikwa. Biashara zimeharibiwa. Magari yamefagiliwa mbali. Majengo yamefunikwa. Maelfu ya watu wamelazimishwa kukimbilia mbali. Wengine wamenaswa, wasiweze kukimbia. Ni nini kilichosababisha hayo? Tetemeko la dunia? Poromoko? La. Hayo ni matukio yanayoendelea ambayo yanasababishwa na lahari (läʹhärs). Hizo ni nini? Lahari ni mitiririko ya maji na matope ya volkeno, kutia ndani majivu, mawe mepesi ya volkeno, na takataka kutokana na milipuko ya sasa na ile ya zamani.

Huenda ikawa mwongo mmoja uliopita hukuwa umepata hata kusikia juu ya Mlima Pinatubo wa Filipino. Lakini baada ya mlipuko mkubwa mnamo Juni 15, 1991, “Pinatubo” likawa neno lijulikanalo na wengi katika sehemu nyingi ulimwenguni. Baada ya kuwa zimwe kwa miaka karibu 500, Mlima Pinatubo ulilipuka na kufanyiza mawingu makubwa zaidi yenye umbo la uyoga katika karne hii. Jivu, mchanga, na mawe yalirushwa angani na volkeno hiyo na kunyesha chini kwa kiasi kisichopata kuonekana na wanadamu mara nyingi.a

Volkeno hiyo ilitupa kiasi kikubwa cha vitu kwa zaidi ya kilometa 20 kwenye angahewa la dunia. Ingawa baadhi ya vitu hivi vilirudi duniani, kiasi kikubwa cha mavumbi kilibaki mawinguni—na si mavumbi tu bali pia kiasi kikubwa cha gesi ya dioksidi ya salfuri, tani milioni 20 hivi!

Yaelekea wakumbuka matokeo yaliyoathiri tufe lote: yale machweo yenye kupendeza kwa kipindi fulani cha wakati; kupatwa kamili kwa jua kulikokuwa kwangavu isivyo kawaida katika Mexico na maeneo jirani katika 1991; badiliko katika halihewa, kutia ndani na ubaridi katika Kizio cha Kaskazini; na kuzorota kwa tabaka la ozoni la dunia. Au huenda ukawa umesikia juu ya ongezeko la njaa na maradhi yaliyowaathiri watu waliohamishwa kwa sababu ya huo mlipuko.

Matokeo ya Baadaye Yenye Kudumu

Mojawapo matokeo ya baadaye mabaya zaidi ya kulipuka kwa Pinatubo, na tokeo ambalo huenda halikutambuliwa sana na ulimwengu, ni kile kiitwacho lahari. Kama ilivyoelezwa katika fungu la kwanza la makala hii, lahari zimetokeza kuteseka kwingi sana kwa makumi ya maelfu ya watu. Kwa sababu ya lahari, matokeo ya baadaye ya mlipuko wa Mlima Pinatubo hayajaisha yote. Bado yanahisiwa kufikia sasa. Huenda hukuathiriwa binafsi, lakini ujiranini mwa Mlima Pinatubo, biashara, kazi, nyumba, uhai, na hata miji mizima iliendelea kufutiliwa mbali. Visababishi vikiwa lahari za Pinatubo.

Ingawa lahari nyingi huonekana kama mito yenye matope ikiwa na kiasi kingi cha matope ya volkeno, wakati lahari huwa na asilimia 60 ya matope ya volkeno, hizo huanza kufanana na saruji inayotiririka. Mitiririko hiyo yaweza kutokeza uharibifu mkubwa sana. Kijitabu A Technical Primer on Pinatubo Lahars chasema: “Matope hayo huwa mazito sana (zaidi ya mara mbili ya uzito wa maji) hivi kwamba miamba, mifuko yaliyojazwa mawe, magari, majengo ya mawe, na hata madaraja huinuliwa na kupelekwa mbali.”

Lahari huanzaje? Utakumbuka kuwa Mlima Pinatubo ulirusha vitu vingi sana ulipolipuka. Baadhi yavyo vilienda juu angani, lakini vingi vilibaki juu ya huo mlima na kwenye ujirani vikiwa mabaki ya mtiririko uliosababishwa na volkeno au utendaji wa kivolkeno. Kiasi gani? Kulingana na ripoti ya Taasisi ya Elimu ya Volkeno na Matetemeko ya Dunia ya Filipino, ni meta bilioni 6.65 za kyubiki. Mtaalamu wa volkeno wa Marekani C. G. Newhall asema kwamba takataka nyingi zilitupwa na Mlima Pinatubo ziwezazo “kutosha barabara pana ya kutoshea magari manne kuvuka Marekani angalau mara 10.” Meta bilioni 3.45 za kyubiki za takataka hizo, ambazo zingeweza kumomonyoka—zilikuwa zikisubiri tu mvua ije na kuzifagia hadi maeneo ya chini zaidi, huku zikifanyiza lahari. Katika Filipino, dhoruba za kitropiki na tufani zaweza kusababisha matatizo ya ziada. Mvua nyingi sana yaweza kunyesha kwa muda mfupi, huku ikitokeza lahari kubwa-kubwa.

Hilo ndilo jambo ambalo limekuwa likitendeka hasa kwa miaka kadhaa sasa. Tena na tena, dhoruba zimelowesha takataka za volkeno kwa maji, na kuzifanya zianze mwendo tena. Lahari zimegeuza ardhi yenye rutuba kuwa isiyofaa kitu na miji imefunikwa huku paa tu zikitokeza juu ya ardhi. Katika visa fulani, hayo yametendeka kwa usiku mmoja. Maelfu ya nyumba yameharibiwa, na watu wameondoshwa makwao, na kulazimishwa kuanza maisha mapya katika eneo jingine. Hadi mwanzoni mwa 1995, lahari zilikuwa zimehamisha asilimia 63 ya takataka za utendaji wa kivolkeno hadi sehemu za chini, lakini bado asilimia 37 ilibaki juu mlimani, ikingoja tu kutokeza hatari siku zijazo. Na kiasi kikubwa cha ile asilimia 63 ambayo tayari imeteremshwa chini bado ni hatari. Maji kutokana na mvua kubwa hufanyiza vijia katika takataka zilizoachwa mbeleni kwenye sehemu za juu za mito. Kisha husababisha lahari tena, ikihatarisha uhai na mali sehemu za chini zaidi za mito. Katika Julai 1995 Manila Bulletin iliripoti: “Barangays (vijiji) 91 . . . vimeharibiwa katika Luzon ya Kati, vikiwa vimezikwa chini ya tani nyingi za takataka za volkeno.”

Msiba Tena

Jumamosi jioni, Septemba 30, 1995, dhoruba kali ya kitropiki Mameng (iitwayo kimataifa Sybil) iliathiri Luzon. Kiasi kikubwa cha mvua kilinyesha katika eneo la Mlima Pinatubo. Hilo lilimaanisha msiba. Lahari zilikuwa mwendoni tena. Chochote kilichokuwa kwenye njia yazo kilimezwa. Katika eneo moja, ukuta wa kuzuia lahari uliporomoka, ukiacha maeneo ambayo awali hayakuwa yamesumbuliwa na lahari yafunikwe kwa lahari zenye kina cha kufikia meta sita. Nyumba zipunguazo orofa mbili zilifunikwa kabisa. Watu walikwea mbiombio kwenye paa ili kuokoa uhai wao. Sehemu ambapo lahari zilikuwa nzito sana, mawe makubwa, magari, na hata nyumba zilibebwa.

Furiko pia ni tokeo jingine la lahari, kwa kuwa hizo hubadili mwendo wa mito na vijito vya maji. Maelfu ya nyumba yalifunikwa kwa maji, kutia ndani nyumba nyingi za Mashahidi wa Yehova, pamoja na Majumba ya Ufalme kadhaa.

Wengine walipatwa na mambo yaliyoonwa mabaya hata zaidi. Mtu anaweza kutumbukia katika lahari iliyo mwendoni au katika matope yaliyomwagwa karibuni na lahari, hilo likifanya iwe vigumu kwake kuponyoka. Hayo matope huwa magumu vya kutosha kukanyagwa baada ya muda wa saa au siku kadhaa. Watu waliponyokaje? Wengine walikaa katika paa au kwenye miti juu ya lahari hadi kutembea kulipowezekana. Wengine walining’inia kutoka au kutembea juu ya waya za simu, kwa kuwa lahari zilikuwa zimefikia kimo hicho. Wengine walitambaa juu ya matope yaliyokuwa yamekauka kidogo yaliyoachwa na lahari. Wengine walipoteza uhai wao. Serikali ilipeleka helikopta kwenye maeneo yaliyokuwa yamekumbwa vibaya, zikiwatoa watu kutoka kwa paa za nyumba.—Kwa maelezo zaidi ona makala andamani “Tuliokolewa Kutoka kwa Lahari!”

Upendo Wasukuma Wengine Kusaidia

Mashahidi wa Yehova walifurahi kujua kuwa ingawa nyumba nyingi na baadhi ya Majumba ya Ufalme yalikuwa yamepotezwa au kuharibiwa vibaya, hakuna ndugu na dada zao wa Kikristo waliokuwa wamepoteza uhai wao. Hata hivyo, ni wazi kwamba kulikuwa na uhitaji mkubwa miongoni mwa wale waliokuwa wamekumbwa na lahari au furiko. Mashahidi kadhaa waliponyoka na mavazi waliyokuwa wamevaa tu, yaliyokuwa yamelowa matope ya lahari. Wakristo wenzao waliitikiaje uhitaji huo?

Wazee wa kutaniko kutoka eneo hilo walijitahidi kujua ikiwa ndugu zao wa Kikristo walikuwa salama au walihitaji usaidizi wa kuhamishwa. Hilo lilifanywa kwa magumu mengi, kwa kuwa matope ya lahari yangali yalikuwa teketeke katika sehemu nyingi. Guillermo Tungol, mzee katika Kutaniko la Bacolor, alisema: “Tulienda kusaidia. Tulitembea juu ya waya za simu ili kuwafikia akina ndugu.” Wilson Uy, mhudumu wa wakati wote katika kutaniko lilo hilo, aliongeza: “Karibu tushindwe kufika huko kwa kuwa tulilazimika kwenda kupitia maji yaliyofika kwenye kifua yaliyokuwa yakienda mbio.” Lakini kwa uangalifu, walifaulu na wakaweza kuchunguza hali ya washiriki wa kutaniko na kusaidia palipowezekana.

Asubuhi ya Jumatatu, Oktoba 2, ofisi ya tawi ya Watch Tower Society ilikuwa na habari kamili juu ya huo uhitaji. Je, wale wafanyakazi wajitoleaji 345 waliokuwa kwenye ofisi ya tawi wangeweza kusaidia? Ndiyo! Itikio lilikuwa la mara moja. Saa nne asubuhi, wafanyakazi hao peke yao walichanga karibu tani moja ya mavazi kwa ajili ya ndugu zao Wakristo waliokuwa wakiteseka. Hizo zilipelekwa pamoja na vyakula na fedha kadhaa kwa kutumia lori lililowasilisha vitu hivyo siku iyo hiyo.

Baada ya siku chache, makutaniko ya eneo la Metro-Manila yalijulishwa uhitaji uliokuwapo. Zaidi ya tani tano za mavazi ya ziada zilipelekwa upesi, pamoja na ugavi mwingine uliohitajiwa. Shahidi mmoja kutoka Japani alikuwa akitembelea Filipino wakati wa msiba huo. Alikuwa tu amekuja kutoka Hong Kong, ambapo alikuwa amejinunulia mavazi kadhaa. Alipojua juu ya hali mbaya ya Wakristo wenzake karibu na Mlima Pinatubo, aliwapa mavazi yote aliyokuwa amenunua na kurudi Japani bila hayo. Jinsi inavyotia moyo kuona Wakristo wa kweli wakiwaonyesha upendo walio na uhitaji—si kwa kuwatakia mema lakini kwa ‘kuwapa mahitaji ya mwili.’—Yakobo 2:16.

Uhakika wa kuwa Mashahidi wa Yehova hawakuruhusu matukio hayo yapunguze bidii yao kwa ajili ya mambo ya kiroho ni jambo linalostahili pongezi. Mikutano ya Kikristo iliendelea—katika kisa kimoja hata mahali ambapo maji yalifunika nyayo katika Jumba la Ufalme. Wakitambua umuhimu wa kuwapelekea wengine ujumbe wa Biblia, Wakristo hao waliendelea kuhubiri nyumba kwa nyumba. Wengine walilazimika kupitia ndani ya maji ili kufika walipopaswa kutoa ushahidi—katika maeneo ambayo hayakuwa yamefurika sana. Walibeba nguo na kuzibadili mahali palipokuwa pakavu zaidi. Hivyo hata ingawa Wakristo hawa walikuwa wakiteseka, hawakuruhusu hilo liwazuie wasiwahangaikie wengine.

Ndiyo, matokeo ya baadaye ya Pinatubo ni mengi zaidi ya yale waliyotarajia wengi. Ni kisa ambacho bado kitaendelea kwa miaka kadhaa. Jitihada za kudhibiti lahari zimefanywa, lakini nyakati nyingine hizo hupita uwezo wa mwanadamu. Jinsi ifurahishavyo kuona kuwa wakati hali kama hizo zitokeapo, Wakristo wa kweli huzitumia zikiwa fursa za kuonyesha upendo wao kwa Mungu na jirani!

[Maelezo ya Chini]

a Kwa habari zaidi, ona ripoti ya awali ya Amkeni! juu ya huo mlipuko, “Siku Iliponyesha Mchanga,” katika toleo la Februari 8, 1992, kurasa 15-17, la Kiingereza.

[Sanduku katika ukurasa wa21]

Jinsi Mlima Pinatubo Ulivyouathiri Ulimwengu

WAKATI mlipuko wa volkeno unaotoshana na ule wa Mlima Pinatubo udidimiapo au kwisha, huo ndio mwisho wa matokeo yao. Je, ni kweli? Sivyo hata kidogo! Ona baadhi ya matokeo yao tufeni ambayo bado yako.

◼ Huenda ukawa uliona mishuko-jua yenye kupendeza sana kwa muda fulani baada ya huo mlipuko.

◼ Wanasayansi huko Mexico walishangazwa na kule kupatwa kamili kwa jua katika Julai 11, 1991 kulikokuwa kwangavu isivyo kawaida. Sababu ilikuwa nini? Mlipuko wa Mlima Pinatubo. Mavumbi yao yalitawanya ile nuru ya korona kupita ilivyo kawaida.

◼ Halihewa pia iliathiriwa. Miezi mitatu hivi baada ya mlipuko, iliripotiwa kuwa Tokyo, Japani, lilikuwa likipokea mwangaza wa jua unaopungua kwa asilimia 10 za ule wa kawaida. Majivu ya volkeno yalizuia sehemu fulani ya mwangaza wa jua. Gazeti Science News lilionyesha upungufu wa karibu digrii 1 Selsiasi ya halijoto ya wastani katika sehemu fulani za Kizio cha Kaskazini.

◼ Tokeo jingine lilikuwa kuongezeka kwa uharibifu wa tabaka la dunia la ozoni. Asidi salfuriki ambayo ilikuwa kwenye angahewa kufuatia huo mlipuko ziliungana na klorini zilizofanyizwa na mwanadamu, zikisababisha kuisha kwa ozoni. Tabaka la ozoni kwa kawaida huandaa ulinzi wa angahewa ambao huwalinda watu wasipatwe na kansa. Punde tu baada ya mlipuko, kiwango cha ozoni katika Antaktika kilishuka chini karibu hata kufikia sufuri; katika ikweta viwango vikishuka kwa asilimia 20.

◼ Njaa na magonjwa yalikuwa matokeo mengineyo. Watu waliopoteza makao yao kwa sababu ya volkeno walilazimika kuhama kwa muda na kuishi kwenye vitovu vya kuhamia, ambapo magonjwa yalienea upesi. Walioathiriwa sana ni Waaeta, kabila la watu waliolazimishwa na huo mlipuko kutoka eneo lao na kuishi kwenye mazingira ambayo hawakuwa wameyazoea.

[Picha]

Waliohama maeneo yaliyofurikwa au kukumbwa na lahari

[Picha katika ukurasa wa 18]

Nyumba iliyobebwa na lahari

[Picha katika ukurasa wa 18]

Majengo ya orofa mbili yakiwa yamefunikwa hadi paa

[Picha katika ukurasa wa 18]

Lahari zimegeuza ardhi yenye rutuba kuwa isiyofaa kitu

[Picha katika ukurasa wa 19]

Juu: Jengo la benki katika Bacolor, Pampanga, nusu yalo ikiwa imefunikwa na lahari, Machi 1995

Chini: Benki iyo hiyo ikiwa imefunikwa kabisa na lahari ya baadaye, Septemba 1995

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki