Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 5/22 kur. 25-27
  • Mamba wa Maji ya Chumvi Mfalme wa Wanyama Wanaotambaa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mamba wa Maji ya Chumvi Mfalme wa Wanyama Wanaotambaa
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Taya!
  • Kimebuniwa kwa Ustadi
  • Ukubwa wa Hali ya Juu
  • Wakati wa Badiliko Kubwa
  • “Vita Dhidi ya Wanyama Hao”
  • Jihadhari na ‘Macho ya Mtoni’!
    Amkeni!—1996
  • Je, Unaweza Kutabasamu na Mamba?
    Amkeni!—2005
  • Kumtazama Mamba kwa Ukaribu Zaidi
    Amkeni!—1995
  • Taya la Mamba
    Amkeni!—2015
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 5/22 kur. 25-27

Mamba wa Maji ya Chumvi Mfalme wa Wanyama Wanaotambaa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA PALAU

MARA nyingi utawala juu ya jamii-visiwa ya Palau, katika Bahari ya Pasifiki umekuwa uking’ang’aniwa. Mamlaka ya kwanza ya kikoloni kutawala visiwa hivi vya kitropiki, vilivyo kilometa 890 mashariki ya Filipino, ilikuwa Hispania. Halafu, mahali pa Hispania pakachukuliwa na Ujerumani, nayo Japani ikachukua mahali pa Ujerumani. Baada ya Japani, Marekani ilichukua hatamu za uongozi na kutawala eneo hilo hadi mwaka wa 1994 Jamhuri ya Palau ilipoanza kujitawala.

Ingawa hivyo, wakati wote huu kulipokuwa na mashindano, aina nyingine ya utawala kwenye kisiwa hicho haikuwahi kupingwa. Ilikuwa gani? Utawala wa mamba wa maji ya chumvi—mtawala asiyepingwa wa wanyama wanaotambaa wa Palau. Hata hivyo, leo, utawala wa mamba hao si thabiti. Kwa hakika, watafiti wanasema kwamba “hatua za haraka na madhubuti zisipochukuliwa kuwalinda wanyama hawa, karibuni mamba wa maji ya chumvi watatoweka kabisa katika makao yao huko Palau.”

Kwa nini mamba wa Palau wako mashakani? Na kwa nini wangepewa jina la cheo mfalme wa wanyama wanaotambaa?

Taya!

Jina la kisayansi la mamba wa maji ya chumvi ni Crocodylus porosus, limaanishalo “mamba mwenye sagamba nyingi.”a Jina hili hurejezea michomozo yake yenye magamba kwenye sehemu ya juu ya pua yake. Hufanyiza safu mbili zinazoanzia kwenye macho hadi kwenye mianzi ya pua. Pua yake ina umbo la pembetatu na hufanyiza karibu sehemu moja ya saba ya urefu wa mwili wote. Mamba mmoja, anayeonyeshwa kwenye Jumba la Makumbusho la Palau, kichwa chake kikubwa kupita kiasi kina upana wa sentimeta 40 kwenye sehemu yake iliyo pana!

Utaya wa chini wa mamba unapojifungua, unaona meno yaliyo makali kama makasi yakiwa katika taya zinazoweza kufungwa kwa nguvu nyingi sana. Sehemu pekee za taya zilizo dhaifu ni misuli ya kuzifungua. Kitabu kimoja chasema kwamba kwa kawaida ukanda wa raba huweza kutosha kumfanya mamba mwenye urefu wa meta mbili asiweze kufungua kinywa.

Kimebuniwa kwa Ustadi

Kichwa cha mamba si kikubwa tu bali pia kimebuniwa kwa ustadi ili kufaana na maisha yake ya majini. Mtazame kwa makini (yaani mamba wa onyesho aliyejazwa vitu!), na utaona kwamba masikio, macho, na mianzi ya pua ziko juu zaidi kwenye kichwa chake. Sehemu hizo hujitokeza juu ya maji mamba anapoelea. Hata hivyo, ni jambo la kushangaza kwamba mnyama huyu anapofunga kinywa chake, hawezi kuzuia maji yasiingie, kwa kuwa hana midomo inayofunika mfupa wa taya. Lakini maji yanayoingia kwenye mdomo hayawezi kuingia kwenye koo kwa sababu kilango huziba mwingilio wa koo. Na kwa kuwa mamba hupumua kupitia mianzi ya pua kisha hewa huingia kwenye mwili nyuma ya kilango hiki, yeye aweza kupumua kinywa chake kinapokuwa kimejaa maji.

Namna gani kuona chini ya maji? Hakuna tatizo lolote. Anapokuwa chini ya maji, mamba huvuta utando ulio wazi kufunika macho yake. Utando huu hulinda jicho huku yeye akiona vizuri.

Ukubwa wa Hali ya Juu

Mamba wa maji ya chumvi ndiye mnyama anayetambaa mkubwa zaidi ulimwenguni. Mamba wa kiume wanapofikisha urefu wa meta 3.2, wanakuwa wamekomaa lakini huendelea kukua kwa miaka mingi zaidi. Mark Carwardine, mwandishi wa The Guinness Book of Animal Records, asema kwamba katika hifadhi moja ya wanyama huko India kuna mamba wa kiume wa maji ya chumvi ambaye ana urefu wa meta 7!

Eneo la mamba huyo lina ukubwa wa hali ya juu vilevile. Kitabu hichohicho chasema kwamba eneo la makao ya mamba wa maji ya chumvi ni kubwa zaidi ya makao ya aina zote za mamba. Mamba wa maji ya chumvi huishi katika maeneo yote ya kitropiki ya Asia na Pasifiki, eneo linalosambaa kutoka India hadi Australia na jamii-visiwa ya Palau.

Wakati wa Badiliko Kubwa

Mabwawa ya mikoko kwenye visiwa vya Palau huandalia mamba kivuli, ulinzi, na chakula tele. Basi, haishangazi kwamba, wanyama hawa wanaotambaa walichagua jamii-visiwa ya Palau kuwa mojawapo ya eneo lao maalumu na la kuzalia. Kwa hakika, idadi ya mamba walioishi katika visiwa hivi katika miaka ya 1960 ilikadiriwa kuwa kati ya 1,500 na 5,000.

Hata hivyo, Desemba 1965, iliashiria wakati wa badiliko kubwa kwa mamba walioko Palau. Mwezi huo mamba wa maji ya chumvi alishambulia na kuua mvuvi wa Palau. Majuma kadhaa baadaye, mnyama huyo alinaswa na kuonyeshwa umma. Umma ulikasirishwa sana na mnyama huyo aliyetekwa hivi kwamba aliuawa.

“Vita Dhidi ya Wanyama Hao”

Muda mfupi baada ya hapo, waeleza wataalamu wa mamba Harry Messel na F. Wayne King, wenye mamlaka walianzisha “kampeni ya kumaliza kabisa mamba wote katika Palau, bila kujali mahali walipotokea. Kwa kweli ilikuwa ni vita dhidi ya wanyama hao.” Fedha zilitolewa, mitego ikawekwa, na mashua za kuwinda zilitumiwa kuwawinda wanyama hao. Kutoka mwaka wa 1979 hadi 1981, wawindaji waliua mamba kati ya 500 na 1,000. Waliwachuna ngozi wanyama hao na kuuza ngozi hizo.

Kwa kuwa mamba waliokomaa wana ngozi kubwa, wakawa shabaha ya pekee. Hata hivyo, kila wakati wawindaji walipoua mamba wa kike aliyekomaa, pia walizuia kuanguliwa kwa watoto 1,000 au zaidi ambao mamba huyo wa kike angezaa katika muda wa maisha yake. Basi, idadi ya mamba ikadidimia. Mapema katika miaka ya 1990, Messel na King waliona kwamba “mamba waliobaki kwenye pori ya Palau walipungua 150.”

Ni kweli kwamba mwanadamu ana sababu za kutahadhari juu ya mamba wa maji ya chumvi, kwa kuwa mashambulizi yao yaweza kusababisha kifo. Ijapokuwa hivyo, asema mwandishi Carwardine, “madhara wanayotusababishia ni duni sana yakilinganishwa na uharibifu ambao tumewasababishia.”

Katika mwaka wa 1997 Hifadhi ya Asili ya Ngardok ilianzishwa. Ingawa hifadhi hii haijaanzishwa hasa ili kulinda mamba wa maji ya chumvi, wananufaika kutokana na hifadhi hii. Mabwawa yanayozunguka Ziwa Ngardok huandalia mamba hawa mahali pa kujificha na kuzalia.

Huenda usimpende mamba wa maji ya chumvi lakini je, hukubali kwamba yeye ni mfalme mwenye kuvutia?

[Maelezo ya Chini]

a Neno porosus latokana na neno la Kigiriki porosis, limaanishalo “-enye sagamba,” na kiambishi tamati cha Kilatini –osus, kinachomaanisha “-enye kujaa.”

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

MACHOZI YA MAMBA

Kusema kuwa mtu fulani anatoa machozi ya mamba humaanisha kwamba anaonyesha kihoro au huruma za unafiki. Lakini kwa nini mamba huonyeshwa kuwa wanafiki? Kulingana na The International Wildlife Encyclopedia, huenda chanzo kimoja cha msemo huu kikawa uhakika wa kwamba macho ya mamba huwa na unyevunyevu daima. Hivyo, “machozi, au maji yaliyonaswa kwenye kope zao, yaweza kutiririka kutoka kwenye pembe za macho yao. Hili, pamoja na kukenua taya zao daima, kungeweza kutokeza sifa yao ya kuwa wanafiki kama isimuliwavyo katika hekaya.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]

JE, NI MAMBA AU NI ALIGETA?

Kuna tofauti gani kati ya mamba na aligeta? Tofauti iliyo wazi zaidi ni meno yao. Kwa maneno rahisi, mamba anapofunga taya zake, unaweza kuona jino lake kubwa la nne kwenye utaya wa chini. Hata hivyo, kuhusu aligeta utaya wa juu hufunika jino hili.

[Picha]

Mamba

Aligeta

[Hisani]

F. W. King photo

[Picha katika ukurasa wa 26]

Tazama hayo meno!

[Hisani]

By courtesy of Koorana Crocodile Farm, Rockhampton, Queensland, Australia

© Adam Britton, http://crocodilian.com

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

By courtesy of Australian International Public Relations

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki