Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g92 9/8 kur. 23-25
  • Kutii Maonyo ya Mwili

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutii Maonyo ya Mwili
  • Amkeni!—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ishara Zenye Kuonya
  • Uangalie Ishara
  • Wakati wa Vipindi Hivyo vya Pekee
  • Kumweleza Binti Yako Kuhusu Hedhi
    Amkeni!—2006
  • Hedhi
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Kupata Uelewevu Mzuri Zaidi
    Amkeni!—1995
  • Kwa Nini Hili Linaupata Mwili Wangu?
    Amkeni!—1991
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1992
g92 9/8 kur. 23-25

Kutii Maonyo ya Mwili

Na mleta habari za Amkeni! katika Ailandi

KWA Una na mume wake, Ron, ono hilo lilikuwa lenye kuogopesha na lenye kutia uchungu. Usiku mmoja wenye baridi wa Januari, Una alizirai. Ron alimwita daktari, aliyefikiri kwamba tatizo lilikuwa kutosawazika kwa hormoni kulikoathiri ovari (mifuko ya mayai) zake na akaagiza apelekwe hospitali. Ron alimpeleka kwa gari mke wake—aliyekuwa akipoteza damu na alikuwa na uchungu mwingi—kupitia njia za milimani zisizo na mwangaza na zenye miinuko-miinuko, kuelekea hospitali iliyokuwa umbali wa kilometa 80.

Hata hivyo, hospitali hiyo haingeweza kushughulikia tatizo hilo, kwa hiyo alihamishwa kwenye hospitali kubwa na ya ki-siku-hizi iliyokuwa karibu. Humo yeye alipasuliwa kwa mafanikio na akafanya maendeleo mazuri.

Ron na Una walikuwa wenye shukrani kwa wafanyakazi wa hospitali kwa ustadi na utunzi wao uliookoa maisha ya Una. Walipokuwa wanatoa shukrani hizo kwa daktari wa nusukaputi, yeye [daktari] alisema jinsi alivyokuwa mwenye furaha kwa vile mambo yalivyofanikiwa. Ndipo akatoa elezo la kupendeza: “Ni mara chache sana ambapo matatizo ya viungo vya uzazi vya wanawake hutokea ghafula. Mengi ya magonjwa hayo huonyesha ishara mapema.” Yeye alimaanisha nini?

Ishara Zenye Kuonya

Una aeleza kwamba alikuwa amepata matatizo miaka miwili iliyopita. Wakati wa hedhi, alikuwa akitokwa na damu wakati ule tu alipofanya kazi nzito, na mara nyingi ilikuwa mgandamano wa damu. Yeye asema: “Ningalipaswa nitafute ushauri wa kitiba, lakini sikushughulika, nikifikiri kwamba labda nilikuwa ninaacha kupata hedhi mapema maishani. Lakini ndipo katika Januari, kipindi changu cha hedhi kilikoma baada ya siku mbili, na siku tatu baadaye kilianza tena kwa kutokwa na damu nyingi sana na migandamano mikubwa ya damu. Sikupata wasiwasi kweli kweli, lakini kwenye siku ya pili, nililazimika kuwa kitandani, kwani nilihisi vibaya sana. Lakini bado, hatukuita daktari. Usiku huo ndio niliolazimika kukimbizwa hospitali.”

Je! tatizo lake lingaliweza kuzuiwa lisikue na kuwa hali ya dharura yenye kutisha uhai? Una anafikiri kwamba labda lingalizuiwa kama angejua jambo la kuangalia na kama angalichukua hatua bila kuchelewa. Kwa kusikitisha, yeye asema, “kama wanawake wengi, mimi nyakati zote nilipuuza jambo lolote linalohusiana na hedhi, bila kulichukua kwa uzito.” Hata hivyo, dalili za ugonjwa za Una zilikuwa zile za ugonjwa wa ovari ambazo kwa kweli zilihitaji kushughulikiwa mara moja.

Kila mwezi wanawake wenye umri wa kuzaa watoto huwa wana kionyeshi cha hali ya afya yao kwa ujumla: hedhi ya kawaida. Hali yoyote isiyo ya kawaida ni ishara ya onyo. Katika visa fulani, kuchelewa kutii onyo hilo kwaweza kumaanisha ama matibabu ya kila wakati ama upasuaji.

Kwa nini, basi, ishara hizo hupuuzwa mara nyingi au kuonwa kuwa si kitu? Katika familia nyingi, mke ndiye anayepanga milo ya familia, anayetoa dawa, na kuchunguza afya ya familia. Katika kufanya hivyo, huenda akaachilia mbali matatizo yake mwenyewe. Labda, kama katika kisa cha Una, yeye hana uhakika kuhusu maana ya dalili zake za ugonjwa. Au yaweza kuwa kwamba pesa za utunzaji wa kiafya hazitoshi, na anawapa watoto na mume wake mahali pa kwanza, akitumaini kwamba tatizo lake litakwisha kwa njia fulani. Huenda akahofu, akipendelea hali yake ya sasa isiyostarehesha kuliko wazio la tatizo lenye kutamausha akiwa hospitalini. Huenda yeye pia akawa mama mfanyakazi, asiyeweza au asiyetaka kuenda kupumzika kwa faida ya afya yake mwenyewe.

Madaktari husema kwamba katika visa vingi, mke anaachwa ashughulikie matatizo yake mwenyewe ya kiafya. Huenda mume wake akawa hahangaishwi sana na “matatizo ya wanawake.” Hata hivyo, waume wanaowapenda wake zao watajifunza juu ya mambo kama hayo ili waweze kushughulikia hali njema ya wake zao. Biblia huwahimiza wanaume: “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe.” (Waefeso 5:28, 33) Kwa hiyo, waume na wazazi wanaweza kusaidiaje wake na binti zao kuepuka hali za dharura zisizohitajiwa?

Uangalie Ishara

Uwe macho kwa matukio yasiyo ya kawaida ambayo huenda yakawa ndiyo ishara za kuonya. Kwa mfano, kutokwa damu kusiko kwa kawaida na usaha, ingawa si lazima kuambatane na uchungu, kwapaswa kuchunguzwa.a Ndivyo na uchovu usio wa kawaida, kuvuja damu sana, na matatizo ya kuenda haja ndogo. Hayo yaweza kuwa ishara za uvimbe wenye vichembechembe kama nyuzinyuzi katika mji wa mimba, ambao hutibiwa vyepesi zaidi ukigunduliwa mapema.

Jambo lisilo la kupuuzwa ni maumivu ya mgongo yenye kurudia-rudia, kuhisi msongo kwenye uke, au kukosa mkojo wakati wa haja. Hayo yaweza kutoa ishara za hali ambayo wakati mwingine yaweza kurekebishwa mapema kwa kufanya mazoezi lakini ambayo inaweza kuhitaji upasuaji baadaye.b

Zaidi ya kuchukua hatua baada ya ishara hizo kutokea, wanawake wenye umri zaidi ya miaka 25 wangefanya vema kuchunguzwa na daktari kwa ukawaida, uchunguzi zaidi ukifanywa kwa matiti na viungo vya tumboni na nyongani. Hilo laweza kufanywa kila baada ya miaka miwili au mara nyingi kadiri historia ya familia na afya ya kibinafsi ya mwanamke ionyeshavyo.

Wakati wa Vipindi Hivyo vya Pekee

Kumbuka pia zile sehemu tatu katika maisha ya mwanamke ambapo wale wanaompenda wanapaswa kumpa uangalifu wa pekee: hedhi inapoanza kwa mara ya kwanza; kuzaa mtoto; na hedhi inapokoma. Wakati wa kila sehemu hizo, hali zaweza kuzuka ambazo ushauri wa haraka wa daktari au matibabu yaweza kuondoa hali ya dharura.

HEDHI INAPOANZA KWA MARA YA KWANZA: Wasichana wachanga wanahitaji elimu ya afya kuwasaidia waelewe jinsi miili yao inavyotenda kazi na ili wasione kule kutokwa na damu wakati wa hedhi kuwa fumbo. Wazazi, na hasa akina mama, wanapaswa kuwa na mazungumzo ya kinaganaga na ya wazi na binti zao. Ikiwa kuna tatizo, wasichana hawapaswi kuachwa wakishangaa ni nini kimewapata au wakihisi kuwa ni lazima wavumilie hedhi nzito sana au maumivu makali katika kipindi hicho cha mwezi. Ikiwa wazazi wao hawawezi kusaidia, labda mwanamke rafiki aliye wa umri mkubwa zaidi aweza kutoa mwongozo kuhusu ushauri unaofaa wa kitiba.

Mwanamke mchanga aweza kujuaje kama vipindi vyake ni vya kawaida? Kwa mtu yule yule, vinaweza kubadilika-badilika. Vipindi vya hedhi visivyopatana ni jambo la kawaida katika miezi sita ya kwanza kufikia mwaka mmoja (au hata miaka miwili katika visa fulani) baada ya hedhi kuanza kwa mara ya kwanza na mara nyingi huwa ni kwa sababu ya mabadiliko madogo ya hormoni. Ikiwa baada ya miaka hii ya mapema, kunakuwa mabadiliko ya mara kwa mara katika muda wa kipindi cha hedhi au katika namna ya kutokwa damu, hiyo huonwa kuwa jambo la kawaida. Jambo zaidi ya hilo laweza kuwa ishara ya onyo inayohitaji uchunguzi wa kitiba.

Sehemu moja ya elimu ya afya inahusu ulaji. Vyakula visivyofaa mwili, vinavyokazia ladha badala ya ulishaji bora, na kuhangaishwa kupita kiasi kuhusu uzito, mara nyingi huzuia wasichana matineja wasipate kiasi kingi cha vyakula vinavyofaa kwa mwili, hasa kalisiamu na chuma. Wanawake wachanga ambao hawajaanza kupata vipindi vya hedhi vya kawaida mara nyingi huwa na kiasi kikubwa cha kupoteza damu kuliko ilivyo kawaida wakati wa hedhi, na hilo huongeza uhitaji wa chuma. Kwa hiyo ni jambo la maana kula vyakula vya aina mbalimbali na kuepuka wingi wa vyakula vya kutengenezwa. Wakati mwingine huenda viongeza chuma vikapendekezwa.

KUZAA MTOTO: Madaktari wa uzalishaji watoto hupendekeza uchunguzi wa mapema wa wanawake wajawazito kabla hawajazaa. Wanaweza kuchunguza damu kuona kama kuna uhitaji wa chuma au asidi jani. Kwa kuwa mwanamke mjamzito anaelekea zaidi kuvuja damu, kutii ishara za maonyo ni kwa maana hata zaidi.

Kutokwa na damu hata iwe kwa kiasi kidogo jinsi gani wakati wa kuwa mjamzito hutaka uchunguzi wa kitiba. Ishara nyingine za kuonyesha hatari wakati huu ni maumivu ya kiuno, viishara vya damu katika mkojo, na maumivu wakati wa haja ndogo. Lakini hali yoyote isiyo ya kawaida au dalili za ugonjwa zapaswa kuripotiwa mapema kwa daktari wa uzalishaji watoto. Pesa zinapopunguka, mume ana daraka la pekee kwa afya na maisha ya yule ambaye amekuwa “mwili mmoja” pamoja naye, si kuacha maisha yake yaelekee hatarini.—Mathayo 19:5, 6; Waefeso 5:25.

HEDHI INAPOKOMA (MENOPAUSE): Huo ndio usemi wa kitiba kwa kikomo kamili cha vipindi vya hedhi vya kawaida. Wakati huu huwa ni wa mabadiliko ya maisha, na ni sehemu ya asili katika maisha ya wanawake. Katika maana iliyo kubwa zaidi, hilo limekuja kumaanisha miezi au hata miaka kabla na baada ya tukio hilo la asili. Wanawake wengi hupata dalili za kimwili zisizostarehesha wakati huo—kama vile hedhi isiyo ya kawaida na kupata wekundu mwilini—lakini yote hayo yatakoma hatimaye. Ikiwa kutokwa damu kunaendelea kwa muda mrefu au kunapita kiasi au kipindi kingine cha kutokwa damu kinatokea miezi sita au zaidi baada ya kile kilichoonekana kuwa cha mwisho, yapasa daktari aonwe mara hiyo.

Ni kweli, si hali zote za dharura zinazoweza kushughulikiwa kwa wakati ufaao. “Wakati na tukio lisilotazamiwa” hutupata sote. (Mhubiri 9:11, NW) Lakini, kama vile daktari wa nusukaputi alivyomwambia Una: “Ni mara chache sana ambapo matatizo ya viungo vya uzazi vya wanawake hutokea ghafula.” Elimu ifaayo ya afya na kutambua jinsi mwili uitikiavyo kwaweza kuwalinda wanawake wasipatwe na hali ya dharura ya viungo vya uzazi. Ni afadhali kuzuia hali ya dharura kuliko kupuuza maonyo mpaka hali ya hatari inapokabiliwa. Kwa hiyo, wake na waume, tiini maonyo ya mwili!

[Maelezo ya Chini]

a Katika visa fulani, ingawa si vyote, hizo zaweza kuwa ishara za kansa ya shingo la mji wa mimba, ambayo, katika visa vilivyo vingi, huweza kutibiwa ikigunduliwa mapema.

b Kushuka kwa mji wa mimba.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mume mwenye huruma aweza kumsaidia mke wake atii maonyo ya mwili wake

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki