Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 1/22 kur. 24-27
  • Jihadhari na ‘Macho ya Mtoni’!

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jihadhari na ‘Macho ya Mtoni’!
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • ‘Macho ya Mtoni’ Yenye Kufisha
  • Uhitaji wa Vitu vya Starehe Watisha Kusalimika Kwao
  • Baadhi ya Ngano Zilizoshikiliwa kwa Muda Mrefu Zaondoshwa
  • Si Ukatili na Jeuri Tupu
  • Kumtazama Mamba kwa Ukaribu Zaidi
    Amkeni!—1995
  • Taya la Mamba
    Amkeni!—2015
  • Je, Unaweza Kutabasamu na Mamba?
    Amkeni!—2005
  • Mamba wa Maji ya Chumvi Mfalme wa Wanyama Wanaotambaa
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 1/22 kur. 24-27

Jihadhari na ‘Macho ya Mtoni’!

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

MWENDA-LIKIZO mjasiri alikuwa akipiga kafi mtumbwi wake polepole katika kijito kinachoungana na Mto East Alligator katika mabwawa yenye kupendeza ya Eneo la Kaskazini la Australia, Hifadhi ya Kitaifa ya Kakadu. Kwa ghafula, kile alichofikiria kuwa kipande kisichoweza kudhuru cha ubao uliokuwa ukielea kilianza kugonga-gonga mtumbwi wake. Kilikuwa mamba wa maji ya chumvi mwenye kuhofiwa sana, na huyo mtalii alikuwa katika eneo lake rasmi katika wakati hatari zaidi wa mwaka.

Kwa wasiwasi mno, yeye alipiga kafi kuelekea mahali penye miti mingi. Alipotoa mguu wake na kukanyaga matawi ya kwanza, huyo mamba alitoka majini, akamvuta chini, na kumbiringisha kwa jumla ya mara tatu. Kila mara mamba alipobadili mshiko wake, huyo mwanamke alijaribu kwa mng’ang’ano kupanda ukingo wa mto wenye matope. Kwa jaribio la tatu, yeye alifaulu kupanda ukingoni, akijiburuta kwa kilometa mbili hadi mtunza-msitu aliposikia vilio vyake vya kukata tamaa vya kuomba msaada. Licha ya majeraha mabaya mno, huyo mwanamke aliokoka.

Hali hii iliyokaribia kuwa msiba ilitukia katika 1985. Miaka miwili baadaye mambo yalikuwa mabaya zaidi kwa mtalii Mmarekani. Yeye alipuuza maonyo ya waandamani wake na kuamua kuogelea katika Mto Prince Regent uliojaa mamba, Magharibi mwa Australia. Alishambuliwa na kuuawa na mamba wa maji ya chumvi. Ripoti kwamba kulikuwa na mamba wachanga majini zadokeza kwamba yaelekea alikuwa mamba wa kike aliyekuwa akikinga wachanga wake.

‘Macho ya Mtoni’ Yenye Kufisha

Chote aonacho mvuvi wa mtoni katika mwangaza wa mwezi ni viwimbi vilivyotokezwa na mdudu anayetua kwenye maji yaliyotulia. Hata hivyo, mvuvi katika kaskazini ya mbali ya Australia ni mwenye tahadhari sikuzote kwa ‘macho ya mtoni’ yasiyoonekana. Ikiwa angewasha tochi yake, macho ya mamba yatokezayo kwa kimya juu ya uso wa maji yangewaka kwa wekundu wenye kung’aa. Yeye ni mdukizi katika eneo la mwindaji wa kale.

Mamba wa Australia wa maji ya chumvi, apatikanaye pia mahali pengine, ni mmojawapo mamba wakubwa zaidi na hatari zaidi kati ya aina 12 za mamba ulimwenguni. Aweza kukua hadi urefu wa meta saba. Windo lisilojua kinachoendelea huona macho yenye kung’aa kuchelewa mno kuweza kuhepa shambulizi lake na mbinu yenye sifa mbaya ya kuzamisha ili kuua kwa kubingirisha ndani ya maji. Mawindo yenye ukubwa wa nyati, ng’ombe, na farasi yameshambuliwa yalipokuwa yakikata kiu chao kwenye ukingo wa maji.

Uhitaji wa Vitu vya Starehe Watisha Kusalimika Kwao

Ngano ya kale kwamba mamba hutoa machozi ya kinafiki ya kumhuzunikia jeruhi wake imeingia katika utamaduni wa kisasa katika ule usemi “machozi ya mamba.” Lakini si machozi mengi yametolewa kuhuzunikia mamba. Badala ya hivyo, mnyama-mtambazi huyu apendaye maji amewindwa bila huruma kwa ajili ya ngozi yake yenye thamani.

Violezo wa fashoni hutembea kwa njia ya kujigamba wakiwa wamevalia vitu vya kimtindo vya ngozi ya mamba kwenye maonyesho ya fashoni, kwa kuwa ngozi ipendezayo ya mamba wa maji ya chumvi huonwa na wengine kuwa ngozi bora zaidi ulimwenguni—nyororo zaidi na ya kudumu sana kuliko zote zipatikanazo. Hivi majuzi mikoba ya mkononi ya mabibi iliyokuwa ikiuzwa kwa bei iliyopunguzwa katika London iligharimu dola 15,000. Ngozi ya mamba bado huonwa kuwa kitu cha fahari ya juu katika sehemu nyingi ulimwenguni.

Kishawishi cha kupata faida kubwa kilitisha kusalimika kwa mamba wa maji ya chumvi katika Australia. Kati ya 1945 na 1971, karibu 113,000 wa wanyama-watambazi hawa waliuawa katika Eneo la Kaskazini pekee. Uwindaji wa mamba uliwekewa mipaka katika miaka ya mapema ya 1970, ili kuzuia kumalizwa kwao kabisa, na tokeo lilikuwa kwamba kufikia 1986, idadi yao mbugani ilikuwa imerudi. Kwa hivyo mamba hayuko tena katika hatari ya kutoweka katika Australia, ingawa wengine hubisha kwamba makao yake ya asili yanahatarishwa.

Kwa karne nyingi idadi ya Wenyeji wa Australia kwa kujua au kutojua walihifadhi idadi ya mamba. Ingawa makabila fulani yalikuwa wawindaji hodari wa mamba, makabila mengine yalikataza kuwindwa kwao kwa sababu za kidini.

Katika miaka ya majuzi kukuza mamba kukishikamanishwa na mkazo kwa elimu kumechangia kuhifadhiwa kwa mamba. Watalii sasa huenda kwa wingi mahali pa kukuzia mamba, wakihakikisha mafanikio yao ya kifedha, huku programu za kuzalisha zikiruhusu utayarishaji wa ngozi na nyama ya mamba bila kuingilia idadi zilizo mbugani.

Mkuzaji-mamba mmoja ajulikanaye sana wa Australia huamini kwamba watu huhifadhi tu vitu wanavyopenda, kuvielewa, na kutoa baadhi ya mahali pao na wakati wao. Yeye alisema hivi: “Kwa hiyo mamba hawapati fursa nyingi ya mafanikio. Lakini thamani yao ya mazingira ni sawa na yoyote ya vitu vyenye kuvutia vinavyovaliwa.”

Kuzuru mahali pa kukuzia mamba kunachangamsha mtu aonapo wanyama-watambazi wenye rangi ya bwawa walio na ngozi ngumu kwa ukaribu—lakini nyuma ya usalama wa uzio wa waya. Wafanyakazi wa mahali hapo hawahofu nao huingia katika mahali walikofungiwa mamba, wakiwakaribisha kufanya michezo na kuwathawabisha kwa nyama ya kuku na nyama nyingine za karibuni. Hata hivyo, mfanyakazi mmoja majuzi alijifunza kwa somo gumu kwamba mamba hapaswi kuchukuliwa vivi hivi. Bila kutazamia, mnyama-mtambazi huyo ghafula alimrukia na kurarua na kuukata mkono wake wa kushoto!

Kwa upande ule mwingine, kumshikilia mamba mwenye miezi 12 ni ono zuri sana na lenye kufurahisha. Ngozi ya sehemu ya chini ya tumbo lake ni nyororo kiajabu, ilhali mabamba yenye mifupa mgongoni mwake yaitwayo osteoderms hufanyiza ngao ya majini yenye nguvu. Sasa inaeleweka kwa nini ngozi yao ina bei kubwa mno. Lakini jihadhari na “kitoto” hicho. Hata mamba mwenye miezi 12 akiwa na taya zilizoshikamanishwa sawasawa ni mwenye nguvu kuliko ukubwa wake.

Watoto wa mamba ambao hawajaanguliwa bado hufurahisha wasikilizaji wakibweka kutoka ndani ya kaka la yai na kwa ghafula kuvunja na kutoka kwa msaada wa jino la muda kwenye ncha ya kijidomo chao. Wengi hukubali kwamba huu ndio wakati pekee ambao mamba huonekana kikweli akiwa mwenye kuvutia!

Baadhi ya Ngano Zilizoshikiliwa kwa Muda Mrefu Zaondoshwa

Kutazama kwa ukaribu tabia ya wanyama-watambazi hawa wenye kutisha wanapokuzwa kwenye mahali pa kukuzia mamba kumesaidia kuondosha ngano zilizoshikiliwa kwa muda mrefu. Kwa miaka mingi ilifikiriwa kwamba mamba huvizia windo lake kwa subira kwa siku nyingi, au hata majuma mengi, kabla ya kushambulia bila kutarajiwa kwa kasi kama umeme. Hata hivyo, mambo yaliyoonwa ya wakati huu yamefunua kwamba mamba kwa kawaida huwa wakali kieneo wakati wa kipindi cha uzazi, wakati wa kaskazi. Windo likiingia eneo lake katika wakati huu, mamba aweza kulifuata kwa ukali, ilhali katika wakati mwingine wa mwaka, huenda mamba akatazama tu mnyama huyohuyo bila upendezi kwa umbali fulani.

Wanapoonwa katika maeneo ya tafrija leo, mamba huondolewa na kuwekwa mahali pengine na wawindaji stadi wa mamba. Sehemu moja ya ustadi wao ni kutia kamba utaya wa chini, kuuinua, na mara moja kufunga utaya wa juu na wa chini pamoja. Hili hufanya utaya wa mamba ukose nguvu kabisa, kwa kuwa ingawa misuli ya kufunga kinywa ya utaya wa chini ina nguvu mno, misuli ya kufunua kinywa ni minyonge. Hata hivyo, mwindaji asipokuwa mwangalifu, anaweza kwa urahisi kuangushwa ardhini kwa mkia wa mamba wenye nguvu.

Si Ukatili na Jeuri Tupu

Taya hizohizo ziwezazo kujeruhi vibaya sana pia zaweza kufanya misogeo yenye ustadi. Mamba wasioanguliwa bado wakiwa wavivu kuvunja kutoka kaka lao la yai, mama wa mamba atabingirisha mayai yake kwa wanana mno, akichochea vianguliwa vitoke.

Meno ya mamba yamebuniwa kushika badala ya kukata. Windo likiwa dogo vya kutosha, hilo humezwa zima-zima. Ikiwa sivyo, hilo huraruliwa na kugawanywa na kuliwa kipande baada ya kingine. Chunguzi za mizoga zimeonyesha mawe katika matumbo yao. Iwe yanaliwa kwa kupenda au la, mawe haya huaminiwa kusaidia usawaziko wakati wa kupiga mbizi.

Wanaozuru mara nyingi hutazama mamba kwenye kingo za mito taya zao kubwa zikiwa wazi. Wengi yaelekea watadhania kwamba kikao hicho humaanisha ukali. Kinyume cha hilo, kikao cha kufunua taya humruhusu ajirekebishe kwa halijoto ya nje. Kama wanyama-watambazi wote, mamba hubadilisha halijoto yao ya mwili kwa kuendelea.

Kwa kushangaza sana, ingawa ni mnyama-mtambazi, mamba ana moyo wenye sehemu nne, kama tu mamalia. Hata hivyo, mamba anaporuka majini, badiliko hutokea, na moyo hutenda ukiwa kama ule wenye sehemu tatu.

Mamba wa maji ya chumvi hutofautishwa na aligeta kwa mdomo mwembamba na kwa meno katika utaya wa chini ambayo huonekana wakati taya zake zimefungwa. Mamba halisi wanaweza kupatikana kuanzia Afrika, ambapo mamba mbilikimo huishi, hadi India, na chini kupita Asia hadi Papua New Guinea. Wao hukaa mbali mno upande wa kusini kama Australia nao hupendelea kanda za kipwani za mikoko na mabwawa ya kitropiki, kwa kuwa wao hutengeneza viota vyao karibu na ukingo wa maji. Ubaya wa kiasili wa jambo hili ni kwamba maji ya mafuriko mara nyingi huzamisha idadi kubwa ya viinitete vya mamba. Kwa sababu ya washambulizi kama vile mamba waliokomaa, samaki baramundi, na ndege kulasitara-kijivu, ni asilimia 50 pekee ya vianguliwa wa mamba husalimika mwaka wavyo wa kwanza.

Kwa kushangaza, mamba huanguliwa wakiwa na ugavi wao wenyewe wa chakula. Hujilisha kwa ute-yai ndani ya miili yao kwa majuma machache ya uhai. Hata hivyo, karibu tu mama yao awachukuapo kwa wanana mdomoni mwake hadi kwenye ukingo wa maji, wao huanza kufanyisha mazoezi midomo yao, wakitaka kuuma chochote kilicho karibu.

Kwa nini usemi ‘macho ya mtoni’ wafaa sana? Kwa sababu hata vikiwa vianguliwa, macho yao madogo hung’aa wekundu chini ya nuru bandia wakati wa usiku. Utando wa fuwele nyuma ya retina huongeza mwono wa usiku na kusababisha mwangaza mwekundu.

Ndiyo, mamba kwa hakika ni myama-mtambazi mwenye kutazamisha—lakini lazima sikuzote tudumishe umbali ufaao. Na kama mvuvi yeyote ajuavyo vizuri, majaribio ya kumfuga leviathani huambulia patupu.

Ushairi wa Ayubu kwa kufaa humfafanua mamba kuwa “Leviathani”: “Je! waweza kumvua [“leviathani,” NW] mamba kwa ndoana? Au kuufunga ulimi wake kwa kamba? Je! waweza kutia kamba puani mwake? Au kutoboa taya yake kwa kulabu? Je! atakusihi sana? Au atakuambia maneno ya upole? Je! atafanya agano pamoja nawe, umtwae kuwa mtumishi wako milele? Je! utamchezea kama ndege? Au kumfunga kwa ajili ya wasichana wako? Je! vikosi vya wavuvi watamfanyia biashara? Watamgawanya kati ya wafanyao biashara? Je! waweza kuijaza ngozi yake na vyuma vyenye ncha? Au kichwa chake kwa vyusa? Mwekee mkono wako; vikumbuke vile vita, wala usifanye tena.”—Ayubu 41:1-8.

Maneno yenye hekima ya tahadhari, yakisihi wasiojihadhari na wenye udadisi: Jihadhari na ‘macho ya mtoni’—mamba mwenye nguvu, mwenye kuhofisha!

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Kwa hisani ya Australian International Public Relations

[Picha katika ukurasa wa 25]

Nuru inapoangazwa kwenye maji usiku, ‘macho ya mtoni’ ya mamba huwaka wekundu

[Hisani]

Kwa hisani ya Koorana Crocodile Farm, Rockhampton, Queensland, Australia

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kushoto: Mtoto wa mamba kwa ghafula atoka nje ya yai

[Hisani]

Kwa hisani ya Koorana Crocodile Farm, Rockhampton, Queensland, Australia

Picha ndogo: Mamba aliyekomaa akiota jua kwenye ukingo wenye matope mengi wa Mto Mary

[Hisani]

Kwa hisani ya Australian International Public Relations

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki