Jinsi Chakula Kijengacho Mwili Kiwezavyo Kuboresha Afya Yako
NI SHANGWE iliyoje kumtazama mtoto aliyelishwa vizuri! Hata hivyo mtoto mwenye afya hatokei tu mwenyewe. “Sikuzote chakula sahili lakini chenye lishe kilikuwa jambo la kutangulizwa katika familia yetu si tu katika matumizi ya kifedha bali pia katika wakati uliotumiwa kukitayarisha na kukifurahia pamoja,” akumbuka Kate, Mkanada anayeishi Brazili. “Kwa sababu mama yangu hakuwa akifanya kazi ya mshahara, kila siku tungekaribishwa nyumbani tukitoka shuleni na harufu tamu ya mlo mkuu uliokuwa ukitayarishwa na labda kashata au keki aliyokuwa ameoka.”
Hata hivyo, badala ya kutegemezwa na chakula chenye kujenga, “watu wapatao [milioni] 780 katika nchi maskini, mmoja katika kila watu watano, hawapati chakula cha kutosha,” kulingana na The Economist. “Watu wengi kufikia bilioni 2 wanaopata vya kutosha kujaza matumbo yao hata hivyo hukosa vitamini na madini wahitajiyo.” Hakika hizo huonyesha si kwamba tu mtu asiye na lishe nzuri adhoofishwa bali pia ana machache mno ya kufaidi wengine nayo. Hivyo basi, kuhusu watoto wasio na lishe nzuri, mwanauchumi Eduardo Giannetti da Fonseca wa Chuo Kikuu cha São Paulo, Brazili, alinukuliwa akisema hivi: “Huu [upotezo wa maliasili ya wanadamu] ni mbaya kuliko wowote ule. . . . Ninaamini kwamba miongoni mwa watoto hawa mna vipawa na uwezo ambao huishia ukingoni kwa sababu ya umaskini. Miongoni mwao, chini ya hali tofauti, kungeweza kutokea Albert Einstein fulani.” Gazeti Veja hutaarifa hivi: “Nchi inapoteza uwezo ambao unamomonyoka kwa sababu ya lishe mbaya na unatapanya hifadhi iwezayo kutokeza mahiri, ubuni, na nishati.” Kwa hivyo, kujapokuwa gharama za juu za kuishi, wazazi wenye hekima watawapa watoto wao msingi ulio imara kwa kutoa chakula chenye lishe.
Masurufu Yenye Hekima
“Kusurufu” humaanisha “kutumia kwa ajili ya faida au manufaa za wakati ujao.” Waweza kusurufuje katika ulishaji? Ikihitajika, je, ungefutilia mbali anasa au bidhaa za hali ya juu na kutumia fedha zako kidogo ili kununua chakula chenye kujenga?
“Hisi hazilali kimya mpaka zitakapochochewa mara wakati wa kuzaliwa; uthibitisho wadokeza kwamba mfumo wa hisi hutenda vizuri kabla ya kuzaliwa,” yasema The New Encyclopædia Britannica. Hivyo, njia nzuri ya kuanza kulisha mtoto ni kuwa na mama aliyelishwa vizuri. Hatua ifuatayo—baada ya kuzaa—ni kitoto kunyonya, kwani maziwa ya mwanadamu huandaa lishe kamili na hata hukinga mwili dhidi ya maradhi ya kawaida. Kichapo cha Umoja wa Mataifa, Facts for Life hutaarifu hivi: “Kwa miezi michache ya kwanza ya maisha ya mtoto, maziwa ya matiti pekee ndicho chakula na kinywaji bora zaidi kiwezekanacho. Vitoto huhitaji vyakula vingine, zaidi ya maziwa ya matiti, vikiwa na umri wa miezi minne hadi sita.”
Ingawa mwili wa mwanadamu hustahimili, kwa njia ya ajabu haupaswi kuchukuliwa vivi hivi tu. Ni muhimu kuujenga kwa chakula chenye kujenga mapema maishani. The World Book Encyclopedia husema hivi: “Kufikia wakati mtu ana umri wa miaka 6, ubongo huwa umefikia uzani wao kamili wa pauni 3 (kilogramu 1.4). Chembe zilizo nyingi za ubongo huwepo wakati wa kuzaliwa, na hivyo ongezeko la uzani hutokea hasa kutokana na ukuzi wa chembe hizo. Wakati wa kipindi hiki cha miaka sita, mtu hujifunza na hupata vigezo vya tabia mpya kwa kiwango cha haraka sana maishani.” Hivyo basi, hata ikiwa mtoto anapata lishe nzuri baada ya mwaka wa sita, kwa kukadiria ni chembe chache zitakazokuzwa. Kate alionelea hivi: “Chakula chenye kujenga, chenye lishe ni mojapo ya zawadi kubwa kuliko zote ambayo wazazi waweza kuwapa watoto wao. Hata ikiwa nyingi za zile ziitwazo mahitaji ya maisha, ambayo kwa kawaida ni anasa, hayawezi kuandaliwa, wazazi wasurufuo katika afya ya kiakili na ya kimwili ya watoto wao wawapa mwanzo maishani kutoka utotoni ambao kamwe haubanduliwi.”
Kwa Nini Uwe na Unamna wa Mlo?
Mtoto huhitaji chakula chenye protini nyingi ili kukua kimwili na kiakili. Lishe mbaya hupunguza ukuzi wa kiakili wa mtoto shuleni, na huenda mtoto awe baridi na mchovu, asiyeweza kutoa uangalifu au kukumbuka kinachofunzwa. Angalau maradhi 25 ya ukosefu wa lishe bora hutokana na ukosefu wa mojapo ya virutubisho vya msingi—protini, vitamini, shahamu zihitajiwazo, au virutubisho vya madini.
Fikiria kisa cha Joaquim. “Familia yetu ilikuwa maskini.” akasema. “Lakini tulikuwa na shamba na tulikuza karibu kila kitu tulichokula. Katika kila mlo tulikula mahindi na mkate wa rai uliotengenezwa kutokana na nafaka-dona, na hiyo ilichangia lishe bora. Karibu kila siku mama yangu alitengeneza supu iliyotia ndani unamna wa mboga, kutia ndani maharagwe, na hii iliandaa mengi ya mahitaji yetu ya kilishe. Hatukula nyama mno, bali tulikula samaki, sana sana sadini, chewa, na heringi.” Yeye aongezea hivi: “Mama yangu alikuwa na watoto watano, na sikumbuki mmoja wetu akiwa mgonjwa isipokuwa homa na mafua. Nafikiri kwamba milo yetu iliyosawazishwa vizuri ilichangia hilo.” Mama fulani wa watoto saba aeleza hivi: “Tulihitaji kuandaa chakula chenye ulishaji kwa gharama ndogo. Hivyo tulipanda kishamba cha mboga, ambacho, ingawa kilikuwa kidogo, kilitokeza mboga za kutosha kwa ajili ya mahitaji yetu.” Yeye aongezea hivi: “Watoto wetu kamwe hawakupata kuwa na magonjwa mabaya sana na sikuzote walifanikiwa sana katika kazi yao ya shule.”
Mwili wako hutaka lishe 22 kati ya elementi za kikemikali 103 zitambulikanazo kirasmi. Ingawa haiwezekani kuamua kiasi hususa cha vitamini, madini, na protini uhitajicho wewe peke yako, mlo uliosawazishwa vizuri utaandaa mahitaji yako. Mamlaka moja ilitaarifu hivi: “Ufunguo wa lishe bora ni unamna wa mlo unaotia ndani kila aina ya virutubisho.”
Na vipi ikiwa watoto wako hawataki aina fulani ya vyakula, kama vile mboga zilizo na ladha chungu? Kulingana na mpishi fulani mzoefu, wazazi wapaswa kuandaa “aina zote za mboga zipatikanazo katika eneo lao. Watu wazima wengi hawali mboga kwa sababu hawakuzizoelea walipokuwa watoto. Kwa sababu mboga huandaa nyuzi-nyuzi na mengi ya mahitaji yetu ya vitamini na si ghali, wazazi wapasa sikuzote kuwa nazo kwa ajili ya watoto wao.” Kwa hivyo kwa nini usijifunze mapishi mapya yatumiayo vizuri mboga na matunda, labda ikipakuliwa pamoja na kitoweo kitamu? Kuhusu zile ziitwazo kalori tupu, yeye adokeza hivi: “Wazazi hawapasi kuwa na tamu-tamu nyumbani isipokuwa wakati wa pindi za pekee. Ikiwa [watoto] hawana hizo, hawatazila.”
Ingawa kula kiasi kitoshacho cha chakula kifaacho hupunguza hatari ya utapiamlo, watu fulani hujiletea matatizo wenyewe kwa kula mno. Ulaji mwingi wa kalori zizidizo mahitaji ya mwili huenda yakunenepeshe mno, ambako kunahusianishwa na ugonjwa wa kisukari na matatizo ya moyo.a Kwa sababu wala dawa wala mazoezi ya kimwili hayawezi kuchukua mahali pa mazoea mazuri ya ulaji, dokezo zuri ni kupunguza ulaji wa mafuta, tamu-tamu, chumvi, na alkoholi. Pia, ensaiklopidia moja yasema, “hatua zapasa kuchukuliwa ili kupunguza njaa, upweke, kushuka moyo, ukimwa, hasira, na uchovu, ambazo kila mojapo hutokeza ulaji mno.”
Mtazamo Uliosawazika wa Chakula na Afya
Biblia si kitabu cha lishe; hata hivyo, hutusaidia ili kuwa na usawaziko katika mambo ya afya. Mtume Paulo alionya dhidi ya wale waamrishao wengine “wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.” (1 Timotheo 4:3) Mungu atutaka turidhike na tutumie vizuri kinachopatikana. “Kuwa na mali chache pamoja na kumcha BWANA; ni bora kuliko mali nyingi na taabu.”—Mithali 15:16.
Hakuna yeyote leo afurahiaye afya kamili. Hivyo kwa nini ukose kiasi, wala kutofikiria wala kuhangaika sana? Tamaa kubwa au mapendezi ya kupita kiasi katika lishe au mambo ya afya yaweza kutusababisha tukose usawaziko.
Tujapojitahidi kutunza afya yetu, jinsi mambo yalivyo sasa, hatimaye tutazeeka na kufa. Ingawa, kwa furaha Biblia yatuhakikishia kwamba Ufalme wa Mungu utamaliza utapiamlo na maradhi. Hata ingawa mipango ya mwanadamu ya kuondoa njaa imeshindwa, tunaweza kutazama mbele kwenye ulimwengu ulio na chakula chenye lishe kwa wote.—Zaburi 72:16; 85:12.
[Maelezo ya Chini]
a “Wastadi fulani huhisi kwamba umenenepa mno ikiwa utazidi uzani ‘utamaniwao’ . . . wa kimo chako, mwili na umri kwa zaidi ya asilimia 20.”—The American Medical Association Family Medical Guide, ukurasa 501. Pia ona Amkeni! la Mei 8, 1994, “Vijana Huuliza . . . Naweza Kupunguzaje Uzito?” na Mei 22, 1989, (Kiingereza), “Je, Kupunguza Uzito Ni Kusikowezekana?”‹c g92 12/8 8›
Sanduku katika ukurasa wa 7]
MADOKEZO ILI KUSAIDIA MTOTO WAKO AWE NA MAZOEA MAZURI YA KULA
◻ Weka mfano mzuri.
◻ Usiruhusu watoto wale kile tu wanachopenda.
◻ Epuka kuwa na chakula kisichofaa mwili au tamu-tamu nyumbani.
◻ Wazoeze watoto kuthamini vyakula vya aina tofauti.
◻ Uwe na saa kamili kwa ajili ya milo, kutia ndani kiamsha-kinywa.
◻ Usiruhusu matangazo ya televisheni yaongoze kile ulacho.
◻ Usiwaruhusu watoto wajichukulie chakula katika friji.
◻ Wazoeze watoto kutayarisha chakula.
◻ Sitawisha uthamini kwa ajili ya maandalizi ya kila siku.