Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 5/22 kur. 22-23
  • Tuliokolewa Kutoka kwa Lahari!

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tuliokolewa Kutoka kwa Lahari!
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Masaibu Yaanza
  • Twaokolewa—Hatimaye!
  • Lahari—Matokeo ya Baadaye ya Mlima Pinatubo
    Amkeni!—1996
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Msiba wa Chile Waongoza Kwenye Upendo wa Kikristo
    Amkeni!—1992
  • Mlima Ulipotaka Kuungana na Bahari
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 5/22 kur. 22-23

Tuliokolewa Kutoka kwa Lahari!

OKTOBA 1, 1995, ilikuwa siku tofauti na siku nyingine zozote ambazo familia ya Garcia ilipata kujionea. Akina Garcia ni Mashahidi wa Yehova watendaji, na nyumba yao ilikuwa katika mtaa fulani katika mji Cabalantian, Bacolor, katika mkoa wa Pampanga, Filipino. Ingawa nyumba yao ilikuwa karibu na maeneo yaliyokuwa yakikumbwa na lahari za Mlima Pinatubo, haikuwa imeathiriwa moja kwa moja. Cabalantian ulikuwa ukilindwa na kuta zilizojengwa ili kuzuia lahari. Lakini mambo yalikuwa karibu kubadilika haraka.

Dhoruba kali ya kitropiki ilimwaga milimeta 216 za mvua kwenye Mlima Pinatubo. Katika saa za mapema za asubuhi, simu ya nyumbani mwa Garcia ililia. Ilikuwa mtu aliyepiga nambari hiyo kimakosa, lakini mpiga simu akasema kuwa ule ukuta ulikuwa umevunjika na kwa hiyo familia ijiandae kwa ajili ya furiko.

Masaibu Yaanza

Nonato Garcia, baba wa hiyo familia na mwangalizi-msimamizi wa Kutaniko la Villa Rosemarie, aeleza: “Jumapili alfajiri kabla ya saa 11, maji yalianza kuinuka kuzunguka nyumba yetu.

“Nilidhani kuwa tungekuwa na furiko la maji tu, hivyo tukaanza kubeba mizigo yetu na kuipeleka kwenye orofa ya juu. Lakini baada ya saa nne asubuhi, nikaona kuwa matope ya lahari yalichanganyika na maji. Mtiririko uliendelea kuongezeka kwa kimo na nguvu hadi ukawa mzito na kubeba miamba. Tulipanda juu kwenye paa.

“Baadaye magari na hata nyumba zilikokotwa na huo mtiririko. Nyumba moja ambayo ilikuwa imegongwa na mwamba mkubwa ilianguka na kupelekwa. Paa ya nyumba hiyo iliachwa na lahari karibu na nyumba yetu. Kulikuwa na watu kwenye hiyo paa. Niliwaita na kuwatia moyo waje kwenye paa ya nyumba yetu. Ili kufanya hivyo, walishikilia kamba waliyotupiwa. Hiyo ilikuwa imefungiwa mwilini mwangu, nami nikawavuta mmoja baada ya mwingine. Watu wengi zaidi na zaidi walihama kutoka kwa paa zilizokuwa zikifunikwa. Wakati wote huo mvua iliendelea kunyesha.

“Alasiri helikopta zilianza kuruka juu ya eneo hilo. Lakini hakuna yoyote iliyoshuka kutuokoa, ingawa tulikuwa tukiashiria mikono kwa bidii. Tulifikiri lazima kuwe na watu wenye uhitaji zaidi nao walitaka kuwachukua hao kwanza. Sikudhani kuwa tungechukuliwa upesi, kwa kuwa kulikuwa na watu wengi waliokuwa wamekwama kwenye paa za nyumba.

“Sala ni kitu muhimu sana kwenye hali za aina hiyo. Hata uwapo katika hatari kubwa, baada ya kusali huogopi. Hatukusali kuwa Yehova afanye muujiza, lakini tuliomba mapenzi yake, tukitambua kuwa mtu yeyote aweza kuathiriwa na msiba. Lakini niliomba nipate nguvu, moyo-mkuu, na hekima. Yote hayo yalitusaidia kukabili hali iliyokuwapo.”

Mke wa Nonato, Carmen, alikubali hivi: “Asemalo mume wangu juu ya sala ni kweli kabisa. Mimi huwa na mwelekeo wa kuwa na wasiwasi nikiwa katika hali ambapo uhai wa wapendwa wangu unahatarishwa. Nilipoona kuwa paa ilikuwa ikijawa na matope ya lahari na kuwa ilikuwa ikigongwa na miamba, nilimwambia mume wangu: ‘Yaonekana hatuna tumaini.’ Lakini alinitia moyo akisema: ‘Tusali.’”

Nonato aliendelea: “Saa kumi alasiri, mtiririko wa lahari bado ulikuwa wenye nguvu sana. Nyumba ilikuwa ikigongwa na mawe makubwa. Takataka za lahari zilifunika karibu nusu ya paa. Nilianza kufikiri kuwa jioni ingefika upesi na ingekuwa vigumu kusafiri. Hivyo kulipokuwa kungali kuna mwangaza tukaamua kuanza kuhama.

“Nilijaribu kurusha kiti kwenye matope ya lahari kuona ikiwa kingezama, na hata nikasimama juu yacho lakini hakikuzama. Kwa hivyo nikachukua kipande kirefu cha mbao na kukidunga kwenye matope. Nilikitumia ili kuona mahali pagumu vya kutosha pa kutembea. Kwa njia hiyo sisi, pamoja na majirani wetu kadhaa, tuliweza kuanza kutembea kwenye hayo matope. Sote tulikuwa watu 26.

“Tulielekea paa iliyokuwa juu zaidi kule mbali. Kwa kutumia kipande cha mbao, tuliendelea kudunga-dunga matope ili kuona pa kukanyaga. Mahali ambapo bado palikuwa na umajimaji mwingi tulitambaa.”

Akitokwa na machozi, Carmen aeleza: “Sehemu nyingine tulikuwa tu ukingoni mwa mtiririko wa lahari na tulilazimika kutembea upande-upande kwenye ardhi nyembamba sana. Wakati mmoja, nilizama kufikia kifuani na kumwambia mume wangu: ‘Siwezi kuendelea. Nitakufa.’ Lakini akasema: ‘La, waweza kufaulu. Toka.’ Kwa msaada wa Yehova tuliendelea kwenda.”

Nora Mengullo, mtu wa ukoo wa familia hiyo, aongeza: “Katika sehemu zilizokuwa teketeke sana hivi kwamba hatukuweza kutambaa, tulijisukuma kwa miguu tukiwa tumelala chali. Nyakati nyingine tulizama sana, lakini tulisaidiana kuvutana, hasa watoto.”

Twaokolewa—Hatimaye!

Nonato aendelea: “Huku tukitambaa kwa shida ukingoni mwa lahari, helikopta ilikuja juu yetu na kuona hatari tuliyokabili—si tukiwa juu ya paa, bali katikati ya takataka za lahari. Mmoja wa waandamani wetu alimwinua mtoto wake wa miezi minane juu, akitumainia kuwa wenye kuokoa watu wataona hali yetu. Walishuka ili kutuchukua. Watoto na wanawake walienda kwanza kwa kuwa hatungeweza kutoshea sote.

“Hatimaye, sisi pia tulichukuliwa na kupelekwa kwenye kitovu cha uhamiaji. Watu huko hawangeweza kutupa nguo zozote za kuvaa, ingawa nguo zetu zote zilijaa matope kutoka kwa lahari. Niliwaambia kuwa familia yangu nami hatutaenda kwenye eneo la kuhamia, kwa kuwa tulitaka kwenda kwa Jumba la Ufalme. Tulipofika huko, mara moja tukavikwa, tukalishwa, na kupewa msaada mwingine. Ndugu wengine kutoka kwa hilo kutaniko wakafika, nao pia walitusaidia.”

Carmen aongeza: “Hata ingawa hatukuweza kutumainia msaada kutoka kwa vyanzo vingine, tulihisi baraka za udugu wetu wa Kikristo.”

Ingawa nyumba yao ya orofa mbili ilifunikwa kwa lahari, yaridhisha kujua kuwa wao na watoto wao watatu, Lovely, Charmy, na Charly, waliokoka hayo masaibu pamoja na Mashahidi wengine wote katika eneo hilo.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Orofa ya pili ya nyumba ya Garcia ikiwa imefukuliwa kwa sehemu

Jamaa ya Nonato Garcia ikiwa mbele ya nyumba yao iliyozikwa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki