Ile Mami Ambayo Ilikuja Kutoka kwa Barafuto
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA
Kwenye mwono wa kwanza huenda ilionekana kama mandhari ya uhalifu. Mzoga ulionyauka ulilala kifudifudi, nusu umenasika katika barafu. Je, ni aksidenti yenye kufisha? Mauaji fulani ya kulipiza kisasi? Ama tu ni mpanda-mlima mwingine aliyepatwa na janga? Kwa vyovyote vile, alikuwa akifanya nini huko kwenye unyamavu wa Tyrolean Alps meta 3,200 juu ya usawa wa bahari? Yeye alikuwa nani? Naye alikufaje?
“MWANABARAFU,” kama alivyoitwa mara hiyo, ama Homo tyrolensis, kama vile wanasayansi wanavyomwita, alipatikana bila kutazamiwa katika Septemba 1991 na mume na mke Wajerumani waliokuwa wakipanda Mlima Similaun (kwenye Ötztaler Alps), kwenye mpaka wa Austria na Italia. Hasa kiangazi kilichokuwa na joto mwaka huo kilikuwa kimeyeyusha nyingi ya theluji, kikifunua masalio ambayo yangebaki kufichika—kwani ni nani ajuaye ni kwa muda mrefu kiasi gani? Baada ya wachunguzi kusuluhisha kutokuwa na uhakika kuhusu ugunduzi huo, mwili ulitolewa barafuni bila ustadi wowote, ukipatwa na uharibifu mnamo wakati wa kutolewa. Hata hivyo, muda si muda ikawa wazi kwamba haukuwa mzoga wa kawaida. Karibu na mwili kulikuwa na vitu kadhaa ambavyo vilikuwa tofauti kabisa na vile hutumiwa kwa ukawaida na wapanda milima wa kisasa wanaosafiri katika umbaliwima kama huo.
Wengine waling’amua kwamba mzoga huo ulikuwa wa zamani sana. Baada ya majaribio ya kwanza, Konrad Spindler, wa Chuo Kikuu cha Innsbruck, Austria, alisema maneno yenye kushangaza—kwamba mwili uliohifadhiwa uliopatikana juu ya Mlima Similaun ulikuwa na umri wa maelfu kadhaa ya miaka! Uchanganuzi na utafiti zaidi kwenye mahali ulipopatikana uliongoza wasomi kufikia mkataa kwamba wao walikuwa wakichunguza “binadamu wa kale sana ambaye amepata kupatikana akiwa mzima.” (Time, Oktoba 26, 1992) Waakiolojia waamini kwamba Mwanabarafu, aliyebandikwa jina Ötzi (kutokana na Ötztal, jina la Kijerumani la bonde lililoko karibu), alikufa karibu 3000 K.W.K.
Mara waakiolojia walipofahamu umuhimu wa ugunduzi huo, walirudi mara kadhaa kwenye Mlima Similaun ili kutafuta aathari nyingine zenye faida katika kujaribu kufahamu kilichokuwa kimempata mwanadamu huyo karne hizo zote zilizopita. Wao wamevumbua nini? Kwa nini kumekuwa na upendezi mwingi katika mami iliyozikwa barafuni? Je, imewezekana kufumbua fumbo lolote linalomhusu?
[Picha katika ukurasa wa 3]
Ötzi, yule Mwanabarafu
[Hisani]
Foto: Archiv Österreichischer Alpenverein/Innsbruck, S.N.S. Pressebild GmbH