Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 2/22 kur. 4-6
  • Pigano Linaloshindwa Kudhibiti Uhalifu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Pigano Linaloshindwa Kudhibiti Uhalifu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uhalifu Huanza na Mambo Madogo
  • Wahalifu Ni Akina Nani?
  • Makusudio Mema Hayatoshi
  • Maofisa wa Sheria Wamejitoa Jinsi Gani?
  • Kujitahidi Kumaliza Uhalifu
    Amkeni!—1996
  • Wewe Unataka Uhalifu Umalizwe?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Wakati Ambapo Hakukuwa na Uhalifu
    Amkeni!—1998
  • Kwa Nini Uhalifu Ni Mwingi Sana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 2/22 kur. 4-6

Pigano Linaloshindwa Kudhibiti Uhalifu

“UHALIFU ungeweza kudhibitiwa haraka sana ikiwa kila mtu alikuwa amejitayarisha kufanya jitihada,” mkuu wa hapo zamani wa Polisi wa Jiji Kuu alinukuliwa akisema katika Liverpool Daily Post la Uingereza. Kwa kweli ikiwa kila mtu angetii sheria, uhalifu ungetoweka.

Na bado, katika mahali pengi uhalifu unaendelea kuongezeka. Maneno yaliyotamkwa maelfu ya miaka iliyopita yanatumika wakati wetu: “Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma.” (Mwanzo 6:11)—Ona sanduku kwenye ukurasa unaoelekeana na huu.

Uhalifu Huanza na Mambo Madogo

Kwa kuvunja sheria katika mambo madogo mtu aweza kuzoea kuivunja katika mambo makubwa. Ili kukazia uhakika huu kwa wanafunzi wake, mwalimu mmoja alieleza: “Wezi wa benki huanza kwa kuiba kalamu shuleni.”

Baadaye, ni nini ambacho mara nyingi hutukia katika mahali pa kazi? Watu hukaa nyumbani bila kwenda kazini wakitoa sababu kuwa wana maradhi kisha kupokea faida za kifedha ambazo hawakustahili kuzipata. Zoea hili lisilo la haki limekuwa la kawaida zaidi kuliko vile mtu angeweza kufikiri. Kwa kielelezo, katika Ujerumani, asilimia 6 ya likizo ya ugonjwa iliyoripotiwa na wafanyakazi huangukia kila Jumatano, asilimia 10 kila Jumanne, na asilimia 16 kila Alhamisi, lakini asilimia kubwa sana 31 huangukia kila Jumatatu, kila Ijumaa ikiongoza kwa asilimia 37! Je, kwa kweli watu ni wagonjwa mara nyingi siku za Jumatatu na Ijumaa, au hii ni namna nyingine tu ya wizi?

Wahalifu Ni Akina Nani?

Bila shaka, vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na watu wa kawaida tu kwa kawaida haviwi na matokeo yaleyale kama vile vinavyofanywa na watu walio na nyadhifa za mamlaka. Katika miaka ya mapema ya 1970, Marekani ilitikiswa na uhalifu wa kisiasa uliokuwa mkubwa sana hivi kwamba jina lililohusishwa nao hata likawa sehemu ya lugha ya Kiingereza.

Kulingana na Barnhart Dictionary of New English, “Watergate,” ni “kashfa, hasa ile inayohusisha jaribio la kusitiri habari zenye kudhuru au shughuli haramu.”a Kisha yaongezea: “Tukio la Watergate lilitia alama kubwa katika lugha ya miaka ya 1970. Neno hilo lilizalisha istilahi mpya za namna mbalimbali na neno -gate, mara nyingi liliongezwa mwishoni mwa neno la msingi ili kuashiria kashfa au ufisadi.”

Tangu wakati huo idadi yoyote ya kashfa zimeonyesha kwamba uhalifu umeenea pote, hata miongoni mwa wale wapaswao kuwa vielelezo vizuri katika kutegemeza sheria. Katika Japani ufisadi wa kisiasa ulikuwa umeenea sana hivi kwamba sheria mpya ilihitaji kupitishwa katika miaka ya mapema ya 1990, ili kupigana nao. Katika 1992 rais wa Brazili aling’olewa mamlakani kwa mashtaka ya ufisadi.

Je, si ni wazi kwamba makosa ya wale walio na nyadhifa za mamlaka, kutia ndani wazazi, walimu wa shule, na maofisa wenye kutekeleza sheria, huchangia vitendo vya uhalifu vya umma?

Makusudio Mema Hayatoshi

Watu wengi wangekubali kwamba serikali zinataka kuondoa uhalifu. Lakini, ofisa aliyestaafu alionelea hivi kuhusu nchi yake: “Serikali imefanya machache sana katika kufanyiza utaratibu wa haki ufanye kazi kwa kasi na kwa kufaa. Hakuna mahakimu wa kutosha, kwa hiyo wale wachache tulio nao wanafanyishwa kazi kupita kiasi. Jeshi la polisi lina upungufu wa watumishi na halina vifaa vya kutosha. Nyakati nyingine polisi hawalipwi mshahara wao kwa wakati unaofaa, hili likifanya wawe rahisi kushawishiwa kuchukua rushwa.”

Gazeti la Italia La Civiltà Cattolica laombolezea “kukosa nguvu kwa serikali katika kushughulika na uhalifu uliopangwa” kisha laonelea: “Uwajibikaji kwa upande wa mashirika ya kutekeleza sheria na mahakama katika kupigana na uhalifu unatambuliwa, lakini inaonekana kwamba serikali haina athari yoyote juu ya uhalifu uliopangwa; kinyume cha hiyo, nguvu na mamlaka yake hukua.”

Makusudio mazuri ya serikali ya kupigana na uhalifu kwa wazi hayatoshi. Anita Gradin, mjumbe wa Ulaya wa uhamiaji na mambo ya hukumu, alionelea hivi kwa kufaa: “Tunahitaji njia bora, na zenye matokeo kwa ajili ya kushirikiana katika pigano dhidi ya magendo na biashara ya madawa ya kulevya, uingizaji haramu wa wageni katika nchi na uhamiaji haramu, uhalifu uliopangwa, upunjaji na ufisadi.”

Maofisa wa Sheria Wamejitoa Jinsi Gani?

Wengine hutilia shaka kiwango ambacho kwa kweli wenye mamlaka wamejitoa ili kupigana na uhalifu. Mkaguzi mkuu wa polisi wa zamani wa nchi moja aonelea kwamba kila mtu, angalau hadharani, “hulaumu ufisadi na uhalifu wa kiuchumi.” Na bado, anasema, hakuna tamaa halisi ya wote ya kukomesha uhalifu na ufisadi. Idadi inayoongezeka ya watu—kutia ndani maofisa wa sheria—yaonekana huona rushwa, kupunja, na kuiba kuwa njia zinazokubalika za kufanikiwa.

Uhakika wa kwamba wengi “wanaofanya uhalifu huachiliwa huru,” kama alivyoeleza ofisa wa ushuru, bila shaka ni sababu moja inayochangia ongezeko la uhalifu. Kwa kielelezo, kichapo kimoja cha Urusi husema juu ya “urahisi ambao wahalifu huponyoka bila kuadhibiwa.” Kichapo hicho huongezea, hili, “huonekana kutia moyo raia wa kawaida kufanya uhalifu ulio wa kinyama zaidi.” Hili ni kama tu vile mwandikaji wa Biblia alivyotaarifu miaka 3,000 iliyopita: “Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya.”—Mhubiri 8:11.

Si kutia chumvi kusema kwamba serikali haziwezi kudhibiti ongezeko la uhalifu. Gazeti la habari la Ujerumani Rheinischer Merkur laeleza: “Hofu ya umma ya ongezeko la uhalifu wenye jeuri ni yenye kina kirefu na inaweza kupunguzwa si na chama cha kawaida cha kisiasa chenye kubishana-bishana wala na takwimu zinazoonyesha kwamba hali si mbaya kama inavyoweza kuonekana.”

Badala ya uhalifu kutokuwa mbaya kama unavyoweza kuonekana, hali yaelekea kuwa kinyume cha hilo. Na bado, kuna fursa ya kuwa na matumaini mema. Ulimwengu usio na uhalifu unaendelea kukaribia daima, na waweza kuishi uuone. Makala inayofuata itaonyesha kwa nini tunasema hivyo.

[Maelezo ya Chini]

a Tukio la Watergate liliitwa hivyo kwa sababu mvunjiko kwenye jengo lililoitwa kwa jina hilo ndio uliosababisha mambo yawe wazi. Hatimaye kashfa hiyo iliongoza kwenye kujiuzulu kwa Rais wa Marekani Richard Nixon na kifungo cha washauri wake wakuu kadhaa.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Watu wengi huona uhalifu kuwa njia inayokubalika ya kufanikiwa

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

Dunia Iliyojaa Uhalifu

AFRIKA KUSINI: “Jeuri isiyodhibitiwa karibu inatisha kila mmoja wetu, na kila tufanyalo—na jambo fulani lenye kuleta mabadiliko lazima lifanywe.”—The Star.

BRAZILI: “Katika kuitikia ongezeko la jeuri, mamia ya maelfu ya watu yalijaza barabara za sehemu ya mjini iliyo na shughuli nyingi za kibiashara [za Rio de Janeiro], kuonyesha hofu na hasira juu ya uhalifu ambao umeteka jiji lao.”—International Herald Tribune.

CHINA: “Magenge ya majambazi yanaibuka tena katika China na uhalifu mkubwa waonekana kuwa usiodhibitiwa. . . . Wataalamu wa China wanasema idadi ya magenge na ‘jamii za siri’ inaongezeka kwa haraka kuliko vile polisi wanavyoweza kuzihesabu.”—The New York Times.

FILIPINO: “Sita kati ya familia kumi katika Filipino zasema kuwa hazijihisi salama nyumbani mwao au barabarani.”—Asiaweek.

IRELAND: “Jamii za wahalifu zinazotenda kama mafia zimetia mizizi katika sehemu za ndani zaidi za Dublin na vitongoji vyake vya magharibi vilivyo maskini zaidi. Magenge hayo yanazidi kuwa na silaha.”—The Economist.

MAREKANI: “Marekani ndilo taifa lililo na jeuri nyingi zaidi katika ulimwengu ulioendelea kiviwanda. . . . Hakuna taifa jingine lililoendelea kiviwanda linaloikaribia.”—Time.

MEXICO: “Uhalifu umeongezeka kwa kasi sana kwa kipindi kifupi cha wakati hivi kwamba unashtua kwa hofu.”—The Wall Street Journal.

NIGERIA: “Kizio cha familia, makanisa, misikiti, shule na vilabu vimeshindwa katika wajibu wao wa kuzuia vijana kujiingiza katika uhalifu, kulingana na msemaji wa polisi, Bw. Frank Odita.”—Daily Champion.

TAIWAN: “Katika Taiwan . . . viwango vinavyoongezeka vya unyang’anyi, mashambulizi na uuaji kimakusudi vimechuruzika ndani ya jamii . . . Kwa kweli, viwango vya uhalifu vinaongezeka polepole na katika visa fulani vinazidi vile vya nchi za Magharibi.”—The New York Times.

UINGEREZA: “Kilele cha jeuri kimepanda juu na kuna uwezekano unaoongezeka wa mkosaji kutumia jeuri kama tegemeo la kwanza.”—The Independent.

UJERUMANI: “Lile pengo kati ya utayari wa kufanya vitendo vya jeuri na hali inayomwongoza mtu kufanya hivyo limekuwa jembamba kwa hakika. Kwa hiyo haishangazi kwamba jeuri imekuwa tukio la kila siku.”—Rheinischer Merkur.

URUSI: “Magenge yanayotenda kama mafia yamegeuza jiji ambalo wakati wa utawala wa Ukomunisti lilikuwa moja ya majiji yaliyo salama zaidi ulimwenguni kuwa makao makuu ya wahalifu. . . . ‘Katika miaka yangu 17 ya doria,’ asema luteni wa polisi Gennadi Groshikov, ‘sijapata kamwe kuona uhalifu mwingi hivi katika Moscow, wala sijaona kitu kilicho kiovu namna hii.’”—Time.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki