Maoni ya Biblia
Je, Umaskini Ni Sababu Halali ya Kuiba?
“Umaskini ni adui mkubwa wa furaha ya binadamu; kwa hakika huharibu uhuru na kufanya isiwezekane kudhihirisha wema-adili fulani, na kufanya nyinginezo kuwa vigumu sana kudhihirishwa.”—Samuel Johnson, mtungaji wa karne ya 18.
MKUU wa serikali ya Roma Magnus Aurelius Cassiodorus alisema: “Umaskini ndicho kiini cha uhalifu.” Maoni haya yaonekana kudai ya kwamba uhalifu fulani huwa ni tokeo la kawaida la umaskini. Wengi leo huelekea kukubali, hasa ikiwa uhalifu huo ni kuiba.
Wengi wamependa ile itikadi ya kwamba uonevu na umaskini ni sababu halali ya kuiba. Fikiria nyimbo zilizopendwa za Uingereza za karne ya 14 zilizohusu Robin Hood, ambazo zilifafanua juu ya mhalifu fulani mashuhuri ambaye aliwaibia matajiri na kugawanya mapato hayo kwa maskini. Kwa karne nyingi ameonwa kuwa shujaa.
Ni kweli kwamba wengi leo wanakabili hali ngumu sana za kiuchumi. Hivi majuzi Benki ya Dunia iliripoti kuwa kuna watu bilioni 1.3 wanaoishi kwa kutegemea mapato yanayopungua dola moja kwa siku. Katika uchunguzi mmoja asilimia 70 ya Wafilipino walisema walijiona kuwa maskini. Katika Brazili watu walio matajiri zaidi, ambao ni asilimia 20 ya idadi ya watu, huchuma mara 32 zaidi ya watu walio maskini zaidi, ambao ni asilimia 20 ya idadi ya watu. Hali kama hizo zaweza kuwavunja moyo watu wengine hadi kufikia kiwango cha kutumia njia yoyote, hata kuiba, ili tu wapate mahitaji yao ya kila siku ya kuwaendeleza.
Biblia hulaumu waziwazi kuiba. Amri ya nane kati ya zile Amri Kumi yasema: “Usiibe.” (Kutoka 20:15) Na bado, wengi ambao huamini katika Biblia huwa na mwelekeo wa kuona kuiba kuwa halali ikiwa mwizi asukumwa na hali mbaya sana za kiuchumi.
Hili latokeza maswali mazito: Je, umaskini kwa kweli ni sababu halali ya kuiba? Mtu afanyeje ikiwa anaishi chini ya hali ngumu sana za kiuchumi? Vipi ikiwa ana watoto wagonjwa au wenye njaa wa kuwatunza? Je, Yehova Mungu angekubali wizi katika visa kama hivi, hasa ikiwa vitu vilivyoibwa ni vya watu ambao huenda hata wasivihitaji?
Mungu Asemaje?
Kwa kuwa Yesu alidhihirisha utu wa Baba yake, kielelezo chake chaweza kutusaidia tufahamu maoni ya Mungu. (Yohana 12:49) Alipokuwa duniani, Yesu alikuwa mwenye huruma sana aliposhughulika na wenye uhitaji. Biblia yasema kwamba “alipouona umati alihisi sikitiko kwa ajili yao.” (Mathayo 9:36) Hata hivyo, katika hali zozote zile hakukubali kamwe wizi. Hivyohivyo, ijapokuwa Mungu huwahangaikia maskini, haoni umaskini kuwa sababu halali ya kuiba. Kwenye Isaya 61:8, Biblia yatuambia kwamba Mungu ‘auchukia wivi na uovu.’ Na mtume Paulo asema waziwazi kwamba wezi hawatarithi Ufalme wa Mungu. Kwa hiyo sisi twaelewa wazi maoni ya Mungu.—1 Wakorintho 6:10.
Hata hivyo, Mithali 6:30 yasema kwamba “watu hawamdharau mwivi, akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa.” Je, taarifa hii hutoa udhuru wa kuiba? Sivyo hata kidogo. Muktadha waonyesha kwamba Mungu bado huona mwizi kuwa anastahili adhabu kwa kosa lake. Mstari ufuatao wasema: “Lakini akipatikana, atalipa mara saba; atatoa mali yote ya nyumba yake.”—Mithali 6:31.
Ingawa mwizi aibaye kwa sababu ya njaa huenda asiwe mwenye hatia kama yule aibaye kwa sababu ya pupa au akiwa na nia ya kumdhuru mhasiriwa wake, wale wanaotamani kibali cha Mungu hawapaswi kuwa na hatia ya aina yoyote ya wizi. Hata chini ya hali za umaskini wa kupindukia, kuiba hakuonyeshi heshima kwa Mungu. Mithali 30:8, 9 lasema hivi: “Unilishe chakula kilicho kadiri yangu. . . . Wala nisiwe maskini sana nikaiba, na kulitaja bure jina la Mungu wangu.” Ndiyo, mwizi hulisuta jina la Mungu. Kwa kuwa kuiba ni kitendo kisicho na upendo, ni dhambi bila kujali imefanywa dhidi ya tajiri au maskini. Kwa wale wanaompenda Mungu na jirani, kuiba hakuwezi kamwe kuwa halali.—Mathayo 22:39; Waroma 13:9, 10.
Hoja ya kwamba mtu aliye katika hali ya kupungukiwa ana haki ya kuiba si ya kiakili. Kusema hivi kungekuwa sawa na kusema kwamba mwanariadha aliye dhaifu ana haki ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku ili apate kushinda. Hata akishinda, ametumia njia zisizo haki. Wengine watahisi kwa haki kuwa amewanyang’anya ushindi wao kwa njia isiyo ya haki. Ndivyo ilivyo na mwizi pia. Achukua mali za wengine kwa njia ya udanganyifu. Hali yake ya kupungukiwa haimtolei sababu halali ya kufanya hivyo.
Mwizi yeyote anayetaka kibali cha Mungu lazima atubie mwendo wake. Biblia yaonya kwa upole: “Mwibaji na asiibe tena, bali acheni afanye kazi ya bidii, akifanya kwa mikono yake kazi iliyo njema.” (Waefeso 4:28) Waliokuwa wezi hapo awali na ambao wametubu kikweli wanaweza kuwa na uhakika wa kwamba Yehova atawasamehe.—Ezekieli 33:14-16.
Walio Maskini Waweza Kufanya Nini?
Biblia yaahidi: “BWANA hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali.” (Mithali 10:3) Mungu hatawasaidia wanaovunja sheria zake kimakusudi ili kutosheleza tamaa zao. Lakini ni mwenye huruma kwa wale wanaojaribu kumtii yeye kwa moyo mweupe, na atabariki jitihada zao za kujipatia wanayohitaji.—Zaburi 37:25.
Mamilioni tayari wameona ya kwamba wafuatapo kanuni za kimungu, hali yao ya maisha huwa bora. Kwa kielelezo, kutumia shauri la Biblia la kuwa wenye bidii ya kazi na kuepuka mazoea mabaya, kama vile kucheza kamari, ulevi, kuvuta sigareti, na matumizi mabaya ya dawa, kumewawezesha kuwa na zaidi ya wanachohitaji hasa. (Wagalatia 5:19-21) Hili hutaka wajizoeze imani, na wale ambao wamefanya hivyo wamejifunza ya kwamba “BWANA yu mwema” na kwa kweli huwasaidia wale wanaomwitibari.—Zaburi 34:8.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]
Robin Hood: General Research Division/The New York Public Library/Astor, Lenox and Tilden Foundations