Kutii Kuliokoa Uhai Wao
YESU KRISTO alionya kimbele kuhusu mwisho wa mfumo wa mambo wa Kiyahudi ambao kitovu chake kilikuwa hekalu la Yerusalemu. Hakutaja tarehe ambayo mwisho huo ungekuja. Lakini alieleza matukio ambayo yangetangulia uharibifu huo. Aliwahimiza wanafunzi wake wakeshe na kuondoka katika eneo la hatari.
Yesu alitabiri hivi: “Mtakapoona Yerusalemu limezingirwa na majeshi yaliyopiga kambi, ndipo jueni kwamba kufanywa ukiwa kwake kumekaribia.” Pia alisema: “Mtakapoona lile chukizo linalosababisha ukiwa . . . likiwa limesimama katika mahali patakatifu, . . . ndipo wale walio katika Yudea waanze kukimbilia milimani.” Yesu aliwasihi wanafunzi wake wasirudi kuchukua mali zao. Walipaswa kukimbia haraka ili kuokoa uhai wao.—Luka 21:20, 21; Mathayo 24:15, 16.
Ili kukomesha uasi uliokuwa ukiendelea kwa muda mrefu, Cestius Gallus, aliyaongoza majeshi ya Roma kushambulia Yerusalemu mwaka wa 66 W.K. Hata aliingia jijini na kulizingira hekalu. Ghasia zilizuka jijini. Wale waliokuwa wakikesha wangeweza kuona kwamba msiba ulikuwa karibu. Lakini, je, wangeweza kukimbia? Bila kutarajia, Cestius Gallus aliyaondoa majeshi yake. Wayahudi waasi waliwatimua mbio. Huo ulikuwa wakati wa kukimbia kutoka Yerusalemu na Yudea yote!
Mwaka uliofuata, majeshi ya Roma yalirudi yakiongozwa na Vespasian na mwanaye Titus. Nchi nzima ilikumbwa na vita. Mwanzoni mwa mwaka wa 70 W.K., Waroma walijenga ngome ya miti iliyochongoka kuzunguka Yerusalemu. Hakukuwa na njia ya kutorokea. (Luka 19:43, 44) Vikundi mbalimbali vilichinjana jijini humo. Watu waliobaki waliuawa na Waroma au kuchukuliwa mateka. Jiji hilo pamoja na hekalu lake liliharibiwa kabisa. Kulingana na Josephus, mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza, zaidi ya Wayahudi milioni moja waliteseka na kufa. Hekalu hilo halijawahi kujengwa tena.
Kama Wakristo wangekuwa bado Yerusalemu mwaka wa 70 W.K., wangeuawa au kuchukuliwa mateka kama watu wengine. Hata hivyo wanahistoria wa kale wanaripoti kwamba Wakristo walitii onyo la Mungu, wakakimbia kutoka Yerusalemu na Yudea yote hadi milima iliyo mashariki mwa Mto Yordani. Baadhi yao walikaa Pela, katika jimbo la Perea. Walikuwa wameondoka Yudea na hawakuwa wamerudi. Kutii onyo la Yesu kuliokoa uhai wao.
Je, Wewe Hutii Maonyo Kutoka Vyanzo Vyenye Kutegemeka?
Watu wengi hupuuza maonyo yote kwa sababu wamesikia maonyo mengi sana yasiyo ya kweli. Hata hivyo, kutii maonyo kwaweza kuokoa uhai wako.
Katika mwaka wa 1975, maonyo kuhusu tetemeko la nchi yalitolewa nchini China. Wenye mamlaka walichukua hatua. Watu walitii na maelfu waliokoka.
Mnamo Aprili 1991, wanakijiji walioishi kwenye miteremko ya Mlima Pinatubo, nchini Ufilipino, waliripoti kwamba mvuke na majivu yalikuwa yakifoka kutoka mlimani. Baada ya kuchunguza hali hiyo kwa miezi miwili, Taasisi ya Ufilipino ya Elimu ya Volkeno na Matetemeko ya Nchi ilionya kwamba eneo hilo lilikuwa hatarini. Makumi ya maelfu ya watu walihamishwa mara moja. Mapema mnamo Juni 15, kulitokea mlipuko mkubwa uliovurumisha majivu angani umbali wa kilometa nane na kuyasambaza katika eneo lote. Maelfu ya watu waliokoka kwa sababu walitii onyo.
Biblia inaonya kuhusu mwisho wa mfumo huu wa mambo. Tunaishi katika siku za mwisho. Je, unakesha mwisho unapokaribia? Je, unachukua hatua ya kuondoka kwenye eneo la hatari? Je, unawaonya wengine wafanye hivyo huku ukizingatia hatari inayotukabili?
[Picha katika ukurasa wa 20]
Kutii maonyo kuliokoa watu wengi wakati Mlima Pinatubo ulipofoka majivu ya volkeno
[Picha katika ukurasa wa 21]
Wakristo waliotii onyo la Yesu waliokoka uharibifu wa Yerusalemu mwaka wa 70 W.K.