“Ni Nini Itakayokuwa Ishara ya Kuwapo Kwako?”
“Mambo haya yatakuwa wakati gani, na ni nini itakayokuwa ishara ya kuwapo kwako na ya umalizio wa mfumo wa mambo?” —MATHAYO 24:3, New World Translation.
1, 2. Ni nini kionyeshacho kwamba watu wanapendezwa na wakati ujao?
WATU walio wengi wanapendezwa na wakati ujao. Je! wewe hupendezwa pia? Katika kitabu chake Future Shock, Profesa Alvin Tofller alisema juu ya “mvuvumko wa ghafula wa mashirika yaliyojitoa ili kujifunza juu ya wakati ujao.” Yeye aliongeza hivi: ‘Sisi tumeona kuanzishwa kwa mashirika yanayofanya utafiti juu ya wakati ujao; kutokea kwa majarida yenye mambo yawezayo kutokea wakati ujao katika Uingereza, Ufaransa, Italia, Ujerumani, na United States; kuenea kwa mitalaa ya chuo kikuu inayohusu kutabiri.’ Tofller alimalizia hivi: “Bila shaka, hakuna mtu anayeweza ‘kujua’ wakati ujao katika maana yoyote kamili.”
2 Kitabu Signs of Things to Come chasema: “Kutazama mistari ya kiganja, kutazama tufe la fuwele, unajimu, karata za kutabiri, I Ching [kitabu cha uaguzi cha Mashariki] zote hizo ni njia zenye utata unaotofautiana zinazotupa wazo fulani juu ya jinsi wakati wetu ujao huenda ukawa.” Lakini badala ya kufuatia njia za kibinadamu, twapaswa tutegemee chanzo kilichothibitishwa—Yehova.
3. Kwa nini inafaa kumwendea Mungu ili kupata ujuzi juu ya wakati ujao?
3 Mungu wa kweli alisema hivi: “Kama vile [n]ilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa; na kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyotokea.” (Isaya 14:24, 27; 42:9) Ndiyo, Yehova ameweza kushauri ainabinadamu juu ya yale yatakayotukia, mara nyingi akifanya hivyo kupitia wasemaji wa kibinadamu. Mmoja wa manabii hao aliandika hivi: “Hakika [Yehova, NW] MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.”—Amosi 3:7, 8; 2 Petro 1:20, 21.
4, 5. (a) Kwa nini Yesu aweza kusaidia kwa habari ya wakati ujao? (b) Mitume wake waliuliza swali jipi lililotia ndani mambo mengi?
4 Yesu Kristo alikuwa nabii mashuhuri zaidi wa Mungu. (Waebrania 1:1, 2) Acheni tukazie fikira mmojawapo unabii mkuu zaidi wa Yesu unaotabiri mambo yanayotukia hivi sasa kutuzunguka. Unabii huo hutupa sisi pia mwono-ndani katika yale yatakayotukia karibuni wakati mfumo huu mwovu wa sasa ufikiapo mwisho na Mungu aweka paradiso ya kidunia mahali pao.
5 Yesu alithibitisha kwamba alikuwa nabii. (Marko 6:4; Luka 13:33; 24:19; Yohana 4:19; 6:14; 9:17) Hivyo, yaeleweka ni kwa nini mitume wake, wakiwa wameketi pamoja naye juu ya Mlima wa Mizeituni uliokuwa juu ya Yerusalemu, wangemuuliza juu ya wakati ujao: “Mambo haya yatakuwa wakati gani, nayo itakuwa ni nini ishara ya kuwapo kwako na ya umalizio wa mfumo wa mambo?”—Mathayo 24:3; Marko 13:4, NW.
6. Ni nini uhusiano kati ya Mathayo 24, Marko 13, na Luka 21; na ni swali jipi lipasalo litupendeze sana?
6 Utapata swali lao na jibu la Yesu katika Mathayo sura ya 24, Marko sura ya 13, na Luka sura ya 21.a Katika mambo mengi masimulizi hayo yanakamilishana, lakini hayafanani kabisa. Kwa kielelezo, ni Luka pekee atajaye “tauni mahali mahali.” (Luka 21:10, 11; Mathayo 24:7; Marko 13:8) Kwa kufuatana na akili, twapaswa kuuliza, Je! Yesu alikuwa akitabiri matukio ambayo yangetokea katika muda wa maisha ya wasikilizaji wake tu, au yeye alitia ndani wakati wetu na mambo ambayo wakati ujao umetuwekea?
Mitume Walitaka Kujua
7. Mitume waliuliza juu ya nini hasa, lakini ni nini iliyokuwa kadiri ya ukubwa wa jibu la Yesu?
7 Siku chache tu kabla ya yeye kuuawa, Yesu alijulisha kwamba Mungu alikuwa amekataa Yerusalemu, jiji kuu la Wayahudi. Jiji hilo na hekalu lalo tukufu lingeharibiwa. Ndipo baadhi ya mitume wakauliza wapewe ‘ishara ya kuwapo kwa Yesu’ na ya umalizio wa mfumo wa mambo. (Mathayo 23:37–24:3) Bila shaka wao walikuwa wakifikiria hasa mfumo wa Kiyahudi na Yerusalemu, kwani hawakuelewa kadiri ya ukubwa wa yale yaliyokuwa mbele. Lakini katika kuwajibu Yesu alitazama wakati wa baadaye sana kuliko yale yaliyotukia hadi na kutia ndani 70 W.K. wakati Waroma walipoharibu Yerusalemu.—Luka 19:11; Matendo 1:6, 7.
8. Ni nini baadhi ya matukio ambayo Yesu alitabiri?
8 Kama vile uwezavyo kusoma katika yale masimulizi matatu ya Gospeli, Yesu alisema juu ya taifa kuinuka juu ya taifa na ufalme juu ya ufalme, upungufu wa chakula, matetemeko ya dunia, maono ya kutisha, na ishara za kimbingu. Katika ile miaka iliyofuata kutoa kwa Yesu ishara hiyo (33 W.K.) na kufikia ukiwa wa Yerusalemu (66-70 W.K.), manabii bandia na Makristo bandia wangetokea. Wayahudi wangewanyanyasa Wakristo, waliokuwa wakihubiri ujumbe wa Yesu.
9. Unabii wa Yesu ulipataje utimizo katika karne ya kwanza W.K.?
9 Sehemu hizo za ishara zilitokea kihalisi, kama vile mwanahistoria Flavio Yosefo athibitishavyo. Yeye aandika kwamba kabla ya Waroma kupata kuwashambulia, Mesiya bandia walichochea uasi. Kulikuwako matetemeko makubwa ya dunia katika Yudea na kwingineko. Vita vilitokea katika sehemu mbalimbali za Milki ya Roma. Je! kulikuwa na njaa kuu? Ndiyo, hakika. (Linganisha Matendo 11:27-30.) Namna gani juu ya kazi ya kuhubiri Ufalme? Kufikia karibu 60 au 61 W.K., wakati kitabu cha Wakolosai kilipoandikwa, ‘tumaini la hizo habari njema’ za Ufalme wa Mungu lilikuwa limesikiwa sana katika Afrika, Asia, na Ulaya.b—Wakolosai 1:23, NW.
“NDIPO” Mwisho
10. Kwa nini tuchunguze neno la Kigiriki toʹte, na umaana walo ni nini?
10 Katika sehemu fulani za unabii wake Yesu alionyesha matukio yakitokea kwa kufuatana. Yeye alisema hivi: “Habari njema ya ufalme itahubiriwa . . . hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.” Mara nyingi Biblia mbalimbali hutumia neno “ndipo” zikiwa na maana sahili ya kusema “kwa hiyo” au “lakini.” (Marko 4:15, 17; 13:23) Hata hivyo, kwenye Mathayo 24:14, “ndipo” linategemea kielezi cha Kigiriki to΄te.c Wataalamu wa Kigiriki waeleza kwamba to΄te ni “kielezi-kionyeshi cha wakati” kinachotumiwa “kujulisha yale yanayofuata katika wakati” au “kujulisha tukio lifuatalo.” Hivyo Yesu alitabiri kwamba kungekuwa na kuhubiriwa kwa Ufalme na ndipo (‘baada ya hilo’ au, ‘kufuatia hilo’) “mwisho” ungekuja. Mwisho gani?
11. Yesu alikaziaje matukio yaliyohusiana moja kwa moja na uharibifu wa Yerusalemu?
11 Utimizo mmoja wa unabii wa Yesu waweza kupatikana katika matukio yaliyoongoza kwenye mwisho wa mfumo wa Kiyahudi. Vita, matetemeko ya dunia, upungufu wa chakula, na mambo mengine, ambayo Yesu alitabiri yalitukia katika kipindi cha miongo mitatu. Lakini kuanzia Mathayo 24:15, Marko 13:14, na Luka 21:20, twasoma juu ya matukio yaliyohusika moja kwa moja na uharibifu uliokuwa karibu, mwisho ulipokuwa karibu sana.—Ona ule mstari mmoja wa madoa-doa kwenye chati.
12. Majeshi ya Roma yalihusikaje katika utimizo wa Mathayo 24:15?
12 Kwa kuitikia uasi wa Kiyahudi katika 66 W.K., Waroma chini ya Sesho Galo walikuja dhidi ya Yerusalemu, wakizingira jiji hilo lililoonwa na Wayahudi kuwa takatifu. (Mathayo 5:35) Yajapokuwa mashambulizi ya Wayahudi, Waroma waliingia kwa nguvu katika hilo jiji. Hivyo wao wakaanza ‘kusimama katika patakatifu,’ sawasawa na utabiri wa Yesu kwenye Mathayo 24:15 na Marko 13:14. Kisha jambo la kushangaza likatukia. Ingawa walikuwa wamelizingira jiji hilo, Waroma waliondoka kwa ghafula. Mara iyo hiyo Wakristo walitambua utimizo wa unabii wa Yesu, na kuondoka huko kuliwaruhusu wakimbie kutoka Yudea kuingia katika milima iliyokuwa ng’ambo ya Yordani. Historia yasema walifanya hivyo.
13. Kwa nini Wakristo waliweza kutii onyo la Yesu la kukimbia?
13 Lakini ikiwa Waroma waliondoka wakaacha kulizingira Yerusalemu, kwa nini mtu yeyote angehitaji kukimbia? Maneno ya Yesu yalionyesha kwamba yale yaliyokuwa yametukia yalithibitisha ‘kwamba kufanywa ukiwa kwa Yerusalemu kulikuwa karibu.’ (Luka 21:20) Ndiyo, kufanywa ukiwa. Yesu alitabiri ‘dhiki ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wala haingekuwapo tena.’ Karibu miaka mitatu na nusu baadaye, katika 70 W.K., kwa kweli Yerusalemu lilipatwa na “dhiki kubwa” kutoka kwa majeshi ya Waroma chini ya Jenerali Tito. (Mathayo 24:21; Marko 13:19) Lakini kwa nini Yesu asimulie dhiki hiyo kuwa kubwa kuliko yoyote yenye kupata kuwako kabla au tangu wakati huo?
14. Kwa nini twaweza kusema kwamba yale yaliyotukia Yerusalemu katika 70 W.K. yalikuwa “dhiki kubwa” ambayo haijapata kutokea namna yake kabla ya hapo na tangu hapo?
14 Yerusalemu liliharibiwa na Wababiloni katika 607 K.W.K., na jiji hilo limepatwa na mapigano yenye kutisha katika karne yetu ya sasa. Bado, yale yaliyotukia katika 70 W.K. yalikuwa dhiki kubwa ya kipekee. Katika kampeni ya karibu miezi mitano, askari wa Tito waliwashinda Wayahudi. Waliua karibu watu 1,100,000 kati yao na kuchukua wapatao 100,000 utumwani. Kisha, Waroma wakabomoa Yerusalemu. Hilo lilithibitisha kwamba mfumo wa Kiyahudi wa ibada iliyokubaliwa zamani uliotegemea hekalu ulikuwa umekoma kabisa. (Waebrania 1:2) Ndiyo, matukio ya 70 W.K. yangeweza kwa kufaa kuonwa kuwa ‘dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake [juu ya jiji, taifa, na mfumo huo] tangu mwanzo wa ulimwengu, wala haitakuwapo kamwe.’—Mathayo 24:21.d
Kama Ilivyotolewa Unabii, Mengine Yangefuata
15. (a) Yesu alitabiri matokeo ya aina gani ambayo yangekuja baada ya dhiki juu ya Yerusalemu? (b) Kulingana na Mathayo 24:23-28, ni lazima tufikie mkataa gani kuhusu utimizo wa unabii wa Yesu?
15 Hata hivyo, Yesu hakutumia utabiri wake kwa habari ya dhiki ya karne ya kwanza pekee. Biblia huonyesha kwamba mengi sana yangefuata dhiki hiyo, kama inavyodokezwa na utumizi wa to΄te, au “ndipo,” kwenye Mathayo 24:23 na Marko 13:21. Ni nini kingetukia katika kipindi ambacho kingefuata 70 W.K.? Baada ya dhiki hiyo juu ya mfumo wa Kiyahudi, Makristo bandia na manabii bandia wengine zaidi wangetokea. (Linganisha Marko 13:6 pamoja na 13:21-23.) Historia huthibitisha kwamba watu hao mmoja-mmoja wametokea katika muda wa karne nyingi tangu kuharibiwa kwa Yerusalemu katika 70 W.K., ingawa hawajawapotosha watu walio na mwono chonjo wa kiroho na ambao wamekuwa wakitazamia “kuwapo” kwa Kristo. (Mathayo 24:27, 28) Hata hivyo, matukio hayo baada ya dhiki ya 70 W.K. yanatoa kionyeshi kimoja kwamba Yesu alikuwa akitazama mbele muda mrefu baada ya dhiki hiyo, uliokuwa utimizo wa kwanza tu.
16. Luka 21:24 laongeza jambo jipi kwenye unabii wa Yesu, na hilo lina umaana gani?
16 Tukilinganisha Mathayo 24:15-28 na Marko 13:14-23 pamoja na Luka 21:20-24, twapata kionyeshi cha pili kwamba utabiri wa Yesu ulihusisha muda mrefu baada ya uharibifu wa Yerusalemu. Kumbuka kwamba Luka pekee ndiye aliyekuwa ametaja tauni. Vivyo hivyo, ni yeye pekee aliyemalizia sehemu hiyo kwa maneno haya ya Yesu: “Yerusalemu litakanyagwa-kanyagwa na mataifa, hata nyakati zilizowekwa za mataifa [“nyakati za Wasio Wayahudi,” King James Version] ziwe zimetimizwa.”e (Luka 21:24, NW) Wababiloni walimwondoa mfalme wa mwisho wa Wayahudi katika 607 K.W.K., na baada ya hapo, Yerusalemu, likifananisha Ufalme wa Mungu, lilikanyangwa-kanyagwa. (2 Wafalme 25:1-26; 1 Mambo ya Nyakati 29:23; Ezekieli 21:25-27) Kwenye Luka 21:24, Yesu alionyesha kwamba hali hiyo ingeendelea hadi wakati ujao mpaka wakati ungefika ambapo Mungu angesimamisha Ufalme tena.
17. Tuna kionyeshi kipi cha tatu kwamba unabii wa Yesu ungefikia muda mrefu baadaye katika wakati ujao?
17 Hapa kuna kionyeshi cha tatu kwamba Yesu alikuwa akionyesha pia utimizo wa muda mrefu baadaye: Kulingana na Maandiko, Mesiya angekufa na kufufuliwa, kisha yeye angeketi kwenye mkono wa kulia wa Mungu hadi Baba amtume aende hali akishinda. (Zaburi 110:1, 2) Yesu alitaja juu ya kuketi kwake kwenye mkono wa kulia wa Baba yake. (Marko 14:62) Mtume Paulo alithibitisha kwamba Yesu aliyefufuliwa alikuwa kwenye mkono wa kulia wa Yehova akingoja wakati ambapo angekuwa Mfalme na Mtekelezaji-Hukumu wa Mungu.—Warumi 8:34; Wakolosai 3:1; Waebrania 10:12, 13.
18, 19. Ufunuo 6:2-8 linahusuje unabii unaofanana na huo katika Gospeli?
18 Ili tuone kionyeshi cha nne ambacho ni cha mwisho na chenye kukata kauli kwamba unabii wa Yesu juu ya umalizio wa mfumo wa mambo wahusu muda mrefu baada ya karne ya kwanza, twaweza kufungua Ufunuo sura ya 6. Akiandika miongo mingi baada ya 70 W.K., mtume Yohana alieleza juu ya mandhari yenye kuvuta fikira ya wapanda farasi wenye bidii. (Ufunuo 6:2-8) Mwono huo wa kiunabii wa kuingia katika “siku ya Bwana”—siku ya kuwapo kwake—hutambulisha karne yetu ya 20 kuwa wakati wa vita kuu (mstari 4), upungufu wa chakula wenye kuenea (mistari 5 na 6), na “tauni” (mstari 8). Kwa wazi, hayo yafanana na mambo ambayo Yesu alisema katika zile Gospeli na yathibitisha kwamba unabii wake una utimizo mkubwa zaidi katika ‘siku hii ya Bwana.’—Ufunuo 1:10.
19 Watu wenye ufahamu hukiri kwamba ishara yenye mambo mengi iliyotabiriwa kwenye Mathayo 24:7-14 na Ufunuo 6:2-8 imedhihirika tangu kutokea kwa mara ya kwanza kwa vita ya ulimwengu katika 1914. Mashahidi wa Yehova wametangaza ulimwenguni pote kwamba sasa unabii wa Yesu unapata utimizo wao wa pili na ulio mkubwa zaidi, kama vile inavyoonyeshwa na vita vya ukatili, matetemeko ya dunia yenye uharibifu mkubwa, njaa zenye maafa makubwa, na maradhi yenye kuenea. Kwa habari hiyo ya mwisho, U.S.News & World Report (Julai 27, 1992) lilisema hivi: “Ugonjwa wa UKIMWI wenye kuenea sana . . . unaua mamilioni ya watu na huenda hivi karibuni ukawa tauni yenye kugharimu na yenye msiba mkubwa zaidi katika historia. Ugonjwa wa Kifo Cheusi uliua watu wapatao milioni 25 katika karne ya 14. Lakini kufikia mwaka 2000, watu wapatao milioni 30 hadi milioni 110 watakuwa na HIV, ile virusi iletayo UKIMWI, ikiwa ni ongezeko zaidi ya wale kama milioni 12 wa leo. Iwapo hakutakuwa na ponyo, wote hao wanakabili kifo kisichoepukika.”
20. Utimizo wa kwanza wa Mathayo 24:4-22 ungehusisha nini, lakini ni utimizo upi mwingine ulio wazi?
20 Kwa hiyo, tufikie mkataa gani juu ya jinsi Yesu alivyojibu swali la mitume? Unabii wake ulitabiri kwa usahihi matukio yaliyoongoza kwenye na kutia ndani kuharibiwa kwa Yerusalemu, na ulitaja mambo fulani ambayo yangefuata 70 W.K. Lakini mengi ya hayo yangepata utimizo wa pili na ulio mkubwa zaidi wakati ujao, yakiongoza kwenye dhiki kubwa ambayo ingekomesha mfumo mwovu wa mambo uliopo. Hilo lamaanisha kwamba utabiri wa Yesu kwenye Mathayo 24:4-22, na masimulizi yanayofanana katika Marko na Luka, ulitimizwa kuanzia 33 W.K. hadi dhiki ya 70 W.K. Lakini, mistari iyo hiyo ingekuwa na utimizo wa pili ambao ungetia ndani dhiki kubwa zaidi wakati ujao. Utimizo huo mkubwa zaidi upo nasi; twaweza kuuona kila siku.f
Unaongoza Kwenye Nini?
21, 22. Tunapata wapi kionyeshi cha kiunabii kwamba matukio ya ziada yangekuja?
21 Yesu hakumalizia unabii wake kwa kutaja manabii bandia wenye kufanya ishara zenye kudanganya katika kile kipindi kirefu kabla ya ‘kutimia kwa nyakati zilizowekwa za mataifa.’ (Luka 21:24, NW; Mathayo 24:23-26; Marko 13:21-23) Aliendelea kusimulia mambo mengine ya kushangaza ambayo yangetukia, mambo ambayo yangeonekana duniani pote. Hayo yangeshirikishwa na kuja kwa Mwana wa Adamu katika nguvu na utukufu. Marko 13:24-27 linawakilisha unabii wa Yesu wenye kuendelea:
22 “Lakini siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu.”
23. Kwa nini twaweza kutazamia utimizo wa Mathayo 24:29-31 muda mrefu baada ya karne ya kwanza W.K.?
23 Mwana wa Adamu, ambaye ndiye Yesu Kristo aliyefufuliwa, hakuja kwa njia hiyo yenye kutazamisha baada ya mwisho wenye uharibifu wa mfumo wa Kiyahudi katika 70 W.K. Kwa hakika makabila yote ya dunia hayakumtambua, kama vile Mathayo 24:30 kionyeshavyo, wala malaika wa kimbingu hawakukusanya Wakristo wote wapakwa kutoka duniani pote wakati huo. Kwa hiyo sehemu hiyo ya ziada ya unabii huo wa Yesu wenye kuvutia sana ingetimizwa wakati gani? Je! hiyo inatimizwa katika yale yanayoendelea wakati huu, au badala ya hivyo, inaandaa mwono-ndani katika mambo tuwezayo kutazamia katika wakati ujao ulio karibu? Kwa hakika twapaswa tutake kujua, kwani Luka arekodi himizo hili la Yesu: “Mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.”—Luka 21:28.
[Maelezo ya Chini]
a Sehemu za sura hizo zaweza kupatikana katika chati kwenye kurasa 14 na 15; mistari ya madoa-doa inatia alama sehemu zinazofanana.
b Kupata mitajo ya kihistoria juu ya matukio hayo, ona Mnara wa Mlinzi la Januari 15, 1970, (Kiingereza) kurasa 43-5.
c Toʹte huonekana zaidi ya mara 80 katika Mathayo (mara 9 katika sura ya 24) na mara 15 katika kitabu cha Luka. Marko alitumia toʹte mara sita pekee, lakini mara nne kati yazo zilihusisha “ishara.”
d Mtunga-vitabu Mwingereza Matthew Henry alisema hivi: “Kuharibiwa kwa Yerusalemu na Wakaldayo kulikuwa kubaya sana, lakini huku kulikupita. Kulikaribia kuwa machinjo ya ulimwenguni pote ya . . . Wayahudi wote.”
e Wengi huona katika simulizi la Luka badiliko la mkazo baada ya Luka 21:24. Dakt. Leon Morris asema: “Yesu aendelea kusema juu ya nyakati za Wasio Wayahudi. . . . Kulingana na maoni ya wasomi walio wengi fikira yaelekezwa sasa kwenye kuja kwa Mwana wa Adamu.” Profesa R. Ginns aandika hivi: “Kuja kwa Mwana wa Adamu—(Mt 24:29-31; Mk 13:24-27). Kutajwa kwa ‘nyakati za Wasio Wayahudi’ kwaandaa utangulizi kwa kichwa hicho; sasa maoni ya [Luka] yanafikia muda mrefu baada ya kuharibiwa kwa Yerusalemu kuingia katika wakati ujao.”
f Profesa Walter L. Liefeld aandika hivi: “Kwa hakika yawezekana kuona kwamba tabiri za Yesu zilitia ndani sehemu mbili: (1) matukio ya A.D. 70 yaliyohusisha hekalu na (2) yale ya muda mrefu baadaye katika wakati ujao, yanayoelezwa katika maneno ya kiapokalipsi [ufunuo] zaidi.” Ufafanuzi uliohaririwa na J. R. Dummelow wasema hivi: “Mengi ya magumu mazito zaidi ya hotuba hiyo kuu hutoweka inapong’amuliwa kwamba Bwana yetu hakurejezea ndani yayo tukio moja bali mawili, na kwamba lile la kwanza lilifananisha lile la pili. . . . [Luka] 21:24 hasa, linalosema juu ya ‘nyakati za Wasio Wayahudi,’ . . . laweka kipindi cha katikati kisicho dhahiri kati ya anguko la Yerusalemu na mwisho wa ulimwengu.”
Je! Wakumbuka?
◻ Jibu la Yesu kwa lile swali kwenye Mathayo 24:3 lilikuwa na utimizo gani ulioongoza kwenye 70 W.K.?
◻ Matumizi ya neno toʹte yanatusaidiaje tuelewe unabii wa Yesu?
◻ Ni katika maana gani kwamba kulikuwa na “dhiki kubwa” ya karne ya kwanza ya namna isiyopata kutokea kabla ya hapo?
◻ Luka arejezea mambo gani mawili ya kipekee ya unabii wa Yesu yanayotuhusisha leo?
◻ Ni vionyeshi vipi vionyeshavyo utimizo wa pili na ulio mkubwa zaidi wa unabii kwenye Mathayo 24:4-22?
[Chati katika ukurasa wa 14 na 15]
4“Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. 5Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. 6Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado.
7“Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. 8Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu.
9“Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. 10Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. 11Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. 12Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. 13Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. 14Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.
15“Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu) 16ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; 17naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; 18wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. 19Ole wao wenye mimba na waamwishao siku hizo! 20Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. 21Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. 22Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.
23“Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule, msisadiki. 24Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. 25Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. 26Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. 27Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
29“Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; 30ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. 31Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.”
5“Yesu akaanza kuwaambia, Jihadharini, mtu asiwadanganye. 6Wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye, nao watadanganya wengi. 7Nanyi mtakaposikia habari za vita na uvumi wa vita, msitishwe; hayo hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.
8“Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko ya nchi mahali mahali; kutakuwako na njaa; hayo ndiyo mwanzo wa utungu.
9“Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao. 10Na sharti Injili ihubiriwe kwanza katika mataifa yote. 11Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lo lote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu [roho takatifu, NW]. 12Na ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, na baba atamsaliti mtoto, na watoto wataondoka juu ya wazazi wao, na kuwafisha. 13Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kusaburi hata mwisho, ndiye atakayeokoka.
14“Lakini mlionapo chukizo la uharibifu likisimama pasipolipasa, (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; 15na mtu aliye juu ya dari asishuke, wala asiingie kuchukua kitu nyumbani mwake; 16naye aliye shambani asirudi nyuma kulichukua vazi lake. 17Lakini ole wao wenye mimba, nao wanyonyeshao siku hizo! 18Ila ombeni yasitokee hayo wakati wa baridi. 19Kwa maana siku hizo zitakuwa na dhiki, jinsi isivyokuwa tangu mwanzo wa kuumba alipoumba Mungu hata sasa, wala haitakuwa kamwe. 20Na kama Bwana [Yehova, NW] asingalizikatiza siku hizo, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule aliowateua amezikatiza siku hizo.
21“Na wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule, msisadiki; 22kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule. 23Bali ninyi jihadharini; nimekwisha kuwaonya yote mbele.
24“Lakini siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, 25na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. 26Hapo ndipo watakapmwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. 27Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu.”
8“Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao. 9Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi.
10“Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; 11kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.
12“Lakini, kabla hayo yote hayajatokea, watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwatia magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu. 13Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu. 14Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; 15Kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. 16Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. 17Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. 18Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. 19Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.
20“Lakini, hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia. 21Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie. 22Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa. 23Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili. 24Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote;
na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia.
25“Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; 26watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika. 27Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi. 28Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Ile dhiki katika 70 W.K. ilikuwa kubwa zaidi ya zote ambazo Yerusalemu na mfumo wa Kiyahudi ilipata kuona wakati wowote