Famasi ya Bahari-Kuu
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kanada
DAWA za asili hutolewa wapi? Bila shaka mara moja tutafikiria kuhusu mimea na magugu. Hata hivyo, Dakt. Michael Allen, akiandika katika The Medical Post, afafanua dawa ambazo hupatikana kutoka chanzo kisicho cha kawaida—bahari-kuu.
Bila shaka, jambo hili si jipya; kwa karne nyingi Wachina wametumia viziduo vya samaki kutibu magonjwa. Na mafuta ya samaki yamekuwako kwa muda mrefu, kama vile wengi walio na umri mkubwa wanavyoweza kuthibitisha. Ingawa, ni machache yanayojulikana kuhusu uwezo wa kutibu wa viumbe vya baharini unapolinganishwa na yanayojulikana kuhusu ule wa mimea na magugu.
Viwavyo vyote, kile ambacho kimevumbuliwa kinavutia. Kwa kielelezo, kemikali inayotokezwa na totovu yaweza kutumiwa kutibu pumu. Kuwapo kwa nuklisidi katika sifongo kulichangia ukuzi wa vidarabini, dawa fulani ya kukinza virusi. Mwani wa hudhurungi umetokeza stypoldione, kiviza mgawanyiko wa chembe ambacho huenda kitumiwe kutibu kansa. Na huu ni mwanzo tu.
Hata hivyo, tiba ya mwisho ya magonjwa haitapatikana katika famasia ya bahari-kuu. Bali, ni Ufalme wa Mungu tu uwezao kutimiza ule unabii wenye kusisimua: “Hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.