Jilinde Dhidi ya Wezi wa Magari!
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI
WIZI au utekaji wa magari, ni tatizo linalozidi kukua katika majiji ulimwenguni pote, toka Karachi hadi Lisbon, Nairobi hadi Rio de Janeiro. Kulingana na Idara ya Marekani ya Takwimu za Sheria, kati ya 1993 hadi 2002, kila mwaka kulikuwa na visa 38,000 vya wizi wa magari nchini Marekani.
Nchini Afrika Kusini, ambako idadi ya watu ni asilimia 17 hivi ya idadi ya watu huko Marekani, kuna idadi kubwa zaidi ya visa vya wizi wa magari kwani kila mwaka kuna visa zaidi ya 14,000. Ukifikiria mifano kadhaa, utaelewa sababu inayowafanya wengi waone wizi wa magari kuwa uhalifu unaoogopesha zaidi. Yafuatayo ni matukio halisi yaliyowapata wakaaji kadhaa wa Johannesburg, jiji kubwa zaidi la Afrika Kusini. Baada ya kusoma kuhusu yaliyowapata, huenda ukajua la kufanya unapokumbana na wezi wa magari, au jinsi unavyoweza kupunguza hatari ya kushambuliwa.
Matukio Halisi
◼ “Mimi na rafiki yangu Susan tulikuwa tumetumika pamoja kwa mwaka mmoja katika kazi ya kuhubiri. Jumatano moja, kabla ya kuelekea kwenye funzo fulani la Biblia kwa kutumia gari, tulisimama ili kunywa chai chini ya mti mkubwa kando ya barabara katika mtaa wa makazi. Susan alitoka garini ili achukue kikapu kilichokuwa nyuma ya gari. Alipokuwa akinipa kikombe, wanaume wawili walitokea ghafula, na mmoja wao akamwekelea Susan bunduki shingoni. Nilishtuka, nami nikajaribu kutoka garini, lakini yule mwanamume mwingine akanisukuma ndani. Wazia yaliyotupata, sisi wanawake wawili tulilazimishwa kuingia garini na kuendeshwa na wanaume wawili—kwa hakika nilidhani watatulala kinguvu au kutuua.”—Anika, mke kijana.
◼ “Nilikuwa nikiendesha gari kuelekea kazini saa moja asubuhi. Nilisimama kwenye makutano ya barabara ambapo watu wengi wanaotafuta kazi husimama. Sikujishughulisha na kilichokuwa kikiendelea hadi mtu fulani alipoingiza bunduki kwenye dirisha lililokuwa wazi la gari langu na kuiwekelea shingoni pangu, kisha akaniambia, ‘Toka nje, au nitafyatua risasi.’ Dakika hiyohiyo helikopta ya trafiki ikatokea angani. Akifikiri ni polisi, mwizi huyo wa magari alifyatua bunduki na kukimbia. Alinipiga risasi shingoni, na kunikata uti wa mgongo. Nilipooza kuanzia shingoni kwenda chini. Siwezi kutumia mikono wala miguu yangu, nayo haina hisia zozote.”—Barry, baba ya mvulana fulani.
◼ “Mimi na mke wangu, Lindsay tulikuwa tukikaribia kwenda kula chakula cha mchana. Nilikuwa nikimsubiri garini mwangu. Milango ya gari ilikuwa imefungwa, lakini madirisha yalikuwa yamefunguliwa kidogo kwa sababu ya joto. Nikiwa nimeketi kwenye kiti cha dereva nikitazama mbele, wanaume wawili walitokea huku wakitembea taratibu sana. Walipokuwa hatua nane hivi kutoka kwenye gari, mmoja alielekea kushoto na mwingine kulia. Kwa ghafula, walikuwa milangoni mwa gari wakinielekezea bunduki na kuniamrisha. Baada ya kuwatii na kupiga gari moto, kwa sauti waliniambia nitoke na kwenda kwenye kiti cha nyuma. Mmoja wao aliendesha gari na yule mwingine akanilazimisha niinamishe kichwa changu. ‘Unaweza kunipa sababu yoyote kwa nini nisikuue?’ akauliza. ‘Mimi ni Shahidi wa Yehova,’ nikamjibu. Aliendelea kusema kuhusu kuniua, nami nikaendelea kusali nikimfikiria mke wangu mpendwa, nikiwazia jinsi atakavyotenda atakapogundua kwamba mume wake ametoweka na gari lake.”—Alan, mwangalizi anayesafiri ambaye pia ni mzazi.
Masimulizi hayo yanaonyesha jinsi wizi wa magari unavyoweza kutokea haraka na bila kutarajiwa. Yanaonyesha pia hali ambazo huwavutia wezi wa magari. Siku hizi katika maeneo mengi si salama kungoja mtu au kupumzika ndani ya gari lililoegeshwa kwenye barabara za mitaa ya makazi. Maeneo mengine hatari ni makutano ya barabara na vijia vya kuingia nyumbani.
Kukabiliana na Matokeo
Kwa kupendeza, kisa cha Susan na Anika kilimalizika vema. Wezi hao walipokuwa wakisafiri nao, wanawake hao wawili walianza kuwaeleza kuhusu kazi yao ya kufundisha Biblia. Yaelekea hilo lilianza kusumbua dhamiri zao. “Waliomba msamaha kwa yale waliyokuwa wakifanya,” anaeleza Anika, “lakini wakasema kwamba kwa sababu ya nyakati tunazoishi wao hulazimika kuiba na kuteka magari ili kujiruzuku. Tuliwaeleza kinachomfanya Mungu aache watu wawe maskini na wateseke.” Ujumbe wa Biblia uligusa mioyo ya wezi hao wawili, nao wakaamua kuwarudishia pesa na saa za mkononi walizokuwa wamechukua, na kuwahakikishia Susan na Anika kwamba hawatawaumiza. “Kisha mmoja wao akaanza kutupa maagizo ya jinsi ya kuepuka kushambuliwa tena na wezi wa magari,” anakumbuka Susan. “Walitushurutisha tuahidi,” aongeza Anika, “kwamba hatutasimama tena kamwe kando ya barabara ili kunywa chai.” Kisha, kama wezi hao walivyokuwa wamewaambia, walilisimamisha gari, wakatoka nje, wakachukua vichapo fulani vya Biblia, na kuwaacha Susan na Anika waende zao salama.
Alan, yule mwangalizi anayesafiri, aliamrishwa atoke garini mwake wezi hao walipofika mahali pasipokuwa na watu. Ingawa alipoteza vitu vyenye thamani, anafurahi kwamba alinusurika bila majeraha yoyote. “Nafikiri kwamba sikuumia sana,” anakumbuka Alan, “kwa kuwa nilitii, sikushindana nao, nami sikuwa na wasiwasi. Lakini ningalikuwa mwenye utambuzi zaidi. Tukio hilo limenifunza kwamba ni lazima tuwe macho nyakati zote hasa wakati huu ambapo tunaishi mwishoni mwa siku za mwisho za mfumo mbovu wa Shetani.” Siku iliyofuata, Alan na Lindsay walirudi kwenye eneo hilohilo ili waendelee kuhubiri pamoja na kutaniko walilokuwa wamegawiwa kutumikia. Alan anaeleza: “Tulisali, nayo macho yetu yalikuwa yakizunguka huku na huku siku nzima. Haikuwa rahisi lakini Yehova alitupa ‘nguvu zinazopita zile za kawaida.’”—2 Wakorintho 4:1, 7.
Barry, ambaye aliathiriwa vibaya zaidi amekuwa akitumia kiti cha magurudumu kwa miaka 11 iliyopita. Barry amefanya vema kwani amedumisha mtazamo unaofaa na hajaacha tukio hilo limtie uchungu. Imani yake katika ahadi ya Yehova Mungu kuhusu ulimwengu mpya wenye uadilifu haijadidimia. (2 Petro 3:13) Barry anaendelea kuhudhuria mikutano ya Kikristo kwa ukawaida naye hutumia kila nafasi kuwahubiria wengine. Anasema: “Sikuzote kumtumikia Yehova kumeniletea shangwe. Hata ingawa mimi huketi kwenye kiti cha magurudumu na siwezi kujifanyia mengi, mara nyingi mimi hufikiria yale ambayo Yehova amenifanyia, na hilo huniwezesha kuvumilia. Hivi karibuni, mfumo huu mwovu utakwisha, na itakuwa siku bora kama nini nitakapoweza kutembea tena!”—Isaya 35:6; 2 Timotheo 3:1-5.
Serikali ya Afrika Kusini imechukua hatua ambazo zimesaidia kupunguza visa vya wizi wa magari. Hata hivyo, bado unaendelea na unazidi kuongezeka katika sehemu nyingine za ulimwengu. Wakristo wa kweli wana hakika kwamba Ufalme wa mbinguni wa Mungu ndiyo serikali pekee itakayomaliza uhalifu na jeuri yote ya aina hiyo.—Zaburi 37:9-11; Mathayo 6:10.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]
PUNGUZA HATARI YA KUSHAMBULIWA NA WEZI WA MAGARI
◼ Ikiwa unaendesha gari kwenye maeneo ambamo visa vya wizi wa magari vimetukia, funga milango na madirisha ya gari lako.
◼ Unapopunguza mwendo ili usimame kwenye makutano ya barabara, uwe macho kuwaona watu wanaozurura-zurura pande zote za barabara.
◼ Kudumisha nafasi ya kutosha kati yako na gari lililo mbele yako kutafanya iwe rahisi kugeuza gari na kukimbia hatari.
◼ Gari lako likigongwa nyuma, uwe mwangalifu kuona hatari inayoweza kutokea iwapo utatoka garini mwako. Huenda huo ukawa mtego. Hilo likitukia katika eneo hatari, huenda ikawa afadhali zaidi kuendesha gari hadi kwenye kituo cha polisi kilicho karibu.
◼ Uwe macho kuwaona watu usiowajua karibu na lango la nyumba yako. Ukiwaona, afadhali uendelee na safari yako na urudi nyumbani baadaye, au unaweza kuamua kwenda kwenye kituo cha polisi kilicho karibu.
◼ Ukihitajiwa kungoja ndani ya gari lililoegeshwa katika eneo lenye hatari au katika mtaa wenye watu wachache, uwe macho kuona mambo yanayotukia mbele na nyuma yako. Ukihisi kuna hatari, piga gari moto na uende kwenye mtaa mwingine kisha urudi iwapo ni salama kufanya hivyo.
[Picha katika ukurasa wa 14]
Barry amedumisha mtazamo unaofaa licha ya kulazimika kutumia kiti cha magurudumu nyakati zote