Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 2/22 kur. 4-6
  • Kupata Uelewevu Mzuri Zaidi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kupata Uelewevu Mzuri Zaidi
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ilivyo
  • Wakati na Sababu Inayofanya Itukie
  • Mabadiliko Makubwa Maishani
  • Vipindi vya Mshuko-Moyo
  • Kipindi cha Maisha
  • Kukabiliana na Komahedhi
    Amkeni!—1995
  • Kukabiliana na Matatizo ya Kukoma kwa Hedhi
    Amkeni!—2013
  • Kufunua Siri Zake
    Amkeni!—1995
  • Kutii Maonyo ya Mwili
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 2/22 kur. 4-6

Kupata Uelewevu Mzuri Zaidi

“NISINGESEMA hicho ni kipindi chenye kupendeza sana maishani mwa mwanamke,” akakiri mwanamke mmoja aliyekuwa amepitia komahedhi, “lakini nafikiri waweza kujifunza kutokana nacho. Nimejifunza jinsi ya kustahi mipaka yangu. Mwili wangu ukihitaji kutunzwa au kupumzika kidogo zaidi, mimi huitikia na kuupa staha unaostahili.”

Uchunguzi wa wanawake ulioripotiwa katika gazeti Canadian Family Physician ulifunua kwamba “kutojua la kutazamia” kulikuwa ndilo jambo baya zaidi kuhusu komahedhi. Hata hivyo, wanawake waliokuja kuelewa komahedhi kuwa ni badiliko la asili walihisi “hangaiko, kushuka moyo, na kuudhika kidogo zaidi nao walikuwa wenye tumaini zaidi kuhusu maisha zao.”

Ilivyo

Kamusi Webster’s Ninth New Collegiate Dictionary hufasili komahedhi hivi: “Kipindi cha ukomo wa asili wa hedhi unaotukia kwa kawaida kati ya umri wa 45 na 50.” Komahedhi pia imetambulishwa hasa kuwa ukomo wa mwisho wa hedhi.

Kwa wanawake fulani, mwisho wa hedhi hutukia ghafula; kipindi kimoja cha hedhi humalizika na kingine hakitukii kamwe. Kwa wengine, hedhi inakosa kuwa na utaratibu fulani, ikitukia baada ya kipindi cha majuma matatu hadi miezi kadhaa. Mwaka mmoja mzima ukipita bila mwanamke kupata hedhi, yeye aweza kwa kufaa kukata maneno kwamba komahedhi ilitukia wakati wa hedhi yake ya mwisho.

Wakati na Sababu Inayofanya Itukie

Mwelekeo uliorithiwa, ugonjwa, mkazo, madawa, na upasuaji waweza kuathiri wakati wayo wa kutukia. Katika Amerika Kaskazini umri wa wastani ambao komahedhi hutukia ni karibu 51. Wakati inapotukia huwa kwa kawaida kati ya miaka ya mapema ya 40 hadi miaka ya katikati ya 50 na ni mara chache mno kutukia mapema zaidi ya hivyo au baadaye zaidi. Takwimu huonyesha kwamba wanawake wanaovuta sigareti huelekea kuwa na komahedhi ya mapema zaidi na kwamba wanawake walio wazito zaidi huelekea kuwa na komahedhi ya baadaye zaidi.

Wakati wa kuzaliwa ovari za mwanamke huwa na mayai yote atakayokuwa nayo wakati wote, yakiwa mamia ya maelfu kadhaa kwa idadi. Katika kila kawaida ya hedhi, mayai 20 hadi 1,000 hukomaa. Halafu yai moja, au zaidi ya moja pindi kwa pindi, huachiliwa na ovari na kuwa tayari kwa ajili ya utungishaji. Yale mayai mengine yaliyokomaa hufifia. Pia, kwa kupatana na utaratibu wa ukomavu kwa yai, viwango vya homoni, estrojeni na projesteroni kwa ukawaida huongezeka na kupungua.

Mwanamke apitapo miaka yake ya mwisho-mwisho ya 30, viwango vya estrojeni na projesteroni huanza kupungua, ama kidato kwa kidato ama bila utaratibu fulani, na huenda yai lisiachiliwe katika kila kawaida ya hedhi. Vipindi vya hedhi haviwi vya kawaida tena, mara nyingi vikitukia baada ya vipindi virefu zaidi; namna ya uzito wa mtiririko wa hedhi inabadilika, ikiwa nyepesi zaidi au nzito zaidi. Hatimaye mayai hayaachiliwi tena, na vipindi vya hedhi vinakoma.

Hedhi ya mwisho ni upeo wa utaratibu wa mabadiliko katika viwango vya homoni na utendaji wa kiovari ambayo huenda ikawa ilichukua muda wa kufikia miaka kumi. Hata hivyo, kiasi kidogo-kidogo cha estrojeni huendelea kutokezwa na ovari kwa muda wa miaka 10 hadi 20 baada ya komahedhi. Tezi adrenali na chembe-mafuta pia hutokeza estrojeni.

Mabadiliko Makubwa Maishani

Tishu zinazonyetishwa na estrojeni au zinazoitegemea zinaathiriwa kadiri kiwango cha estrojeni kipunguavyo. Joto la ghafula mwilini linafikiriwa hutokana na athari za kihomoni kwenye sehemu ya ubongo inayohusika na kurekebisha halijoto ya mwili. Jambo hasa lisababishalo hilo halijulikani, lakini yaonekana kwamba kipimo cha sehemu inayorekebisha joto mwilini huteremshwa ili halijoto zilizoonwa kuwa zenye kufaa zinakuwa zenye joto sana ghafula, na mwili hupatwa na joto ghafula na hutoa jasho ili kujipoesha.

Katika kitabu chake, The Silent Passage—Menopause, Gail Sheehy asema hivi: “Nusu ya wanawake wanaopatwa na joto la ghafula mwilini wataanza kupatwa nayo wanapokuwa bado na hedhi ya kawaida, mapema sana kuanzia umri wa miaka arobaini. Uchunguzi mbalimbali huonyesha kwamba wanawake walio wengi hupatwa na joto la ghafula mwilini kwa muda wa miaka miwili. Robo moja ya wanawake hupatwa nayo kwa muda wa miaka mitano. Na asilimia 10 hupatwa nayo baki la maisha zao.”

Katika wakati huu wa maisha ya mwanamke, tishu za uke huwa nyembamba zaidi na zenye unyevu kidogo zaidi kadiri viwango vya estrojeni vipunguapo. Dalili nyingine zinazowapata wanawake, asema Gail Sheehy, zaweza kutia ndani “mitoko ya ghafula ya jasho jingi usiku, kukosa usingizi, kutoweza kuzuia mkojo, vipindi vya ghafula vya kufura kiuno, viherehere vya moyo, kulia bila sababu yoyote, mifoko ya hasira, maumivu makali ya kichwa yanayosababisha kutapika, mwasho wa ngozi, [na] kusahau-sahau mambo.”

Vipindi vya Mshuko-Moyo

Je, kupungua kwa estrojeni husababisha mshuko-moyo? Swali hili limekuwa mada ya kujadiliwa sana. Jibu laonekana kuwa kwamba inafanya hivyo kwa habari ya wanawake fulani, kama vile wale waliokuwa na mabadiliko-badiliko katika hali ya moyoni kabla ya vipindi vyao vya hedhi na wale ambao hukosa usingizi kwa sababu ya mitoko ya ghafula ya jasho jingi usiku. Wanawake katika kikundi hiki huonekana kuwa wenye hisia nyepesi kuelekea athari za kihisiamoyo za mabadiliko-badiliko ya kihomoni. Kulingana na Gail Sheehy, kwa kawaida wanawake hawa “hupata kitulizo kikubwa wanapofikia kipindi cha baada ya komahedhi” na viwango vya homoni vinasawazika.

Dalili zilizo mbaya zaidi zaelekea kuwapata wanawake wanaofikia komahedhi ghafula kwa sababu ya mnururisho, tibakemili, au kuondolewa ovari zote mbili kwa upasuaji. Taratibu hizi zaweza kusababisha mshuko wa ghafula wa viwango vya estrojeni na hivyo kuanzisha dalili za komahedhi. Madawa ya kurudisha estrojeni yaweza kuamriwa katika hali hizi, ikitegemea afya ya mwanamke.

Kiwango cha maumivu na aina ya dalili zinazompata mtu hutofautiana sana kutoka mwanamke mmoja hadi mwingine, hata miongoni mwa wanawake wenye ukoo mmoja. Hii ni kwa sababu viwango vya homoni hutofautiana kutoka mwanamke mmoja hadi mwingine na hupungua kwa kadiri zinazotofautiana. Kwa kuongezea, wanawake huwa na hisiamoyo, mikazo, uwezo mbalimbali wa kukabiliana, na matazamio tofauti-tofauti wanapofikia komahedhi.

Mara nyingi komahedhi hutukia wakati uleule ambao hali nyingine zenye mkazo maishani mwa mwanamke hutukia, kama vile kutunza wazazi waliozeeka, kuanza kazi ya kuajiriwa, kuona watoto wakikua na kuondoka nyumbani, na marekebisho mengine ya kipindi cha katikati cha maisha. Mikazo hiyo huenda ikasababisha dalili za kimwili na za kihisiamoyo, kutia ndani kupoteza kumbukumbu, kasoro za makini, kuhangaika, kuudhika, na kushuka moyo, ambazo huenda zikaonwa kimakosa kuwa zinasababishwa na komahedhi.

Kipindi cha Maisha

Komahedhi si mwisho wa maisha ya utendaji wenye matokeo ya mwanamke—ni mwisho tu wa maisha yake ya uzazi. Baada ya kipindi cha hedhi cha mwisho cha mwanamke, kwa kawaida hali yake ya moyoni husawazika zaidi, ikiacha kubadilika-badilika kwa sababu ya kawaida za homoni za kila mwezi.

Ingawa tumekazia ukomo wa hedhi kwa sababu ni badiliko la wazi, hilo ni dhihirisho tu la utaratibu wa badiliko mwanamke aachapo wakati wa uzazi wa maisha yake. Ubalehe, uja-uzito, na kuzaa mtoto ni nyakati za badiliko pia zinazoambatana na mabadiliko ya kihomoni, ya kimwili, na ya kihisiamoyo. Basi, komahedhi ni wakati wa mwisho, lakini si wakati pekee, wa mabadiliko yenye kusababishwa na homoni maishani mwa mwanamke.

Hivyo, komahedhi ni kipindi cha maisha. “Labda,” akaandika aliyekuwa mhariri mkuu wa Journal of the American Medical Women’s Association, “watu wataacha kuona komahedhi kuwa hali ngumu, au hata kuwa ‘lile badiliko,’ na kuiona kwa kufaa zaidi kuwa ‘badiliko jingine tena.’”

Kwa kutumainisha, kitabu Women Coming of Age chasema kwamba mwisho wa uwezo wa kuzaa wa mwanamke “ni jambo la asili na lisiloepukika kama vile mwanzo wake uliopangwa kimbele. Kufikia komahedhi kwa kweli ni ishara ya kuwa mwenye afya kimwili—ishara ya kwamba saa ya mwilini [mwake] inafanya kazi vema.”

Lakini, nini kiwezacho kufanywa ili kulifanya badiliko hili liwe rahisi iwezekanavyo? Na mwenzi wa ndoa na washiriki wa familia wanaweza kuwaje wenye kutegemeza wakati wa badiliko hili maishani? Makala ifuatayo itazungumzia mambo haya.

[Picha katika ukurasa wa 6]

Mara nyingi komahedhi hutukia wakati uleule ambao hali nyingine zenye mkazo hutukia, kutia ndani kutunza wazazi waliozeeka

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki