Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w75 3/1 kur. 110-113
  • Mwisho wa Taratibu ya Mambo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mwisho wa Taratibu ya Mambo
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MWISHO WENYE KUOGOFISHA
  • MAMBO YENYE KUELEKEZA KWENYE MWISHO
  • USHUHUDA WA KUKARIBIA KWA MWISHO
  • ‘WATU’ FULANI WAOKOLEWA
  • “Mahali Patakatifu Paharibiwa—Maana ya Jambo Hilo Leo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
  • “Ni Nini Itakayokuwa Ishara ya Kuwapo Kwako?”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • “Mambo Haya Lazima Yatukie”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Je, Utaokolewa Mungu Atendapo?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
w75 3/1 kur. 110-113

Mwisho wa Taratibu ya Mambo

Makala hii ni ya kutumia kwa mafunzo ya kitabu ya kundi

1-3. (a) Ni mambo gani yalikuwamo ndani ya taratibu ya mambo ya Kiyahudi? (b) Ni tumaini gani la Wayahudi lililokatishwa Yerusalemu ulipoharibiwa?

SI TUKIO dogo kwa taratibu ya mambo kuharibiwa baada ya kuwapo miaka 1,582. Ndivyo ilivyo hasa ikiwa taratibu ilianzishwa na Mungu mwenyewe. Taratibu tunayoisema ni ile ya taifa la kale la Kiyahudi. Kwa sababu gani ilikwisha, na ni nini kilichouleta mwisho huo namna ulivyokuja?

2 Inajulikana sana kwamba Mungu alianzisha taratibu ya mambo chini ya agano la Torati kupitia kwa mpaji wa sheria Musa katika 1513 B.C.E. Taratibu hii ilikuwa na mambo mengi ya kutazamisha​—sabato zake mbalimbali, sheria zake za usafi wa kidini, mipango yake ya urithi, hekalu Yerusalemu pamoja na ukuhani wake na dhabihu na mambo mengine. Hivi vyote viliharibiwa kabisa mwaka wa 70 wa Wakati wetu wa Kawaida. Ilitoweka pamoja na tumaini la Kiyahudi kwamba mfalme wa ukoo wa Daudi angekalia kiti cha enzi kwa mara nyingine Yerusalemu na kuyashinda majeshi yenye uonezi ya Mataifa.

3 Sababu za kuharibiwa kwa Yerusalemu na namna ya kuharibiwa kwake zilielezwa katika maneno ya unabii na nabii mkuu zaidi wa Mungu, Yesu Kristo, siku chache tu kabla hajauawa na mamlaka ile ile ambayo baadaye iliiharibu taratibu ya mambo ya Kiyahudi. Lakini Wayahudi ndio waliomtia mikononi mwa mamlaka hiyo kwa njia isiyo ya wazi wakapaza sauti auawe.

MWISHO WENYE KUOGOFISHA

4-6. Ni wakati gani Kristo alipotoa unabii juu ya namna ambavyo Yerusalemu ungeharibiwa, naye alisema nini juu yake?

4 Unabii wa Yesu ulitolewa kwa sababu ya ulizo walilouliza mitume wake. Walikuwa wakimwonyesha Yesu fahari ya majengo ya hekalu. Alijibu hivi akiyatazama: “Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.”​—Mt. 24:1, 2.

5 Siku mbili kabla yake, Yesu alikuwa ametangulia kuonyesha kwa unabii namna ambavyo mji na hekalu lake ungeharibiwa. Aliuambia Yerusalemu hivi:

6 “Siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.”​—Luka 19:43, 44.

7. Maneno ya Yesu yaliyoandikwa katika Luka 19:43, 44 yaliwahusuje mitume wake?

7 Hili liliwavuruga hata mitume wa Kristo, waliokuwa Wayahudi waliotahiriwa. Hawakuelewa bado kwamba Kristo angetawala kutoka mbinguni, si kutoka katika kiti cha enzi cha kidunia Yerusalemu. Maneno ya Yesu yalionyesha kwamba Mungu asingeshughulika tena na Yerusalemu wa kidunia, lakini wao hawakuelewa hivyo kabisa wakati huo. (Matendo 1:6) Pia, maneno ya Yesu yalimaanisha kwamba makuhani wa nyumba ya Haruni wangeondolewa katika kazi zao. Kwa sababu gani?

8, 9. Kwa sababu gani mwisho wa taratibu za mambo za Kiyahudi ulikuwa unakaribia?

8 Sababu kwa nini mwisho wa mambo haya yote ulikuwa ukikaribia ni kwamba Yehova alikusudia kuleta mambo bora kupitia kwa Masihi wake. Dhabihu za wanyama na mambo mengine ya Torati, pamoja na unabii mbalimbali, zilikuwa zimewaelekeza Waisraeli waaminifu kwenye Yesu Kristo nazo zilitoa uhakikisho kamili na utambulisho wa kuwa kwake Masihi. Lakini dhabihu hizo hazikuwa vitu ambavyo Yehova alitaka hasa, kwa sababu zisingeweza kuondoa dhambi. (Ebr. 10:5-10) Zilipaswa zifikie mwisho. Dhabihu ya Kristo ingezifanya kuukuu.

9 Kwamba mwisho wa ukuhani wa Kiyahudi ungekuja wakati wa mwisho wa taratibu za mambo za Kiyahudi yahakikishwa zaidi katika Waebrania 9:26-28, NW inayoonyesha kwamba haikuwa lazima Yesu arudie-rudie kujitoa kama dhabihu, nayo yasema: “Kama ndivyo, ingalimpasa ateseke mara nyingi tangu kuimarishwa kwa ulimwengu. Lakini sasa amejidhihirisha mara moja tu penye mwisho wa taratibu za mambo ili kuondoa dhambi kupitia kwa dhabihu yake mwenyewe.”​—Linganisha 1 Wakorintho 10:11.

10. (a) Je! kusudi la Mungu lenyewe lilihitaji Yerusalemu upatwe na mwisho wenye kuogofisha? (b) Kwa sababu gani makuhani wa Kilawi walipaswa wapoteze kazi zao?

10 Lakini sababu gani mwisho huo wenye kuogofya sana uliupata Yerusalemu? Kusudi la Mungu kuikomesha Torati kwa Kristo halikuhitaji tendo hili la nguvu sana. (Rum. 10:4) Kwa kweli, Wakristo waaminifu hawakuufikiria kuwa wajibu wao kulibomoa hekalu wala mji wa Yerusalemu tangu Pentekoste na kuendelea (baada ya dhabihu ya Kristo kukubaliwa na Yehova mbinguni). Walilitambua hekalu kama chombo cha Mungu kilichokuwa kimetimiza kusudi lake. Hawakulidharau. Lakini walijua kwamba Yesu Kristo akiwa mbinguni alikuwa ndiye Kuhani Mkuu wao, kwa maana agano jipya lilikuwa limeanzwa, na kwa hiyo lilikuwako badiliko la ukuhani. (Ebr. 7:11-14) Hata wengi wa makuhani wa Kiyahudi walimkubali Kristo kama dhabihu ya kweli ya dhambi zao na kutambua kwamba kazi yao hekaluni ilikuwa imetimiza kusudi lake na haikuwa ikiendelea kulingana na maoni ya Yehova. (Matendo 6:7) Sababu gani basi uharibifu huo wenye jeuri uliupata mji wa Wayahudi na hekalu lao?

11, 12. Ni sababu gani alizotoa Yesu kwa mwisho wa Yerusalemu wenye jeuri?

11 Yesu alikuwa ameonyesha sababu yake alipokuwa hekaluni, alipouambia Yerusalemu hivi:

12 “Angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji; hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu. Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki. Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka! Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa. Kwa maana nawaambia, Hamtaniona kamwe tangu sasa, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la [Yehova].”​—Mt. 23:34-39.

MAMBO YENYE KUELEKEZA KWENYE MWISHO

13-16. (a) Yesu alianzaje kulijibu ulizo la mitume? (b) Maneno haya katika Mathayo 24:4-6 yalitimizwaje?

13 Bila shaka, tangazo hili la Yesu lilitokeza katika akili za mitume ulizo hili: “Mambo haya yatakuwa lini, na ni nini itakayokuwa ishara ya kuwapo kwako na ya mwisho wa taratibu ya mambo?” (Mt. 24:3, NW) Kwa kujibu, Yesu alieleza matukio ambayo yangeelekeza kwenye uharibifu wa Yerusalemu:

14 “Angalieni, mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado.”​—Mt. 24:4-6.

15 Wayahudi wangetokea, si wakijidai kuwa Yesu aliyerudi akiwa na mwili wa nyama, bali wakijionyesha kama Masihi au Kristo aliyeahidiwa. Uasi wa Kiyahudi juu ya Warumi katika 66 C.E. ulikuwa jitihada hiyo ya kimasihi. Lakini hakuna lo lote kati ya haya lililokuwa ushuhuda wa “kuwapo” au parousia ya Kristo (neno linalotumiwa katika Maandiko ya Kigiriki kwa kurudi kwake katika mamlaka ya Ufalme).

16 Pia, zingekuwako vita ambazo zingelipata taifa la Kiyahudi wakati huo. Lakini wanafunzi wa Kristo hawakupaswa waogofishwe wachukue hatua ya kabla ya wakati wake. Yesu aliendelea kusema hivi juu ya kipindi hicho:

17-19. (a) Iliwapasa wanafunzi waelewe nini walipoyaona mambo yaliyoelezwa katika Mathayo 24:7, 8? (b) Ni mambo gani ya wazi yangewapata wanafunzi wa Yesu kati ya kipindi hicho na mwisho wa Yerusalemu?

17 “Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu.”​—Mt. 24:7, 8.

18 Mambo haya yangekuwa maonyesho hakika kwa Wakristo kwamba mwisho ulikuwa unakaribia. Pia, mambo ya wazi yangewapata wanafunzi wake kwa sababu walimtangaza Masihi wa kweli na kuufuata mfano wake. Yesu aliendelea kusema hivi:

19 “Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.”​—Mt. 24:9-14.

20. Maneno ya Yesu yalitimizwaje kwa habari ya jambo ambalo lingewapata wanafunzi wake?

20 Hii ilitimizwa maana uasi wa watu wote na ukosefu wa upendo kwa Mungu uliongezeka. Ko kote ambako Wayahudi walikuwa wametapanywa, walijidai kumtumikia Mungu walipowatesa wanafunzi wa Kristo. Hata hivyo, Wakristo walizihubiri habari njema za ufalme katika dunia yote inayokaliwa na watu, zaidi katika mataifa ambako Wayahudi walikuwa wametapanywa.​—Kol. 1:6, 23.

USHUHUDA WA KUKARIBIA KWA MWISHO

21-23. Ni nini kilichopaswa kionyeshe kukaribia kwa mwisho wa taratibu ya mambo ya Kiyahudi, nalo hili lilikuwa onyo kwa wanafunzi wafanye nini?

21 Ndipo Yesu alipoonyesha wazi jambo hasa ambalo lingeonyesha kukaribia sana kwa mwisho wa taratibu ya mambo ya Kiyahudi. Alisema:

22 “Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu) ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; . . . kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.”​—Mt. 24:15-22.

23 Hili lingekuwa onyo la hakika kwa Wakristo watoke Yerusalemu na jimbo la Uyahudi wakati huo, mbio mbio, bila mizigo isiyo ya lazima, kwa njia ya moja kwa moja.

24. “Chukizo” lilikuwa nini, nalo lilisimamaje “patakatifu”?

24 “Chukizo” hili lilikuwa nini, nalo lilisimamaje “patakatifu”? Akitenda kwa sababu ya uasi wa Wayahudi katika Oktoba mwaka wa 66 C.E., jemadari wa Kirumi Galo alishuka kutoka Shamu wakati wa Sikukuu ya Vibanda ya Kiyahudi akauzingira Yerusalemu na ‘majeshi yake yenye kupiga kambi (NW).’ Baada ya pigano aliviingiza vikosi vyake katika mji wa Yerusalemu, kwa kweli, alifikia hatua ya kufukua sehemu ya ukuta wa hekalu akitaka kuubomoa. Bila shaka hili lilikuwa shambulio juu ya kile ambacho Wayahudi walikifikiria kuwa kitakatifu. Lakini Galo aliondoka kwa ghafula na bila kutazamiwa. Wayahudi walitoka mjini wakalifuata na kulitaabisha jeshi lake, wakateka silaha za mazingiwa na kurudia Yerusalemu wakiwa na hakika zaidi juu ya usalama wao.

25. Wakristo walifanya nini walipoyaona majeshi ya Galo yakiuzingira mji kisha kwa ghafula yakaondoka?

25 Mara tu Galo alipoondoka, Wakristo katika Yerusalemu waliuacha mji kuelekea kwenye jimbo lenye milima kuvuka Mto Yordani katika jimbo la Perea. Waliokolewa na kifo wakati Jemadari Tito alipouteka Yerusalemu miaka minne baadaye.

‘WATU’ FULANI WAOKOLEWA

26. Mazingiwa na kutekwa kwa Yerusalemu na majeshi ya Tito yalikuwa yenye kuogofya kadiri gani?

26 Katika kipindi cha kati ya mwaka wa 66 na 70 C.E., kulikuwa na msukosuko mwingi Yerusalemu, jamii nyingi za wafitini zikipigana ziusimamie mji. Halafu, mwaka wa 70 C.E. Jemadari Tito, mwana wa Mfalme Vespasia aliujia mji, akauzingira kwa boma lenye vijiti vilivyochongoka kama Yesu alivyokuwa ametangulia kuonyesha kwa unabii, na kuwaingiza wakaaji katika hali ya kuhurumika ya njaa kali. Ilielekea kuwa “mtu ye yote” aliyekuwamo mjini asingeokoka kama mazingiwa yangaliendelea zaidi. Lakini, kama Yesu alivyokuwa amesema kwa unabii juu ya hii “dhiki kubwa,” iliyo kubwa kupita zote zilizoupata Yerusalemu, “kama [Yehova] asingalizikatiza siku hizo, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule aliowateua amezikatiza siku hizo.”​—Marko 13:19, 20.

27. ‘Watu’ fulani waliokolewaje, na kwa ajili ya “wateule” kwa njia gani?

27 Kwa uongozi wa Mungu, mazingiwa yalikuwa ya siku 142 tu. Hata hivyo, ugonjwa wa kipuku na upanga uliangamiza watu 1,100,000, ukiwaacha waokokaji 97,000 wakauzwe utumwani au wakawe wapigana na wanyama-mwitu katika uwanja wa michezo wa Kirumi. Hivyo, “wateule” wa Yehova walikuwa wameukimbia mji uliopasishwa hukumu. Kwa sababu hiyo haikuwa lazima Yehova aurefushe wakati wa dhiki, lakini angeweza kufikiliza kisasi kwa muda mfupi, akiwaachilia watu 97,000, kwa njia hiyo akiokoa ‘watu’ fulani.

28. (a) Uharibifu wa Yerusalemu ulikuwaje mwisho kamili kwa taratibu ya mambo ya Kiyahudi? (b) Ni nani peke yake awezaye kuhakikisha haki yake ya ufalme na ukuhani, naye awezaje kufanya hivi?

28 Kwa njia hii taratibu ya mambo ya Kiyahudi ilifikia mwisho wake. Hawakuwa na hekalu lao tena. Kumbukumbu zao zote ziliharibiwa, hivi kwamba leo hakuna Myahudi awezaye kujihakikishia ukoo wa kikuhani, wala kwamba yeye ni wa kabila la kifalme la Yuda. Yesu Kristo ndiye wa pekee aliyehakikishiwa ukoo wake kuwa wa Yuda kupitia kwa Daudi. Yeye peke yake ndiye Mfalme wa haki. (Eze. 21:27) Ana cheo cha Ukuhani Mkuu kwa ajili ya wanadamu wote, si kulingana na ukoo wa Haruni, bali “kwa mfano wa Melkizedeki,” kwa kuwekwa moja kwa moja na Baba yake Yehova Mungu.​—Ebr. 7:15-17.

29. Je! jibu la Yesu kwa maulizo ya mitume lilikuwa na utimizo kamili Yerusalemu ulipoharibiwa? Eleza.

29 Lakini jibu kwa ulizo la mitume, “Mambo haya yatakuwa lini, na ni nini itakayokuwa ishara ya kuwapo kwako na ya mwisho wa taratibu ya mambo?” lilihitaji jibu hata zaidi, kwa maana parousia ya Yesu, “kuwapo” kwake katika mamlaka ya Ufalme, hakukutukia wakati wa uharibifu wa Yerusalemu. Kwa hiyo, Yesu alizungumza juu ya mwisho wa taratibu kubwa zaidi ya mambo, akitoa habari zaidi juu ya “ishara.” Hii itazungumzwa katika toleo la baadaye.

—Kutoka Kitabu God’s Kingdom of a Thousand Years Has Approached.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki