Kuutazama Ulimwengu
Sababu ya Watoto Kukubali Dawa za Kulevya
“Tunaweza kuwazuiaje watoto wetu wasitumie dawa za kulevya na alkoholi, na kwa nini watoto wengine huona rahisi ‘kusema la’ kuliko wengine?” Maswali hayo yalitokezwa hivi majuzi katika gazeti la Parents, lililopata yale yaelekeayo kuwa majibu katika uchunguzi uliofanywa na watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Arizona, Marekani. Huo uchunguzi ulichunguza watoto wapatao 1,200 katika darasa la sita na saba nao ulitoa uangalifu kwenye visababishi kumi vilivyofikiriwa kuweza kuathiri mtoto kutumia dawa za kulevya na alkoholi. Vionyeshi viwili viongozavyo vilikuwa “na mwelekeo wa kusongwa na marika, na kuwa na marafiki ambao hutumia alkoholi ama dawa za kulevya.” Kwa upande ule mwingine, huo uchunguzi ulipata kwamba mafanikio ya kielimu yangeweza kusaidia kukinza—labda kwa sababu huboresha hali ya kujistahi na nadra sana yasitawishe urafiki na watumia vileo.
Uvutio wa Maogofyo
“Matineja wamekuwa waraibu wa michezo yenye kuogofya,” laripoti The Globe and Mail la Kanada. Hilo gazeti lataarifu kwamba “kuna kadi za kubadilishana, vitabu vya vichekesho, usanii, sinema na hata muziki zote za maogofyo, zote zikiwa maarufu katika vikundi vya wabalehe.” Mchapishaji mmoja wa vitabu aliongeza utokezaji wa vitabu vya michezo vyenye kuogofya kwa ajili ya matineja kutoka vinne kwa mwaka hadi kimoja kwa kila mwezi, ili kuridhisha hiyo hamu nyingi mno ya kuvisoma. Wengine wanachapisha vitabu viwili vya michezo yenye kuogofya kwa mwezi. Kwa nini kuna uvutio wa maogofyo kama hayo? Kulingana na mtungaji Shawn Ryan, “kutokana na historia, maogofyo yamependwa sikuzote kunapokuwa na kutamauka ama kukosa furaha.” Kulingana na The Globe, Bw. Ryan alisema hivi: “Bila shaka, katika mwongo wa tisini haturidhiki na serikali, twakosa furaha na kupatwa na hofu kutokana na uhalifu. Hizi ndizo nyakati ambazo mambo ya kuogofya yapendwa sana.”
Kunawa Mikono Ifaavyo
Madaktari husema lile tendo sahili la kunawa mikono kwa ukawaida “husaidia kuondoa vijisumu na virusi vinavyosababisha homa, mafua, vidonda vya kooni, matatizo ya tumbo na magonjwa mazito zaidi,” laripoti The Toronto Star. Hilo gazeti laongezea hivi: “Uchunguzi . . . fulani uliofanywa na daktari wa kuzuia mweneo wa maradhi wa Montreal Dakt. Julio Soto waonyesha kwamba kunawa mikono ifaavyo kwaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa mweneo wa maambukizo ya maradhi ya virusi na bakteria—kwa asilimia ipatayo 54 ya maradhi ya upumuaji na asilimia 72 ya visa vya kuhara.” Shirika la Tiba ya Watoto la Kanada ladokeza kwamba kunawa mikono ifaavyo kwapasa kutia ndani kumwagia mikono maji mferejini na kuisugua kwa sabuni na kuhesabu hadi 30, kuisuza na maji safi ukihesabu hadi 5, na hatimaye, kuikausha kwa taulo safi ambayo haijatumiwa ama taulo ya karatasi ama kikausha mikono. Wanaoshikashika chakula mikahawani, katika vibanda vya vitafunio, na katika maduka makubwa ya kuuza chakula hasa wanahitaji kuwa waangalifu kunawa mikono ifaavyo.
Dhiki kwa Maskini
Maskini wanaoishi mashambani ulimwenguni wako katika hali mbaya sana kulingana na Mkutano wa Ulimwenguni kuhusu Maendeleo ya Kijamii, kongamano la hivi majuzi la UM lililofanywa katika Copenhagen, Denmark. Iliripotiwa kwenye huo mkutano kwamba zaidi ya watu bilioni moja huishi wakiwa maskini kabisa na kwamba zaidi ya nusu ya hawa hushinda njaa kila siku. Kichangizi cha hilo tatizo ni kukosa kazi. Kadirio la jumla ya watu wasio na kazi ama wenye kazi duni ni la juu kufikia milioni 800. Wote wakijumlishwa, asilimia ipatayo 30 ya idadi ya watu ulimwenguni wawezao kufanya kazi hawajaajiriwa kwa njia yenye kutokeza. Watu wapatao bilioni 1.1 hadi bilioni 1.3 huishi kwa mapato yapunguayo dola moja (ya Marekani) kwa siku. Kutojua kusoma na kuandika, ambako kwa hakika hukuza hilo tatizo, sasa kwaathiri watu wapatao milioni 905. Idadi yao haipungui haraka; watoto milioni 130 hawasomi ingawa wastahili, na idadi yao yatarajiwa kupanda hadi milioni 144 kufikia mwaka 2000.
Kulipia Ulevi wa Chuoni
Ulevi wa kupindukia wa wanafunzi wa chuo watokeza gharama za juu siku hizi—hata miongoni mwa wale wasiokunywa kupindukia, kulingana na U.S.News & World Report. Ikiweka kwa ufupi matokeo ya uchunguzi wa vyuo 140, uliochapishwa katika The Journal of the American Medical Association, hilo gazeti liliripoti kwamba asilimia 44 ya wanafunzi wa chuo waliochunguzwa walikuwa walevi wa kupindukia—yaani, nyakati nyingine kwa majuma mawili yaliyopita, wanaume walikunywa chupa tano kwa mfululizo na wanawake walikunywa nne. Asilimia 19 walikuwa walevi wa kupindukia wa kawaida; walikuwa wamekunywa kupindukia angalau mara tatu kwa majuma mawili yaliyopita. Asilimia ya juu ya walevi wa kupindukia walipatwa na matokeo ambayo yeyote angetazamia—walijihisi kichwa kizito, walijihusisha na ngono wasizopangia, walikosa masomo, walipata majeraha, waliharibu mali, na kadhalika. Lakini wanafunzi wengine waliathiriwa pia. Kwenye shule zenye walevi wa kupindukia, wanafunzi 9 kwa 10 walibidika kushughulika na baadhi ya matatizo yaliyosababishwa na ulevi wa wengine, kama vile ushawishi wa kingono usiotakikana, uharibifu wa mali, kusumbuliwa usingizi, na matusi yenye kufedhehesha.
Ardhi Iliyosumishwa Katika Uingereza
Hivi majuzi, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilikubali kwamba inamiliki maeneo kadhaa ya ardhi ambayo yamechafuliwa na uchafuzi wa kisilaha hivi kwamba maeneo hayo hayawezi kuuzwa kamwe, likaripoti gazeti la New Scientist. Hiyo Wizara inamiliki maeneo 3,400 katika Uingereza, yenye ukubwa wa eka 242,000. Thuluthi mbili ya hayo maeneo yametumiwa kufanyia mazoezi na kulenga shabaha. Kwa sababu ya kupunguzwa kwa matumizi ya kijeshi, hiyo Wizara imelazimika kuuza baadhi ya ardhi hii lakini kwa wazi haijui ni kiasi gani cha hayo maeneo ambacho kimechafuliwa sana kwa binadamu kuweza kuishi. Angalau nane ya hayo maeneo yafikiriwa kuwa yamechafuliwa na unururifu wa rangi yenye kung’aa iliyotumiwa wakati mmoja katika dira na mabamba ya kijeshi. Maeneo mengi ya ulengaji shabaha yamezagawa na silaha hatari ambazo hazijalipuliwa. Na angalau eneo moja la ardhi laaminiwa kuwa limechafuliwa na silaha za Vita ya Ulimwengu 1 zenye gesi ya haradali ambayo ilitupwa isivyofaa huko nyuma katika 1918.
Viashiria-Magari vya Wanyama?
Vivuko vya wanyama kwa muda mrefu vimekuwa mahali hatari pa waendesha magari na wanyama pia. Gazeti la mambo ya asili la Kifaransa Terre Sauvage laripoti kwamba kama tokeo la aksidenti nyingi zisababishwazo na wanyama wakivuka barabara za msituni usiku, mafundi kutoka Ofisi ya Kitaifa ya Ufaransa ya Misitu wametokeza uvumbuzi wenye kushangaza. Wanyama husimama waonapo nuru nyekundu! Majaribio yameonyesha kwamba kasimawimbi ya nuru nyekundu huzubaisha wanyama kwa muda mfupi. Kandokando ya barabara za msituni katika Ufaransa, viwakisa vyekundu ambavyo hunasa nuru kutoka kwa mataa ya mbele ya magari yajayo vimewekwa, lakini badala ya kuwakisa nuru kuelekea waendesha magari, vinawakiswa kuelekea msituni. Kabla ya kuruka barabarani, wanyama sasa hungoja hadi hiyo nuru imepotea.
Mayatima wa UKIMWI wa Rumania
Katika Rumania, asilimia 93 ya visa vyote vya maambukizo ya HIV isababishayo UKIMWI viko miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka 12, akaandika ripota Roxana Dascalu kwa ajili ya shirika la habari la Reuters. Aandika kwamba idadi iliyo juu zaidi kupita yote ya watoto wenye HIV katika Ulaya iko katika jiji la bandari la Constantsa, ambapo kumekuwa na watoto 1,200 kama hao 420 wakiwa wamekufa tayari. Nusu ya watoto hawa waliripotiwa kuambukizwa kupitia utiaji-damu mishipani na sindano zisizo haswa kabla ya utawala wa kale kuporomoka katika 1989. Nyingi ya damu yenye UKIMWI iliuzwa na mabaharia kadhaa wenye kuugua na kupelekwa moja kwa moja kwenye mahospitali na makao ya mayatima. Katika makao ambapo watoto wenye HIV hutunziwa, hiyo ripoti yataja kwamba mafanikio “hayapimwi kwa viwango vya uokokaji bali jinsi watoto hutumia siku zao za mwisho na mtazamo wao wakabilipo kifo.” Akasema mfanyakazi mmoja wa makao hayo: “Hatuwaachi watoto wafe peke yao kwenye vitanda vyao. Muuguzi huwabeba mikononi mwao, hukaa kitini kuwapakata.”
Je, Ni Tumaini Jipya kwa Wenzi wa Ndoa Wasiozaa?
Ufundi mpya wa kitiba unawasaidia wenzi wa ndoa wasiozaa kushinda utasa wao, laripoti shirika la habari la Kifaransa la France-Presse. Ufundi huu uliovumbuliwa Denmark, huhusisha utumiaji wa sindano nyembamba ya kioo ili kuweka shahawa moja kwenye yai ndani ya mwanamke. Ingawa huo ufundi wahitaji uangalifu kabisa na ustadi mkubwa (shahawa ikiwa sehemu mbili kwa elfu za milimeta; yai, sehemu ya kumi ya milimeta), hiyo mbinu imefaulu. Ina manufaa ya ziada ya kutukia ndani ya mwili wa mwanamke na kutumia shahawa ya mume badala ya ile ya mtoaji shahawa asiyejulikana—hivyo ikiepusha maswali ya kimaadili na kidini. Kwa sababu udhaifu wa shahawa ndio kisababishi cha utasa kwa thuluthi ya wenzi wote wa ndoa wasiozaa, daktari fulani anayetumia hiyo mbinu ahisi kwamba wenzi wengi wa ndoa huenda sasa wakawa na matumaini mapya ya kuanzisha familia.