Wakati Ambapo Hakukuwa na Uhalifu
JE, WAWEZA kuwazia ulimwengu usio na uhalifu? Huenda usiwazie hivyo ikiwa umesoma ripoti za habari kama ile iliyotokea katika gazeti la kila siku la Ujerumani Süddeutsche Zeitung: “Wataalamu wa elimu jinai wanaongea kuhusu namna ambavyo uhalifu umeenea upya kwa kiwango kikubwa. Usemi wao umejaa ubashiri na picha inayotokezwa ni yenye kutabiri maafa makubwa.”
Kulingana na ukaguzi wa 1995 wa maelfu ya Wanaulaya, karibu kila mtu ana wasiwasi juu ya kusumbuliwa na uhalifu. Katika Ujerumani, Uholanzi, Poland, Urusi, na Uingereza, uhalifu uko katika nafasi ya kwanza katika orodha ya mambo ambayo watu huhofu zaidi. Hofu ya uhalifu iliorodheshwa nambari mbili katika Denmark, Finland, na Uswisi na ikaorodheshwa nambari tatu katika Ufaransa, Ugiriki, na Italia. Kati ya mataifa 12 yaliyofanyiwa ukaguzi, ni Hispania pekee ambayo haikuorodhesha uhalifu miongoni mwa sababu tatu zilizo kuu za hofu.
Kiwango cha uhalifu kimeongezeka sana katika Ulaya Mashariki. Katika baadhi ya nchi hizi, ongezeko limekuwa kati ya asilimia 50 na 100, ilhali katika nchi hizo nyingine, linafikia hata asilimia 193 mpaka 401!
Na bado, katika wakati fulani kulikuwako ulimwengu ambao haukuwa na uhalifu. Ni wakati gani huo, na ulimwengu huo uliharibiwaje?
Uhalifu Ulitoka Wapi?
Uhalifu unaofasiliwa kama “uvunjaji mzito wa sheria,” asili yake ni katika makao ya roho. Wanadamu wa kwanza, Adamu na Hawa, hawakuumbwa wakiwa na mielekeo ya kuhalifu sheria, wala hawakuwa na daraka lote la kuanzisha uhalifu katika jamii ya kibinadamu. Mwana-roho mkamilifu wa Mungu aliruhusu mawazo mabaya yatie mizizi ndani ya moyo wake, ambayo, yalipokuzwa, yaliongoza kwenye uhalifu. Huyo ndiye aliyekuwa na daraka la kufisidi ulimwengu wa awali usiokuwa na uhalifu. Kwa kuvunja sheria ya Mungu, alijifanya mwenyewe kuwa mhalifu, na anatambulishwa katika Biblia kuwa Shetani Ibilisi.—Yakobo 1:13-15; Ufunuo 12:9.
Baada ya kuanzisha mwendo wa upinzani dhidi ya Mungu katika mbingu zisizoonekana, Shetani alikuwa ameazimia kusambaza njia zake za uhalifu kwa wanadamu walioko duniani. Simulizi la Biblia la jinsi Ibilisi alivyofanya hivi ni fupi na sahili, lakini lenye ukweli. (Mwanzo, sura ya 2-4) Kwa kuongozwa vibaya na kwa hila na mhalifu huyu mwenye uwezo upitao wa binadamu, Adamu na Hawa, walikataa kufuata viwango vya Mungu. Wakawa wahalifu kwa kutomtii Mungu. Baadaye, hapana shaka waliogopa wakiwa katika hali ya kitisho wakati mwana mzaliwa wao wa kwanza, Kaini, alipofikia kiwango cha kumpokonya ndugu yake Abeli mali yake yenye thamani sana, uhai wenyewe!
Hivyo, kati ya wale watu wa kwanza wanne kukaa duniani, watatu waligeuka kuwa wahalifu. Kwa hiyo, Adamu, Hawa, na Kaini walipoteza fursa yao ya kuishi katika ulimwengu usiokuwa na uhalifu. Kwa nini, baada ya muda huu wote, twaweza kuwa na uhakika wa kwamba ulimwengu wa namna hiyo sasa u karibu?