Kufunua Siri Zake
WANAWAKE wanapozeeka, komahedhi hutukia maishani mwao. Hata hivyo, imeeleweka vibaya sana. Kulingana na kitabu The Silent Passage—Menopause, wakunga wa karne ya 19 waliamini kwamba komahedhi “huvuruga mfumo wa neva wa mwanamke na hupokonya wanawake uvutano wao wa kibinafsi.”
Huko kufahamu kimakosa kwaendelea. Likiwa tokeo, wanawake wengi wanahofu na kuogopa tazamio la komahedhi. Kushinda matatizo ya kiakili yanayohusiana na hali hiyo kulirejezewa kuwa “mojapo mambo magumu zaidi maishani mwa mwanamke,” katika kitabu Natural Menopause—The Complete Guide to a Woman’s Most Misunderstood Passage.
Katika jamii ambamo ujana na sura ya ujana hukaziwa, mwanzo wa dalili za komahedhi huenda ukaleta kufahamu kimakosa huku: mwisho wa ghafula wa ujana na mwanzo wa uzee. Hivyo, wanawake wengine wamekuja kuhofu komahedhi kwa sababu hiyo yaonekana kuwakilisha mwanzo wa kipindi kipya cha maisha, kisichotamanika. Hata imeonwa na wengine kuwa “nusu kifo.”
Wanawake wa kisasa hawahitaji kuteseka kwa kutojua wanapopitia kipindi hiki cha maisha. Siri za komahedhi zinafunuliwa. Utafiti zaidi unafanywa, na tiba za kurahisisha badiliko hili zinasitawishwa. Magazeti, magazeti ya habari, na vitabu vinakazia habari hii, vikiandaa maelezo kwa maswali ambayo wengine waliona aibu kuuliza wakati mmoja. Taaluma ya kitiba pia, imepata habari zaidi juu ya matatizo ambayo huenda wanawake wakakabili.
Kwa nini habari hii yakaziwa uangalifu huu wote? Kwa sababu kuelewa komahedhi vizuri zaidi kwaweza kuondoa hofu, ushirikina, na kuvunjika moyo ambako huwapata wanawake wengi. Wanawake katika nchi nyingi wanaishi muda mrefu zaidi, nao wanataka kuvunja kile ambacho kimeonekana kuwa njama ya kutosema lolote juu ya habari hii na wanataka kupata habari zaidi. Wanataka majibu sahili, ya moja kwa moja. Na hilo lafaa, kwa kuwa wengi wao wana muda wa zaidi ya theluthi moja ya maisha yao kuishi baada ya komahedhi.
Vigezo vya takwimu za idadi ya watu katika Marekani vyatabiri ongezeko la asilimia 50 kwa muda wa miaka kumi ijayo katika idadi ya wanawake wenye umri wa komahedhi. Wanawake hao watamani kujua juu ya hatari za kiafya, lile joto la ghafula mwilini, kule kubadilika-badilika kwa hali ya moyoni, yale maumivu, na mabadiliko ya kimwili na ya kihisiamoyo. Kwa nini mambo haya hutendeka? Je, maisha ya utendaji wenye matokeo ya mwanamke huisha wakati wa komahedhi? Je, komahedhi hubadili utu wa mwanamke? Makala zifuatazo zitachunguza maswali haya.