Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 9/8 kur. 12-14
  • 1995—Vipi Kuhusu Wakati Wetu Ujao?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • 1995—Vipi Kuhusu Wakati Wetu Ujao?
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Nani Huwasha Cheche ya Chuki?
  • Wakati Ujao Ulio Tofauti Waahidiwa
  • Hatua ya Mwisho Iliyoahidiwa na Mungu
  • Jinsi Ulimwengu Utakavyoungana
    Amkeni!—1993
  • Tafuta Sana Amani ya Kweli na Kuifuatia!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Kukoma kwa Vita
    Amkeni!—1999
  • Ulimwengu Wetu Unaobadilika—Wakati Ujao Una Nini kwa Kweli?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 9/8 kur. 12-14

1995—Vipi Kuhusu Wakati Wetu Ujao?

“Ulimwengu wahitaji dira iliyo bora kuliko wito sahili wa demokrasi na masoko huru—lakini hakuna yoyote inayopatikana.”—Will Hutton, Guardian Weekly.

KUTOKANA na mtazamo wa kibinadamu, taarifa hiyo huenda ionekane kuwa kweli. Ulimwengu waonekana kukosa dira yenye kutegemeka ili kuuelekeza kwenye upande wa amani, usalama, haki, usawa, na serikali nzuri. Mwanadamu amejaribu karibu kila mfumo wa serikali, tangu umaliki hadi jamhuri, kutoka udikteta hadi demokrasi, na bado apata ulimwengu kuwa usiotawalika. Sasa tunapaswa kugeukia njia gani?

Kunaonekana kuwa na uchaguzi—kijia kinachoteremka kuelekea ulimwengu wa ujeuri zaidi, uhalifu, ufisadi, ukosefu wa haki, unafiki wa kidini na kisiasa, chuki ya kitaifa, na kutumia vibaya walio maskini. Hiyo ndiyo njia ambayo wengine husema huongoza kwenye mvurugo.

Ama kuna, mpando mgumu wa kujisulubu kuelekea ulimwengu ulio bora unaotegemea suluhisho la Mungu la serikali, linalopatikana katika Biblia. Huo ni mgumu kwa sababu unahitaji ujasiri wa kimaadili, kujidhabihu, kutazama maisha kwa njia ya kiroho, na kuitikadi katika Mungu mwenye kusudi. Lakini ili mpando huo ufanikiwe ni lazima mwanadamu awe mnyenyekevu pia—mnyenyekevu mbele za Muumba wake. Ni lazima ageukie Mungu kwa ajili ya utawala mwadilifu. Petro mtume Mkristo alishauri hivi: “Nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.”—1 Petro 5:6, 7; Ufunuo 4:11.

Ni Nani Huwasha Cheche ya Chuki?

Mwanadamu peke yake hawezi kubadili ulimwengu huu uwe mzuri kwa kudumu—vile vikundi vya ubinafsi na uovu viko vingi mno na vina nguvu sana. Nabii Yeremia alikuwa sawa alipoandika: “Ee BWANA, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” (Yeremia 10:23) Bila Mungu, mwanadamu hawezi kuelekeza hatua zake kwa mafanikio kwa faida ya familia nzima ya kibinadamu. Kwa nini iko hivyo? Kwa sababu kwa kuongezea kutokamilika kwetu tulikorithi sikuzote kuna yule adui asiyeonekana Shetani, ambaye yuko tayari kuwasha cheche, kama alivyofanya katika Rwanda, kuwasha miongoni mwa watu mgongano wenye kumwaga damu.—Mwanzo 8:21; Mathayo 4:1-11.

Ili kuwasha cheche ya ubaguzi, chuki, na uuaji kimakusudi katika mioyo na akili za watu, Shetani amekaza kikiki katika mataifa lile wazo la ukuu wa kitaifa, kikabila, na kidini. Elimu hii ya chuki iliyokazika sana hupandwa tangu utotoni na wazazi ambao akili zao zimeishikilia, mara nyingi kupitia karne nyingi za mapokeo. Kisha mapokeo haya huimarishwa na mifumo ya shule na mafundisho ya kidini. Hivyo mamilioni ya watu wanakua wakiwa na chuki na ubaguzi katika mioyo yao. Wamedhibitiwa, kupumbazwa tangu utotoni, kuwageuka wanadamu wenzao kwa amri ya viongozi wao wa kisiasa na kidini walio walaghai. Kutajwa kwa shime bila kufikiri ama taarifa rasmi katika vyombo vya habari kwaweza kuwasha cheche, kwaweza kuwasha moto mkubwa, ambao huishia katika “usafishaji wa kikabila” ama machinjo makuu.

Akionyesha kile kiwezacho kutokezwa na wakati ujao wa karibuni, Martin van Creveld, mwanahistoria wa jeshi katika Israeli, aliandika katika The Transformation of War: “Kutokana na yale tunayoona sasa, yaonekana sana kwamba ushupavu . . . wa kidini utachangia fungu kubwa sana katika kutokeza migongano ya kijeshi” katika ulimwengu wa Magharibi kuliko wakati mwingineo wote “kwa miaka 300 iliyopita.” Hivyo dini, badala ya kuwa kani ya amani na ya kuinua hali ya kiroho ya jamii ya kibinadamu, yadumaa katika fungu layo la kihistoria la kuchochea chuki, mgongano, na mauaji.

Wakati Ujao Ulio Tofauti Waahidiwa

Ikiwa jamii ya kibinadamu itastahili uhai katika ulimwengu mpya wenye haki, basi ni lazima ishiriki katika kutimiza unabii wa Isaya: “Naye [Yehova] atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake. . . . Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu, taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.”—Isaya 2:3, 4.

Ni nani leo wanaotii unabii huu wenye kutokeza ulimwenguni pote? Ni nani waliokufa katika Rwanda badala ya kuua waumini wenzao wa kabila tofauti? Ni nani waliofia katika kambi za mateso za Nazi badala ya kutumika katika majeshi ya Hitler? Ni nani ambao wamefungwa katika magereza ya nchi nyingi badala ya kujifunza vita? Ni wale ambao wamefurahia utimizo wa Isaya 54:13: “Na watoto wako wote watafundishwa na BWANA; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi.”

Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wana amani hiyo sasa kwa sababu wamekubali mafundisho ya Yehova kutoka kwa Neno lake, Biblia. Wao hufuata mafundisho na kielelezo cha Kristo Yesu. Naye alisema nini? “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” (Yohana 13:34, 35) Mashahidi wa Yehova huzoea upendo huu kwa kiwango cha kwamba, ingawa awali walikuwa Wakatoliki na Waprotestanti, sasa wanafanya kazi pamoja kwa upatano katika Ireland Kaskazini. Ingawa awali walikuwa maadui wa kidini, sasa washirikiana wakiwa Wakristo katika Israeli, Lebanoni, na nchi nyinginezo. Wao hawajifunzi vita tena. Ingefanyiza tofauti iliyoje ikiwa watu wote ulimwenguni wangetii maneno ya Yesu na kuyatumia katika maisha zao!

Mashahidi wa Yehova huamini kwamba ulimwengu mpya ulioahidiwa na Mungu uko karibu, ulimwengu ambao utatawalwa na serikali ya kimbingu. Wana msingi gani wa kuwa na tumaini chanya kama hilo?

Hatua ya Mwisho Iliyoahidiwa na Mungu

Katika Neno lake, Biblia, Mungu ameahidi utawala mwadilifu kwa wanadamu wote watiifu. Kupitia kwa nabii wake Danieli, yeye alitabiri kwamba katika wakati wa mwisho wa mfumo wa sasa, angesimamisha serikali ya kudumu na yenye uadilifu. “Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele.” (Danieli 2:44) Huu ni utawala wa Ufalme uleule ambao Kristo alifunza waamini kuuomba katika sala yake ijulikanayo sana: “Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.”—Mathayo 6:9, 10.

Katika sala hiyo twamwomba Mungu atimize ahadi zake kuhusu utawala wake mwadilifu. Na tunajua kwamba Mungu hawezi kusema uwongo. Paulo alisema kuhusu “uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele.” (Tito 1:2; Waebrania 6:17, 18) Na Mungu ameahidi nini? Mtume Petro ajibu hivi: “Kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.”—2 Petro 3:13; Isaya 65:17; Ufunuo 21:1-4.

Kabla ya utawala huo mwadilifu kuweza kufurahiwa kikamili hapa duniani, usafishaji mkubwa lazima utukie. Unabii wa Biblia huungana kuonyesha kwamba tendo hili la kusafisha ulimwengu wa Shetani na nguvu zake za uovu karibuni litatukia. (Ona Mathayo, sura 24; Luka, sura 21; na Marko, sura 13.) Tendo hili la mwisho la kusafisha laitwa pigano la Har–Magedoni, “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.”—Ufunuo 16:14, 16.

Licha ya vile wengi huenda wakafikiri, mwaka wa 2000 si wa maana. Vyovyote viwavyo, tarehe hiyo ni yenye umuhimu kwa Jumuiya ya Wakristo tu. Tamaduni nyinginezo zina mifumo yazo ya kuwekea tarehe. Jambo lililo la maana ni kwamba sasa ndio wakati wa kumgeukia Mungu na Neno lake ili kujithibitishia ni nini “mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” (Warumi 12:1, 2) Kile cha maana ni kwamba sasa ni wakati wako kuchagua—ama kutembea kuelekea baraka za wakati ujao kutoka kwa Mungu ama kuteremkia kijia cha mvurugiko ambacho ulimwengu wa Shetani hutoa. Twakuhimiza kuchagua njia ya Mungu. Chagua uhai!—Kumbukumbu la Torati 30:15, 16.

[Blabu katika ukurasa wa 14]

“Kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya.”—2 Petro 3:13

[Picha katika ukurasa wa 13]

Kwa kweli mataifa yanaweza kufua panga zao ziwe majembe chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki