Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 10/8 kur. 6-8
  • Kujitahidi Kumaliza Uhalifu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kujitahidi Kumaliza Uhalifu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je, Hili Ni Oni Hasi Mno?
  • Serikali Zinajaribu Kudhibiti Uhalifu
  • Kupoteza Uhakika
  • Pigano Linaloshindwa Kudhibiti Uhalifu
    Amkeni!—1998
  • Wewe Unataka Uhalifu Umalizwe?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Je, Tutawahitaji Polisi Sikuzote?
    Amkeni!—2002
  • Kwa Nini Uhalifu Ni Mwingi Sana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 10/8 kur. 6-8

Kujitahidi Kumaliza Uhalifu

“VIJANA Wadai Uchoshi Ndio Kisababishi Kikuu cha Uhalifu wa Vijana,” kikataja kichwa kikuu kimoja katika gazeti moja la habari lililo mashuhuri katika Uingereza. “Zogo la Nyumbani Latokeza Ongezeko la Uhalifu,” likasema gazeti jingine. Na gazeti la tatu likasema: “Uraibu ‘Wasababisha Maelfu ya Uhalifu.’” Gazeti Philippine Panorama lilikadiria kwamba asilimia 75 ya uhalifu wote katika Manila ulifanywa na watumiaji wa dawa za kulevya.

Mambo mengine yaweza pia kuchochea tabia ya uhalifu. “Umaskini waandamana na utajiri mwingi” ndio uliorejezewa na inspekta-mkuu wa polisi wa Nigeria. Msongo wa marika na matazamio madogo ya kazi, ukosefu wa vizuizi vikali vya kisheria, mvunjiko wa ujumla wa maadili katika familia, ukosefu wa staha kwa mamlaka na sheria, na ujeuri wenye kupita kiasi katika sinema na vidio pia zilitajwa.

Jambo jingine ni kwamba watu wengi hawaamini tena kwamba uhalifu hauna faida. Mwanasosholojia kwenye Chuo Kikuu cha Bologna katika Italia alionelea kwamba kwa zaidi ya miaka mingi, “idadi za wizi ulioripotiwa iliongezeka na idadi ya watu waliohukumiwa makosa hayo ilipunguka.” Yeye alitaja kwamba “kwa kulinganisha, idadi ya watu waliohukumiwa na jumla ya wizi ulioripotiwa imepunguka kutoka asilimia 50 hadi 0.7.”

Maneno ya The New Encyclopædia Britannica ni yenye kuhuzunisha lakini ni ya kweli: “Ongezeko la uhalifu laonekana kuwa sehemu ya jumuiya zote zenye maendeleo, na hakuna maendeleo katika sheria au kutoa adhabu yawezayo kuonyeshwa kwamba umepunguza sana tatizo hilo. . . . Kwa jumuiya ya kisasa ya mijini, ambamo ukuzi wa kiuchumi na mafanikio ya kibinafsi ndiyo mambo ya kutangulizwa, hakuna sababu ya kufikiria kwamba viwango vya uhalifu havitaendelea kuongezeka.”

Je, Hili Ni Oni Hasi Mno?

Je, hali ni mbaya sana hivyo? Je, maeneo mengine hayaripoti upungufu wa uhalifu? Ni kweli, uhalifu umepungua katika maeneo fulani, lakini takwimu zaweza kudanganya. Kwa kielelezo, iliripotiwa kwamba uhalifu katika Filipino ulipungua kwa asilimia 20 baada ya bunduki kupigwa marufuku. Lakini Asiaweek lilieleza kwamba ofisa mmoja aamini kwamba wezi wa magari na wanyang’anyi wa benki walikuwa wameacha kuiba magari na kupora benki nao walikuwa “wameanza kuteka watu nyara.” Unyang’anyi mchache zaidi wa benki na wizi wa magari ulisababisha upungufu katika jumla ya visa vya uhalifu, lakini upungufu huo ulipoteza umuhimu wao mwingi kwa kuwa kulikuwa na ongezeko la mara nne katika utekaji-nyara!

Likitoa ripoti juu ya Hungaria, gazeti HVG liliandika: “Kwa kulinganisha na miezi sita ya kwanza ya 1993, hesabu za uhalifu zilipungua kwa asilimia 6.2. Lakini kile ambacho polisi walisahau kutaja ni kwamba upungufu huo . . . hasa watokana na mabadiliko ya usimamizi.” Kiasi cha kifedha ambacho visa vya wizi, upunjaji, au uharibifu wa mali kiliandikishwa kilikuwa kimeongezeka kwa asilimia 250. Hivyo uhalifu wa mali chini ya kiasi hicho hauandikishwi tena. Kwa kuwa uhalifu wa mali ni robo tatu za uhalifu wote katika nchi hiyo, upungufu huo si wa kweli hata kidogo.

Ni kweli kwamba ni vigumu kupata tarakimu sahihi za uhalifu. Sababu moja ni kwamba uhalifu mwingi—labda kufikia asilimia 90 katika hali fulani-fulani—hauripotiwi. Lakini kubisha kama uhalifu umeongezeka au kupunguka si suala kuu. Watu wanatamani uhalifu uondolewe, si kupunguzwa tu.

Serikali Zinajaribu Kudhibiti Uhalifu

Uchunguzi mmoja wa 1990 uliofanywa na Umoja wa Mataifa ulifunua kwamba nchi zenye maendeleo zaidi zinatumia wastani wa asilimia 2 hadi 3 wa bajeti zao za kila mwaka kudhibiti uhalifu, huku nchi zenye kuendelea zikitumia hata zaidi, wastani wa asilimia 9 hadi 14. Kuongeza idadi ya polisi na kuwaandalia vifaa bora ni mambo ya kutangulizwa katika nchi fulani. Lakini matokeo ni tofauti-tofauti. Wananchi fulani wa Hungaria wanalalamika hivi: “Hakuna kamwe polisi wa kutosha kushika wahalifu lakini sikuzote kuna polisi wengi zaidi wa kushika wavunjaji wa sheria za barabarani.”

Hivi majuzi serikali nyingi zimepata ikiwa jambo la lazima kuweka sheria kali zaidi za uhalifu. Kwa kielelezo, kwa kuwa “utekaji-nyara unaongezeka katika Amerika ya Latini,” lasema gazeti Time, serikali za huko zimeitikia kwa kutunga sheria ambazo “ni kali na hazitumiki. . . . Ni rahisi kupitisha sheria,” hilo lakiri, “lakini ni vigumu zaidi kuzitekeleza.”

Inakadiriwa kwamba katika Uingereza zaidi ya programu 100,000 za majirani kuchungiana nyumba, ambazo zinachunga angalau nyumba milioni nne, zilikuwapo katika 1992. Programu kama hizo zilitekelezwa katika Australia katika miaka ya katikati ya 1980. Lengo lao, yasema Taasisi ya Australia ya Uhalifu, ni kupunguza uhalifu “kwa kuboresha ufahamu wa umma kuhusu usalama wa peupe, kwa kuboresha mtazamo na mwenendo wa wakazi katika kuripoti uhalifu na visa vyenye kutilika shaka katika ujirani na kwa kupunguza urahisi wa kupatwa na uhalifu kwa kuwekea alama mali zao na kuweka vifaa vya usalama vinavyotumika vizuri.”

Televisheni za ulinzi hutumiwa katika sehemu fulani kuunganisha vituo vya polisi pamoja na maeneo ya biashara. Kamera za vidio hutumiwa pia na polisi, benki, na maduka ili kuzuia uhalifu au kuwa vyombo vya kutambulisha wavunja-sheria.

Katika Nigeria polisi wana vizuizi vya barabarani katika jitihada za kushika wanyang’anyi na wezi wa magari. Serikali imeanzisha kikosi cha kupambana na uhalifu wa kibiashara na upunjaji. Kamati za uhusiano kati ya polisi na jumuiya ambayo imefanyizwa kwa viongozi wa jumuiya huarifu polisi juu ya utendaji wa uhalifu na watu wenye kutilika shaka.

Wageni ambao huenda Filipino huona kwamba nyumba nyingi mara nyingi haziachwi bila mtu wa kulinda na kwamba watu wengi wana mbwa. Wafanyabiashara hutumia walinzi wa kibinafsi kulinda biashara zao. Vifaa vya kuzuia gari lisiibwe huuzwa sana. Watu wawezao kufanya hivyo huingia katika maeneo au makao yao yenye ulinzi mkali.

Gazeti la Uingereza The Independent lilisema: “Watu wakosapo uhakika katika sheria, wananchi wengi huzidi kujiundia kinga za jumuiya zao zenyewe.” Na watu wengi zaidi na zaidi wanajihami. Kwa kielelezo, katika Marekani, inakadiriwa kwamba nusu za nyumba zote zina angalau bunduki moja.

Daima serikali zinasitawisha njia mpya za kupambana na uhalifu. Lakini V. Vsevolodov, wa Chuo cha Mambo ya Kitaifa katika Ukrainia, asema kwamba kulingana na ripoti za UM, watu wengi wenye vipawa hupata “njia za kipekee sana za kutenda uhalifu” hivi kwamba “mazoezi ya watekelezaji sheria” hayawezi kuwafikia. Wahalifu wenye akili hurudisha pesa nyingi sana katika biashara na mambo ya kijamii, wakijitambulisha na jamii na “kujipa wenyewe vyeo vya juu katika jamii.”

Kupoteza Uhakika

Idadi yenye kuongezeka ya watu katika baadhi ya nchi hata imeanza kuamini kwamba serikali yenyewe ni sehemu ya tatizo hilo. Gazeti Asiaweek lilinukuu mkuu wa kikundi fulani cha kupambana na uhalifu akisema: “Karibu asilimia 90 ya washukiwa wote tunaowakamata ama ni polisi ama ni wanajeshi.” Ziwe ni za kweli au sivyo, ripoti hizo zilimfanya mtungaji-sheria mmoja kueleza hivi: “Ikiwa wale wanaoapishwa kutegemeza sheria wenyewe ndio wavunjaji wa sheria, jamii yetu imo matatani.”

Kashfa za ufisadi zinazohusu maofisa wa ngazi za juu zimekumba serikali nyingi katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, jambo lenye kudhoofisha hata zaidi uhakika wa wananchi. Mbali na kupoteza imani katika uwezo wa serikali kudhibiti uhalifu, watu sasa wanatilia shaka azimio lao la kufanya hivyo. Mwelimishaji mmoja aliuliza: “Hawa wenye mamlaka wanawezaje kupambana na uhalifu ikiwa wao wenyewe wamejiingiza sana katika uhalifu?”

Serikali huja na kwenda, lakini uhalifu unadumu. Lakini kuna wakati unaokuja karibuni ambapo uhalifu hautakuwapo tena!

[Picha katika ukurasa wa 7]

Vizuia-uhalifu: Kamera za televisheni za ulinzi, malango ya chuma, na mlinzi mwenye mbwa aliyezoezwa

[Picha katika ukurasa wa 8]

Uhalifu hufanya watu wawe wafungwa wa nyumba zao wenyewe

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki