Todi au Chura—Tofauti Ni Nini?
KWA karne nyingi todi na vyura wamekuwa na sifa mbaya. “Husababisha chunjua.” “Wachawi wanaweza kugeuza watu kuwa todi na vyura.” Ni nani hajasikia ile hekaya ya chura mwenye sura mbaya anayegeuka kuwa mwana-mfalme mwenye kuvutia anapobusiwa na binti-mfalme? Hata hivyo, tangu ule umashuhuri wa Kermit the Frog katika kipindi cha watoto cha televisheni “Sesame Street” na katika “The Muppet Show,” vyura wameonekana ifaavyo zaidi na watu wengi. Ukweli ni nini kuhusu vyura na todi? Wanatofautianaje?
Acheni tuondoe dhana zozote zinazoshikiliwa—ni virusi husababisha chunjua wala si todi. Na hekaya ni kile zinachoeleweka kuwa—hekaya tu, zilizo na hadithi na ngano. Na ingawa wachawi wapo, hawawezi kugeuza mtu kuwa chura au todi.
Vyura na todi hupatikana katika sehemu zilizo nyingi za ulimwengu, lakini hakuna vyura katika Antaktika, wala hakuna todi katika Aktiki. Kuna yapata spishi 3,800 za vyura na todi, ambazo kati yazo zaidi ya 300 ni todi. Kwa hiyo waweza kutofautishaje todi na chura. The World Book Encyclopedia yajibu hivi: “Todi halisi walio wengi wana mwili mpana, uliotandazika na mweusi zaidi, na wenye ngozi iliyo kavu kuliko walivyo vyura halisi. Todi halisi kwa kawaida wametapakawa na chunjua, lakini vyura halisi wana ngozi laini. Tofauti na vyura wengi halisi, wengi wa todi halisi huishi nchi kavu. Todi waliokomaa huenda majini kuzaana tu.” Kwa kawaida vyura hupatikana karibu na maji, wakiwa tayari kuruka wanapokusikia ukija. Vyura walio wengi huwa na meno kwenye utaya wao wa juu tu. Todi hawana meno. Hivyo, wote wawili humeza windo lao likiwa zima.
Vyura na todi wengi hutokeza sumu zenye nguvu. Chura mshale-sumu (Dendrobates pumilio) wa Kosta Rika mwenye rangi nyekundu-nyekundu ni kielelezo kimoja. Sumu fulani za vyura zaweza kwa urahisi kuua mtu. Kitabu Biology chataarifu hivi: “Makabila ya kienyeji katika nchi za tropiki mara nyingi hutia sumu ncha za mishale yao kwa kuisugua kwenye vyura hawa.” Katika kitabu cha Biblia cha Ufunuo, “semi zisizo safi zilizopuliziwa” zafananishwa na vyura. Kwa nini iwe hivyo? Kwa sababu katika Sheria ya Kimusa, vyura walikuwa wasio safi kwa ajili ya chakula. Todi hawatajwi katika Biblia.—Ufunuo 16:13, NW; Mambo ya Walawi 11:12.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Kulia: Todi. Chini: Chura