HEDHI
(hedhi)
Pindi ambapo damu, umajimaji, na mabaki ya tishu kutoka katika mji wa mimba wa mwanamke. Kwa kawaida mwanamke hupatwa na hedhi kila mwezi, kila baada ya majuma manne hivi. Wasichana huanza kupata hedhi wanapobalehe, na hali hiyo huendelea kwa ukawaida mpaka wakati wa kukatika kwa hedhi huku kila mzunguko wa hedhi ukidumu kati ya siku tatu mpaka tano.
Maandiko yanahusianisha hedhi na uchafu na kutokuwa safi (Law 12:2; Eze 22:10; 36:17), neno la Kiebrania linalohusiana nalo ni (nid·dahʹ) mara nyingine hutafsiriwa ‘uchafu wa hedhi.’ (Law 15:25, 26) Neno lingine la Kiebrania linalotafsiriwa, da·wehʹ, ambalo linaweza kumaanisha ugonjwa (Omb 5:17), hutafsiriwa “mwanamke asiye safi kwa sababu ya hedhi.” (Law 15:33; Isa 30:22) Usemi “desturi ya wanawake imenijia” unamaanisha hedhi.—Mwa 31:35; maelezo ya chini.
“Si Safi” Chini ya Sheria. Kulingana na Sheria ya Musa, mwanamke hakuwa safi kwa siku saba alipokuwa katika hedhi ya kawaida. Kitanda au vyombo vyovyote ambavyo mwanamke mwenye hedhi alikalia au kulalia vilionwa kuwa si safi pia. Mtu yeyote aliyemgusa au aliyegusa vitu alivyofanya kuwa si safi alipaswa kufua mavazi yake na kuoga, na mtu huyo hangekuwa safi mpaka jioni. Ikiwa mwanamume aliguswa na uchafu wa hedhi wa mwanamke aliyelala naye (huenda bila kukusudia, mume akafanya ngono na mke wake mwanzoni mwa hedhi), mwanamume huyo hangekuwa safi kwa siku saba, na kitanda alicholalia kilionwa pia kuwa si safi.
Mwanamke alionwa pia kuwa si safi ikiwa atatokwa na damu kwa siku nyingi au “akitokwa na damu kwa muda unaozidi kipindi chake cha hedhi,” kitanda chochote alicholalia na kitu chochote anachokalia pamoja na watu aliwagusa watakuwa si safi. Baada ya damu kukoma kutoka kwa muda unaozidi wa kawaida, alipaswa kuhesabu siku saba, kisha angekuwa safi. Katika siku ya nane, mwanamke huyo angeleta njiwa tetere wawili au hua wawili wachanga na kumpatia kuhani aliyetoa dhabihu kwa niaba yake, na kumtoa ndege mmoja kwa Yehova kama dhabihu ya dhambi na mwingine kama dhabihu ya kuteketezwa.—Law 15:19-30; tazama SAFI, USAFI.
Ikiwa mwanamume na mwanamke wangefanya ngono kimakusudi huku mwanamke akiwa kwenye hedhi, wote wawili walipaswa kuuawa. (Law 18:19; 20:18) Huenda sheria ya kutofanya ngono wakati wa hedhi ilichangia afya bora, na huenda hata kuzuia maumivu katika eneo la viungo vya uzazi. Huenda Waisraeli walikumbushwa pia kuhusu utakatifu wa damu na masharti ya Sheria yaliyohusu hedhi au kutoka kwa damu. Sheria hizi hazikuwekwa ili kuwabagua wanawake, kwa kuwa wanaume pia walitokwa na umajimaji na kuwa si safi. (Law 15:1-17) Kanuni hizo kuhusu hedhi zilionyesha kwamba Yehova anawathamini wanawake. Ingawa mume Mkristo hayuko chini ya Sheria (Ro 6:14; Efe 2:11-16), anapaswa kufikiria hali za mke wake zinazobadilika na kalenda ya hedhi, akikaa naye “kulingana na ujuzi” na akimpa heshima “kama chombo dhaifu zaidi, yaani mwanamke.”—1Pe 3:7.