Vijana Huuliza . . .
Kwa Nini Nisiibe?
“Nina umri wa miaka 16 na nina tatizo kubwa mno. Juzijuzi, nimekuwa nikiiba sana. Nilikwenda tu madukani na kuiba jozi saba za vipuli. Nina hofu kumweleza mtu yeyote kuhusu tatizo langu. Tafadhali nisaidieni!”
NDIVYO alivyoandika tineja mmoja aliyetatanika kiakili kwenye safu ya ushauri ya gazeti fulani. Mwandikaji mmoja aliripoti hivi: “Bidhaa zenye thamani ya kukadiriwa ipatayo dola bilioni kumi . . . huibwa, kuporwa, au kubekuliwa kutoka kwenye maduka kila mwaka [katika Marekani]. Matineja ndio hufanyiza yapata nusu ya kufungwa kwa sababu ya kuiba dukani.”
Kulingana na mahojiano ya kupata maoni yatakayochanganuliwa ya hivi majuzi, zaidi ya thuluthi moja ya wanafunzi wa shule ya upili (shule ya sekondari) walikubali kuwa waliiba dukani. Na kulingana na mahojiano mengine kama hayo, yaliyofanywa na watafiti Jane Norman na Myron Harris, “karibu wote [vijana] wanakubali walikuwa wamechukua kitu fulani bila kukilipia kwa wakati mmoja au mwingine.”
Sababu ya Wao Kuiba
Mwivi ni mtu ambaye huchukua kwa kukusudia kitu cha mtu mwingine bila ruhusa. Wakati mwingine huenda uhitaji wa kibinafsi ukafanya wivi uonekane kuwa wenye kufaa. “Nilikuwa katika hali ngumu,” akumbuka kijana mmoja aliyefukarika. “Ningekwenda upande wa nyuma wa [mkahawa] na kupiga teke mlango na kuufungua na kuchukua vipande kadhaa vya kuku. Lakini ni hilo tu. Nilifanya hivyo kwa sababu nilikuwa na njaa.”
Yasema methali ya Biblia: “Watu hawamdharau mwivi, akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa.” Hata hivyo, kuiba ni kosa kiadili. Hivyo mstari ufuatao wa Biblia ulionyesha kwamba hata mwivi aliye na njaa ilimlazimu ‘kulipa’ kwa adhabu kali.—Mithali 6:30, 31.
Ingawa hivyo, la kushangaza ni kwamba ni wachache tu wa wevi matineja wanaoiba kwa sababu ya uhitaji wowote ulio halali. Kielelezo halisi ni Mary Jane ambaye alikiri hivi: “Ndiyo, nimepata kuiba dukani na lilikuwa jambo geni sana, kwa sababu sijui kwa nini nilifanya hivyo. Wazazi wangu hunipa fedha kwa ajili ya kila kitu. Sikuhitaji chochote.”a Gazeti Seventeen liliripoti vivyo hivyo hivi: “Katika uchunguzi uliofanywa na Halmashauri ya Kitaifa ya Kukinga Uhalifu, sababu ya kawaida kupita zote iliyotolewa na wakosaji ilikuwa kwamba walitaka kupata kitu fulani bure.” Vijana wengine hata wametetea mikono yao mirefu kwa kusababu kwamba hayo maduka ‘hulipisha ghali mno!’
Kwa vijana wengi, kuiba ni njia ya kupunguza ukimwa tu. “Lilikuwa tu jambo la kufanya baada ya shule,” akaeleza mmoja aliyekuwa mwivi anayeitwa Jeremy. Kuiba pia yaonekana hutumika kama namna fulani ya mchezo hatari; wengine yaonekana wanapenda ule msisimko unaokuja wanaposhindilia blausi iliyoibwa ndani ya pochi au kuingiza diski-songamano ndani ya shanta.
Ni Kusitiri Maumivu?
Bila shaka, kuna njia salama zaidi za kushindana na ukimwa kuliko kujihatarisha kifungo cha jela. Basi, je, yaweza kuwa kwamba kuna visababishi vinavyochangia utafutaji huo wa msisimko kuliko tamaa ya kupata furaha kidogo? Wastadi wengi huamini kwamba kunavyo. Ladies’ Home Journal lilionelea kwamba vijana fulani “huona ikiwa vigumu kupambana na misongo ya kukua. Mabishano na wazazi wao, mvunjiko wa urafiki, maksi za chini katika mtihani, vyaweza kuwafanya wajihisi wamekosa udhibiti juu ya maisha yao; kuvunja sheria huwarudishia hisi ya kuwa na uwezo.”
Ndiyo, kilichojificha nyuma ya tendo la ushupavu la mwivi huenda kikawa umizo na umivu jingi. Kama Biblia inavyosema, “hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni.” (Mithali 14:13) Uthibitisho waonyesha kwamba kuiba dukani kunakorudiwa-rudiwa kwaweza kuwa ishara ya mshuko-moyo. Wevi fulani wachanga wamepatikana wakiwa na historia ya kutendwa vibaya kingono walipokuwa watoto. Hata kisababishi cha umivu kiwe nini, msisimko wa kuiba huenda ukaonekana kuwa wenye kukandamiza umivu—angalau kwa muda mfupi.b Kwa kielelezo, fikiria kijana mmoja Mmarekani anayepata furaha yake kutokana na kuiba magari na kwenda nayo kwa ajili ya uendeshaji wa kufurahia wa kijahili. “Hufanya uhisi vizuri,” yeye asema. “Unapata hii hisi ya kuogopa, kama unavyohisi kusisimka.”
Marika na Msongo Wao
Biblia husema hivi: “Mashirika mabaya huharibu mazoea yenye mafaa.” (1 Wakorintho 15:33, NW) Ukweli huu unatambuliwa kwa mapana. Mwandikaji Denise V. Lang alionelea hivi: “Ni mara chache sana kijana anapojipata hatarini akiwa peke yake.” Mara nyingi, marika watasaiana kuiba kitu. Kwa kusikitisha, vijana wengi mno hujiacha washindwe na huo msongo.
“Nilijihusisha na kikundi cha wasichana katika shule ya sekondari,” asema Kathy mchanga. Gharama ya uanashirika katika kikundi chao chenye kujitenga ilikuwa nini? Kuiba fulana ya bei ghali. “Nilitaka kuwa katika kikundi hicho, kwa hiyo nilikwenda kwenye duka na kuiba fulana yangu,” yeye aungama.
Kupata Maoni ya Mungu
Lile taraja la kumiliki vitu usivyoweza kulipia, la kufurahia misisimko yenye hatari mno, au la kukubaliwa na marika laweza kufanya kuiba kuonekane kukivutia. Hata hivyo, moja ya zile Amri Kumi katika Biblia ni: “Usiibe.” (Kutoka 20:15) Mtume Paulo aliandika kwamba ‘wevi hawataurithi ufalme wa Mungu.’ (1 Wakorintho 6:9, 10) Maoni ya Mungu yapasa kuwa ya hangaiko hususa kwa vijana ambao wamelelewa wakiwa Wakristo. Utakuwa unafiki ulioje kuvaa sura ya uadilifu na kuendelea kutenda ukiwa mwivi! Mtume Paulo alisema hivi: “Basi wewe umfundishaye mwingine, je! hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?”—Warumi 2:21.
Lile taraja lenye kufedhehesha la kufungwa ni sababu ya kutosha ya kuepuka sifa mbaya ya kuiba. Baada ya kufungwa, mwivi mmoja mchanga alisema hivi: “Nilitaka nife.” Kujua kwamba Yehova ‘huchukia wivi’ ni sababu yenye nguvu kuliko zote ya kuepuka kujiacha kushindwa na msukumo—au msongo—ili kuiba. (Isaya 61:8) Hata ikiwa mtu aweza kuficha wivi kutoka kwa maofisa wa duka, polisi, na wazazi, mtu hawezi kuuficha kutoka kwa Yehova. Kufunuliwa ni jambo lisiloepukika.—Isaya 29:15.
Kumbuka pia, kwamba dhambi hufanya mtu kuwa mgumu. (Waebrania 3:13) Wivi mdogo huelekea kuendelea na kuwa vitendo vya ushupavu na kijahili zaidi. Kwa kielelezo, Roger mchanga, alianza maisha yake ya uhalifu kwa kuiba pesa kutoka katika pochi ya mama yake. Hatimaye alikuwa akipiga kumbo wanawake wazee hadi kuwaangusha na kuiba pochi zao!
Kushindana na Kishawishi
Ni kweli kwamba, ikiwa mtu ameanza kuiba kwa siri, kuacha huenda kusiwe jambo rahisi. “Kulikuwa kama uraibu hivi,” akakiri kijana mmoja. Ni nini kiwezacho kusaidia kijana abadili njia zake?
Ungama dhambi yako kwa Mungu. Yeye ‘atasamehe kabisa’ wale wanaotubu makosa yao na kuungama waziwazi kwake.—Isaya 55:7.
Pata msaada. Wasomaji wengi wa gazeti hili wanafahamu vizuri kutaniko la Kikristo la Mashahidi wa Yehova katika mahali pao. Hao wanaweza kwenda kwa waangalizi Wakristo wa mahali pa kwao na kuomba msaada wa kiroho na sahihisho. (Yakobo 5:14, 15) Wazazi walio na kanuni njema za kiadili wanaweza kuthibitika kuwa chanzo cha msaada na utegemezo. Ikiwa umizo, umivu, au ukimwa sahili ndiyo yanasababisha mwenendo usiofaa, kuzungumza mambo na msikilizaji mwenye huruma kwaweza kuthibitika kuwa kwenye msaada.—Mithali 12:25.
Fanya malipo. Chini ya Sheria ya Kimusa, wevi walihitajika kulipa vitu walivyoiba pamoja na riba. (Mambo ya Walawi 6:4, 5) Kufanya vivyo hivyo hakusaidii tu kufanya dhamiri ya mtu kuwa safi bali pia humkazia mtu huyo magumu ambayo wivi husababisha kwa wengine. Biblia huahidi kwamba mtu ‘anapomrudishia mtu mali aliyomnyang’anya na kuzifuata sheria za uzima . . . , hakika ataishi.’—Ezekieli 33:15.
Komesha hisia za wivu na pupa. Amri ya mwisho ya zile Amri Kumi ni, “Usitamani . . . cho chote alicho nacho jirani yako.” (Kutoka 20:17) Ikiwa kuna kitu unachohitaji kwelikweli—au unachotaka—lakini huwezi kukilipia, labda waweza kutafuta njia ya kuchuma pesa ili ukinunue. Mtume Paulo alishauri hivi: “Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe.”—Waefeso 4:28.
Chunga washirika wako. “Ukiwa na rafiki au kikundi cha marafiki wanaofanya kitu kibaya au kutenda uhalifu,” akumbusha mwandikaji Denise Lang, “wewe pia utachukuliwa kuwa mwenye hatia kwa kuwa tu kwenye mahali hapo pamoja nao.” Uwe na nguvu ya kusema hapana ikiwa marika wanadokeza ufanye jambo fulani lisilo halali.—Mithali 1:10-19.
Fikiria dhara ambalo wivi hufanya kwa wengine. Mwivi hujifikiria yeye tu. Lakini Yesu atushauri hivi: “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo.” (Mathayo 7:12) Wakati mtu ajifunzapo kujali watu wengine, mtu haelekei sana kutenda jambo ambalo lingeweza kusababishia wengine dhara.
Fikiria yatakayotokea kwako. (Wagalatia 6:7) Badala ya kufikiria jinsi itakavyopendeza kuwa na kipambo au kidude hicho chenye kumeta ambacho huwezi kukilipia, fikiria jinsi itakavyofedhehesha kushikwa na kushtakiwa; fikiria suto utakaloleta juu ya wazazi wako na juu ya Mungu mwenyewe! Kwa hakika utafikia mkataa kwamba viwavyo vyote kuiba si wazo zuri.
[Maelezo ya Chini]
a Baadhi ya majina yamebadilishwa.
b Hatuzungumzii kleptomania—tatizo la kiakili linaloainishwa na shurutisho lenye nguvu la kuiba. Madaktari wanasema kwamba kleptomania ni nadra sana, ikipata chini ya asilimia 5 ya waibaji-madukani wanaojulikana. Tatizo hili mara nyingi hutibiwa kwa dawa.
[Picha katika ukurasa wa 18]
Waiba-madukani mara nyingi hupata fedheha ya kushikwa