Machozi ya Asili
NI MAPEMA asubuhi, na hewa ni baridi na tuli. Kila jani na unyasi wametameta kwa vitone, vinavyong’aa kwenye mwanga wa kwanza wa siku. Kwa njia moja, yaonekana kana kwamba majani yametoa machozi ya shangwe katika kuamkua maawio ya jua. Si ajabu kwamba umande umechochea washairi—na wapiga picha.
Hata hivyo, umande hufanya zaidi ya kuburudisha roho ya binadamu. Tukio hili la kianga, lililo la kawaida kotekote kwenye sayari isipokuwa katika ncha za kaskazini na kusini, ni blanketi la unyevu wenye kutegemeza uhai. Yehova Mungu alibuni anga katika njia ya kwamba linapokuwa baridi wakati wa usiku chini ya hali fulani, hufikia kile kinachoitwa kiwango cha umande. Hii ni halijoto ambayo katika hiyo hewa haiwezi kushikilia unyevu wayo zaidi ya hapo na huubwaga kwenye nyuso zilizo baridi kuliko hewa inayozunguka. Kupitia majani yayo, mimea yenye kiu imejulikana kufyonza maji mengi ya umande kufikia kiwango kipatacho uzito wayo, mengi yayo yakiondolewa kupitia mizizi yayo kwa ajili ya uhifadhi mchangani.
Katika mabara ya Biblia, ambapo kuna misimu mirefu ya ukame, umande yaelekea waweza kuwa chanzo pekee cha maji kwa mimea. Hivyo katika Biblia, umande mara nyingi huhusianishwa na pato la mimea—na ukosefu wa umande, na njaa.
Umande waweza pia kuwa na maana ya kibinafsi zaidi. Katika wimbo wake wa kuaga kwa watu wa Mungu, Musa aliandika hivi: “Mafundisho yangu yatadondoka kama mvua, maneno yangu yatatona-tona kama umande; kama manyunyu juu ya majani mabichi; kama matone ya mvua juu ya mimea.” (Kumbukumbu la Torati 32:2) Musa alisema maneno yaliyokuwa yenye kutoa uhai kama umande. Kwa kuwa alikuwa mpole zaidi ya wanadamu wote, ni hakika kwamba yeye alikuwa kwa kawaida mwanana na mwenye ufikirio katika usemi wake vilevile. (Hesabu 12:3) Kama umande au manyunyu, maneno yake yalijenga bila kusababisha uharibifu.
Wakati ujao ushangazwapo na uvutio mwanana wa umande wa asubuhi—machozi ya asili yenyewe—huenda ukataka kufikiria kwa uzito hekima yenye kutisha ya Muumba wa umande.