Kuzuru Soko la Ngamia la Omdurman
“IKO wapi Mowaleeh?” twauliza. Gari letu lenye kujipeleka kwa magurudumu yote manne limetuchukua kutoka jiji kuu, Khartoum, hadi kwenye ukingo wa magharibi wa Omdurman ya kale, jiji kubwa kupita yote katika Sudan.
Hakuna ishara za barabara, isipokuwa mzingo wa vijia vya mchanga. Kwa hiyo twawauliza wanaume wanaopanda punda zao kama ilivyo juu. Wanyama wao wa mizigo wamebeba mitungi ya maji ya kunywa. Wapandaji ni wenye kusaidia na wanatuelekeza upande ufaao. Baada ya kilometa zingine nane, twaendesha gari letu kupita juu ya fungu la mchanga lililo juu na twaona mandhari yenye kutazamisha, soko la ngamia la Omdurman, ile Mowaleeh.
Kwa Nini Hapa?
Hii ni tofauti kabisa na maduka ya kununua bidhaa yenye mfumo wa upishaji hewa safi katika nchi za Magharibi. Soko hilo hufanya kazi nje chini ya anga lenye joto la Jangwa la Sahara. Likiwa na ukubwa wa yapata kilometa tatu za mraba, bila mipaka iliyo dhahiri, halina miti wala mimea. Kwa hakika, kuna mchanga kwa umbali uwezao kuonwa na macho. Lakini pia waweza kuona ngamia kwa mamia na wachungaji waliovalia mavazi ya kitaifa yanayoitwa jalabeeya.
Tukiwa twatazama vumbi jembamba la manjano likivuma kuvuka jangwa lisilo na utulivu twajiuliza ‘Kwa nini waliweka soko hili hapa?’ Muda si mwingi jibu lawa wazi. Likikatiza upeo wa macho tambarare usiobadilika, tangi kubwa mno la maji linaloning’inia ambalo hujazwa kwa maji kutoka katika kisima ambacho maji yacho huja juu bila kutumia bomba laweza kuonekana. Chanzo hiki cha maji yenye thamani hufanya hapa pawe mahali pafaapo kwa soko kama hilo. Kutoka hapa, wengi wa hao wanyama watapelekwa nje hadi Misri na Libya.
Tukiwa twakaribia, twakaribishwa na wachungaji wenye kutabasamu wa Kiarabu. Kila mwenye ngamia huzikusanya ngamia zake pamoja. Twaona kwamba wengi wa hao wanyama miguu yao ya mbele ya kushoto imefungwa ikiwa imekunjwa. Kwa nini wao husababisha ulemavu wa muda kwa wanyama wao? Kuna wazo la kishirikina kwamba mguu wa kushoto ni wa Shetani! Licha ya ushirikina, kufunga mguu mmoja huzuia huyo mnyama kutokana na kuranda-randa na hufanya iwe rahisi kwa wateja kuwachunguza.
Wenye Kutafutwa Sana
Kwa nini ngamia ni bidhaa yenye kutafutwa sana hivyo? Kwa sababu amejiandaa vilivyo kwa hali ngumu za jangwani; hutumika vyema akiwa namna ya usafirishaji katika mahali hapa pakame. Mianzi yake ya pua, mirefu iliyo kama mpasuko hujifunika haraka katika dharuba ya jangwa. Masikio yake yako karibu na upande wa nyuma ya kichwa chake na yamejawa na nywele ambazo huzuia mchanga kuingia. Nundu lake kubwa, linalofanyizwa hasa kwa shahamu, hutumika kuwa hifadhi ya chakula wakati wa safari ndefu. Sugu zilizo kwenye kifua na magoti yake humkinga kutokana na mchanga ulio na moto na wadudu wenye kudhuru. Na zaidi, ngamia wanaweza kula mimea ya jangwani iliyo migumu na yenye miiba kuliko yote ambayo mtu aweza kupata na wanaweza kusafiri kwa siku kadhaa bila kunywa maji.a
Kwa kupendeza, ngamia wengi hawatumiki kuwa njia ya usafirishaji. Wengine wananunuliwa tu kuwa mali yenye thamani ya kudumu. Kwani, hadi hivi majuzi, ngamia walitumiwa kulipia mahari! Wengi wa wanyama hawa huishia kwenye sahani. Katika Omdurman kwenyewe, mahali kadhaa pa kula huwa mahali maalum pa nyama iliyochomwa ya ngamia. Chakula kingine kipendwacho sana, maakuli ya nyama ya ngamia yaliyokolezwa kwa chumvi yaitwayo basturma, mara nyingi hutengenezwa kutokana na nyama ya ngamia na huonwa kuwa chakula kitamu zaidi katika Misri na nchi nyinginezo za Mashariki ya Kati.
Si ajabu basi, soko la ngamia la Omdurman linakuwa mahali pa shughuli nyingi za utendaji wakati ngamia hawa wa Uarabuni wenye nundu moja waletwapo mara mbili kwa juma, hasa kutoka magharibi mwa Sudan. Wanunuzi yaelekea wanasongwa na wachungaji Waarabu ambao wana nia ya kuonyesha makundi yao.
Upiganiaji-Bei Mkali
Mnunuzi anayetarajia kununua kwanza atachunguza hao wanyama kwa jicho lililozoezwa na lenye ujuzi. Atashika nundu ili kuona ikiwa kuna hifadhi nzuri ya shahamu. Hata hivyo, ngamia huwekewa bei kulingana na saizi na umri wao. Ngamia wa mwaka mmoja huitwa heowar, wa miaka miwili huitwa mafrood, na wad laboon ni utambulisho wa ngamia wa miaka mitatu. Ingawa hivyo, wanyama wenye thamani zaidi ni wale waliofikia upevu. Ngamia wa kike hufikia kwenye umri wa miaka minne hivi, na wa kiume kwenye umri wa miaka minane hivi. Jike huitwa heek na dume sudaies. Anapoonyeshwa tu wanyama hawa waliokomaa, mnunuzi anayetarajia kununua atawachunguza ili kuamua kama huyo mnyama kwa kweli amefikia upevu.
Mara tu mnunuzi afurahishwapo na ngamia, upiganiaji-bei waanza. Uwezo wa kupigania bei ni ufundi wa lazima katika Mashariki ya Kati! “Be esm Allah” (Kwa jina la Mungu) ni maneno ya kwanza kuongewa. Sasa maafikiano ya bei yaanza. Mazungumzo huendelea kwa utulivu, bila mipaazo yoyote ya sauti, na bila haraka. Ikiwa muuzaji na mnunuzi hawafikii mwafaka, humalizia kwa kusema tu “Yeftaah Allah” (Mungu atafungua fursa nyingine).
Hata hivyo, tumekuja kutazama, si kununua. Tukiwa tumekaa kwa muda mfupi tu katika joto la mchana lenye kuwaka, tuko tayari kwenda nyumbani. Ingawa hivyo, yaonekana ngamia hawasumbuliwi na hilo joto. Kwa hivyo, twakumbushwa jinsi hizi ‘meli za jangwani’ zilivyojitengeneza ili kupatana na mazingira yazo. Hakuna shaka kwamba hili lamaanisha utendaji wa kibiashara ulioendelezwa hapa katika soko la ngamia lenye kuvutia la Omdurman!
[Maelezo ya Chini]
a Ona makala “Ngamia wa Uarabuni—Gari la Afrika Lenye Matumizi Mengi” katika toleo la Amkeni! la Juni 8, 1992 (Kiingereza).