Jinsi ya Kununua Gari Lililotumiwa
NANI hangependa kununua gari kwa nusu au chini ya nusu ya bei ya gari jipya? ‘Je, hilo lawezekana kweli?’ waweza kuuliza. Ndiyo—ikiwa lilimilikiwa mbeleni au kama lijulikanavyo sana gari lililotumiwa. Tatizo ni kwamba watu wengi hawaoni faida ya kununua gari lililotumiwa. Magari, sawa na mashine nyingine, huharibika. Hivyo, thamani ya gari hupungua kwa kutegemea umri, umbali ambao limesafiri, na jinsi ambavyo limetumiwa.
Je, naweza kujijulisha kwenu? Mimi nimekuwa fundi wa magari kwa zaidi ya miaka 15. Kwa hiyo acheni niwajulishe baadhi ya mambo ambayo nimejifunza. Yafuatayo ni maswali machache upaswayo kujiuliza kabla ya kununua gari lililotumiwa.
Naweza Kutumia Fedha Kiasi Gani?
Kwanza, hesabu kiasi uwezacho kutumia kununua gari. Matangazo ya biashara katika magazeti yaweza kukusaidia kujua ni gari la mwaka gani na la aina gani lilinganalo na kiasi unachokusudia kulipa. Katika nchi fulani, mabenki, mashirika ya kukopesha, na maktaba fulani yana miongozo ya kila mwezi inayoorodhesha bei za magari yaliyotumiwa. Hakikisha unahesabu si bei ya gari tu bali pia gharama za kodi, usajili, na bima. Pia panga uwe na pesa kiasi fulani kwa ajili ya marekebisho yasiyotazamiwa ambayo huenda gari litahitaji baada ya kulinunua.
Nahitaji Gari la Aina Gani?
Unapoamua unachohitaji, tambua kilicho cha maana kwako. Fikiria ukubwa wa familia yako na shughuli mbalimbali ambazo gari litatumiwa kutimiza, kama vile kwenda nalo kazini, kuwasafirisha watoto shuleni, na kwenda katika huduma ya Kikristo. Je, hilo gari litatumiwa kwa ajili ya safari fupi-fupi au zile ndefu? Usifikirie tu aina au muundo fulani; badala ya hivyo, tafuta gari lililotunzwa vizuri na lililo katika hali nzuri. Tafuta gari lililo rahisi kurekebisha. Magari yote yatahitaji spea hatimaye. Je, kuna duka la spea zinazotakikana katika eneo lenu? Spea za magari ya zaidi ya miaka kumi iliyopita zaweza kuwa vigumu kupatikana. Ikiwa una pesa kidogo, epuka kununua magari ya starehe au yaliyonunuliwa kutoka nchi nyingine, kwa kuwa lazima spea na marekebisho yatakuwa ya gharama zaidi. Ingawa huenda magari hayo yakawa yenye kutegemeka sana, yaweza pia kuwa gharama kubwa kuwa nayo.
Je, Ni Gari Zuri?
Gari zuri ni lile ambalo limedumishwa vizuri. Kwa ujumla yafaa kuepuka magari ambayo yamesafiri sana—hasa ikiwa limesafiri kwenye mji badala ya kwenye barabara kuu. Maoni kuhusu umbali wa kusafiri hutofautiana mahali mahali. Hakuna gari lililotumiwa lililo kamilifu. Hata hivyo, je, utaweza kulipia marekebisho yanayohitajiwa kwa gari lako? Kwa kawaida, marekebisho hayataongeza thamani ya gari lako. Kwa mfano, ukinunua gari la dola 3,000 na kisha utumie dola 1,000 kwa marekebisho yahitajiwayo, haimaanishi kuwa hilo gari litakuwa la thamani ya dola 4,000. Kwa kawaida, kununua gari lililo katika hali nzuri hugharimu kiasi kidogo kuliko kununua gari bovu na kulitengeneza.
Hapa pana madokezo machache ya kuchagua gari zuri:
• Lichunguze gari kabisa kabla ya kulinunua. Ili kuwa na picha kamili, epuka kulitazama gari wakati wa usiku au kwenye mvua. Lizunguke gari. Walionaje? Je, sehemu za ndani na nje zaonyesha kwamba mwenye gari wa awali alilithamini na kulitunza hilo gari? Je, sehemu hizo zimetunzwa vyema? Je, muuzaji aweza kuandaa rekodi ya udumishaji uliofanywa katika hilo gari? Ikiwa sivyo huenda hilo gari lilipuuzwa. Huenda usitake kuliangalia gari hili zaidi.
• Lijaribu gari kwa kuliendesha. Ongeza mwendo wa gari haraka kufikia mwendo wa barabara kuu katika jaribu la kuliendesha. Pia lisimamishe na kisha kuliendesha tena mara kadhaa katika milima-milima na kwenye barabara tambarare.
Injini:
Je, injini huanza ifaavyo?
Je, bomba linatoa moshi mchache istahilivyo?
Je, injini inafanya kazi vizuri?
Je, injini inafanya sawa hata ikiwa haijawekwa gea?
Je, injini haina makelele?
Je, injini ina nguvu za kutosha kuongeza mwendo upesi?
Ikiwa jibu ni la kwa lolote la maswali yaliyopo juu, basi huenda injini ikahitaji marekebisho madogo-madogo au hata marekebisho makubwa. Hali hizi pia zaweza kuwa ishara za injini iliyochakaa. Uwe mwangalifu ikiwa muuzaji asema kwamba lahitaji marekebisho madogo-madogo tu. Marekebisho hayo madogo-madogo yalipaswa kuwa sehemu ya utunzaji wa kawaida wa gari.
Transmisheni:
Je, transmisheni ifanyayo kazi yenyewe huteleza au kukosa kuingiza gea?
Je, hiyo hushindwa kubadili gea kwa wepesi?
Je, kuna makelele ya kusaga katika zozote za gea hizo?
Ikiwa jibu ni ndiyo kwa lolote la maswali haya, huenda transmisheni ikahitaji kufanyiwa marekebisho.
Breki na saspensheni:
Je, hilo gari huelekea upande mmoja uliendeshapo au upigapo breki?
Je, hilo gari hutetema lifikapo mwendo fulani au upigapo breki?
Je, kuna makelele upigapo breki au kugeuka au uendeshapo kwenye barabara zenye matuta?
Ikiwa jibu ni ndiyo kwa lolote la maswali haya, huenda gari likahitaji kurekebishwa breki na saspensheni.
• Tafuta sehemu nyingine zinazohitaji kurekebishwa. Vaa nguo zitakazokuwezesha kulitazama gari ndani, nje, na chini.
• Lichunguze gari ikiwa lina kutu. Epuka magari yaliyo na kutu. Yaliyo mengi ya magari ya majuzi yamejengwa kwa “muungano.” Sehemu za bodi hutumika kushikilia sehemu mbalimbali ili kuzitia nguvu. Sehemu hizi zishikapo kutu, kwa ujumla huwa gharama kubwa kuzirekebisha kikamili. Kutu kwenye kingo yaweza kuwa juu juu tu lakini kwa kawaida ni ishara ya kwamba maeneo fulani pia yana kutu. Angalia ikiwa kuna kutu kwenye sehemu ya chini ya gari. Uwe mwangalifu ikiwa gari limepakwa rangi majuzi; hilo gari laweza kuwa kaburi lililopakwa chokaa.
• Tafuta uharibifu uliosababishwa na aksidenti. Angalia ikiwa kuna uharibifu uliosababishwa na aksidenti uliojificha chini ya boneti na kwenye buti. Je, milango, boneti, na buti hufungika vizuri? Je, kuna ishara za rangi iliyopakwa pasipofaa, kama vile kwenye vishikilio vya milango? Je, kuna mvujo katika buti au maeneo yaliyofunikwa? Mivujo hiyo yaweza kusababisha kutu.
• Chunguza mafuta ya injini. Angalia kijiti cha kuchunguza mafuta. Je, kiwango cha mafuta kiko chini? Hilo laweza kuwa tokeo la matumizi ya juu ya mafuta au kuvuja. Je, mafuta yana uchafu mwingi au ni meusi sana? Je, mafuta yaonekana kuwa na mchanga? Tafuta uone ikiwa kuna mafuta yanayozingira kuzunguka vifuniko vya vali. Ingia ndani ya gari, na kuliwasha lakini usilianzishe. Je, ile taa ya kuonya kwamba hakuna kanieneo ya mafuta ya kutosha yawaka? Ikiwa gari lina kipimio cha kanieneo la mafuta, chapasa kuonyesha kipimo cha sufuri. Sasa anzisha injini, na uache ingurume polepole na uangalie ile taa ya kanieneo ya mafuta inachukua muda gani kabla ya kuzimika au kile kipimio kuonyesha kanieneo ya kawaida ya injini. Ikichukua muda uzidio sekunde chache kwa taa hiyo kuzimika au kipimio kuonyesha kipimo cha kawaida kwaweza kuonyesha kwamba injini imechakaa sana. Kwenye magari mapya zaidi ya Marekani, taa ya “Chunguza Injini” au “Rekebisha Injini Upesi” yapaswa kuwaka gari liwashwapo bila injini kufanya kazi. Taa hiyo yapaswa kuzimika injini ifanyapo kazi. Ikiwa nuru hiyo yaendelea kuwaka injini ikifanya kazi, hili kwa kawaida hudokeza kwamba kuna kasoro katika injini, labda katika mfumo upunguzao uchafuzi wa hewa au katika upitishaji mafuta ya gari.
• Angalia umaji-maji wa transmisheni ifanyayo kazi yenyewe. Je, ni mdogo au umeungua? Chunguza ikiwa kuna mivujo chini ya transmisheni. Hali hizi zaweza kudokeza uhitaji wa marekebisho makubwa ya transmisheni. Ikiwa gari laendeshwa kwa magurudumu ya mbele, angalia chini yalo uone ikiwa vifuniko vya mpira vinavyolinda miungano yenye kasimwelekeo isiyobadilika vimepasuka. Ikiwa ndivyo, bereu yaweza kutupwa nje na hilo laweza kusababisha uharibifu wa haraka katika hiyo miungano, ambayo hugharimu sana kurekebisha.
• Chunguza magurudumu yote manne. Ikiwa yameisha sana tarajia kuyabadili. Ikiwa yameisha isivyo kawaida, huenda ikawa kwamba kuna uhitaji wa kunyooshwa au kubadilisha sehemu za usukani.
• Chunguza mfumo wa usukani-nguvu. Je, umaji-maji waonekana kuwa mweusi au mdogo? Anzisha gari na ugeuze usukani mara kadhaa toka upande mmoja hadi ule mwingine. Kufanya hivyo kwapasa kuhitaji nguvu zilezile ili kugeuza kushoto na kuume. Je, kuna vizuizi vyovyote ugeuzapo usukani? Kutenda kwa usukani-nguvu kwapaswa kuwa kunyamavu kwa kadiri. Matatizo yoyote katika kuutumia yaweza kumaanisha marekebisho ya gharama kubwa.
• Uchunguzi mwingine mbalimbali.
Chunguza hali ya mishipi na ya mabomba.
Chunguza utendaji wa breki za mkono kwenye kilima.
Chunguza ikiwa kikanyagio cha breki kimechakaa isivyo kawaida.
Chunguza hali ya mfumo wa bomba la moshi. Je, una makelele? Je, umelegea?
Chunguza vifyonza-mtikiso na springi. Je, gari laonekana likiwa chini sana, au usukumapo pembe moja ya gari baada ya nyingine, je, gari hurukaruka zaidi ya mara tatu?
Ikiwa kuna kisafisha hewa, je, kinafanya kazi kwa vipimo vyacho mbalimbali?
Je, taa, vifuta-maji, honi, mishipi ya viti, na madirisha yafanya kazi?
Chunguza chini ya sehemu ya nyuma ya gari ikiwa kuna ishara zozote kwamba wakati mmoja lilikuwa na kifundo cha kukokota. Ikiwa ndivyo, yapendekezwa utahadhari, kwa kuwa kukokota kwaweza kuwa kumeweka mkazo wa kupita kiasi kwenye transmisheni.
Ukikosa uhakika kwa yoyote ya uchunguzi uliotajwa katika makala hii, laweza kuwa jambo la hekima gari lako lichunguzwe na fundi stadi wa magari kabla hujalinunua. Mwombe aliangalie gari zima na kutengeneza orodha ya yafuatayo:
1. Marekebisho ambayo gari lahitaji mara moja na kadirio la bei ya spea na gharama ya utengenezaji.
2. Marekebisho ambayo gari huenda likahitaji katika mwaka ufuatao na kadirio la bei ya spea na gharama za utengenezaji.
Ukaguzi huu ukifanywa na fundi stadi wa magari wapaswa kuchukua muda unaopungua saa moja. Ingawa huenda hili likakugharimu gharama ya kufanyiwa kazi inayolipwa kulingana na wakati unaotumiwa, hiyo gharama ni kidogo ikilinganishwa na bei isiyojulikana ya marekebisho yahitajiwayo. Mwulize muuzaji, gari limefanyiwa marekebisho gani majuzi. Omba kuona rekodi ya utunzaji. Je, mafuta ya injini na kichujio chayo yalibadilishwa kwa ukawaida? Je, transmisheni ifanyayo kazi yenyewe imepata kurekebishwa? Mara ya mwisho hilo gari kufanyiwa marekebisho madogo ilikuwa lini? Kumbuka kwamba gari zuri ni lile ambalo limetunzwa na lisilohitaji marekebisho mengi.
Kaa na kuhesabu gharama kwanza—ukiwa na mambo yote ya hakika na tarakimu za gari. Kisha uamue ikiwa hilo gari lastahili na ikiwa una fedha za kutosha si kwa ajili ya gari tu bali pia gharama nyingine mbalimbali.—Imechangwa na fundi wa magari.
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Waweza kuwaje na uhakika kwamba gari lililotumiwa unalonunua ni zuri?
Yaliyoonyeshwa hapa ni machache kati ya mambo unayohitaji kufikiria
Fundi wa magari achunguze gari kabla hujalinunua
Je, mafuta ya injini na kichujio chayo yalibadilishwa kwa ukawaida?
Tafuta ikiwa kuna uharibifu wa aksidenti. Je, milango, boneti, na buti vyajifunga vizuri?
Magurudumu yaliyoisha isivyo kawaida yaweza kudokeza matatizo makubwa katika kunyooka kwa magurudumu au usukani