Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 3/22 kur. 16-18
  • Kumtazama Mamba kwa Ukaribu Zaidi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kumtazama Mamba kwa Ukaribu Zaidi
  • Amkeni!—1995
  • Habari Zinazolingana
  • Jihadhari na ‘Macho ya Mtoni’!
    Amkeni!—1996
  • Je, Unaweza Kutabasamu na Mamba?
    Amkeni!—2005
  • Mamba wa Maji ya Chumvi Mfalme wa Wanyama Wanaotambaa
    Amkeni!—1999
  • Taya la Mamba
    Amkeni!—2015
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 3/22 kur. 16-18

Kumtazama Mamba kwa Ukaribu Zaidi

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA

MTALII Mmarekani alikuwa akipiga picha za viboko kwa hamu kando ya Mto Mara alipoteleza kwenye miamba fulani na kutumbukia ndani. Hili lilivuta fikira za hayawani fulani aliyekuwa mwenye ngozi ngumu ambaye alikuwa akiota jua wakati huo, mamba. Ingawa mnyama-mtambazi huyu kwa kawaida hula samaki, kuona mlo huo mtamu kulitosha kumvutia bila kukawia. Mara moja alijitelezesha ndani ya maji ili kuchunguza. Kwa uzuri, mtalii huyo alimwona mamba yule akija naye akatoka mtoni—kwa haraka sana hivi kwamba alionekana kama alikuwa akitembea juu ya maji!

Wanaozuru mito, maziwa, na mabwawa ya Afrika mara nyingi hupata kuona mamba, ingawa kwa mtalii mwenye kuogofywa aliyetajwa juu, mkabiliano huo yaelekea ulikuwa hatari zaidi. Kenya ni makao ya mamba Naili. Wakifikia hadi urefu wa meta saba, mamba ni wanyama-watambazi, walio wepesi kwenye nchi kavu na majini. Majini wanaweza kwenda mwendo wa kasi sana kwa sababu ya umbo la mikia yao iliyotandazika na iliyo na umbo kama kafi. Wanaweza kuogelea kwa mwendo wa kilometa 40 kwa saa! Na si jambo lisilo la kawaida kwao kukaa chini ya maji kwa saa mbili, hata tatu. Kwenye nchi kavu wanaweza kukimbia kwa miendo mifupi-mifupi, lakini ya kasi.

Si ajabu basi, kwa hakika Biblia humwita mamba kuwa kielelezo cha uumbaji wenye kutisha wa Mungu unaoitwa Leviathani. Ayubu 41:8, 10 husema hivi: “Mwekee mkono wako [Leviathani]; vikumbuke vile vita, wala usifanye tena. . . . Hapana aliye mkali hata akathubutu kumwamsha.” Maonyo yenye hekima kwelikweli! Kulingana na kitabu The Fascination of Reptiles, kilichoandikwa na Maurice Richardson, mamba wamekuwa hata wakijulikana kwa kushambulia motaboti! Ayubu 41:25 kwa kufaa husema: “Anapojiinua, mashujaa huogopa; kwa sababu ya woga wao huvunjwa moyo.”

Kwa nini watu hukimbia kwa ogofyo wanapomwona hayawani huyu mwenye magamba? Mstari wa 14 waeleza sababu moja: “Ni nani awezaye kuifungua milango ya uso wake? Meno yake yatisha kandokando yake.” Kila moja la taya za mamba, zote mbili ya juu na ya chini, zina kufikia meno 24 ya saizi tofauti-tofauti, yote yaking’oka na kumea kwa kuendelea katika maisha yake yote. Kwa kupendeza, jino la nne la mamba la taya ya chini huingia vizuri katika mfuo uliopo kwenye taya ya juu na laweza kuonekana kwa urahisi taya zinapofungwa. Hili husaidia kumtofautisha na binamu yake, aligeta. Tatizo ni kwamba ukisonga karibu sana ili kufanya uchunguzi huu wa meno waweza kuishia katika kuhesabu meno yote ukiwa ndani ya mdomo wake!

Hiyo ndiyo sababu huenda ukachagua kumtazama mamba kwa ukaribu kutoka mahali pafaapo palipo salama, na kuna mahali pengi katika Kenya ambapo waweza kufanya hivyo. Kwa kielelezo, Mamba Village, ni mahali huko Mombasa ambako mamba hulelewa katika makao ya wanyama.

‘Lakini kwa nini,’ wauliza, ‘kwanza yeyote afuge mamba?’ Jambo moja ni kuwahifadhi kutokana na kutoweka. Wakiwa mbugani, mamba wana asilimia 99 ya kiwango cha kadiri ya kufa katika mwaka wa kwanza wa maisha. Yaonekana kwamba kenge, korongo, na hata watu fulani huwa na hamu ya mayai na vianguliwa vidogo vya mamba. Hata hivyo, kadiri ya kufa ya mamba aliyetunzwa vizuri katika sehemu ya kutunzia mamba hushuka chini kuliko asilimia 10. Katika kipindi cha mwaka mmoja, mamba wadogo hufikia urefu wa meta 1.5—bila shaka wakubwa vya kutosha kuondosha vitisho vingi. Yaweza kuchukua hadi miaka mitatu kwa mamba wadogo kufikia urefu uo huo mbugani.

Sehemu za kutunzia mamba pia hulea viumbe hawa kwa madhumuni ya kibiashara. Kwenye soko la kimataifa, waweza kupata viatu, mishipi, mikoba, na vitu vingine vya fashoni vilivyotengenezwa kwa ngozi laini ya matumbo ya mamba. Ngozi 2,000 hupelekwa nje kutoka Mamba Village kila mwaka kwa nchi nyingine, kama vile Italia na Ufaransa, ili kutiwa dawa zisioze. Nini hutukia kwa sehemu iliyobaki ya mnyama huyo? Katika Kenya, nyama ya mamba hutumiwa katika huduma za kitalii kuwa mlo maalum wa wageni.

Kuanzia Oktoba hadi Aprili huwa kipindi cha mamba cha uzazi. Mbugani mamba wa kike aweza kutaga kati ya mayai 20 hadi 80. Wakati huo, mamba wa kike aweza kutaga mayai 36 hivi katika sehemu za kutagia kwenye vidimbwi kadhaa. Kisha mayai hayo hukusanywa na kuhamishwa kwenye vifaa vya utamio ili kuanguliwa. Hili huchukua hadi miezi mitatu.

Mamba Village hutoa fursa nzuri sana ili kuona viumbe hawa wenye kuvutia bila hatari. Mamba Village iko katika chimbo la hekari nane ambalo limetengenezwa upya ili litumike kuwa sehemu ya kutunzia mamba, bustani ya kibotania, hifadhi-maji ya viumbe wa baharini, na jengo kuu la utumbuizo. Zaidi ya 10,000 wa wanyama-watambazi hawa huishi hapa. Bila shaka hutawaona wote. Lakini katika mahali pawili pa uzazi, waweza kuona zaidi ya mamba waliokomaa mia moja, na katika sehemu nyingine, kuna mamia ya mamba wachanga walio katika hatua zote za kukua.

Wakati wa kula mamba hutoa wonyesho wa kupendeza. Wengine hata huruka kutoka majini ili wapate nyama iliyoning’inizwa juu ya kiziwa. Hapa waweza kumwona yule mamba mwenye sifa mbaya anayeitwa Big Daddy aliyeogofya watu sehemu ya Mto Tana, akiua watu watano kabla ya kushikwa na kupelekwa kwenye sehemu hiyo ya kutunzia mamba. Ikiwa kuona mamba uso kwa uso hukufanya uone wasiwasi, waweza kuwaona vyema sana katika jumba la kuonyeshea video.

Kumtazama kwako mamba kwa ukaribu zaidi kwaweza kukuvutia au labda kukushtua. Lakini utafahamu vizuri zaidi kwa nini Biblia ilisema hivi kuhusu mamba katika Ayubu 41:34: “Ni mfalme juu ya wote wenye kiburi.”

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kulia: Tazamo la eneo lote la Mamba Village

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kulia kabisa: Mamba wakati wa kula akiruka kutoka majini ili kupata nyama

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki