Gari Lako—Kimbilio au Mtego?
“Baada ya karibu kila msiba,” yaonya FEMA (U.S. Federal Emergency Management Agency), “vikundi vya uokoaji hupata majeruhi ambao wangaliokoka ikiwa wangalijua ama kukaa ndani ya magari yao au kuyaacha.” Ndiyo, uamuzi wenye kosa waweza kukugharimu uhai wako. Je, wajua la kufanya katika tukio la msiba? Jibu chemsha-bongo lifuatalo halafu ulinganishe majibu yako na yale yaliyo chini.
1. TETEMEKO LA DUNIA
□ Kaa ndani ya gari
□ Toka ndani ya gari
2. CHAMCHELA
□ Kaa ndani ya gari
□ Toka ndani ya gari
3. UPEPO MKALI WENYE THELUJI
□ Kaa ndani ya gari
□ Toka ndani ya gari
4. FURIKO
□ Kaa ndani ya gari
□ Toka ndani ya gari
MAJIBU:
1. Tetemeko la dunia: KAA NDANI YA GARI.
Ingawa mfumo wa maelezi wa gari utasababisha litikisike kwa nguvu mno, yaelekea uko salama kabisa ndani—mradi hauko karibu na majengo, madaraja yavukayo juu ya barabara, au waya za umeme.
2. Chamchela: TOKA NDANI YA GARI.
Ndani ya gari yaelekea ndipo mahali hatari zaidi ya pote kuwapo wakati wa chamchela. Lakini namna gani ikiwa hakuna maficho salama karibu? FEMA yasema hivi: “Lala ukiwa umenyooka katika shimo au mbonyeo mwingine wowote wa ardhi mikono yako ikiwa juu ya kichwa chako.”
3. Upepo mkali wenye theluji: KAA NDANI YA GARI.
Isipokuwa waona kimbilio katika umbali wa kiasi, ni vyema zaidi kungojea uokoaji. Injini yaweza kuwashwa kwa vipindi vifupi ili kuandaa joto, lakini acha dirisha likiwa limefunguka kidogo ili kuzuia kusumishwa kwa kaboni monoksaidi. Acha taa ya ndani ikiwa imewaka kuwa kiashirio kwa waokoaji.
4. Furiko: TOKA NDANI YA GARI.
“Ikiwa gari lakwama katika maji ya furiko,” yaonya FEMA, “toka nje mara moja na uende kwenye ardhi iliyoinuka. Maji ya furiko huenda yakaendelea kupanda na gari laweza kufagiliwa mbali wakati wowote.” Usijasirie. Maji yaweza kuwa ya kina kuliko yaonekanavyo, na viwango vyayo vyaweza kupanda kwa uharaka.
FEMA yashauri kwamba uweke habari hii kwenye kijichumba cha kuwekea glovu cha gari lako. na pia hupendekeza kwamba katika kila hali, “kanuni ya maana zaidi ni: Usiwe na wasiwasi.”