Ulimwengu Wetu Ukoje leo?
IKIWA una umri mkubwa kutosha kukumbuka 1945 je, umeona mabadiliko yoyote katika viwango na maadili? Wengi wamekubali “maadili mapya,” ambayo yadhaniwa eti hutoa uhuru mwingi zaidi. Lakini kwa gharama gani?
Mwanamume mzee mwenye umri wa miaka 70 aliyetumika katika Jeshi la Wanamaji la Marekani wakati wa vita ya ulimwengu ya pili alitaarifu hivi: “Katika miaka ya 1940 kulikuwa na kutumainiana sana, na majirani walisaidiana. Mahali ambapo tuliishi katika California, hata hatukuhitaji kuweka kufuli kwenye milango yetu. Hakukuwa na uhalifu wa mitaani, na kwa hakika hakukuwa na ujeuri wa kutumia silaha shuleni. Tangu wakati huo kutumainiana kumetokomea kihalisi.” Hali ikoje leo katika eneo lenu? Imeripotiwa kwamba katika New York City, nusu ya matineja walio na umri wa zaidi ya miaka 14 hubeba silaha. Vichungua-vyuma vyatumiwa katika shule nyinginezo katika jitihada ya kuondoa visu, vikata-sanduku, na bunduki. Kila mwaka matineja wapatao milioni moja katika Marekani hupata mimba, na 1 kati ya 3 hutoa mimba. Tayari matineja ni akina mama—watoto wakiwa na vitoto.
Vile vikundi vyenye nguvu vya wagoni-jinsia-moja wa kike na kiume vimesitawisha mtindo-maisha wao kwa matokeo sana hivi kwamba watu wengi wameuruhusu na kuukubali. Lakini, pamoja na wengineo, wamelipa gharama za juu katika magonjwa na kifo kwa sababu ya maradhi yapitishwayo kingono kama vile UKIMWI. Kipuku cha UKIMWI kimeenea kwa wafanya ngono ya kawaida na watumizi wa dawa za kulevya. Kimefyeka Afrika, Ulaya, na Amerika Kaskazini. Na hakuna matumaini yaliyo karibu.
A History of Private Life chataarifu: “Ujeuri, uraibu wa alkoholi, dawa za kulevya: hizi ni aina za tabia kuu zenye kupotoka katika jamii ya Sweden.” Taarifa hiyo yatumika pia kwa nchi zilizo nyingi katika ulimwengu wa Magharibi. Kukiwa na mporomoko wa maadili ya kidini, kumekuwa na furiko la mdhoofiko wa kimaadili, hata miongoni mwa makasisi wengi.
Utumizi wa Dawa za Kulevya —Wakati Huo na Sasa
Huko nyuma katika miaka ya 1940, matumizi ya dawa za kulevya yaelekea yalikuwa hayajulikani miongoni mwa umma katika ulimwengu wa Magharibi. Naam, watu walikuwa wamesikia kuhusu mofini, kasumba, na kokeni, lakini kwa kulinganishwa ni kikundi kidogo mno kilichotumia dawa hizi za kulevya. Hakukuwa na magwiji wa dawa za kulevya ama walanguzi wa dawa za kulevya kama tuwajuavyo leo. Hakukuwa na wachuuzi wa dawa za kulevya kwenye pembe za mitaa. Sasa hali ikoje katika 1995? Wengi wa wasomaji wetu wanajua jibu kutokana na maono yao katika mahali pao. Mauaji ya kimakusudi yanayohusiana na dawa za kulevya yamekuwa matukio ya kila siku katika majiji makuu ya ulimwengu. Wanasiasa na mahakimu wamedhibitiwa na magwiji wa dawa za kulevya wenye uwezo ambao wanaweza kuamrisha kuuawa kwa mtu yeyote mwenye mamlaka asiyekubali kushirikiana nao. Historia ya majuzi ya Kolombia na mahusiano yao ya dawa za kulevya ni ithibati ya hili.
Pigo la dawa za kulevya huua watu wapatao 40,000 kila mwaka katika Marekani pekee. Kwa hakika tatizo hilo halikuwako katika 1945. Si ajabu kwamba baada ya serikali kujaribu kuondoa utumiaji wa dawa za kulevya kwa miongo mingi, Patrick Murphy, aliyekuwa kamishna wa polisi katika New York City, aliandika makala fulani kwenye Washington Post yenye kichwa “Vita vya Dawa za Kulevya Vimekwisha—Dawa za Kulevya Zimeshinda”! Yeye alisema kwamba “biashara ya dawa za kulevya . . . sasa iko miongoni mwa biashara zenye kufanikiwa zaidi katika [Marekani], ikiwa na faida ambayo ingeweza kufikia dola bilioni 150 mwaka huu.” Hilo ni tatizo kubwa na laonekana kutoisha. Utumizi wa dawa za kulevya, kama uovu mwingineo wowote, una wadhibitiwa wayo wenye kukua na kuraibika. Ni biashara ambayo hutegemeza uchumi wa mataifa kadhaa.
John K. Galbraith, profesa wa uchumi, aliandika hivi katika kitabu chake The Culture of Contentment: “Ulanguzi wa dawa za kulevya, mifyatuo ya bunduki kiholela-holela, uhalifu mwingine na kutokuungamana na kuvunjika kwa familia sasa ni sehemu ya maisha ya kila siku.” Ataarifu kwamba jamii ndogo-ndogo katika majiji mengi makubwa ya Kiamerika “sasa ni vitovu vya tisho na mtamauko.” Aandika kwamba “uchukizo na mvurugiko mwingi wa kijamii unapaswa kutazamiwa.” Kwa nini iko hivyo? Kwa sababu, yeye asema, matajiri wazidi kutajirika na maskini, “akina yahe,” wanaozidi kuongezeka kwa idadi, wanazidi kuwa maskini.
Mshiko wa Uhalifu wa Kimataifa
Uthibitisho sasa unazidi kuongezeka kwamba vikundi vya uhalifu vinaeneza athari zavyo ulimwenguni pote. Kwa miaka uhalifu wa magenge makubwa, ukiwa na “jamii za uhalifu,” umekuwa na miungano kati ya Italia na Marekani. Lakini sasa Katibu-Mkuu wa UM Boutros Boutros-Ghali ameonya kwamba “uhalifu wa magenge makubwa kwenye viwango vya kimataifa . . . hupita mipaka na huja kuwa muungano wa ulimwenguni pote.” Yeye alisema hivi: “Katika Ulaya, katika Asia, katika Afrika na katika Amerika, vikundi vya uhalifu vinatenda kazi na hakuna jamii imeachwa bila kufikwa.” Pia alisema kwamba “uhalifu wa kimataifa . . . huharibu misingi yenyewe ya utaratibu wa demokrasi wa kimataifa. [Huo] hufisidi hali ya kibiashara, hufisidi viongozi wa kisiasa na huharibu haki za kibinadamu.”
Ramani Imebadilika
Vaclav Havel, rais wa Jamhuri ya Cheki, alisema katika hotuba aliyotoa katika Philadelphia, Marekani, kwamba matukio mawili ya kisiasa yaliyo muhimu sana katika nusu ya pili ya karne ya 20 yalikuwa kuporomoka kwa ukoloni na kuanguka kwa Ukomunisti katika Ulaya Mashariki. Mlinganisho wa ramani ya 1945 na ile ya 1995 mara huonyesha miamko ya kisiasa iliyotukia ulimwenguni, hasa katika Afrika, Asia, na Ulaya.
Ebu linganisha hali ya kisiasa ya hizo tarehe mbili. Wakati wa miaka 50 iliyo katikati, Ukomunisti ulifikia upeo wao na hatimaye kuondolewa katika nchi nyingi zilizokuwa za Ukomunisti. Katika mataifa hayo utawala wa kimabavu umeachia njia aina fulani ya “demokrasi.” Hata hivyo, watu wengi wanateseka kutokana na matokeo ya mbadiliko wa jamii zao kuwa za masoko huru. Ukosefu wa kazi umeenea mno, na mara nyingi fedha hazina thamani. Katika 1989 ruble ya Kirusi ilikuwa na thamani ya dola 1.61 (ya Marekani). Wakati wa uandishi huu, wahitaji ruble 4,300 kwa dola moja!
Lile gazeti Modern Maturity liliripoti kwamba leo karibu Warusi milioni 40 ni maskini. Mrusi mmoja alisema: “Hatuwezi hata kumudu kufa. Hatuwezi kugharimia maziko.” Hata maziko yaliyo ya chini hugharimu yapata ruble 400,000. Miili ambayo haijazikwa yarundamana kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti. Wakati uleule, inapaswa kufahamika kwamba Wamarekani zaidi ya milioni 36 ni maskini!
Mleta-habari wa kifedha wa Guardian Weekly, Will Hutton, aliandika kuhusu matatizo ya Ulaya Mashariki. Chini ya kichwa “Ingia Enzi ya Hangaiko,” yeye alitaarifu hivi: “Kule kuporomoka kwa ukomunisti na Urusi kuurudia udogo wayo tangu karne ya 18 ni matukio ambayo maana yayo bado hayaeleweki kabisa.” Mataifa 25 yamechukua mahali pa ile iliyokuwa milki ya Sovieti. Yeye asema kwamba “ule mshangilio ambao kuporomoka kwa ukomunisti ulikaribishiwa kwao sasa umebadilika kuwa hangaiko lenye kukua kuhusu wakati ujao. . . . Mteremko kuelekea kutokuwako na usalama wa kiuchumi na kisiasa wazidi kuwa dhahiri—na Ulaya magharibi haiwezi kutazamia kubaki bila kuathiriwa.”
Kukiwa na mtazamo hasi kama huo, si ajabu kwamba Hutton amalizia makala yake kwa kusema: “Ulimwengu wahitaji dira iliyo bora kuliko wito sahili wa kuhodhi demokrasi na masoko huru—lakini hakuna yoyote inayopatikana.” Hivyo basi mataifa yanaweza kugeukia wapi ili kupata suluhisho? Makala ifuatayo itatoa jibu.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]
UM Tangu 1945
Kwa nini UM, uliobuniwa katika 1945, umeshindwa kuzuia vita vingi hivyo? Katibu-Mkuu Boutros Boutros-Ghali alitaarifu hivi katika hotuba yake “Ajenda ya Amani”: “Umoja wa Mataifa ulikuwa hauna uwezo wa kushughulikia mengi ya matatizo haya kwa sababu ya wapiga-kura—279 kati yao—wakipinga Baraza la Usalama, ambao ulikuwa wonyesho dhahiri wa migawanyiko ya kipindi hicho [cha Vita Baridi kati ya serikali za kikabaila na Kikomunisti].”
Je, ni kwamba UM haujajaribu kudumisha amani katikati ya mataifa? Umejaribu, lakini kwa gharama za juu. “Juhudi 13 za kudumisha amani zilianzishwa kati ya miaka ya 1945 na 1987; 13 nyingine tangu wakati huo. Kadirio la wafanyakazi 528,000 walio wanajeshi, polisi na raia walitumika chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa kufikia Januari 1992. Zaidi ya 800 kati yao kutoka nchi 43 wamekufa wakitumikia hilo Shirika. Gharama za hizi juhudi za amani zimeongezeka kufikia yapata dola bilioni 8.3 kufikia 1992.
[Hisani]
Kifaru na kombora: Picha ya U.S. Army
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Televisheni
Mwelimishaji au Mpotoaji?
Kwa kulinganishwa ni nyumba chache zilizokuwa na televisheni katika 1945. Ilikuwa bado katika mianzo yayo ya taswira nyeusi na nyeupe. Leo, televisheni ni mwizi wa wakati na mjiingizaji katika karibu kila nyumba katika ulimwengu uliositawi na katika kila kijiji katika ulimwengu unaositawi. Ingawa vichache vya vipindi ni vyenye kuelimisha na kujenga, vingi vyavyo ni vyenye kushusha kanuni za maadili na kuchochea uchu uwao wowote wa umma. Tukifikiria umaarufu wa filamu kwenye video, kule kuonyesha kwa ponografia na sinema chafu ni msumari mwingine kwenye jeneza la ladha nzuri na maadili yenye kufaa.
[Picha katika ukurasa wa 9]
Vita, kama ile ya Vietnam, vimegharimu zaidi ya uhai milioni 20 tangu 1945
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
Patrick Frilet/Sipa Press
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
Luc Delahaye/Sipa Press