Vidokezo kuhusu lile fumbo la Mwanabarafu
KWA karne nyingi, Ötzi alikuwa katika mahali pazuri pa kupumzikia akiwa mfu. Alilala kwenye meta 3,200 juu ya usawa wa bahari katika kijito chembamba, kilichojaa theluji katika kibonyeo kilichomsitiri kutoka kwa miendo ya barafuto iliyo karibu. Ikiwa mwili wake ungeganda ndani ya tungamo la barafuto, ungekuwa umevunjwa-vunjwa na kufagiliwa mbali. Yaelekea sana, mahali pake palipositirika palimhifadhi akiwa mzima.
Meta kadhaa kutoka kwenye mwili kulikuwa na vitu ambavyo yaonekana vilikuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku: upinde wa mvinje, podo lililotengenezwa kwa ngozi ya paa likiwa na mishale 14 (2 ikiwa tayari kwa ajili ya kutumiwa, ile mingine ikiwa bado kukamilishwa), jambia la jiwe, shoka, kitu fulani kifikiriwacho kuwa ubuni wa mfuko wa kubeba wa kikale, mfuko wa ngozi, kiwekeo kilichotengenezwa kwa ganda la mti, na vipande vya nguo, pamoja na vyombo na vitu vingine.
Alipopatikana, Mwanamume wa Similaun (jingine la majina yake) alikuwa angali amevaa baadhi ya vifaa vyake vya mavazi na alikuwa na viatu vya ngozi vilivyojazwa majani ili kumlinda kutokana na baridi. Karibu na kichwa chake kulikuwa na “jamvi” la majani yaliyofumwa. Ilikuwa kana kwamba, akiwa ameshindwa na uchovu na baridi jioni moja, Mwanabarafu alilala usingizi mnono tu “kuona” mwangaza wa mchana maelfu ya miaka baadaye. Ugunduzi huo ulikuwa “picha ya kitamathali ya muhula fulani, ya jamii na idadi fulani ya kibiolojia,” asema mwakiolojia Francesco Fedele, aliyemfafanua Mwanamume wa Similaun kuwa “kibonge cha wakati.”
Yeye Alihifadhiwaje?
Si wote huafikiana juu ya njia ambayo Ötzi alihifadhiwa akiwa mzima kwa muda mrefu hivyo katika hali hizo. “Kuhifadhiwa kwake ni kama muujiza, hata mmoja anapofikiria kusitirika kwake katika kibonyeo alichopatikana ndani yacho,” lasema Nature. Nadharia ambayo kwa sasa yafikiriwa kuwa yenye kuaminika ni kwamba uhifadhi ulitukia kwa sababu ya muungano wa “matukio matatu ya hakika”: (1) utaratibu wa haraka wa kiasili wa kuhifadhi mwili (kufyonza maji), matokeo ya athari za baridi, jua, na upepo wenye ujoto na mnyaufu; (2) ufunikaji wa haraka wa theluji ambao ulificha mwili kutokana na wanyafuaji; na (3) usitiri kutokana na miendo ya barafuto ulioandaliwa na kibonyeo. Hata hivyo, wengine hata hawapati maelezo hayo yakiwa yenye kusadikisha, wakithibisha kwamba pepo zenye joto na nyaufu hazifiki kwenye umbaliwima wa juu hivyo katika eneo hili la Alps.
Hata hivyo, mambo fulani kuhusu Mwanabarafu yako hakika. Imewezekana kuhakikisha kwamba alikuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 40, alikuwa na urefu wa sentimeta 160, na karibu uzani wa kilogramu 50. Alikuwa mwembamba na mwenye nguvu, na nywele zake za hudhurungi zilitunzwa vizuri na yaonekana zilikatwa kwa ukawaida. Uchunguzi wa majuzi wa sampuli za tishu za DNA ulihakikisha kwamba alikuwa wa mfanyizo uleule wa jeni kama ule ulioko na wakaaji wa Ulaya ya kati na kaskazini. Meno yake yaliyoisha-isha yalifunua kwamba alikula mkate wa kawaida, ikidokeza kwamba huenda alikuwa wa jamii ya kilimo, kama ilivyothibitishwa na nafaka za ngano zilizopatikana katika nguo zake. Kwa kupendeza, imekuwa rahisi kuamua kwamba alikufa kuelekea mwisho wa kiangazi ama mwanzo wa kipupwe. Jinsi gani? Katika mfuko wake mlipatikana masalio ya aina fulani ya zambarau-mwitu ziivazo mwishoni-mwishoni mwa kiangazi; labda, zilikuwa sehemu ya mwisho ya ugavi wake.
“Mwanajeshi wa Muhula wa Kati Akibeba Bunduki”
Lakini Ötzi afunua nini? Jarida la Italia Archeo liliandika kwa ufupi idadi ya maswali yaliyotokezwa na uvumbuzi kwa njia hii: “Je, alikuwa mwanavita ama mwindaji? Je, alikuwa mtu aliyeishi peke yake, je, alikuwa akisafiri pamoja na kikundi chake, ama kwa upande ule mwingine, je, alikuwa safarini kwenye milima hiyo katika uandamani wa kikundi fulani kidogo chake? . . . Je, alikuwa peke yake, kuzungukwa na barafu yote hiyo, ama twaweza kutazamia nyuso nyingine?” Wasomi wametafuta kuhakikisha majibu hasa kupitia uchunguzi wa vitu vinavyopatikana kwenye Mlima Similaun na kujaribu kuvumbua maana yavyo. Nadharia mbalimbali kuhusu sababu ya Ötzi kujipata kwenye mwinuko wa zaidi ya meta 3,200 zilidokezwa, lakini kila moja yazo yapingana na baadhi ya maelezo mengine. Acheni tuchunguze vielelezo vichache.
Upinde, ambao kamwe haukuwa na uzi, na mishale ungeweza kudokeza mara moja kwamba alikuwa mwindaji. Je, hilo linafumbua lile fumbo? Labda, lakini upinde, ukiwa na urefu wa karibu meta 1.8, “ulikuwa mkubwa mno kwa mtu wa kimo chake,” asema mwakiolojia Christopher Bergman, na “kwa uamuzi ulikuwa mkubwa kuwinda windo la Alpine.” Kwa nini alikuwa na upinde ambao hangeweza kuutumia? Zaidi ya yote, mtu akisafiri milimani huhitaji kupunguza uzito wote wa ziada, “jambo ambalo hufanya hasa itatanishe kwamba upinde na 12 ya mishale 14 yake ilikuwa haijakamilika, ilhali silaha nyingine zake (jambia na shoka) zilikuwa zimeisha kwa matumizi ya muda mrefu,” laonelea Nature.
Na vipi kuhusu shoka ambalo lilipatikana meta kadhaa mbali kidogo na mwili? Mwanzoni, lilifikiriwa kuwa shaba nyeusi, lakini majaribio yalifunua kwamba, kwa uhakika, lilitengenezwa kwa shaba nyekundu. Kwa sababu hii na nyingine nyingi, waakiolojia wengi wafikiria kumwekea Ötzi tarehe ya nyuma mwanzoni mwa ule uitwao Muhula wa Shaba, yaani, mileani ya nne-tatu K.W.K. “Majaribio ya kaboni 14 . . . yalihakikisha kwamba aliishi kati ya miaka 4,800 na 5,500 iliyopita,” likataarifu gazeti Audubon.a Hata hivyo, vitu vingine vingeelekea kushawishi baadhi ya wastadi kumweka Mwanabarafu katika kipindi cha kale zaidi. Yaonekana, haiwezekani kumweka Mwanamume wa Similaun katika ustaarabu hususa wa kale. Akirejezea kwa shoka la shaba, mwakiolojia mmoja aamini kwamba Ötzi “alihodhi silaha fulani ambayo ilikuwa ya juu sana kitekinolojia kwa muhula ambao aliishi. Ilikuwa kana kwamba tulipata mwanajeshi wa muhula wa kati akibeba bunduki. Kwa hakika, katika muhula huo shaba ilijulikana tu katika tamaduni za Mashariki.”
Zaidi ya hayo, kama tulivyoona tayari, shoka lingeweza kuwa kitu cha thamani miongoni mwa watu walioishi wakati mmoja na Mwanabarafu. Aathari nyingine, kama vile ala ya jambia lake, pia zilikuwa safi sana na kwa wazi zilikuwa “vitu vya umaarufu.” Lakini ikiwa Ötzi alikuwa mtu wa cheo cha juu, chifu, kwa nini alikuwa peke yake wakati wa kifo chake?
Kulingana na gazeti Popular Science, Konrad Spindler, wa Chuo Kikuu cha Innsbruck, alidhani hivi: “Kile walichokifikiria mwanzoni kuwa chale za kifumbo chalingana kabisa na maungo ya goti na vifundo vya mguu vilivyochakaa na vetabra itokayo katika uti wake. Daktari wa Mwanabarafu yawezekana alitibu hali kwa kuchoma mahali palipouma, kisha kusugua kwa majivu ya miti-shamba ndani ya kidonda.”
Hivi majuzi, katika mkutano wa wastadi wa tiba ya balagha katika Chicago, wazo lilitokezwa, kwamba Ötzi huenda akawa mtoro aliyepigwa na kujeruhiwa aliyekufa katika maficho wengine wakiwa wangali wakimwinda. Imepatikana kwamba alikuwa na mbavu kadhaa zilizovunjika na taya lenye mwatuko. Hata hivyo, haiwezi kusemwa wakati hususa alipopata majeraha haya—kabla au baada ya kifo. Ingawaje, ikiwa alikuwa amekuwa jeruhi wa jeuri, “kwa nini alikuwa angali na zana zake zote, hata zile za ‘thamani’?” kama vile shoka la shaba, likauliza Archeo.
Wachunguzi wakadiria kwamba kweli zilizoko hazitoshi kukamilisha yaliyotukia, na maswali mengi bado yabaki bila majibu. Lakini ni wazi kwamba ustaarabu wa Ötzi ulikuwa umeratibiwa kwa hali ya juu na ulio tata.
Ötzi na Ulimwengu Alioishi
Katika kueleza ulimwengu wa Mwanamume wa Similaun, wasomi hutegemeza maoni yao juu ya ugunduzi kutoka maeneo ya Alpine ambayo yafikiriwa yalikuwa yakikaliwa na watu walioishi wakati mmoja naye. Walakini, waakiolojia hutuambia, maeneo fulani yalisitawi zaidi kuliko mengine, nao ubuni mwingi wa kiufundi, kama vile kuunda shaba, ulitoka katika Mashariki ya Kati.
Kulingana na maelezo fulani, Ötzi huenda aliishi katika mojapo majiji ya kilimo ya majaruba ya Mto Adige. Mto huu ulikuwa barabara muhimu iliyounganisha Peninsula ya Italia na Ulaya Kati. Idadi kadhaa ya vijiji imepatikana katika maeneo mbalimbali katika sehemu hiyo ya Alps, hata katika umbaliwima wa yapata meta 2,000. Vijiji vya kilimo vya kipindi hicho vilifanyizwa kwa nyumba tatu ama nne, labda dazani kadhaa vikiwa vingi zaidi. Nyumba za aina gani? Uchimbuzi umefunua tu sakafu, sikuzote karibu za udongo uliosindiliwa. Makao yalikuwa na chumba kimoja, kwa ujumla kikiwa na meko katikati na nyakati nyingine jiko la kuokea. Dari huenda ilikuwa imechongoka, sawa na makao yaliyokuwa yamejengwa juu ya viguzo vya chuma na mbao yaliyopatikana katika baadhi ya maziwa ya Alpine. Kila kibanda kimoja huenda kilikaa familia moja.
Ni uhusiano wa aina gani uliokuwako kati ya jamii hizo za wafugaji na za wakulima? Bila shaka, ni biashara. Kwa kielelezo, shoka lililopatikana juu ya Mlima Similaun lafanana na yale yaliyotengenezwa kuelekea kusini, katika fuo za Ziwa Garda, na huenda ilikuwa bidhaa ya mbadilishano wa kibiashara. Pia miongoni mwa zana za Ötzi kulikuwa mawe magumu kadhaa, bidhaa za zamani katika biashara ya kandokando ya barabara ya Bonde la Adige. Mmoja wa utendaji ambao ulichangia mihamo mikubwa ulikuwa uhamaji wa kimsimu wa mifugo. Kama wafanyavyo bado katika Tirol leo, wachungaji waliongoza makundi yao kupitia mipito ya Alpine katika kutafuta malisho mabichi. Ni mikataa gani mingine imefikiwa kuhusu chimbuko la Mwanabarafu?
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari kuhusu kutotegemeka kwa jaribio la kaboni 14, ona Amkeni! la Septemba 22, 1986, kurasa 21-26, (Kiingereza) na Life—How Did It Get Here?—By Evolution or by Creation?, ukurasa 96, vilivyotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 5]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mwanabarafu alipatikana ndani ya Barafuto ya Similaun mpakani mwa Italia
GERMANY
AUSTRIA
Innsbruck
SWITZERLAND
SLOVENIA
ITALY
Bolzano
Similaun Glacier
Adriatic Sea
[Picha katika ukurasa wa 7]
X yatia alama mahali hususa Ötzi alipopatikana. Picha ndogo: 1. Shoka la shaba, 2. Jambia la jiwe gumu, 3. Yawezekana kuwa ni hirizi, 4. Pembe ya paa katika kishikio cha mti
[Hisani]
Fotos 1-4: Archiv Österreichischer Alpenverein/Innsbruck, S.N.S. Pressebild GmbH
Foto: Prof. Dr. Gernot Patzelt/Innsbruck