Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 10/8 kur. 3-5
  • Ni Nchi Gani Isiyo na Uhalifu?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ni Nchi Gani Isiyo na Uhalifu?
  • Amkeni!—1996
  • Habari Zinazolingana
  • Kujitahidi Kumaliza Uhalifu
    Amkeni!—1996
  • Wewe Unataka Uhalifu Umalizwe?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Pigano Linaloshindwa Kudhibiti Uhalifu
    Amkeni!—1998
  • Kwa Nini Uhalifu Ni Mwingi Sana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 10/8 kur. 3-5

Ni Nchi Gani Isiyo na Uhalifu?

Maziko yake yalikuwa mojayapo maziko makubwa mno ambayo yamepata kuonekana katika Moscow kwa miaka mingi. Maelfu ya watu yalijipanga kando za barabara ili kutoa heshima za mwisho kwa Mrusi mmoja mchanga ambaye uhai wake ulikatizwa kwa ghafula mnamo Machi 1, 1995, kwa risasi za wauaji. Akiwa amepigwa risasi mlangoni pake tu, Vladislav Listyev, aliyekuwa amechaguliwa kuwa mwandikaji bora wa habari katika 1994, alikuwa mashuhuri katika televisheni mwenye kupendwa sana.

MUDA upunguao majuma matatu baadaye, mnamo Machi 20, mfumo wa reli ya chini wa Tokyo ulikuwa na msongamano wao wa kawaida kipindi cha asubuhi wakati uliposhambuliwa kwa gesi ya sumu. Watu kadhaa walikufa; wengine wengi walijeruhiwa vibaya.

Kisha, mnamo Aprili 19, Oklahoma City likawa habari kuu kwa watazamaji wa televisheni ulimwenguni pote. Wao walitazama kwa hofu kubwa wafanyakazi walipokuwa wakitoa miili iliyopondwa-pondwa kutoka kwenye magofu ya jengo la serikali lililotoka tu kuharibiwa kwa bomu la haramia. Watu 168 walikufa.

Katika mwisho-mwisho wa Juni mwaka huu, shambulizi jingine, karibu na Dhahran, Saudi Arabia, liliua Wamarekani 19 na kujeruhi wengine wapatao 400.

Visa hivyo vinne vyaonyesha kwamba uhalifu unaongezeka. Uhalifu “wa kawaida” unaendelea kuongezwa kwa matendo makatili ya uharamia. Na visa hivyo vyote vinne—kila kimoja kwa njia yacho ya kipekee—vyaonyesha jinsi kila mtu awezavyo kupatwa kwa urahisi na shambulizi la uhalifu. Uwe nyumbani, kazini, au barabarani, unaweza kupatwa na uhalifu. Hata uchunguzi mmoja wa Uingereza ulionyesha kwamba karibu robo tatu za Waingereza hufikiri kwamba wao waweza kupatwa na uhalifu kwa urahisi zaidi sasa kwa kulinganisha na miaka kumi iliyopita. Huenda hali ikawa hivyo mahali unapoishi.

Wananchi wenye kutii sheria hutamani serikali ambayo itafanya mengi zaidi ya kudhibiti tu uhalifu. Wao hutaka serikali ambayo hakika itamaliza uhalifu. Na ingawa ulinganifu wa viwango vya uhalifu waweza kudokeza kwamba baadhi ya serikali zina matokeo zaidi katika kuzuia uhalifu kuliko nyinginezo, hali ya ujumla yaonyesha kwamba serikali ya kibinadamu inapoteza pigano layo dhidi ya uhalifu. Na bado, si jambo lisilowezekana au la kimawazo tu kuamini kwamba karibuni serikali hiyo itamaliza uhalifu. Lakini ni serikali ipi? Na itamaliza uhalifu lini?

[Sanduku/Ramani katika kurasa za 4 and 5]

ULIMWENGU ULIOJAA UHALIFU

ULAYA: Kitabu fulani cha Kiitalia (“Fursa na Mwizi”) kilisema kwamba katika kipindi kifupi, idadi ya uhalifu dhidi ya mali katika Italia ilikuwa “imefika viwango ambavyo [pindi moja] vilikuwa vimeonwa kuwa haviwezi kufikiwa.” Ukrainia, jamhuri moja ya ile iliyokuwa Muungano wa Sovieti, iliripoti uhalifu 490 kwa kila idadi ya watu 100,000 katika 1985 na 922 kwa kila idadi ya watu 100,000 kufikia 1992. Idadi hiyo inaendelea kuongezeka. Si ajabu kwamba gazeti la habari la Urusi (“Hoja na Mambo Hakika”) liliandika hivi: “Tunatamani kuishi—kubaki tukiwa hai—kuokoka kipindi hiki chenye kuhofisha . . . hofu ya kupanda gari-moshi—linaweza kuacha reli au kuharibiwa kimakusudi; hofu ya kupanda ndege—utekaji-nyara ni mwingi au ndege hiyo yaweza kuanguka; hofu ya kupanda gari-moshi la chini ya ardhi—kwa sababu linaweza kugongana na jingine au kulipuka; hofu ya kutembea barabarani—unaweza kupatwa na risasi kimakosa kutoka kwa vikundi vyenye kupigana au kunyang’anywa mali, kubakwa, kupigwa, au kuuawa; hofu ya kupanda gari—kwa sababu laweza kuchomwa moto, kulipuliwa, au kuibwa; hofu ya kuingia katika sebule za majengo ya makazi, mikahawa, au madukani—unaweza kujeruhiwa au kuuawa katika mojawapo.” Na gazeti la Hungaria HVG lililinganisha jiji moja lenye jua katika Hungaria na “makao makuu ya majambazi,” likisema kwamba katika miaka mitatu ya majuzi, jiji hilo limekuwa “chanzo cha kila aina mpya ya uhalifu . . . Mambo ya kutokeza hofu yanazidi huku watu wakiona polisi wakiwa hawajajitayarisha kupigana na majambazi.”

AFRIKA: Gazeti Daily Times la Nigeria liliripoti kwamba “vyuo vya elimu ya juu” katika nchi fulani ya Afrika Magharibi vilikuwa vikipatwa na “maogofyo mengi, yenye kusababishwa na washiriki wa madhehebu fulani ya kisiri: karibu kufikia hatua ya kukomesha mfuatio wowote wa elimu.” Liliendelea kusema: “Maogofyo yanazidi kuenea, yakiandamana na kupoteza uhai na mali.” Kuhusu nchi nyingine ya Afrika, The Star la Afrika Kusini liliripoti: “Kuna aina mbili za jeuri: pambano kati ya jumuiya mbalimbali, na ujeuri wa uhalifu wa kawaida. Ujeuri kati ya jumuiya mbalimbali umepunguka sana, ujeuri wa uhalifu wa kawaida umeongezeka sana.”

MABARA YA AMERIKA: The Globe and Mail la Kanada liliripoti kwamba kuna ongezeko la uhalifu wenye jeuri nchini Kanada katika kipindi cha majuzi cha miaka 12 mfululizo, yote hayo yakiwa “sehemu ya mwelekeo ambao umetokeza ongezeko la asilimia 50 la jeuri katika mwongo ambao umepita.” Kwa wakati uo huo, El Tiempo la Kolombia liliripoti kwamba katika Kolombia, kulikuwa na utekaji-nyara 1,714 katika mwaka mmoja wa majuzi, “idadi ambayo ni zaidi ya maradufu ya utekaji-nyara wote uliorekodiwa katika ulimwengu wote katika kipindi hichohicho.” Kwa mujibu wa Idara ya Sheria ya Mexico, uhalifu wa ngono ulifanywa katika jiji layo kuu kila baada ya saa nne katika mwaka mmoja wa majuzi. Msemaji mmoja alisema kwamba karne ya 20 imepatwa na upungufu wa thamani ya watu. “Twaishi katika kizazi cha kutumia na kutupa,” yeye akamalizia.

MAENEO YA BAHARI-KUU: Taasisi ya Uhalifu ya Australia ilikadiria kwamba huko uhalifu unagharimu “angalau dola bilioni 27 kila mwaka, au karibu dola 1600 kwa kila mwanamume, mwanamke na mtoto.” Hiyo ni karibu “asilimia 7.2 ya jumla ya mazao ya nchi.”

ULIMWENGUNI POTE: Kitabu The United Nations and Crime Prevention chasema kwamba kuna “ongezeko lenye kuendelea ulimwenguni pote la uhalifu katika miaka ya 1970 na 1980.” Chasema: “Idadi ya uhalifu ulioripotiwa iliongezeka kutoka milioni 330 hivi katika 1975 hadi karibu milioni 400 katika 1980 na inakadiriwa kuwa ulifikia nusu bilioni katika 1990.”

[Habari kuhusu chazo cha ramani]

Ramani na tufe: Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Dunia kwenye kurasa 3, 6, na 9: Picha ya NASA

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki