Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 3/8 kur. 3-4
  • Chakula Chako ni Chenye Lishe Kadiri Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Chakula Chako ni Chenye Lishe Kadiri Gani?
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Fedha Hazitoshi
  • Jinsi Chakula Kijengacho Mwili Kiwezavyo Kuboresha Afya Yako
    Amkeni!—1995
  • Visababishi Vilivyotia Mizizi, Athari Mbaya za Utapiamlo
    Amkeni!—2003
  • Chakula cha Kutosha kwa Wote!
    Amkeni!—1995
  • Vyakula Bora Unavyoweza Kupata
    Amkeni!—2002
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 3/8 kur. 3-4

Chakula Chako ni Chenye Lishe Kadiri Gani?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI

Wewe huchaguaje chakula chako? Unaponunua chakula, ni mambo gani hukuongoza? Je, ni kujaza kikapu tu? Je, ni bei? Je, vifaa vya kukitayarisha? Je, ni madai yenye ushawishi katika matangazo ya biashara? Au tu ni jinsi chakula kinavyoonekana au ladha yacho? Kufanya machaguo yanayofaa huenda kuamue kama unakula chakula chenye lishe au kisicho na lishe, kama afya yako inakuwa bora ama inaharibiwa.

UMASKINI ni kisababishi kikubwa cha utapiamlo. Wakati wengi wanapokichukua chakula vivi hivi tu, mamilioni mengine hufurahia mlo wenye lishe mara haba mno. “Hapa nyumbani sisi hula chochote kinachopatikana,” akasema mwashi mmoja Mbrazili, aliye baba wa watoto sita. Kwa kawaida hiyo yamaanisha mkate usio na ladha na kahawa chepechepe au wali na maharagwe. Kwa kweli, kulingana na ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa, la Chakula na Kilimo asilimia 20 ya idadi ya watu ulimwenguni huteseka kwa njaa. Kujapokuwa uenezi mkubwa wa njaa katika baadhi ya nchi za Afrika, kuna idadi kubwa ya watu wenye njaa katika Asia. Hata katika Marekani, asilimia 12 ya watu, au watu milioni 30, waripotiwa kuwa hawana chakula cha kutosha.

Lishe mbaya si kwamba tu ni hatari bali yaweza kuua. “Utapiamlo unaosababishwa na mazoea mabaya ya ulishaji mtoto huua zaidi ya mara 10 kuliko njaa yenyewe,” akaandika mtafiti William Chandler. “Ukiambatana na kuhara kunakomaliza maji mwilini, utapiamlo ni muuaji anayeongoza ulimwenguni.” Laripoti UNICEF (Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa): “Hakuna mweneo wa ugonjwa, hakuna furiko, wala tetemeko lolote lile au vita imepata kupokonya uhai wa watoto 250,000 kwa juma moja tu.” Lakini hiyo ndiyo idadi ya watoto wanaokufa ulimwenguni pote kwa sababu ya utapiamlo na magonjwa utokezao, kulingana na mwakilishi huyo wa UM. Kwa kweli, madhara yanayofanywa na utapiamlo hayahesabiki: Uwezo wa kujifunza wapungua, wafanyakazi wadhoofika, ubora na matokeo ya kazi yadidimia.

Hata hivyo, ulaji unaotosha wa chakula kifaacho waweza kuzishinda athari za kando za lishe kama vile ukosefu wa damu na magonjwa mengine. Misaada ya kiserikali kama vile chakula cha mchana na supu shuleni huenda kupunguze utapiamlo katika maeneo fulani, lakini kulingana na maofisa wa UNICEF, dola bilioni 25 huhitajiwa kila mwaka ili kupunguza vifo vya watoto visababishwavyo na kuhara, ambukizo la mapafu, na ukambi. ‘Pesa nyingi mno,’ huenda wengine waseme. Lakini hizo zaripotiwa kuwa ndizo fedha Wamarekani hutumia katika mavazi ya michezo na Wanaulaya kwenye kileo kwa mwaka mmoja. Tatizo jingine lililo gumu ni kupunguza utumizi mbaya wa maliasili. Ingawa idadi iliyokadiriwa kuwa milioni 32 ya Wabrazili hulala njaa, Wizara ya Kilimo ya Brazili yaripoti “kwamba upotezo baada ya mavuno [wenye thamani ya dola bilioni 1.5] katika usafirishaji au kuweka akibani husababisha hasara ya asilimia 18 hadi 20 ya mazao ya kilimo ya taifa.” Kuna matatizo makubwa katika kilimo, unyunyiza-mashamba, uwekaji wa chakula, na usafirishaji katika mataifa mengi; bado, dunia yaweza kuandaa kwa wingi kwa ajili ya wote. Basi waweza kukabilije lile tatizo la kulisha familia yako?

Fedha Hazitoshi

Katika nchi zinazositawi mara nyingi watu huweza kulisha familia kwa kuwa na kazi mbili au tatu. Katika Brazili milioni 1.5 kila mwaka huacha familia au marafiki kuhamia majiji makubwa ili kutafuta kazi na chakula. Ingawa kwa kiwango fulani afya hutegemea kile watu wanachokula, sehemu kubwa ya fedha zao hutumiwa katika mavazi, makazi, na usafiri.

Kwa kupendeza, vyakula vya kawaida, kama vile wali, maharagwe, mahindi, viazi, muhogo, na ndizi, vikiliwa pamoja na nyama na samaki, ni vyanzo vikuu vya lishe kwa familia ulimwengu kote. Mwanalishe Mbrazili José Eduardo de Oliveira Dutra alitaarifu hivi: “Maharagwe na wali ni muungano ulio na thamani ya juu ya lishe. Kukiwa na mlo sahili kama huo na wa bei ya chini, yawezekana kukomesha njaa katika [nchi].” Naam, chakula kisicho ghali na chenye lishe huenda kipatikane mahali unapoishi. Au hata huenda ujikuzie baadhi ya vyakula vyako.

Ingawa huenda uwe na fedha za kutosha, je, wazitumia kwa chakula chenye lishe kwa ajili ya familia yako? Au je, wavutwa na utangazaji wa kiujanja na wenye kusisitiza ili upendelee tamu-tamu au chakula kisicho na lishe bora na hivyo ukipuuza uhitaji wa protini, madini, na vitamini? Je, ladha yavutia kuliko ujengaji mwili? The World Book Encyclopedia yaandika hivi: “Ili kufikia na kudumisha afya njema, ni lazima watu wawe na ujuzi wa msingi kuhusu mwili wa binadamu na jinsi utendavyo kazi. Ndipo basi wataweza kuamua kitakacho ama kisichosaidia ama kidhurucho afya yao. Kujifunza kuhusu afya kwapasa kuwa sehemu ya elimu ya kila mtu mmoja.”

Kwa kweli, hatuishi kwa kula tu, bali chakula ni sehemu ya maana maishani mwetu. Biblia husema juu ya kula vizuri kuwa thawabu kwa ajili ya kazi ya jitihada, ikisema hivi: “Ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote.” (Mhubiri 3:13) Je, wewe hukiona chakula chenye kujenga kuwa chenye thamani na kihitajikacho? Ikiwa ndivyo, tafadhali chunguza makala ifuatayo juu ya jinsi lishe ifaayo iwezavyo kukufaidi wewe na familia yako.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki