Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 3/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kupuuza ule “Utume Mkubwa”
  • Palipo na Moshi Pana Moto
  • Jeuri ya Televisheni Yapimwa
  • Utapiamlo wa Tufeni Pote
  • Bahari Nyeusi ama “Baharifu”?
  • Bangi na Kupoteza Kumbukumbu
  • Matineja na Video za Ponografia
  • Ni Muujiza au Ni Vijiumbe Maradhi?
  • UKIMWI Kutoka kwa Damu?
  • Mgeni Mwadimifu
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1997
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2000
  • Utiaji-damu Mishipani—Ni Salama Kadiri Gani?
    Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako?
  • UKIMWI—Je! Nimo Hatarini?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 3/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kupuuza ule “Utume Mkubwa”

Kwa miaka mingi Jumuiya ya Wakristo imerezejea ile amri ya Yesu kwa wafuasi wake ya kufanya wanafunzi wa mataifa yote kuwa ule “Utume Mkubwa.” Hata hivyo, kulingana na uchunguzi uliofanywa majuzi na Chuo cha Utafiti Katika Sayansi ya Kijamii kwenye Chuo Kikuu cha North Carolina, Marekani, “Wakristo” wachache zaidi na zaidi katika Marekani hata huuona utume huu kuwa wa maana sana. Nje ya majimbo ya Kusini, ambayo kwa kidesturi huwa ya kidini zaidi, asilimia 32 pekee ya wale ambao hujidhania kuwa Wakristo walihisi kwamba kuwageuza wengine kwa imani yao kulikuwa daraka la “umuhimu sana” kwa kanisa lao. Katika Kusini, tarakimu hizo zilikuwa asilimia 52 tu.

Palipo na Moshi Pana Moto

Kati ya madhara mengi yanayojulikana sana ya uvutaji-sigareti, kuna moja ambalo mara nyingi lakosa kujulikana: moto. Kulingana na Shirika la Ulinzi wa Moto la Kitaifa la Marekani, lilionyesha bidhaa za tumbaku zilizowashwa zilisababisha karibu mioto 187,000 katika Marekani katika 1991 pekee, ikiua watu 951 (bila kutia wazima-moto). Hivyo, asilimia 25 ya vifo vyote vya moto katika makao ya watu mwaka huo vilitokana na uvutaji-sigareti—misiba zaidi kuliko iliyotokana na mioto iliyosababishwa na chochote kingine. Mioto inayohusiana na uvutaji-sigareti pia ilisababisha majeraha 3,381 na dola milioni 552 katika uharibifu wa mali wakati wa mwaka huohuo. Vifaa vya nyumbani vilivyochomwa moto vilikuwa fanicha zenye matakia na ngozi, magodoro, na matandiko ya kitanda.

Jeuri ya Televisheni Yapimwa

Uchunguzi mpya wenye kubishaniwa hudai kwamba kujapokuwa malalamiko kuhusu jeuri kwenye televisheni ya Marekani—na kujapokuwa na ahadi nyingi kutoka kwa mfumo wa televisheni kuichuja—kwa kweli jeuri katika televisheni imeongezeka katika miaka miwili iliyopita. Uchunguzi huo ulifanywa na Kitovu cha Utangazaji na Mambo ya Umma na ulifikia mkataa wao kwa kuchunguza programu ya siku moja kwenye vituo kumi na kulinganisha yaliyomo na programu ya siku hiyohiyo miaka miwili mapema. Ulipata kwamba matendo ya jeuri, yanayofafanuliwa kuwa matendo ya makusudi ya nguvu za kimwili yanayotokeza madhara ya kimwili au uharibifu wa mali, uliongezeka kwa asilimia 41 katika kipindi cha miaka miwili. Vitendo vya jeuri nzito vilifafanuliwa kuwa vyenye kutisha uhai au vielekeavyo kusababisha majeraha mabaya, na idadi ya hivi ilipanda kwa asilimia 67. “Kiasi cha wastani cha vitendo vya jeuri kiliongezeka kutoka 10 kufikia karibu maonyesho 15 kwa kila kituo kwa saa,” yaripoti TV Guide.

Utapiamlo wa Tufeni Pote

Tufeni, kunazo habari nzuri na habari mbaya kuhusu utapiamlo. Kulingana na Global Child Health News & Review, asilimia ya watoto wote walio chini ya miaka mitano wapatwao na utapiamlo ilipungua kutoka asilimia 42 katika 1975 hadi asilimia 34 katika 1990. Hata hivyo, jumla ya idadi ya watoto walio na utapiamlo imekua. Karibu watoto milioni 193 chini ya miaka mitano katika nchi zinazositawi walikuwa na uzani uliopungua kwa kiasi au sana, na karibu theluthi moja ya hao walikuwa na lishe mbaya zaidi. Gazeti hilo lilisema kwamba wakati mtoto anapolishwa isivyofaa kwa kadiri ndogo, hatari ya kifo kutokana na maradhi huongezeka mara mbili. Hatari huwa mara tatu kwa watoto walio na lishe isiyofaa. Kwa mtoto asiye na lishe bora kwelikweli, hatari ya kufa kwa maradhi ni mara 11 juu zaidi. Katika mabara yaliyoendelea, gazeti hilo laripoti, aina ya utapiamlo iliyo ya kawaida ni kunenepa mno. Kwa kielelezo, katika Amerika Kaskazini, watoto hupata kufikia asilimia 50 ya nishati zao kutoka kwa shahamu—ambayo ni “mara mbili ya kiasi kipendekezwacho.”

Bahari Nyeusi ama “Baharifu”?

“Bahari Nyeusi imekuwa bahari iliyochafuliwa sana ulimwenguni na yaendelea kufikwa na kifo chenye kuumiza.” Ndivyo linavyoripoti gazeti la Kirusi Rossiiskaya Gazeta, likiandika kwamba wakati wa miaka 30 iliyopita, Bahari Nyeusi “imekuwa mahali pa maji machafu pa nusu ya Ulaya—mahali pa kutupa kiasi kikubwa cha misombo ya fosforasi, hidrajiri, DDT, petroli na vinyesi vyenye sumu kutoka kwa wakaaji milioni 160 kwenye pwani zake.” Uchafuzi huo umetokeza dalili kadhaa zenye kutisha. Kati ya namna 26 za samaki ambao wavuvi awali walivua katika Bahari Nyeusi katika miaka ya 1960, ni aina 5 tu zilizobaki. Idadi ya dolfini (mamalia) wa bahari hiyo, wakati fulani iliyokuwa chekwachekwa kufikia 1,000,000, imefyekwa hadi 200,000. Wengi wa dolfini waliosalia wameambukizwa na homa ya nguruwe kwa sababu mashamba mengi ya nguruwe hutupa uchafu kwenye Delta ya Danube.

Bangi na Kupoteza Kumbukumbu

“Wakiwa wa kwanza kabisa,” laripoti The Sydney Morning Herald la Australia, “watafiti wa Sydney wameonyesha kile ambacho watu wengi kwa muda mrefu walishuku—kwamba kupoteza kumbukumbu na kukosa umakini kunakosababishwa na kuvuta bangi huendelea kwa muda mrefu baada ya watu kuacha kuitumia.” Utafiti huo, uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Macquarie, ulithibitisha kwamba madhara yanayosababishwa na bangi yawiana na kiasi kilichovutwa na muda wa zoea hilo. Habari hizo zaendelea kuwa mbaya: “Madhara haya huenda yasiondoleke.” Uchunguzi huo ulionyesha kwamba waliokuwa wakitumia walipatwa na “kasoro ya utambuzi” sawa na wale wangali wakivuta bangi. Zaidi ya kumbukumbu huathiriwa, hasa kwa wale ambao wametumia bangi kwa miaka mitano na zaidi. Watu hao walipatikana kuwa wapokeao habari polepole sana na wasioweza kumakinika na kuepuka vikengeusha mawazo. Ripoti hiyo yamalizia kwamba, kulingana na uthibitisho wa ujumla, kuvuta bangi kwa hakika hubadili utendaji wa ubongo.

Matineja na Video za Ponografia

Asilimia 77 yenye kusikitisha ya wavulana wa sekondari na asilimia 24 ya wasichana wa sekondari katika Japani walipata kutazama video za ponografia, kulingana na uchunguzi uliofanywa na Shirika la Japani la Usimamizi na Usawazishaji. Hata miongoni mwa wavulana wadogo wa sekondari walio na umri mdogo kufikia miaka 13 ama 14, asilimia 25 wamepata kuona video kama hizo. Na matokeo ni nini? “Uchunguzi huo waonyesha,” likaripoti Mainichi Daily News, “kwamba wanafunzi ambao wamepata kuona video za watu wazima wana hisi ya dhamiri iliyokua vibaya juu ya uhalifu wa kingono na uthamini mdogo wa hisia za majeruhi wa uhalifu kama huo.” Je, wazazi walijua hali hiyo? Uchunguzi huohuo ulifunua kwamba ni asilimia 12 tu ya wazazi wa wanafunzi hao ndio waliojua au kushuku kwamba watoto wao walikuwa wakitazama video za ponografia.

Ni Muujiza au Ni Vijiumbe Maradhi?

“Mmoja wa miujiza ujulikanao sana wa kanisa Katoliki huenda ulihusu vijiumbe maradhi badala ya kimungu,” likaripoti gazeti New Scientist majuzi. “Muujiza wa Bolsena” uliokusudiwa ulitukia huko nyuma katika 1263, wakati padri Mbohemia alipochukua kipande cha mkate cha sakramenti katika msherehekeo wa Misa. Kama vile hekaya hiyo isemavyo, alikuwa akishangaa kama kwa kweli mkate huo ungegeuka kuwa mwili wa Kristo kama vile Kanisa Katoliki lifunzavyo. Kisha, kwa kushangazwa, aliona kwamba kipande cha mkate kilikuwa kikitokwa na kile kilichoonekana kuwa damu! Hata hivyo, kwa muda mrefu wanasayansi wamedadisi kuwa dhana hiyo ilisababishwa na kuvu, nyekundu nyangavu ambayo hukua kwenye vyakula vyenye uwanga katika tabia-anga yenye ujoto. Johanna Cullen wa Chuo Kikuu cha George Mason katika Virginia, Marekani, majuzi alitokeza upya hali zielekeazo kuwa za muhula wa kati na akakuza jamii ya bakteria iliyoshukiwa kuwa kwenye kipande cha mkate cha sakramenti. Mara iligeuka kuwa nyekundu kama damu.

UKIMWI Kutoka kwa Damu?

Uwezekano wa kupata UKIMWI kutokana na kutiwa damu au kutoka kwa vifanyiza-damu ukoje? Kulingana na gazeti la The Star la Johannesburg, watu 600,000 ulimwenguni pote—au asilimia 15 ya wote walioathiriwa—wameambukizwa virusi ya UKIMWI kutoka kwa damu au vifanyiza-damu tangu UKIMWI ugunduliwe. Kwa sasa, kuchunguza damu kwa ajili ya HIV yachukua wakati mwingi mno na ni ghali. Wengine hukata kauli kwamba damu yapaswa kufanyiwa uchunguzi angalau kwa chunguzi saba tofautitofauti. Mara nyingi, nchi zinazositawi hazina fedha au stadi ili kufanya chunguzi hizi. Hata katika nchi mahiri, zinazotumia chunguzi hizo, kunakuwa na makosa. Paul Strengers, mkubwa wa kitiba wa huduma ya kutia damu ya Uholanzi, akubali hivi: “Hatuwezi kusema kwamba kila kifanyiza-damu ni asilimia 100 salama kuhusu virusi ya HIV au mchochota wa ini.”

Mgeni Mwadimifu

Kometi ambayo ilionekana katika Machi 1993 na waastronomia katika Australia na Ufaransa ilitambuliwa kirasmi na Muungano wa Kimataifa wa Kiastronomia Januari iliyofuata na ikaitwa McNaught-Russel. Lakini waastronomia Wachina huenda wakawa waliiona kwanza—karibu karne 14 zilizopita! Kulingana na gazeti la New Scientist, mwastronomia mmoja alikadiria kwamba kometi hii huchukua muda mrefu isivyo kawaida ili kuzunguka jua: miaka 1,419. Kwa kupendeza, rekodi za kale huonyesha kwamba waastronomia Wachina waliona “nyota” iliyozunguka-zunguka ambayo yaelekea ilikuwa kometi hiyohiyo. Walirekodi wakati wa kuiona kwao kwenye mwaka wa tatu wa pindi iitwayo Keen Tih, wakati wa mwezi wa pili, kwenye siku iitwayo Woo Woo—au Aprili 4, 574 W.K. Kometi itazuru ujirani wetu wa mfumo wa jua karibu mwaka 3412.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki