Ulimwengu Wetu—Unaobadilika Huo Waelekezwa Wapi?
MABADILIKO mengine yanaathiri sana na tena kwa muda mrefu maisha za mamilioni, hata watu wote ulimwenguni na vizazi vijavyo. Uhalifu wa jeuri, utumizi wa dawa za kulevya, kuenea kwa UKIMWI, uchafuzi wa maji na hewa, na kuharibiwa kwa misitu ni baadhi tu ya matukio yanayotuathiri sote. Pia mwisho wa Vita Baridi na kuenea kwa demokrasia ya mtindo wa Magharibi na soko yayo huru yanabadilisha maisha na kuathiri wakati ujao. Ebu tuchunguze baadhi ya mambo hayo.
Jinsi Uhalifu Umebadili Maisha Zetu
Barabara za ujirani wenu zikoje? Je! wewe huhisi ukiwa salama kutembea nje usiku peke yako? Miaka 30 au 40 tu iliyopita, watu wengi hata wangeweza kuacha nyumba zao bila kuzifunga kwa kufuli. Lakini nyakati zimebadilika. Sasa milango fulani ina makufuli mawili au matatu, na madirisha yametiwa vyuma.
Watu leo huogopa kuvaa mavazi na vito vyao vilivyo bora zaidi wanapotembea barabarani. Wakazi wengine wa jijini wameuawa kwa sababu ya jaketi ya ngozi au koti ya ngozi ya nyengere. Wengine wameuawa katika mfyatuliano wa risasi kati ya magenge ya dawa za kulevya. Wapita njia wasio na hatia, kutia na watoto wengi, wanajeruhiwa au kuuawa karibu kila siku. Magari hayawezi kuachwa nje kwa usalama bila kuwa na kifaa fulani kifaacho ili kujaribu kukinza wevi wanyonyaji. Katika hali hiyo iliyopotoka ya ulimwengu, watu wamebadilika. Unyoofu na uaminifu-maadili ni kanuni ambazo karibu zimesahauliwa. Kutumainiana kumetoweka.
Uhalifu na jeuri ni kumbo la ulimwenguni pote. Habari kuu zifuatazo kutoka vyanzo mbalimbali zinadhihirisha jambo hilo: “Polisi Kuwasaka Wevi, Magenge na Maisha Mapotovu; Moscow Yagundua Inao Wote”; “Muhula Mpya Waanza Katika Korea, Ukifuatwa na Uhalifu”; “Uhalifu Barabarani Wakumba Maisha ya Kila Siku Jijini Prague”; “Japan Yapambana na Magenge, Nayo Magenge Yapambana Pia”; “Uwezo wa Mafia—Mpiganaji Mashuhuri wa Italia Dhidi ya Mafia Alipuliwa kwa Bomu.” Uhalifu ni tatizo la ulimwenguni pote.
Uhalifu wa leo ni wenye jeuri zaidi pia. Uhai unaonwa kuwa si kitu. Katika Rio de Janeiro, Brazili, sehemu ya mtaa wa hali ya chini iliyo ukingoni mwa jiji “imetambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa kuwa sehemu yenye jeuri zaidi ulimwenguni. Watu zaidi ya 2,500 huuawa huko kila mwaka.” (World Press Review) Katika Kolombia, wauzaji wakuu wa dawa za kulevya hutuma wabalehe waitwao sicarios, au wauaji wa kulipwa wenye pikipiki ili wajilipize kwa washindani na wadeni wao kwa njia ya mauaji ya haraka ya aina ya pekee. Na mara nyingi, ole wako ukishuhudia uhalifu—uwe uko Kolombia au kwingineko. Huenda wewe ukafuata kuuawa.
Badiliko jingine kubwa ni kwamba wahalifu wengi zaidi na zaidi wanabeba silaha za kuua zilizo hatari zaidi, na watu wengi zaidi na zaidi wanaamua kubeba bastola ili kujikinga. Ongezeko hilo la silaha linamaanisha ongezeko la vifo na majeruhi, iwe ni kutokana na uhalifu au kwa aksidenti. Sasa ni jambo lililo hakika ulimwenguni pote kwamba bastola iliyo mfukoni au nyumbani yaweza kumfanya mtu yeyote aelekee kuua.
Uhalifu na Dawa za Kulevya
Miaka hamsini iliyopita, ni nani hata aliwazia dawa za kulevya kuwa tatizo la ulimwengu? Sasa hizo ndizo kisababishi kikuu cha uhalifu na jeuri. Katika kitabu chake Terrorism, Drugs and Crime in Europe after 1992, Richard Clutterbuck anatabiri kwamba “hatimaye, ukuzi wa biashara ya dawa za kulevya waweza kuwa tisho kuu kupita zote kwa ustaarabu wa binadamu. . . . Faida hazitoi uwezo mwingi wa kiuchumi na wa kisiasa tu kwa wauzaji wakuu wa dawa za kulevya [mfano wa wazi ni Kolombia], bali pia hutegemeza kifedha uhalifu mwingi ajabu ulimwenguni pote.” Yeye pia asema: “Mojawapo vichochezi vikuu zaidi vya uharamia na jeuri ya uhalifu ulimwenguni ni biashara ya kokeni kutoka mashamba ya mkoka katika Kolombia hadi kwa wazoevu katika Ulaya na USA.”
Ongezeko la uhalifu na idadi ya wafungwa ulimwenguni inaonyesha kwamba kuna mamilioni ya watu wenye makusudio ya uhalifu na hawataki kubadilika. Wengi sana wameona kwamba uhalifu unaleta ufanisi. Tokeo ni kwamba ulimwengu wetu umebadilika—ukawa mbaya zaidi. Umekuwa hatari zaidi.
UKIMWI—Je! Umeleta Badiliko?
Ule ulioonekana kuwa ugonjwa unaoathiri hasa wagoni-jinsia-moja umekuwa tauni inayoathiri watu wa kila rangi na mtindo-maisha. UKIMWI haupendelei watu fulani tena. Katika nchi nyingine za Afrika, unaua sehemu kubwa ya wagoni-jinsia-tofauti. Kama tokeo, ukosefu wa maadili katika ngono kwa ghafula umekuwa usiopendwa na wengine, si kwa sababu yoyote ya kimaadili, lakini kwa sababu ya hofu ya kuambukiwa. “Ngono salama” ndio shime sasa, na utumizi wa kondomu (mipira) ndio kizuizi hasa kinachopendekezwa. Kutofanya ngono isiyo ya kiadili ni usalama usiopendelewa sana. Lakini UKIMWI utaathirije familia ya kibinadamu katika wakati ujao ulio karibu?
Hivi karibuni, gazeti Time liliripoti hivi: “Kufikia mwaka 2000 UKIMWI waweza kuwa ugonjwa wenye kuenea zaidi katika karne hii, ukidunisha ugonjwa wa mafua makali ya 1918. Msiba huo uliua watu milioni 20, au asilimia 1 ya idadi ya watu ulimwenguni—zaidi ya mara mbili ya idadi ya wanajeshi waliokufa katika Vita ya Ulimwengu 1.” Kama vile mstadi mmoja alivyosema, “ugonjwa huo ni wa kiwango cha kihistoria.”
Kujapokuwa mamilioni ya dola na aina nyinginezo za pesa zinazotolewa kwa ajili ya utafiti wa UKIMWI, hakuna suluhisho linaloonekana. Mkutano wa hivi karibuni kuhusu UKIMWI katika Amsterdam, Uholanzi, ulikutanisha wanasayansi na wastadi wengineo 11,000 ili kuchunguza tatizo hilo. “Hali ilikuwa ya huzuni, ikionyesha mwongo mzima wa mfadhaiko, kushindwa pamoja na msiba unaoongezeka. . . . Huenda ikawa tangu binadamu aanze kupambana na UKIMWI hajafanya maendeleo yoyote. Hakuna chanjo, hakuna dawa wala hata matibabu yenye matokeo yasiyotilika shaka.” (Time) Kwa wale sasa ambao wana vairasi ya HIV, wanaoelekea tayari kuambukiwa UKIMWI, mataraja ni madogo. Katika jambo hilo pia, badiliko limekuwa baya tu.
Badiliko Katika Siasa za Ulimwengu
Hali ya kisiasa ambayo imebadilika katika miaka minne iliyopita imewashangaza viongozi wengi na labda hasa wale wa United States. Kwa ghafula inajipata haina mshindani yeyote anayefaa katika uwanja wa siasa. Imefananishwa na timu ya mchezo wa vikapu yenye msukumo mwingi na isiyoshindika ambayo kwa ghafula inapata kwamba hakuna mtu anayetaka kucheza nayo tena. Hali hiyo yenye kutatanisha imefanyiwa muhtasari na mhariri Charles William Maynes katika makala ya gazeti Foreign Policy la 1990: “Leo jukumu kubwa la mwongozo wa mambo ya kigeni wa U.S. si kuepusha nchi hiyo na vita vyenye msiba bali ni kusimamia amani isiyotazamiwa ambayo imetokea ghafula kati ya United States na [iliyokuwa] Muungano wa Sovieti.”
Ongezeko la utaalamu wa nyukilia linatoa matisho mapya, huku vita vya silaha za kawaida vikiendelea kusitawi—kwa faida ya wauzaji wa silaha wa ulimwengu. Katika ulimwengu unaotamani amani, viongozi wengi wa kisiasa wanaongeza majeshi yao na silaha zao. Na Umoja wa Mataifa ambao karibu umefilisika unashughulika ukijaribu kutatua matatizo ya ulimwengu bila kufanikiwa.
Laana Isiyobadilika ya Utukuzo wa Taifa
Ukomunisti ulipoanza kuvunjika, aliyekuwa rais wa U.S. Bush alisifu wazo la “utaratibu wa ulimwengu mpya.” Hata hivyo, kama vile viongozi wengi wa kisiasa wamegundua, kutoa shime za werevu ni rahisi; kufanya mabadiliko yafaayo ni kugumu zaidi. Katika kitabu chake After the Fall—The Pursuit of Democracy in Central Europe, Jeffrey Goldfarb asema: “Tumaini kubwa sana la ‘utaratibu wa ulimwengu mpya’ limefuatwa upesi na ufahamu wa kwamba tungali na matatizo ya kale sana, na nyakati nyingine kwa kiasi kikubwa. Msisimko wa uhuru . . . mara nyingi umezimwa na kutamauka kwa sababu ya msukosuko wa kisiasa, mizozo ya kitaifa, ushupavu wa kidini, na kuvunjika kwa uchumi.” Kwa kweli vita vya wenyewe kwa we-nyewe katika ile iliyokuwa Yugoslavia ni mfano wa wazi wa athari zenye kugawanya za siasa, dini, na utukuzo wa taifa.
Goldfarb aendelea kusema: “Kuogopa wageni na ukosefu wa usalama kwa mtu binafsi yamekuwa mambo ya hakika ya maisha ya Ulaya ya Kati. Demokrasia haitoi moja kwa moja matokeo yanayoahidiwa ya kiuchumi, kisiasa, na kitamaduni, na uchumi wa soko huru hauahidi tu utajiri, bali pia hufanyiza matatizo makubwa kwa wale wasiojua jinsi ya kuutumia.”
Lakini ni wazi kwamba hayo si matatizo ya Ulaya ya Kati na jamhuri za iliyokuwa Muungano wa Sovieti pekee; kuogopa wageni na ukosefu wa usalama wa kiuchumi yako ulimwenguni pote. Familia ya kibinadamu hupata hasara kwa kuteseka na kifo. Na wakati ujao ulio karibu hauna tumaini lolote la mabadiliko katika mitazamo hiyo iliyoshikiliwa sana ambayo huchochea chuki na jeuri. Kwa nini iko hivyo? Kwa sababu elimu ambayo wengi tunapokea—iwe kutoka kwa wazazi au mifumo ya shule inayotia moyo utukuzo wa taifa—hukazia chuki, kutovumiliana, na mawazo ya ukuu yanayotegemea utukuzo wa taifa, asili ya rangi na ukabila, au lugha.
Utukuzo wa taifa, ulioitwa na gazeti la kila juma Asiaweek “Wazo Ovu la Mwisho,” ni mojawapo mambo yasiyobadilika linaloendelea kutokeza chuki na umwagaji damu. Gazeti hilo lilisema: “Ikiwa fahari ya kuwa Mserbi inamaanisha kuchukia Mkroati, ikiwa uhuru wa Mwarmenia unamaanisha kumlipiza kisasi Mturuki, ikiwa uhuru wa Mzulu wamaanisha kutiisha Mkosa na demokrasia kwa Mromania yamaanisha kufukuza Mhangaria, basi utukuzo wa taifa tayari umesitawi kwa ubaya zaidi.”
Tunakumbushwa yale ambayo Albert Einstein alisema wakati mmoja: “Utukuzo wa taifa ni mtazamo wa kitoto. Ni ukambi wa ainabinadamu.” Karibu kila mtu huupata wakati mmoja au mwingine, na huzidi kuenea. Huko nyuma katika 1946, mwanahistoria Mwingereza Arnold Toynbee aliandika: “Uzalendo . . . umepita sana Ukristo ukiwa dini ya Ulimwengu wa Magharibi.”
Je! kuna tumaini lolote la mabadiliko katika mwenendo wa kibinadamu katika hali ya sasa? Wengine wanasema kwamba yanaweza kupatikana tu kwa mabadiliko makubwa katika elimu. Mwanauchumi John K. Galbraith aliandika: “Sifa za watu ndizo huamua mwendo wa maendeleo. Kwa hiyo . . . maendeleo hayawezekani ikiwa watu hawajafanya maendeleo, na maendeleo ni ya hakika wakati watu wanapowekwa huru na kuelimishwa. . . . Kushinda kutojua kusoma na kuandika kwaja kwanza.” Kuna tumaini gani kwamba mifumo ya elimu ya ulimwengu itapata kufunza upendo na uvumiliano badala ya chuki na shuku? Ni lini ambapo mahali pa uhasama mwingi wa kikabila au rangi patachukuliwa na kutumainiana na kuelewana, kwa kutambua kwamba sote tumetoka kwa familia moja ya kibinadamu?
Kwa wazi, mabadiliko yafaayo yanahitajiwa. Sandra Postel aandika katika State of the World 1992: “Katika sehemu inayobaki ya mwongo huu ni lazima kuwe na mabadiliko ya kutokeza na yenye kuenea pote hata zaidi ikiwa tutaendelea kuwa na matumaini halisi ya kupata ulimwengu bora zaidi.” Na sisi tunaelekezwa wapi? Richard Clutterbuck asema: “Hata hivyo, ulimwengu unaendelea kuwa wenye msukosuko na hatari. Jitihada za kitaifa na kidini zitaendelea. . . . Huenda mwongo wa miaka ya 1990 ukawa ama wenye hatari zaidi ama wenye maendeleo zaidi karne hii.”—Terrorism, Drugs and Crime in Europe After 1992.
Mazingira Yetu Yanayobadilika
Katika miongo michache iliyopita, ainabinadamu imetambua jambo la kwamba utendaji wa kibinadamu unakuwa na matokeo ya hatari kwa mazingira. Uharibifu mkubwa wa misitu unaua aina za wanyama na mimea isiyohesabika. Na kwa kuwa misitu ni sehemu ya mfumo wa kuandaa hewa duniani, uharibifu wa misitu pia unapunguza uwezo wa dunia wa kugeuza kaboni-dayoksaidi kuwa oksijeni yenye kutegemeza uhai. Athari nyingine ni kumomonyoa udongo na hatimaye kuongoza kwenye kuenea kwa jangwa.
Watu fulani wamelalamika juu ya suala hilo, na mmoja wao ni mwanasiasa wa U.S. Al Gore. Katika kitabu chake Earth in the Balance—Ecology and the Human Spirit, yeye aandika: “Kati-ka kiwango cha sasa cha uharibifu wa misitu, karibu misitu yote ya mvua ya tropiki itatoweka katika karne inayokuja. Tukiruhusu uharibifu huo, ulimwengu utapoteza ghala muhimu sana la habari za urithi-tabia wa sayari, pamoja na uwezekano wa tiba kwa magonjwa mengi yanayotupata. Kwelikweli, mamia ya dawa muhimu zinazotumiwa sana sasa hupatikana kwa mimea na wanyama wa misitu ya kitropiki.”
Gore anaamini kwamba athari ya mwanadamu kwa mazingira inawakilisha tisho la kuokoka. Yeye asema: “Tunapoendelea kuenea hadi kwenye kila kona iwaziwayo ya mazingira, hali ya kuangamia kwa ustaarabu wetu wenyewe inaonekana wazi zaidi. . . . Katika muda wa kizazi kimoja, tutakuwa katika hatari ya kubadili hali ya anga la tufe letu kwa kiwango kikubwa zaidi ya volkeno yoyote katika historia, na athari zaweza kuendelea kwa karne zitakazokuja.”
Si kwamba tu angahewa yetu inatishwa, bali pia kulingana na Gore na wengineo, ugavi wetu muhimu wa maji umo hatarini, hasa katika ulimwengu unaositawi, “ambapo athari za uchafuzi wa maji huhisiwa zaidi na kwa matokeo mabaya kwa sababu ya kiasi kikubwa cha vifo kutokana na kipindupindu, homa ya matumbo, kuhara damu, na kuhara.” Kisha Gore aonyesha jambo la kwamba “watu zaidi ya bilioni 1.7 hawana ugavi wa kutosha wa maji safi ya kunywa. Zaidi ya watu bilioni 3 hawana mifereji ifaayo ya kuondoa maji machafu, hivyo kukiwa hatari ya kuchafuliwa kwa maji yao. Katika India, kwa mfano, miji na majiji mia moja kumi na manne humwaga kinyesi cha wanadamu na uchafu mwingine usio na dawa ndani ya mto Ganges.” Na mto huo ndio tegemeo la maji kwa mamilioni ya watu!
Gautam S. Kaji, makamu wa rais wa Benki ya Dunia, alionya wasikilizaji katika Bangkok kwamba “ugavi wa maji katika Esia Mashariki huenda ndio utakaokuwa suala muhimu la karne inayokuja. . . . Kujapokuwa na manufaa zinazojulikana sana za maji safi ya kunywa yaani kiafya na kimazao, serikali za Esia Mashariki sasa zinakabiliwa na mifumo ya umma inayoshindwa kuandaa maji safi . . . Hilo ndilo suala lililosahauliwa la maendeleo yafaayo ya kimazingira.” Ulimwenguni pote, mojawapo mambo muhimu kwa uhai—maji safi—linapuuzwa na kutumiwa ovyo.
Hayo yote ni mambo ya ulimwengu wetu unaobadilika, ulimwengu unaobadilishwa kuwa hatari katika mahali pengi na unaotisha wakati ujao wa kuwapo kwa ainabinadamu. Swali kuu ni, Je! serikali na biashara kuu zina tamaa na msukumo wa kuchukua hatua za kuzuia kumalizwa kwa wingi kwa nyenzo za dunia?
Je! Dini Inabadili Ulimwengu?
Katika uwanja wa dini, labda tunaona kule kushindwa kubaya zaidi kwa ainabinadamu. Ikiwa mti hukadiriwa kwa matunda yao, basi ni lazima dini itoe jibu kwa matunda ya chuki, kutovumilia, na vita miongoni mwa waamini wayo yenyewe. Inaonekana kwamba kwa watu wengi dini ni kama urembo—wa juujuu tu. Ni kifuniko kinachoondoka upesi chini ya mkazo wa urangi, utukuzo wa taifa, na ukosefu wa usalama wa kiuchumi.
Kwa kuwa Ukristo ni dini ya ‘kumpenda jirani na adui yako,’ ni nini kimetukia kwa Wakatoliki na Waorthodoksi wa ile iliyokuwa Yugoslavia? Je! makasisi wao watawasamehe dhambi zao zote za uuaji na chuki? Je! karne nyingi za mafunzo ya “Kikristo” zimetokeza chuki na mauaji ya kukusudia tu katika Ailandi ya Kaskazini? Na vipi juu ya dini zisizo za Kikristo? Je! zimetokeza matunda mema yoyote? Je! dini za Uhindu, Sikh, Ubuddha, Uislamu, na Ushinto zaweza kuelekeza kwenye rekodi ya amani ya kuvumiliana?
Badala ya kutumika kuwa uvutano ufaao kuelekea kustaarabisha ainabinadamu, dini imekuwa na jukumu layo yenyewe la kishupavu la kuchochea uzalendo wenye jeuri nyingi na katika kubariki majeshi katika vita viwili vya ulimwengu kutia na mizozo mingine mingi. Dini haijakuwa kani ya kuleta mabadiliko.
Kwa hiyo, tunaweza kutazamia nini kutoka kwa dini katika wakati ujao ulio karibu? Kwa kweli, tunaweza kutazamia nini kwa wakati ujao wa mfumo wetu wa ulimwengu uliopo—kutakuwa na mabadiliko gani? Makala yetu ya tatu itazungumza kuhusu maswali hayo kutoka kwa maoni ya pekee.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Ongezeko katika uhalifu wa jeuri ni dalili nyingine ya mabadiliko
[Picha katika ukurasa wa 8]
Utukuzo wa taifa na chuki ya kidini huendelea kuchochea umwagaji damu
[Hisani]
Jana Schneider/Sipa
Malcom Linton/Sipa
[Picha katika ukurasa wa 9]
Matumizi mabaya ya mazingira ya mwanadamu yanabadili usawaziko wa mazingira ya viumbe hai ambayo ni rahisi kuharibiwa
[Hisani]
Laif/Sipa
Sipa
[Picha katika ukurasa wa 10]
Hitler akisalimiwa na papa nuncio Basallo di Torregrossa, 1933. Kihistoria, dini imehusika katika siasa na utukuzo wa taifa
[Hisani]
Bundesarchiv Koblenz