Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 2/22 kur. 7-11
  • Kukabiliana na Komahedhi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kukabiliana na Komahedhi
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wanawake Wanapokabiliana Vizuri Zaidi
  • Kile Wanawake Wanachohitaji
  • Chakula na Mazoezi
  • Kukabiliana na Joto la Ghafula Mwilini
  • Namna Gani Mkazo?
  • Washiriki wa Familia Waweza Kusaidia
  • Maisha Baada ya Komahedhi
  • Kupata Uelewevu Mzuri Zaidi
    Amkeni!—1995
  • Kukabiliana na Matatizo ya Kukoma kwa Hedhi
    Amkeni!—2013
  • Kufunua Siri Zake
    Amkeni!—1995
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 2/22 kur. 7-11

Kukabiliana na Komahedhi

KOMAHEDHI ni “ono la kipekee sana” na ni “mwanzo wa sura mpya ya kuwekwa huru maishani mwako,” wasema watungaji wa Natural Menopause—The Complete Guide to a Woman’s Most Misunderstood Passage. Utafiti huonyesha kwamba kadiri uhisivyo vizuri zaidi juu yako mwenyewe na juu ya maisha yako—kule kujistahi kwako mwenyewe na ule utu wako wa kipekee—ndivyo badiliko hilo litakavyokuwa rahisi zaidi.

Ni kweli kwamba, ni vigumu zaidi kwa wanawake fulani kuliko kwa wengine katika wakati huu wa maisha. Ikiwa una magumu, hilo halimaanishi kwamba una matatizo ya kujistahi au unapungukiwa na akili, na hali yako ya kike, na welekevu wako, au na kupendezwa kwako na ngono. Badala yake, tatizo kwa kawaida ni la kibiolojia.

“Hata wanawake waliopatwa na dalili mbaya sana wakati wa komahedhi husema baadaye walikuwa na hisi mpya ya kusudi na nguvu,” laripoti gazeti Newsweek. Kwa maneno ya mmoja mwenye umri wa miaka 42: “Ninatazamia kwa furaha ule utulivu, wakati mwili wangu utaacha kunichezea-chezea.”

Wanawake Wanapokabiliana Vizuri Zaidi

Jinsi wanawake wenye umri mkubwa zaidi wanavyoonwa ni jambo la maana kwa habari ya jinsi wakabilianavyo vizuri na komahedhi. Mahali ambapo ukomavu, hekima, na uzoefu wao unathaminiwa, wakati wa komahedhi unaambatana na maradhi machache zaidi ya kimwili na ya kihisiamoyo.

Kwa kielelezo, The Woman’s Encyclopedia of Health and Natural Healing yaripoti kwamba katika makabila ya Kiafrika “ambapo komahedhi inakaribishwa kama kijia chenye kupendeza maishani, na wanawake ambao wamepitia komahedhi wanastahiwa kwa ajili ya uzoefu na hekima yao, ni mara chache sana wanawake hulalamika juu ya dalili za komahedhi.” Vivyo hivyo, The Silent Passage—Menopause husema: “Wanawake Wahindi wa tabaka la jamii ya Rajput hawalalamiki juu ya mshuko-moyo wala dalili za kiakili” wakati wa komahedhi.—Italiki ni zetu.

Katika Japani pia ambapo wanawake wazee-wazee hustahiwa sana, tiba ya homoni kwa ajili ya komahedhi haijulikani sana. Zaidi ya hayo, yaonekana wanawake wa Asia wana dalili za komahedhi zilizo chache zaidi na zisizo mbaya sana kama za wale wa utamaduni wa Magharibi. Yaonekana chakula chao ni jambo lichangialo hili.

Kwa kweli wanawake wa Maya walitazamia komahedhi kwa furaha, kulingana na uchunguzi mbalimbali wa mtaalamu mmoja wa elimu na historia ya binadamu. Kwa wanawake hao komahedhi ilimaanisha kitulizo kutoka katika kule kuzaa watoto kwa kuendelea. Bila shaka, hilo liliwaletea uhuru pia wa kufuatia mapendezi mengine maishani.

Wakati uleule, hofu zinazohusiana na komahedhi hazipasi kupuuzwa kivivi-hivi tu. Katika tamaduni zinazokazia thamani ya ujana na sura ya ujana, wanawake ambao hawajapatwa bado na komahedhi huihofu mara nyingi. Ni nini kiwezacho kufanywa kwa ajili ya watu hao mmoja-mmoja ili kupunguza magumu ya badiliko hilo?

Kile Wanawake Wanachohitaji

Janine O’Leary Cobb, mtungaji na wa kwanza kujifunza elimu ya komahedhi, aeleza hivi: “Kile wanawake wengi wanachohitaji ni aina fulani ya uthibitisho wa jinsi wanavyohisi—kwamba hawako peke yao.”

Uelewevu, na pia kuwa na mtazamo wenye furaha, ni muhimu. Mama mmoja mwenye umri wa miaka 51 anayepitia komahedhi alisema hivi: “Naamini kwa unyoofu kwamba ni mtazamo wako wa ujumla kuelekea maisha utakaoongoza jinsi utakavyopitia komahedhi. . . . Najua uzee uko. Tupende tusipende, hilo litatukia. . . . Niliamua kwamba hii [komahedhi] si ugonjwa. Ni maisha yangu.”

Kwa hiyo sura hii mpya maishani mwako ikaribiapo, fanya wakati wa kufikiri sana juu ya mapendezi mapya, yaliyo magumu. Jambo lisilopasa kupuuzwa ni athari za kimwili za komahedhi. Madaktari na wenye mamlaka wengine hupendekeza kufuata kanuni za kawaida za afya njema katika kutayarishia badiliko hili—chakula chenye kujenga, pumziko la kutosha, na mazoezi ya kiasi.

Chakula na Mazoezi

Uhitaji wa lishe bora (protini, kabohidrati, mafuta, vitamini, madini) haupungui mwanamke anapokuwa mwenye umri mkubwa zaidi, lakini uhitaji wake wa kalori hupungua. Kwa hiyo, ni jambo la maana kula vyakula vyenye lishe bora na kuepuka vyakula vyenye sukari, vilivyo na mafuta ambavyo ni “kalori zisizo na thamani yoyote.”

Mazoezi ya kawaida huongeza uwezo wa kukabiliana na mkazo na mshuko-moyo. Huongeza nishati na kusaidia kuzuia ongezeko la uzani. Kima cha uvunjaji wa kemikali mwilini hupungua hatua kwa hatua kadiri umri uzidivyo kuongezeka, na kisipoongezwa kwenye mazoezi, mwelekeo ni kuongezeka kwa uzani hatua kwa hatua.

Ni jambo la maana sana kwa wanawake kujua kwamba mazoezi yakiunganishwa na nyongeza za kalsiamu mwilini kwaweza kupunguza usitawi wa osteoporosisi, hali ya mifupa itokezayo unywelevu na udhaifu. Kitabu Women Coming of Age chasema kwamba “mazoezi ya ndani ya nyumba ya kupumua kasi yafanywayo ifaavyo, kutembea, kukimbia, kuendesha baiskeli na michezo mingine ya kupumua kasi, pamoja na kujizoeza kwa kunyanyua uzani,” yanafikiriwa kuwa mazuri hasa. Kwa kupendeza, osteoporosisi haipatikani katika jumuiya fulani za ndani-ndani ambamo watu huendelea kuwa wenye utendaji kimwili kwa muda mrefu katika uzee wao. Katika mahali hapo wanawake huishi kwa kawaida hadi miaka yao ya 80 na 90. Hata hivyo, kabla ya kuanza programu yoyote ya mazoezi, lingekuwa jambo la hekima kushauriana na daktari wako.

Kukabiliana na Joto la Ghafula Mwilini

Kwa wanawake walio wengi, joto la ghafula mwilini ni usumbufu. Lakini kwa wengine, hilo huwa tatizo kwelikweli kwa sababu ama linatukia mara nyingi ama linakatiza usingizi daima. Ni nini kiwezacho kufanywa?

Kwanza kabisa, usiwe na wasiwasi sana. Kuongezea hali hiyo hangaiko kutaifanya iwe mbaya zaidi. Mazoezi ya kawaida yenye juhudi ni ya manufaa kwa sababu husaidia mwili ujifunze kukabiliana na joto la kupita kiasi na kupoa upesi zaidi. Pia jaribu ile hatua sahili ya kunywa bilauri la maji baridi au kutia mikono yako katika maji baridi.

Kwa kuongezea, fanya zoea la kuvaa mavazi yasiyokaza, moja juu ya nyingine ili yaweze kuvuliwa au kuvaliwa kwa urahisi. Nguo za pamba na za kitani huruhusu jasho livukizwe vizuri zaidi kuliko nguo za kutengenezwa kibandia. Usiku jaribu ile njia ya kuweka mablanketi kadhaa, moja juu ya jingine, ili moja-moja liweze kutumiwa au kuondolewa kulingana na uhitaji. Weka karibu mavazi ya kulala ya kubadilisha.

Jaribu kupambanua ni nini yaonekana husababisha joto lako la ghafula mwilini. Kunywa alkoholi, kafeini, kula sukari, na vyakula vikali au vyenye viungo vingi kwaweza kulichochea, kama vile kuvuta sigareti kuwezavyo. Kuweka maandishi ya wakati na mahali joto la ghafula mwilini hutukia kwaweza kukusaidia utambulishe vyakula na utendaji mbalimbali unaoisababisha. Halafu epuka vitu hivi.

Matabibu wenye ustadi katika tiba ihusuyo chakula chenye lishe bora hudokeza viponyo mbalimbali vya kupunguza joto la ghafula mwilini, kama vile vitamini E, mafuta ya ua dogo la kondeni liitwalo evening primrose, na mimea iitwayo Ginseng, dong quai, na black cohosh. Kulingana na madaktari fulani, dawa za kupendekezwa Bellergali na klonidini huandaa kitulizo, lakini tembe au vipande vya estrojeni vya kutiwa katika ngozi husemwa kuwa vyenye matokeo zaidi.a

Kukauka kwa uke kwaweza kuponywa kwa kupaka mafuta ya mimea au ya matunda, vitamini E na geli za kuulainisha. Hizo zikithibitika kutotosha, krimu ya estrojeni itasaidia kuta za uke zinenepe zaidi na kuwa laini. Kabla ya kuanza tiba yoyote, ni jambo la hekima kushauriana na tabibu kwanza.

Namna Gani Mkazo?

Wakati uleule ambapo ni lazima mwanamke ashughulike na mabadiliko ya kihomoni na ya kimwili yajayo na komahedhi, mara nyingi ni lazima akabili mambo yenye mkazo, mengi yakiwa yale yaliyotajwa katika makala lililotangulia. Kwa upande ule mwingine, mambo mazuri kama vile kuzaliwa kwa mjukuu au kufuatia utendaji mpya mbalimbali baada ya watoto kuondoka nyumbani kwaweza kusawazisha mkazo hasi.

Katika kitabu chao Natural Menopause, Susan Perry na Dakt. Katherine A. O’Hanlan hutoa madokezo fulani yenye kutumika ili kushughulika na mkazo vizuri zaidi. Wao waelekeza kwenye uhitaji wa kutambulisha vyanzo vya mkazo halafu kupumzika muda kwa muda. Huenda hilo likamaanisha kupata msaada katika kutunza mshiriki wa familia aliye mgonjwa sana. “Jiwekee mwendo wenye kiasi,” wao wahimiza. “Jaribu kuepuka kuratibu mambo mengi kupita kiasi . . . Itikia dalili za mwili wako.” Wao waongeza hivi: “Kutumikia wengine . . . kwaweza kuwa kipunguza-mkazo kikubwa. . . . Fanya mazoezi kwa kawaida. . . . Pata msaada wa kitiba ikiwa mkazo maishani mwako wapita uwezo wa kuudhibiti.”

Washiriki wa Familia Waweza Kusaidia

Mwanamke anayepitia komahedhi ahitaji uelewevu wa kihisiamoyo na utegemezo wenye kutumika. Akifafanua kile alichokuwa akifanya alipokuwa na vipindi vya kuhangaika, mke mmoja alisema hivi: “Nilikuwa nikizungumzia mambo pamoja na mume wangu, na baada ya uelewevu wake wenye huruma, nilikuwa naona kwamba matatizo hayakuwa makubwa kama vile hali yangu ya akili yenye kuhangaika ilivyokuwa imeyaona kuwa.”

Mume mwenye hisia nyepesi hufahamu pia kwamba mke wake hataweza sikuzote kuwa na mwendo uleule anapopitia komahedhi. Kwa hiyo atakuwa chonjo kuchukua hatua ya kwanza kusaidia na madaraka ya familia, labda kufua nguo, kununua chakula, na kadhalika. Kwa huruma, yeye ataweka mahitaji ya mke wake mbele ya mahitaji yake mwenyewe. (Wafilipi 2:4) Huenda akadokeza waende kula mlo nje pindi kwa pindi au kwa njia fulani kufanya jambo la kupendeza lililo tofauti na kawaida ya kila siku. Yeye ataepuka kutoelewana kwa kadiri iwezekanavyo naye atategemeza jitihada zake za kudumisha mazoea ya kula yenye afya.

Zaidi ya yote, mume atatimiza uhitaji wa mke wake kwa kumhakikishia kwa kawaida juu ya upendo wake kwake wenye kuendelea. Yeye apaswa kuwa mwenye utambuzi na apaswa kufahamu kwamba huu si wakati wa kumfanyia mke wake utani kuhusu mambo ya kibinafsi. Mume amtendeaye mke wake kwa njia yenye upendo anafuata onyo la upole la Kimaandiko la ‘kukaa naye kwa akili, na kumpa heshima.’—1 Petro 3:7.

Vivyo hivyo, watoto wapaswa kujitahidi kikweli kuelewa sababu ya mabadiliko-badiliko ya kihisiamoyo ya mama yao. Wanahitaji kufahamu uhitaji wake wa kuwa na wakati wa faragha. Kuonyesha wepesi wa hisia kuelekea hali ya moyoni ya mama yao kutampelekea ujumbe wenye uhakikishio wa kwamba wao humjali kwelikweli. Kwa upande ule mwingine, kufanyia ucheshi hali yake ya kubadilika-badilika ghafula kutaharibu mambo hata zaidi. Uliza maswali yafaayo ili kuelewa vizuri zaidi kile kinachotendeka, na usaidie na kazi za nyumbani bila kuombwa kufanya hivyo. Hizo ni njia chache tu za kumtegemeza mama katika kipindi hiki maishani mwake.

Maisha Baada ya Komahedhi

Sura hii maishani mwa mwanamke imalizikapo, mara nyingi kuna miaka mingi iliyo mbele. Hekima na uzoefu ambazo amepata ni zenye thamani kubwa. Uchunguzi mbalimbali wa mtungaji Gail Sheehy wa “Wamarekani elfu sitini walio watu wazima ulithibitisha kwamba wanawake katika miaka yao ya hamsini, kulingana na yale waliojionea, walihisi wakiwa na hali njema zaidi kuliko jinsi walivyohisi katika sehemu nyingine yoyote maishani mwao iliyotangulia.”

Ndiyo, wanawake wengi ambao wamepitia miaka hii ya mabadiliko hupata mtazamo mpya. Uwezo wao wa kubuni hufanywa upya. Wanaendelea kuishi, wakijihusisha na utendaji wenye matokeo. “Naitendesha akili yangu. Naendelea kuchunguza mambo mapya na kujifunza,” akasema mwanamke mmoja ambaye amepita komahedhi. Yeye aliongeza hivi: “Huenda nikafanya mambo polepole zaidi, lakini sihisi kwamba huu ndio mwisho wa maisha yangu. Ninatazamia kwa furaha miaka mingi zaidi.”

Jambo la maana ni kwamba, katika kuwahoji wanawake, Sheehy alipata kwamba wale “ambao baada ya komahedhi wanakuwa na hali bora nao hujistahi zaidi ni wale wafanyao kazi ambamo akili, uamuzi, ubuni, au nguvu za kiroho zinathaminiwa hasa.” Kuna wanawake wengi wa jinsi hiyo ambao wamejitoa kwa furaha ili kupanua ujuzi na kuelewa kwao Biblia na wanaofundisha wengine kanuni zake zinazostahiki.—Zaburi 68:11.

Zaidi ya kudumisha mtazamo chanya kuelekea maisha na kufanya kazi yenye maana, wanawake wa umri zote ni wenye hekima kujikumbusha kwamba Muumba wetu mwenye upendo ajua hisia zetu na atujali kikweli. (1 Petro 5:7) Kwa kweli, Yehova Mungu ameandalia wote wanaomtumikia ili wafurahie maisha hatimaye katika ulimwengu mpya wenye uadilifu ambapo hakutakuwako tena ugonjwa, kuteseka, au hata kifo.—2 Petro 3:13; Ufunuo 21:3, 4.

Kwa hiyo, wewe unayepitia komahedhi, kumbuka kwamba hiyo ni sehemu ya maisha. Itapita, ikikuachia miaka ya maisha itakayokuwa yenye kuthawabisha sana ikitumiwa kwa faida katika kutumikia Muumba wetu mwenye upendo.

[Maelezo ya Chini]

a Amkeni! haipendekezi namna yoyote hususa ya tiba.

[Sanduku katika ukurasa wa 8]

Namna Gani Tiba ya Kurudisha Estrojeni?

Estrojeni yaweza kulinda dhidi ya ugonjwa wa moyo na osteoporosisi, ambavyo ni visababishi viwili vikuu vya maradhi katika wanawake ambao wamepitia komahedhi. Viwango vya estrojeni vipunguapo, maradhi haya huanza kusitawi nayo hudhihirika katika miaka mitano hadi kumi. Tiba ya kurudisha estrojeni au tiba ya kurudisha homoni (estrojeni na projesteroni) imependekezwa ili kuzuia magonjwa haya.

Kurudishwa kwa estrojeni kwaweza kupunguza kima cha kupoteza mifupa nako huzuia mwanzo wa ugonjwa wa moyo. Kuongeza projesteroni kwenye utaratibu wa kurudisha homoni hupunguza kutokea kwa kansa ya matiti na ya tumbo la uzazi lakini hupinga matokeo yenye manufaa ya estrojeni dhidi ya ugonjwa wa moyo.

Uamuzi wa ama kutumia ama kutotumia tiba ya kurudisha homoni lazima utegemee changanuo la hali, afya, na historia ya familia ya kila mwanamke.b

[Maelezo ya Chini]

b Ona Amkeni!, Septemba 22, 1991, kurasa 14-16 (Kiingereza).

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

Ni Chakula Kipi Kilicho Bora Zaidi?

Madokezo yafuatayo yamenukuliwa kutoka katika kitabu Natural Menopause—The Complete Guide to a Woman’s Most Misunderstood Passage, cha Susan Perry na Dakt. Katherine A. O’Hanlan.

Protini

• Punguza kiasi cha protini unachokula ili kisizidi asilimia 15 ya jumla ya kalori unazokula.

• Pata protini zako zaidi kutoka kwa mimea na kidogo zaidi kutoka kwa nyama.

Kabohidrati

• Kula kabohidrati zaidi zilizo tata, kama vile nafaka-dona, mikate, na pasta, maharagwe, njugu, wali, mboga, na matunda.

• Kula sukari kidogo zaidi na vyakula vichache zaidi vyenye kiasi kikubwa cha sukari.

• Kula chakula kingi zaidi kilichojaa makapi.

Mafuta

• Punguza jumla ya kiasi cha mafuta unachokula ili kisizidi asilimia 25 hadi 30 ya jumla ya kiasi cha kalori unazokula.

• Uzidipo kupunguza jumla ya kiasi cha mafuta unachokula, ongeza uwiano wa ‘mafuta mazuri’ (yaliyo rahisi kuyeyuka) kwa ‘mafuta mabaya’ (yaliyo magumu kuyeyuka).

Maji

• Kunywa bilauri sita hadi nane zenye kiasi cha aunsi nane kila siku.

Vitamini na Madini

• Kula mboga na matunda ya aina mbalimbali kila siku.

• Maziwa, vyakula vinavyotokana na maziwa, brokoli, na mboga za kijani-kibichi zenye majani ni vyanzo vizuri vya kalsiamu.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Kile washiriki wa familia waweza kufanya ili kusaidia: Kuonyesha shauku, kusaidia na kazi za nyumbani, kuwa msikilizaji mwangalifu, mara kwa mara kufanya mambo tofauti

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki