Jinsi ya Kuuona Urembo Unaotuzunguka
“Katika lugha zote, moja ya maneno yetu ya kwanza ni ‘hebu nione!’”—William White, Jr.
MTOTO mdogo anayetazama kipepeo anayeruka, mume na mke wazee-wazee wanaotazama machweo yenye fahari, mke-nyumbani anayependezwa na mpangilio wake wa waridi—wote kwa muda fulani wanakaza fikira zao kwenye urembo.
Kwa kuwa urembo wa uumbaji wa Mungu uko kila mahali, si lazima kusafiri mamia ya kilometa ili uuone. Mandhari zenye kutia hofu zaweza kuwa mbali, lakini usanii wenye kupendeza waweza kupatikana katika ujirani wako ikiwa utautafuta—na la maana hata zaidi—ikiwa wajua jinsi ya kuutafuta.
Imesemwa mara nyingi kwamba “urembo wategemea mtu anayeuona.” Hata hivyo, ingawa urembo upo, si kila mtu atauona. Huenda ikawa ni mchoro au picha itakayotufanya tuonyeshe upendezi na kutazama. Kwa hakika, wasanii wengi huamini kwamba kufanikiwa kwao hutegemea zaidi uwezo wao wa kutazama kuliko uwezo wao wa kuchora. Kitabu The Painter’s Eye, kilichoandikwa na Maurice Grosser, chaeleza kwamba “mchoraji huchora kwa macho yake, si kwa mikono yake. Chochote anachokiona, akikiona wazi, anaweza kukichora. . . . Kuona wazi ndilo jambo la maana.”
Tuwe wasanii au la, twaweza kujifunza kuona waziwazi zaidi, kutambua urembo unaotuzunguka. Kwa maneno mengine, twahitaji kutoka na kuangalia vitu kwa njia tofauti.
Kuhusiana na hili John Barrett, mwandikaji wa historia ya asili, hukazia thamani ya kujihusisha kibinafsi. “Hakuna kitu kinachochukua mahali pa kujionea mwenyewe, kugusa, kunusa na kusikia wanyama na mimea ikiwa katika mazingira yayo ya kiasili,” yeye asema. “Acha urembo upenye ndani . . . Popote ulipo, tazama kwanza, furahia, kisha tazama tena.”
Lakini tutafute nini? Twaweza kuanza kwa kujifunza kuona zile sehemu nne za urembo. Sehemu hizi zaweza kutambuliwa karibu katika kila upande wa uumbaji wa Yehova. Mara nyingi kadiri tutuapo ili kutazama, ndivyo tutakavyozidi kufurahia usanii wake.
Kutambulisha Sehemu za Urembo
Maumbo na Vigezo. Twaishi katika ulimwengu wenye maumbo mengi. Mengine ni ya kimstari kama ile mihimili ya kichaka cha mwani au ya mistari kama utando wa buibui, ilhali mengine hayana umbo kama vile wingu ambalo hubadilika daima. Maumbo mengi yanavutia, yawe okidi yenye kupendeza, mistari ya kimviringo ya kombe, au hata matawi ya mti ambao umepukutika majani.
Umbo lile lile linaporudiwa, hufanyiza kigezo ambacho chaweza kuvutia macho. Kwa kielelezo, wazia kikundi cha mashina ya miti katika msitu. Maumbo yayo—kila moja likiwa tofauti, na bado yakifanana—hufanyiza kigezo chenye kupendeza. Lakini ili kutambua maumbo na vigezo yanavyofanyiza, lazima kuwe na nuru.
Nuru. Kusambazwa kwa nuru hutoa ubora wa pekee kwa maumbo tunayoona yakiwa yenye kuvutia. Mambo madogo-madogo yanaonekana wazi, mfanyizo unatiwa rangi, na hali inafanyizwa. Nuru hutofautiana kulingana na wakati wa siku, majira ya mwaka, halihewa, na hata mahali tunapoishi. Siku yenye mawingu ikiwa na nuru yayo iliyofifia inafaa kwa ajili ya kuvutiwa na rangi za mbali za maua ya porini au majani yenye rangi nyingi ya wakati wa masika, ilhali majabali na vilele vya milima huonyesha maumbo yayo yenye kutazamisha yanaponakshiwa na jua linalozuka au linalotua. Nuru ya jua isiyo kali ya wakati wa kipupwe katika Kizio cha Kaskazini hupa mandhari ya mashamba uvutio wa kihisia. Kwa upande ule mwingine, jua jangavu la maeneo ya Kitropiki hugeuza bahari isiyo na kina kirefu kuwa mahali pa kufurahia panapopenyeka nuru kwa waogelea-kinyambizi.
Lakini bado kuna sehemu moja ya maana inayokosekana.
Rangi. Hiyo hufanya vitu tunavyoona vipendeze zaidi. Ingawa maumbo yavyo yaweza kuvitofautisha, rangi yavyo hutokeza upekee wavyo. Zaidi ya hilo, kusambazwa kwa rangi katika vigezo vyenye upatano hufanyiza urembo wavyo vyenyewe. Huenda ikawa ni rangi nyangavu sana kama nyekundu au rangi ya machungwa ambayo hutaka uangalifu wetu, au rangi tulivu kama vile buluu au kijani kibichi.
Wazia mahali padogo palipo na maua ya manjano katika mahali peupe mwituni. Nuru huangaza maua hayo ya manjano, ambayo huonekana yakimeta katika upepo wa asubuhi, huku mashina meusi ya miti yaliyopambwa na jua la asubuhi yakifanyiza mandhari-nyuma kamili. Sasa tuna picha. Tunachohitaji tu ni “kuiweka fremu,” na ndipo mtungo huja.
Mtungo. Namna ambavyo zile sehemu tatu za msingi—umbo, nuru, na rangi—huunganika ndiyo huamua mtungo. Na hapa sisi, tukiwa watazamaji, tuna fungu muhimu sana. Kwa kusonga kidogo tu mbele, nyuma, upande mmoja, juu zaidi, au chini zaidi, twaweza kurekebisha sehemu hizo au nuru katika picha tunayoona. Hivyo twaweza kuzuia picha iwe na sehemu tunazotaka tu.
Mara nyingi, tunatunga picha kikawaida katika akili zetu tunapopata kuona mandhari yenye kutazamisha inayozungukwa na miti au mimea iliyo karibu kana kwamba kwa fremu. Lakini picha nyingi zenye kupendeza, katika kiwango kidogo, ni ndogo sana na karibu na ardhi.
Kuona Vidogo na Vikubwa
Katika kazi ya mikono ya Mungu vyote vidogo na vikubwa vinavutia, na furaha yetu itaongezeka ikiwa twajifunza jinsi ya kuona mambo ya ndani, ambayo pia huunganika kwa kupendeza. Hayo hufanyiza michoro midogo mno ambayo imeenea kote katika kitambaa kikubwa cha asili. Ili kupendezwa nayo, tunachohitaji kufanya tu ni kuinama na kutazama kwa ukaribu.
Picha hizi zilizo ndani ya picha zinafafanuliwa na mpiga-picha John Shaw katika kitabu chake Closeups in Nature: “Huwa sikomi kamwe kushangazwa kwamba mwono wa karibu wa mambo ya ndani ya asili sikuzote hukaribisha mwono wa karibu hata zaidi. . . . Kwanza twaona mandhari iliyoenea sana, kisha sehemu ndogo ya rangi pembeni mwa fremu. Tazamo la karibu lafunua maua na, kwenye ua moja, kipepeo. Mabawa yake yanafunua kigezo halisi, kigezo hicho kinatokezwa na mpangilio maalum wa magamba ya bawa, na kila gamba ni kamili lenyewe. Ikiwa tungefahamu kikweli ukamilifu unaofanyiza gamba hilo moja la kipepeo, tungeweza kimawazo kuanza kufahamu ukamilifu wa ubuni ambao ni asili.”
Mbali na raha ya kisanaa inayotupatia, sanaa ya asili—kubwa na hata ndogo—hutuvuta karibu na Muumba wetu. “Inueni macho yenu juu, mkaone,” akasihi Yehova. Kwa kusimama ili kuona, kutazama, na kustaajabia, iwe twaelekeza macho yetu kwenye mbingu zenye nyota au wowote wa uumbaji wa Mungu, tunakumbushwa juu ya Yule “aliyeziumba hizi.”—Isaya 40:26.
Watu Waliojifunza Kuona
Katika nyakati za Biblia watumishi wa Mungu walikuwa na upendezi wa pekee katika uumbaji. Kulingana na 1 Wafalme 4:30, 33, “Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, . . . Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.”
Labda upendezi wa Sulemani katika utukufu wa uumbaji kwa sehemu ulikuwa kwa sababu ya kielelezo cha baba yake. Daudi, ambaye alitumia mingi ya miaka yake ya mapema akiwa mchungaji, mara nyingi alitafakari juu ya kazi ya mikono ya Mungu. Urembo wa mbingu hasa ulimfurahisha. Kwenye Zaburi 19:1, yeye aliandika hivi: “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake.” (Linganisha Zaburi 139:14.) Kwa wazi, kushughulika kwake na uumbaji kulimvuta karibu zaidi na Mungu. Kwaweza kutufanya vivyo hivyo.a
Kama walivyojua wanaume hawa wenye kumwogopa Mungu, kutambua na kuthamini kazi ya mikono ya Mungu hufurahisha moyo na kuboresha maisha zetu. Katika ulimwengu wetu wa kisasa uliokumbwa na utumbuizo usioshirikisha mtu kikamili ambao mara nyingi ni wenye kushusha kiadili, kuona uumbaji wa Yehova kwaweza kuandaa utendaji wenye kujenga kwa ajili yetu na familia zetu. Kwa wale wanaotamani ulimwengu mpya wa Mungu ulioahidiwa, kutafakari uumbaji wa Yehova ni kipitisha-wakati tutakachoweza kufurahia wakati ujao.—Isaya 35:1, 2.
Tuonapo si sanaa inayotuzunguka tu bali pia kutambua sifa za Msanii Mahiri aliyefanya yote, bila shaka tutasukumwa kutolea mwangwi maneno haya ya Daudi: “Hakuna kama Wewe, Bwana [“Yehova,” NW], wala matendo mfano wa matendo yako.”—Zaburi 86:8.
[Maelezo ya Chini]
a Waandikaji wengine wa Biblia, kama vile Aguri na Yeremia, walikuwa pia watazamaji makini wa historia ya asili.—Mithali 30:24-28; Yeremia 8:7.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Vielelezo vya vigezo na umbo, nuru, rangi, na mtungo
[Hisani]
Godo-Foto